SEHEMU YA 52
Hawakuchukua muda mrefu wakafika klabu ambapo wakateremka na kuelekea ndani. Humo, Fareed alionekana kama kuchanganyikiwa, alikuwa akicheza kila wimbo uliokuwa ukipigwa na kila alipotaka kunywa, alikwenda sehemu ya kununulia vinywaji na kunywa kwani alikuwa na mtu mwenye pesa.
Wakati hayo yote yakiendelea, vijana wa Keith walikuwa humo ndani, walikuwa wakifuatilia kila kitu, walimwangalia, wao wenyewe walihisi kwamba alikuwa mwanamke kwa jinsi alivyokuwa amejiremba na kuonekana mrembo kupita kawaida.
Muziki uliendelea mpaka iipofika saa tisa ambapo wakatoka huku Fareed akiwa amechoka kupita kawaida. Wakaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo.
Wala hawakuchukua mwendo mrefu, Mickey akasimamisha gari pembezoni mwa barabara ambapo hakukuwa na mwanga mkali na kisha kuteremka, Fareed alishangaa, naye akateremka kwa kuhisi kulikuwa na kitu lakini hata kabla hajafanya kitu chochote kile, gari moja likasimama, wanaume wawili waliokuwa na miili mikubwa wakateremka, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumfuata, wakamkamata na kumziba mdomo kisha kumuingiza ndani ya gari lao na kuondoka.
Fareed aliogopa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendela, hakujua wale watu walikuwa wakina nani na kwa sababu gani walikuwa wamemteka kama walivyofanya.
Wakati akijiuliza hilo, mwanaume aliyekaa pembeni ya dereva akageukia kule nyuma na kumwangalia Fareed, walipogonganisha macho, akashtuka baada ya kugundua kwamba alikuwa Keith.
“Keith…” aliita Fareed.
“Yes my love!” (ndiyo mpenzi wangu) alisema Keith huku akitoa tabasamu.
“What are you doing?” (unafanya nini?)
“I just want to play a game! A nice one, it is Flecks of Blood,” (ninataka tucheze mchezo! Mchezo mzuri, unaitwa Michirizi ya Damu) alijibu Keith huku akiwa kwenye tabasamu pana.
Safari iliendelea, Fareed alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake, alijua kabisa kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake, hakutegemea kuona mwanaume huyo akimfuatilia mpaka huko.
Akaanza kuomba msamaha kwa kuamini kwamba angesamehewa lakini hicho hakikuwa kipindi cha kusamehewa bali kilikuwa kipindi cha kuuawa kwa kile alichokuwa amekifanya.