Kuna wakati fulani nilikuwa nasikiliza redio moja, nadhani ilikuwa inaitwa 'Kwa Neema FM'. Kulikuwa na mtu mmoja alikuwa akieleza kuwa miaka mingi amefanya kazi ya uganga wa kienyeji. Na uganga wake zaidi ilikuwa kuwafanya wachungaji waweze kutenda miujiza wanapokuwa kwenye makanisa yao.
Akasema aliwahudumia wachungaji wengi sana. Akasema hawezi kuwataja lakini ataeleza ishara ya hao wachungaji. Alitaja ishara kadhaa, sikumbuki zote lakini moja kubwa aliyoitaja na ninayoikumbuka alisema, 'hawawezi kuhudhuria msiba wowote maana ndiyo sharti kubwa alilowapa'. Akasema, wafuatilieni wachungaji, na historia zao. Wapo ambao mtagundua hata siku moja hawajawahi kuhudhuria misiba. Watakwenda kuwatazama wagonjwa, watawaombea, lakini wale wagonjwa wakifariki tu, mchungaji hatafika kwenye matanga wala kwenye maziko.
Akihudhuria tu shughuli yoyote ya msiba, anakuwa amekiuka masharti. Hakusema akihudhuria kutatokea nini.