Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,007
- 9,873
Moshi. Meya wa manispaa ya Moshi, Juma Raibu ameagiza kukamatwa kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya kiwanja cha gofu cha klabu ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na kuwekwa ndani kwa madai ya kutolipa Sh26 milioni za kodi ya ardhi tangu mwaka 2013.
Pia, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuingilia kati suala hilo ili wanachama wa klabu hiyo wapate haki zao.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 29, 2021 katika kikao cha baraza la madiwani na kubainisha kuwa wanachama wamekuwa wakilipa kiingilio cha Sh100,000 kila mwaka.
"Nashangaa mpaka sasa mmiliki wa Moshi klabu hajakamatwa na kupelekwa mahakamani kwa kutolipa kodi ya ardhi kwa muda mrefu hadi kufikia Sh26 milioni," amesema Raibu.
Ameiomba Takukuru kuingilia kati na kuchunguza ada za wanachama zaidi ya 100 wanaotozwa Sh100,000 kwa kuwa hajui fedha hizo zinatumika katika jambo gani.
Ofisa ardhi manispaa ya Moshi, Jimson Msemwa amesema wanalifanyia kazi suala hilo kuhakikisha uongozi unafikishwa mahakamani.
MWANANCHI