Ashraf amshangaa Kimbau Send to a friend Tuesday, 15 March 2011 21:01
Imani Makongoro
VITENDO vya baadhi ya waratibu na waandaji wa mapambano ya ngumi za kulipwa hapa nchini kuwa upande wa mabondia wakati wa mapambano yao wanapokuwa ulingoni ni ukiukwaji na uvunjaji wa imani kwa mabondia hao dhidi ya wapinzani wao.
Hayo yalisemwa na bondia mkongwe wa ngumi za kulipwa visiwani Zanzibar,Ashraf Suleiman ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alipokea mkong'oto kwa Techinical Knock Out (TKO) dhidi ya Awadh Tamim pambano lililofanyika kwenye Ukumbi wa DDC Mlimani Park, Mwenge huku mratibu wa pambano hilo ambaye ni ofisa Habari wa Kampuni ya ulinzi ya Aurora ambao ndiyo walikuwa waandaaji wa pambano hilo Shomari Kimbau akiwa upande wa Tamim.
Katika pambano hilo Mwananchi ilimshuhudia Kimbau ambaye alikuwa na jukumu la kuhakikisha pambano hilo linafanyika kama lilivyopangwa huku akiwa na jukumu la upromota, lakini alionyesha wazi yupo upande wa Tamim .
Kimbau alikuwa mstari wa mbele kila baada ya raundi kumalizika kumpepea Tamim na kila bondia huyo alipoonekana kushambuliwa promota huyo alimuhimiza ili aongeze mashambulizi.
Suleiman aliiambia Mwananchi kuwa mbali na promota huyo kufanya hivyo katika pambano lake na Tamim, lakini si kitendo kizuri katika masumbwi kwani kinamwondolea imani bondia wa upande wa pili.
Ashraf ambaye alikubaliana na matokeo yake siku hiyo huku akidai kuwa amezidiwa kimchezo alisema,"Unajua muandaaji ndiye anayefanya kila kitu, anawalipa waamuzi na mambo yote kabla na wakati wa pambano huwa chini yake hivyo kitendo kama alichofanya Kimbau ni uvunjanji wa imani kwangu."
Hata hivyo Mwananchi ilipozungumza na Rais wa Organizesheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah alisema kuwa Kimbau alikuwa sahihi kumshangilia Tamim kwa kuwa bondia huyo yuko chini ya Kimbau tangu anaanza masumbwi.
Alisema pambano hilo liliandaliwa na kampuni ya Aurora na Kimbau kupewa jukumu la kuratibu ikizingatiwa kuwa bondia wake ndiye alikuwa akipanda ulingoni hivyo hawezi kuacha kumshangilia na kuongeza kuwa Ashraf akubali matokeo aliyopata siku hiyo kwani alijiuzulu mwenyewe bila shinikizo lolote.