Elections 2010 Mgombea uraisi UPDP yu hoi kitandani anaumwa

Thursday, 30 September 2010 19:34 0diggsdigg

Fredy Azzah
AFYA ya mgombea urais wa Muungano kwa tiketi ya UPDP, Fahmi Dovutwa bado tete na yuko kitandani kwa siku tisa sasa kutokana na tumbo lake kujaa gesi, na hivyo kupata maumivu makali ya vichomi tumboni.

Akizungumza na Mwananchi jana, Dovutwa alisema tatizo hilo limekuwa likimsumbua tangu Septemba 22 mwaka huu na kwamba alienda Hospitali ya Tumaini na kupewa dawa ambazo anatakiwa kuzitumia mpaka Oktoba 2.
"Bado nipo kitandani... tumbo linajaa gesi na kunisababishia vichomi ambavyo vinanipa maumivu makali kweli," alieleza Dovutwa jana.

Dovutwa alisema kutokana na maumivu hayo, anashindwa hata kunyanyuka kutoka kitandani.
Alisema tarudi tena katika hospitalini mwezi huu ili kupata matibabu zaidi,
Akionekana kukata tamaa, Dovutwa alisema hajui lini ataanza lini kampeni kwa kuwa afya yake haionyeshi matumaini ya kuimarika mapema.

"Bwana wee acha tuu; hali ni mbaya; sijui lini nitaanza kampeni. Kwa sasa wenzangu wanapambana huko mimi nimelala kitandani," alisema.
"Sasa sijui itakuwaje kwa sababu siku zinakwisha na mimi nitakuja kuanza kampeni wakati wenzangu wanamalizia, sijui itakuwaje," elieleza.

Akizindua Ilani ya uchaguzi ya chama chake Septemba 15 mwaka huu, Dovutwa aliahidi kuanzisha kiwanda cha silaha; kufukuza wageni; kujiondoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na kufukuza wawekezaji.

Dovutwa, ambaye ofisi za makao makuu ya chama chake ziko Magomeni Kagera, aliwaambia waandishi wa habari kwenye hoteli ya nyota tatu ya Blue Pearl kuwa nia ya kuanzisha kiwanda cha silaha ni kuwezesha Tanzania kujilinda kwa ufanisi zaidi.
"Ili nchi iweze kuwa na maendeleo zaidi, ni lazima iwe na ulinzi wa kutosha unaotokana na utengezaji wa silaha zake zenyewe bila ya kununua nje ya nchi," alisema mgombea huyo.

Alisema, silaha zinazokamatwa nchini na Jeshi la Polisi, zinaletwa na walifu kutoa nje ya nchii baada ya kufanya uhalifu katika nchi zao.
"Katika baadhi ya vipaumbele vilivyoviainishwa kwenye ilani yangu ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kutengeneza silaha. Hii italeta heshima kwa nchi dhidi ya wahalifu wanaofanya vitendo hivyo katika nchi zao na kukimbilia hapa nchini," alisema Dovutwa.
Aliongeza kipaumbele kingine ni pamoja na kuvunja jumuiya iliyofufuliwa ya Afrika Mashariki ambayo anaona haina faida kwa wananchi.




Source:Mwananchi
 
Back
Top Bottom