RIWAYA; MDUNGUAJI WA GOMA.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SEHEMU YA KUMI NA SITA.
Alipohakikisha kila kitu kipo kama alivyokusudia, aliongeza mwendo wa gari lake huku akizima taa za gari na kuendesha kwa kukadiria njia.
Kwa mtu mwingine ile ilikuwa ni hatari kubwa kuendesha bila kuwasha taa, lakini kwake ulikuwa ni mchezo wa kawaida kabisa ambao haukumpa shida kuucheza.
Akiwa amebakiza kilomita mbili kuufikia mtaa wa Mailimbili, macho yake yaliweza kuona gari mbili kwa mbele yake, mita kama mia sita hivi. Gari lililokuwa limetangulia lilikuwa na kimulimuli juu, huku likipiga ving'ora na likiwasha taa za kuashiria hatari. Gari la nyuma lenyewe lilikuwa linatembelea kasi ileile iliyotembelewa na gari la mbele yake.
“Kumekucha!” Alijisemea huku akiongeza kasi na kuhamia upande ambao, gari za mbele yake zilipita na kuwachanganya zaidi, alichukua bunduki na kuachia risasi kadhaa bila mpangilio, kisha alivuta begi lake na kulivaa huku usukani akiwa ameuachia na gari likiwa kwenye kasi ile ile.
Alipohakikisha begi lake limemkaa vema, alishika tena usukani na kuliweka sawa gari, kisha aliachia na kupita pale alipokuwa amevunja kioo na kusimama kwenye boneti na bunduki yake mkononi.
Mbele yake aliweza kuona matokeo ya kurusha risasi, huku akiwa amezima taa za gari lake kwani; dereva wa gari lililokuwa mbele na kimulimuli, alivuta breki za ghafla bila kutoa tahadhari kwa dereva wa gari la nyuma yake na, kilichotokea ndicho kilichotarajiwa. Gari la nyuma liligonga gari la mbele ambalo lilikuwa linaserereka barabarani, gari la mbele nalo liliongezewa mwendo na kwenda kugongana uso kwa uso na gari la jeshi ambalo lilikuwa limeachwa na Miguu ya kuku lijiendeshe lenyewe.
Miguu ya kuku ambae aliyatarajia yaliyotokea, alikuwa amefanikiwa kuruka na kwenda kuanguka pembeni ya barabara, akiwa ametumia mtindo safi wa kikomando, akiwa ametanguliza upande wa bega lake la
kushoto kisha, akajikunja kama tairi na kutua
kwa mikono, huku akiwahi kuiondoa chini ili
isielemewe na uzito wa muaguko wake na
kuvunjika. Japo aliweza kupata majeraha, lakini aliweza kusimama huku bunduki ikining'inia begani na begi lake mgongoni.
“Baboon” Alijisemea wakati akishuhudia ajali ya kutisha, ajali ambayo alijua matokeo yake yatakuwa kama alivyokusudia na ili kujihakikishia ushindi, alivurumusha risasi zizizo na idadi kwenye yale magari ambayo bado yalikuwa yanabiringita bila mpango.
Lengo la kuvurumusha risasi lilikuwa ni kuwasha moto, kwa kuwa aliamini ni lazima tanki za mafuta zitakuwa zimepasuka. Kilichotokea ndicho alichokuwa amekusudia; moto mkubwa uliwaka na kushika gari zote tatu.
Haraka aliirusha ile bunduki kwenye ule moto, kisha aliondoka akiwa na begi lake mgongoni. Hakutaka kuendelea kwenda na ushahidi utakao wahi kumtia kizuizini.
Alijichanganya mtaani licha ya kukabiliwa na maumivu makali mwilini mwake, alikuwa akipishana na watu ambao walikuwa wakielekea kwenye ajali usiku ule.
Mtaa ule wa Mailimbili ulikuwa ni mtaa ambao ulikuwa umechangamka sana, nyumba nyingi na vichochoro vya hapa na pale. Mtaa ule ulichangamka pengine kwa sababu ya kuwa karibu na mji wa Goma.
Usiku huo kuna baadhi ya baa zilikuwa bado ziko wazi, muziki na kelele za walevi zilisikika kutokea sehemu mbalimbali. Hakujali kelele hizo, alizidi kutembea, akiwa na lengo la kuingia Goma usiku huo huo na hakutaka kutumia usafiri wowote kwa sababu, hakutaka kutengeneza mnyororo wa ushahidi.
Kutoka Mailimbili hadi Goma, lilikuwa na umbali wa kilomita mbili, hivyo kwake ilikuwa ni mwendo wa dakika chache, licha ya kutumia njia zisizo rasmi.
Alitembea kwa zaidi ya dakika ishirini bila kupumzika. Alitembea hadi alipohakikisha ameingia mjini Goma. Kama kawaida ya Goma, usiku ni kama mchana. Alikuta kumbi nyingi za starehe zikiwa wazi, huku baadhi ya shughuli nyingine za kibinadamu zikiendelea, ikiwemo usafiri wa daladala na gari binafsi.
Alisogea kwenye kituo cha dalaladala cha Ruesake, kituo ambacho kiligawanya magari ya kuelekea Mailitatu, kiwanjachandege, nduguwatwana, Lucy lameck, MtaawaNyerere na mtaa wa Angani.
Kutoka pale kituoni hadi mtaa wa mailitatu, kulikuwa na umbali mdogo. Lengo lake lilikuwa ni kwenda huo mtaa, lakini aliamua kupanda daladala za Nduguwatwana kupitia mtaa wa Nyerere.
Alikuwa na sababu zake kupanda daladala hizo, akiwa na lengo la kuendelea kukwepa mnyororo wa ushahidi. Pia alitaka kuona kitu fulani usiku huo, kabla hajalala.
Dakika ishirini na tano zilitosha kuwafikisha kwenye kituo cha daladala cha Nduguwatwana. Alishika yeye na abiria wengine.
Miguu ya kuku hakuwa mgeni wa mitaa ya Goma, hivyo alichukua njia kuelekea nyuma ya kituo cha daladala, ambako kulikuwa na kituo cha dereva taxi.
Alitumia dakika tano hadi alipofika kwenye hicho kituo na, alipanda kwenye gari na kuomba afikishwe mtaa wa mailitatu, kupitia kwenye barabara ya kambi ya jeshi ya Katindo, kambi ambayo iliongozwa na Brigedia jenerali Deonus Mwanawasa, alimaarufu Papaa Deo.
Safari ilianza kimya kimya na kama kawaida alijifanya kusinzia, wakati dereva alipozidi kuikata mitaa.
Walipofika karibu na kambi ya jeshi ya Katindo, alifumbua macho yake na kutazama kwa makini kambi ile kubwa, kisha alitizama upande ambao alitaka kuona na aliona alichotaka kuona, kisha akirudi kusinzia.
“Tumefika bwana” Dereva alimwamsha.
Aliamka na kufungua kibegi chake, alitoa pesa walizokubaliana na kumpa kisha alishuka na kukutana na mitaa iliyopoa kidogo.
Alichukua simu iliyokuwa kwenye kile kibegi na kuitazama.
“Shiit!” Aliropoka baada ya kuona ilivyokuwa imeharibika kwa kupasuka kioo chake. Alijua ilipasuka wakati alipojirusha kutoka kwenye gari na kubiringita chini kama chatu aliyenasa windo lake.
Alijaribu kuiwasha na iliwaka. Tabasamu likajiumba usoni mwake, huku akipiga hatua kuelekea upande wa pili, ambako kulikuwa na bar inayokesha.
Dakika chache alikuwa tayari ameshafika kwenye hiyo bar. Aliangaza upande aliyoutaka na alimwona dereva wa pikipiki akiwa amelala juu ya pikipiki yake. Alipiga hatua zake na kuelekea upande huo.
Alimwamsha dereva na kumuomba amfikishe La Paix hotel. Hoteli ulikuwa nyuma ya kambi ya jeshi, umbali wa kilomita tatu hadi nne na, wakati alipopita kambi ya jeshi ya Katindo, alitaka kuona kama angeliweza kuiona hoteli ile akiwa upande wa mbele wa kambi.
Aliiona kama alivyotarajia, hivyo kumchukua tena dereva pikipiki na kutaka kupelekwa huko, ulikuwa ni mpango wake aliousuka tangu akiwa nyumbani kwake Tegeta.
Pikipiki ilianza safari na yeye aliendelea kuitazama simu yake, isije ikazima kabla hajafika La Paix hotel.
******
Pikipiki ilisimama kando ya geti la kuingilia pale hotelini. Miguu ya kuku alishuka na kulipa, kisha alipiga hatua ndefu kuelekea getini, ambapo alijitambulisha na kuonesha vitambulisho vyake.
Vitambulisho vyake vilimuonesha yeye ni raia wa Malawi na jina lake aliitwa Tabo Fransis Mkorofi.
Ilikuwa ni kawaida yake kulitumia jina hilo, pale anapokuwa kwenye nchi ngeni ijapokuwa, mipakini hupita kwa jina lake kamili la Zuki Gado kutokea Tanzania.
Baada ya kukaguliwa na kuruhusiwa kuingia, alielekea moja kwa moja mapokezi. Huko alionesha risiti ya malipo kupitia kwenye simu yake.
“Mbona simu yako imepasukasuka!?” Mhudumu alimuuliza huku akimtizama kwa makini.
“Wakati nakuja nilipata ajali ya pikipiki” Alijibu huku akijaribu kuunda tabasamu la kirafiki.
“oooh, pole sana! Hujaumia kweli?”
“Sijaumia sana ndo maana waona nimefika hapa nikitabasamu”
“Pole sana kaka”
“Nishapoa.”
Ukapita ukimya mfupi huku mhudumu akihamishia macho yake kwenye kompyuta. Aligusa hapa na pale, kisha alimgeukia..
“ Karibu sana na risiti yako imedhibitishwa kwa malipo uliyokwisha kufanya. Chumba chako kipo tayari na ni chumba namba 225. Chumba hicho ni VVIP kulingana na gharama ulizolipa. Humo ndani kuna kila kitu, endapo utapenda kujihudumia mwenyewe au utapewa mhudumu atakaekuhudumia hadi utakapoondoka” Mhudumu alifafanua kwa kirefu na kumkabidhi ufunguo, ambao ulikuwa ni kadi(kichanjio).
“Shukrani sana” Alisema huku akipokea kadi na kuelekea upande wa kambarau.
Dakika tano baadae, Miguu ya kuku alikuwa maliwatoni akiswafi mwili wake, huku akiwa na kiboksi cha huduma ya kwanza, ambacho alikikuta kwenye kile chumba.
Alijihudumia vile alivyoona inafaa, kisha alioga na kutoka ambapo moja kwa moja alielekea upande ambao kulikuwa na jiko, huko alichagua kile alichoona kinafaa kulika kwa usiku huo na kuanza kupika.
Nusu saa baadae alikuwa anaweka chakula kwenye meza na kuanza kuhudumia tumbo lake. Alikula hadi alipohisi tumbo halihitaji tena chakula kingine tena.
Alisimama na kujinyoosha licha ya kuwa bado na maumivu mwilini mwake. Alipohisi mwili utamsumbua kwa maumivu, alifungua kibegi chake na kufungua mifuko iliyokuwa ndani, ambapo alitoka na kichupa kidogo, ambacho kilikuwa na tembe sita za vidonge. Alichukua tembe moja na kuibugia, kisha alirejesha alipokitoa.
Zilikuwa ni dawa za kuondoa maumivu na kuupa nguvu mwili.
Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, alijilaza kitandani na kuutafuta usingizi.
Alilala ikiwa ni saa kumi alfajiri.
****
Usingizi ulimpaa ikiwa ni saa nne ahsubuhi. Aliamka na kujinyoosha kidogo, kisha alianza kupiga mazoezi mepesi ili kujiweka sawa. Alipomaliza alienda kuandaa kifungua kinywa, kilipokuwa tayari alijipendelea kisha akashushia na maji mengi.
Alipojihisi yupo sawa, alienda kuwasha runinga ili kupata taarifa mbili tatu, kuhusu mji wa Goma na Congo kiujumla.
Alibadilisha chaneli nyingi na kitu alichogundua ni kuwa, kulikuwa na taarifa iliyokuwa imepewa uzito zaidi, kwa sababu alikuwa akiona maandishi madogo yakipita chini, hata kama kulikuwa na kipindi cha kawaida kikiendelea na, alipoyasoma yale maandishi, alijikuta akitabasamu kwa ushindi.
Yalikuwa ni maandishi yaliyotangaza kifo cha Brigedia Fredi Mutesa, ambae alikufa kwa ajali ya moto baada ya gari alilokuwamo kugongana na gari nyingine ya jeshi usiku uliyopita. Pia kulikuwa na vifo vya wanajeshi wengine sita, ambao walikuwa wanamlinda usiku huo.
“Man down!” Alijisemea huku akisimama na kuelekea dirishani. Alitizama mazingira ya nje jinsi yalivyokuwa ya kuvutia, nyumba nyingi zikiwa zimejengwa kwa mpangilio huku rangi za bati zikifanana.
Lengo lake la kusimama pale, si kuona mandhari ya kuvutia; lengo lake kilikuwa ni kuona kambi ya jeshi iliyokuwa kilomita chache kutoka pale hotelini
.
.
.
.NB; SASA UNAWEZA KUIPATA RIWAYA HII IKIWA HADI MWISHO KWA BEI YA TSH 2500/
NAMBA ZA MALIPO...
0656741439.Tigopesa.
0658564341.Tigopesa(WhatsApp)
0758573660.Mpesa.(WhatsApp)
0624155629.Halopesa.
NAMBA ZOTE JINA NI, BAHATI K MWAMBA.
UNAWEZA KUTUMA PESA UKIWA POPOTE DUNIANI
.