SoC02 Mfumo wetu wa elimu na matokeo kwa Taifa

Stories of Change - 2022 Competition

Ceo_crypto

Member
Aug 27, 2022
6
3
Nawasalimu wote kwa jina la taifa hili la thamani kwa kila mmoja wetu na mali yetu ambayo Mungu wetu alitubariki kuwa nayo, tunaamka kila asubuhi kulijenga hili taifa kwa nguvu zetu zote tukivuja jasho lenye chachu kubwa ya kuendeleza taifa letu.

Wengi wa wananchi wa taifa hili kwa asilimia kubwa tulipita hatua yoyote ya elimu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu vikubwa vya taifa hili na matumaini yetu yalikuwa tukifika shuleni tukipata elimu tutakuwa na maisha mazuri tutakuwa na kazi nzuri, tukiongozwa na hii hali ndio ilitupa chachu ya kupambana kusoma kwa bidii tukipambana pia na changamoto mbalimbali za kitaaluma na kijamii

Tulibebe vidumu vya maji kupeleka shuleni, tulibeba kuni na vitu vingine ambavyo tuliagizwa na walimu wetu wapendwa waliopambana pia nasi tupate elimu, kuna wakati changamoto zilikuwa nyingi zilisababisha wengine kuishia njiani katika safari hii ya elimu ila sisi wengine tuliobaki tulizidi kupambana na wengi wetu tukafika hatua kubwa ya kuhitimu vyuo vikuu kwenye kozi mbalimbali na kurudi mitaani na vijijini kwetu tukisubiri yale maisha mazuri ambayo elimu ingetupatia na hapo ndio tunagundua kuwa elimu tuliyopewa sio kile kinachotajika kwenye taifa kwasasa,

Mfumo wetu wa elimu unachangia kudumaa kwa taifa kwasababu zifuatazo ambazo kwa binafsi yangu kama mmoja wa wanafunzi ambao nimepitia kwenye mfumo huu wa elimu kwa asilimia mia hadi kuhitimu chuo kikuu

Mfumo wa elimu yetu upo kwenye mlengo mmoja tu ambao ni kuajiri, katika mifumo yetu ya elimu kuanzia msingi hadi chuo kikuu wanafunzi wanaandaliwa kuwa waajiriwa tu, hii ni kuanzia masomo yanayofundishwa mada zinazofundishwa kwenye masomo zote zipo moja kwa moja na kwenye kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajiriwa hata maneno ambayo walimu wanawaambia wanafunzi ni kuajiriwa tu.

Mfumo wetu wa elimu unamuweka mwanafunzi miaka mingi shuleni bila ujuzi wowote, katika mifumo yetu ya elimu kuanzia msingi hadi kumaliza sekondari mwanafunzi anatumia miaka kumi na tatu kupata elimu bila ya kuwa na ujuzi wa kitu chochote mwanafunzi ambaye amemaliza kidato cha sita ambaye anakuwa ametumia miaka kumi na tatu shuleni hana ujuzi wowote na hawezi kufanya jambo lolote la kimaendeleo na ikitokea ameshindwa kufika chuo kikuu anakuwa hana tofauti na yule aliyeishia kidato cha nne.

Mfumo wa elimu haumpi nafasi mwanafunzi kuchagua sehemu sahihi kwake, kwenye elimu yetu wanafunzi wanabebeshwa masomo mengi ambayo kuna mengine hayana umuhimu kabisa kwa taifa na hata kwa mwanafunzi na mwanafunzi hapati nafasi ya kuchagua masomo yale ambayo yeye binafsi atayaweza anaweza kusoma kwa ufanisi ila anabebeshwa yote hivyo kusababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu masomo.

Mfumo wa elimu ni wa nadharia sana kuliko vitendo, katika utoaji wa elimu kwenye shule zetu nadharia ni nyingi kuliko vitendo vyenyewe wanafunzi wamekuwa wakihadithiwa kuliko kuona uhalisia wenyewe shule zetu hazina Vifaa na bajeti ya kutosha ya kufundisha kwa vitendo hili tatizo lipo hadi kwenye baadhi ya vyuo pia.

Kuna mambo yanapaswa kufanyika ili kusaidia kuondoka hizi changamoto kwenye mfumo wetu wa elimu ili uwe na tija kwa taifa na uchumi vilevile kwa wanafunzi wenyewe na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kwenye jamii

Kubadilisha mlengo wa mfumo wetu wa elimu na elimu inayotolewa kwa ujumla, inapaswa kuwa na mfumo wa elimu ambao utamuandaa kijana kujitegemea na sio kutegemea kuajiriwa mfumo huu utafanikiwa kwa kupewa kipaumbele kwenye masomo ya ujasiriamali vilevile masomo ya teknolojia kama akili bandia, sarafu za mtandao na biashara za kimtandao hii itaongeza chachu ya faida ya elimu.

Kupunguza miaka ya kukaa shuleni au miaka ya masomo, hii itasaidia kwa wanafunzi kusoma kwa muda mfupi na kupunguza wimbi la wanafunzi kuacha shule, vilevile elimu ya kidato cha tano na sita ifutwe na iwe mwanafunzi akimaliza kidato cha nne aende moja kwa moja chuo cha kati apate diploma na serikali ihakikishe na hawa wanafunzi wanapata mikopo ili kuwasaidia wazazi na gharama za chuo.

Mfumo wa elimu uwe shirikishi kwa wanafunzi pia ili kila mwanafunzi asome kile ambacho kinamfaa na anakiweza kukimudu kwenye kusoma hii itasaidia kupata wataalamu bora katika Nyanja husika ikiwa ni michezo, sanaa ,uchumi, biashara, sayansi na ubunifu ambapo itachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la tatizo la ajira katika jamii na mitaa yetu.

Kuongeza Vifaa vya kujifunzia kwa vitendo maswala yote ya kielimu, na serikali inapaswa kuhakikisha mitaala yote ya elimu inafundishwa kwa vitendo pia na kusaidia wanafunzi kupata ujuzi wa kile wanachofundishwa kwa njia rahisi ya kuona kwa macho na wenyewe kufanya mazoezi kwenye Vifaa husika au eneo husika kabisa,

Kuongeza idadi ya walimu bora ambao sio wale waliofeli na kushindwa kusomea kozi nyingine na wakaamua kuingia kwenye ualimu kwasababu hata jamii inajua kuwa wengi wanaosomea ualimu ni wale wenye alama chache ambazo haziwezi kuwafikisha walipokuwa wanataka kwenda, hivyo serikali inapaswa kusimamia na kuweka vigezo ambavyo vitawezesha kupatikana kwa walimu bora kwenye shule zetu.

Kwa pamoja jamii na serikali zinaweza kushirikiana kuboresha mfumo wa elimu jamii ikisimama kama wazazi na kubadili baadhi ya mitazamo ambayo wanaijenga kwa watoto wao pia serikali isimamie mitaala yake ya elimu ifanyiwe maboresho ili iendani na kasi ya dunia na maendeleo, mabadiliko haya yatachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa hili na mabadiliko chanya ya taifa letu hili.

Imeandikwa na David Jerome (CEO_CRYPTO)
 
Back
Top Bottom