Hizi habari zimekuwa zinazunguka kwa muda sasa, ila kwa karibuni zimepata kasi na mwelekeo mpya.
Kwa wale wanaokumbuka, vijana wa UVCCM Pwani walitamka wazi kwenye kikao chao kuwa Rais Kikwete anamjua nani atakuwa Rais, na mengineyo kuwa hatatoka kaskazini. Salva na Premi hawajawahi kukanusha wala kutoa tamko lolote kama kawaida pale ambapo JK 'anasingiziwa' kitu.
Taarifa za watu ambao tumekuwa na mawasiliano nao pale Magogoni na Lumumba ni kuwa sasa mkakati ni kama umekuwa wazi. Kuna masuala ambayo wamekuwa wanafanya na kutekeleza, ila sasa wamekuwa wanaulizwa kila hatua kuwa, je, Membe anajua au Membe amepewa taarifa?
Mengi ya masuala hayo hayahusiani kabisa na shughuli za Membe ki-chama wala ki-serikali, ila ni mambo ambayo yanabidi yaende juu hadi kwa Rais au Waziri Mkuu, au kwa Mwenyekiti au Katibu Mkuu.
Uzito wa masuala hayo yanategemeana na nini. Kuna suala moja zito la ki-serikali ambalo Mkulu alipewa taarifa na yeye akatoa kauli kuwa Mwambie Membe aliangalie. Masuala ya aina hiyo kawaida hupitia kwa Rais au Waziri Mkuu kwani ni mojawapo ya masuala ya ki-utendaji na ki-maamuzi serikalini, na yanagusa wizara ambazo siyo za Membe.
Kwa upande wa ki-chama, kuna maamuzi na mikakati ambayo imependekezwa na inafanyiwa kazi kwa nia ya kupunguza nguvu nyingi za vikao vya chama, na kumfanya Mwenyekiti au Katibu Mkuu kupitia Sekretariati kuwa na nguvu pasipo kikomo. Yote haya yanasukumwa ili yaweze kutekelezeka kabla ya 2012, ili kupunguza nguvu za Mkutano Mkuu na uchaguzi wa chama 2012. Kuna wanaoamini kuwa hiyo ni njia ya kumpa Membe mwanya ndani ya chama, kwani inaeleweka kuwa hana nguvu yo yote ndani ya Kamati Kuu, NEC wala Mkutano Mkuu, na hivyo hataweza kupata nafasi yo yote ya kupitishwa kwa kutumia katiba na kanuni zilizopo sasa.
Kwa wafuatiliaji wazuri wa masuala haya, tutakumbuka kuwa Moi alijaribu kufanya hivyo 2002 wakati wa KANU na Project Uhuru. Moi alibadilisha uongozi wa juu wa KANU, na kuvuruga taratibu zote za ki-chama ili kumpa nguvu Uhuru ndani ya KANU ili aweze kugombea na kushinda u-Rais wa Kenya. Matokeo yake ni kuwa akina Odinga (NDP), Kamotho, Kilonzo, Ntimama, Saitoti, Mudavadi na wengine waliitosa KANU na hatimaye kusababisha KANU kupoteza. Na pia kutokana na mabadiliko hayo, yaliidhoofisha KANU kiasi kwamba kanuni na taratibu zao mpya, zikawa ndiyo kikwazo cha KANU kujaribu kufufuka tena.
Mukama, kwa ushauri wa Kikwete na Membe, wanaipeleka CCM huko huko na Mukama anaelekea kuifanya CCM jinsi alivyolifanya Jiji la Dar, kabla ya jiji kuja kuokolewa na Keenja.
Lakini vile vile hili linaweza kuwa jambo jema, kwani hakuna kitu kibaya kama kubadilisha sheria na kanuni mathubuti ili kuwabana watu au kundi fulani, halafu kesho na kesho kutwa mabadiliko hayo hayo yanakuja kuwabana hao hao walioasisi.
Tumeona Kenya kwa KANU, Malawi kwa Mulunzi, Zambia kwa Chiluba, South Africa kwa Mbeki na kabla ya hapo De Clerk kwa Mandela, Ivory Coast kwa Gbagbo, Mexico kwa Salinas/Fox, na pengine sasa inaweza ikawa zamu yetu pia.