Luteni Makamba ammiminia mabusu mfadhili wa miradi
2005-07-21 14:57:21
Na Maabad Msuya, Temeke
Baada ya kushindwa kujizuia kuonyesha furaha yake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusuph Makamba, amejikuta akimfagilia mfadhili wa miradi mbalimbali wilayani Temeke Bwana Yusuph Manji na kumtaka agombee ubunge wa jimbo la Kigamboni kwa tiketi ya CCM.
Kama vile haitoshi Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuonyesha ni jinsi gani alivyovutiwa na kufurahishwa na ufadhili huo, aliamua kumpa mabusu Bw. Manji kama ishara ya shukrani na furaha.
Luteni Makamba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, baada ya kuvutiwa na mwamko wa wakazi wa eneo hilo, naye ameahidi kuchangia Sh. milioni 1.5, kati ya hizo, milioni moja ikitoka mfukoni mwake na laki tano kwenye mfuko wa ofisi yake.
'Kusema kweli umenifurahisha sana na ili kukuonyesha ni jinsi gani umenifurahisha nakuomba usogee tena hapa karibu yangu ili nikupe busu la furaha,' akasema Mkuu huyo wa Mkoa na kisha akaanza kumimina mabusu mfululizo.
Source: Alasiri