Internazionale yashinda 2-0 kuzidisha upinzani kwa AC Milan Send to a friend Monday, 28 February 2011 20:49
ROME, Italia
UHSINDI wa mabao 2-0 ilioupata Internazionale Milano juzi dhidi ya Sampdoria umeirejesha katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Italia, Serie A na upinzani mkali kwa timu ya AC Milan.
Mabao ya Wesley Sneijder na Samuel Etoío yalitosha kuipa ushindi Inter Milan katika mchezo wa Jumapili wa Serie A.
Sneijder alifunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo ambao uliupenya ukuta wa wapinzani wao dakika ya 73, kisha Etoío akaongeza jingine dakika za majeruhi na kumaliza ukame uliodumu kwa mechi nne dhidi ya Sampdoria kwenye Uwanja wa Luigi Ferraris.
ìNimeridhika. Ushindi wa leo ulistahili umetokana na juhudi na kujituma kwa kila mmoja wetu, umemaliza kipindi kigumu kwetu ,î alisema kocha Leonardo.Sneijder ambaye alikuwa majeruhi alikuwa makini katika kipindi cha pili, kiasi cha kukaribia kufunga bao la pili, pia kwa mkwaju wa aadhabu ndogo, dakika ya 80.
Naye kiungo wa Sampdoria, Andrea Poli alipiga mkwaju ambao uligonga mwamba, dakika ya 43, huku wenyeji wakitengeneza nafasi zaidi za kupata mabao kuliko Inter katika kipindi cha kwanza.
Kipa wa Inter, Julio Cesar pia alikuwa makini baada ya kulaumiwa kwa kosa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wiki jana dhidi ya Bayern Munich.
Kwa matokeo hayo, Inter imepunguza pengo la pointi na kubakia mbili kati yake na AC Milan, ambayo jana ilikuwa ikicheza na Napoli inayoshika nafasi ya tatu.
Mapema , Udinese ilikaribia kukata tiketi ya michuano ya Ulaya msimu ujao bada ya kuiadhibu Palermo kwa mabao 7-0, huku Palermo ikimaliza mchezo na wachezaji tisa, kipigo ambacho huenda kikamwondoa kibaruani kocha Delio Rossi.
Mshambuliaji raia wa Chile, Alexis Sanchez alifunga mabao manne kati ya hayo na Antonio Di Natale akiongeza matatu (hat trick) na kufikisha mabao 21, akimpiku Edinson Cavani wa Napoli kwenye orodha ya vinara wa mabao Serie A msimu huu.
Rais wa Palermo , Maurizio Zamparini alisema kuwa Rossi amepewa nafasi moja ya mwisho kujiokoa kitanzini.
ìRossi ameharibu kikosi chetu. Nimemweleza abadili safu ya ulinzi, lakini hakufanya hivyo,î alisema Zamparini. ì Timu haiwezi kucheza vibaya namna ile.î
Rossi alitangaza pia kwamba hatajiuzulu, lakini alieleza kuwa anakubali lawama kwa kipigo hicho kibaya.
Kwingineko, mshambuliaji wa zamani wa Juventus , Amauri alifunga mabao mawili kwa Parma ambayo ilitokea nyuma na kupata sare ya 2-2 dhidi ya AS Roma na kutibua mwanzo mzuri wa Vincenzo Montella kama kocha wa Roma.
Roma ilitangulia kufunga kwa penalti ya nahodha Francesco Totti, ambaye alicheza mechi yake ya 600 akiwa mjini Rome na jingine la beki Mbrazili Juan.Pia, Roma ilimpoteza kiungo wake mahiri David Pizarro aliyeumia katika mchezo huo.
Montella, amerithi mikoba ya Claudio Ranieri aliyejizulu baada ya Roma kufungwa mabao 24 msimu huu.
ìHadi dakika ya 75hatukuruhusu shuti langoni mwetu ,î alisema Montella. ìTunahitaji kuongeza kasi yetu na mfumo wa uchezaji wetu, lakini hilo haliwezi kufanyika ndani ya siku tatu.î
Jirani zao, Lazio walifungwa 1-0 na Cagliari kwa kosa la beki Andre Dias.Matokeo mengine : Bari 1-1 Fiorentina; Brescia 2-2 Lecce ; na Cesena 1-0 Chievo Verona. Catania 2-1 Genoa.