Mgogoro wa Nafsi: Uhuru Wako Unaanzia Wapi?

Mgogoro wa Nafsi: Uhuru Wako Unaanzia Wapi?

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
944
Reaction score
804
Uhuru wako na utoshelevu unaanzia pale ‘wewe’ wa faraghani anapokaribiana na ‘wewe’ wa kufikirika (ideal self) unayemleta hadharani. Ikumbukwe kuwa huyu ‘wewe’ wa hadharani hubeba taswira unayoitaka—au unayejua ndio inayotarajiwa na watu —wakati ‘wewe’ wa faraghani hubeba taswira halisi (real self) lakini usiyojivunia nayo wala kutaka kuhusishwa nayo.

Ukaribiano wa hawa ‘wewe’ wawili wanaogombana, unakuondolea mgogoro wa nafsi, ambao kwa kawaida, huleta hofu na shinikizo la kukidhi matarajio yanayokuelemea na kukunyima furaha ya kuishi uhalisia wako. Uhuru wako, Carl Rogers anasema, unapatikana kwa namna mbili:

Kwanza, kujikubali, kwa maana ya kutokuwa na matarajio makubwa kupindukia, kutokujikweza kuliko uhalisia wako, uishi bila hofu ya kuhukumiwa, kudhalilika na kudharaulika pale ‘wewe’ wa kufikirika, usiyetaka ajulikane na watu atakapofahamika.

Lakini pia, kujifunza kumruhusu ‘wewe’ wa faraghani kumkaribia ‘wewe’ wa hadharani kwa kushughulikia tabia zako usizozipenda na unazojua zikifahamika heshima yako itakuwa rehani. Uhuru, Carl Rogers anasema, ni kuukwepa mtego wa kutaka kuonekana mkamilifu mbele za watu, na kuukabali ukweli kuwa una mengi usiyojivunia nayo lakini unapambana kuwa mtu bora siku kwa siku.
 
Back
Top Bottom