Adaiwa kumteua kinyemela Mkurugenzi wa NHC
Mchakato wadaiwa kutumia Sh. milioni 82
Mwenyewe aziita tuhuma ni za kipuuzi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati
Mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), umegharimu Sh. milioni 82, imebainika.
Mchakato huo ambao uliendeshwa na kampuni ya Price WaterHouse Coppers (PWC) ambayo ilikuwa mshauri mwelekezi, kwa takribani miezi mitatu, haukufanyiwa kazi na badala yake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, aliamua kumteua bosi mpya wa NHC kwa kutumia Sheria Na. 2 ya 1990 inayounda shirika hilo, kifungu cha 18 (1).
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya shirika hilo zinaeleza kuwa bosi huyo mpya wa NHC, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), Nehemia Msechu (37), ameelezwa kutokuwa na sifa za kusimamia shirika hilo. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Msechu (37) ni mmoja kati ya watu waliowania nafasi hiyo wakati ilipotangazwa na kampuni ya PWC, lakini hakuitwa kwenye usaili kutokana na kutokuwa na sifa muhimu za kushika wadhifa huo.
Pamoja na kwamba Msechu aliomba nafasi hiyo, hakuwa short listed, kibaya sana, kama serikali ilijua ina mtu wake ambaye ingemteua, kwa nini walitumia Sh. milioni 82 kumlipa mshauri mwelekezi wa kumtafuta Mkurugenzi Mkuu, kilieleza chanzo chetu.
Chanzo hicho pia kilieleza kuwa iliyokuwa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo, ilipitia orodha ya waombaji iliyowasilishwa kwake na kampuni ya PWC na kupendekeza majina matatu ya wakurugenzi wa vitengo ndani ya NHC ambao pia waliomba nafasi hiyo na kuonekana kuwa na sifa, lakini wizara ilipuuza mapendekezo hayo na kuamua kufanya uteuzi.
Bodi ilifanya hivyo kwa kuamini kuwa watu wenye sifa na uzoefu wa kutosha kuhusu shirika hilo ni wafanyakazi wenyewe, hiyo pia tulidhani ingewapa wafanyakazi motisha ya kufanyakazi kwa bidii, alisema mjumbe mmoja wa bodi ya NHC iliyomaliza muda wake.
Waziri Chiligati alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema ni maneno ya hovyo na majungu ambayo yatawapotezea Watanzania muda.
Hilo la hela muulize Katibu Mkuu, maana ndiye anayetoa fedha naamini yeye atakuwa na taarifa zaidi kuliko mimi, alisema.
Alipoulizwa sababu za kuajiri mshauri mwelekezi wa kumtafuta Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo wakati sheria inampa nguvu ya kumteua mtu mwenye sifa, alikwepa kujibu na kumwelekeza mwandishi amuulize Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi.
Alieleza kuwa uteuzi wa Mkurugenzi wa NHC, unapitia mikononi mwa watu wengi na kwamba kama angekuwa na kasoro, zingebainika mapema.
Sikumteua mimi mwenyewe, amepita mikononi mwa watu wengi vikiwemo vyombo vya dola, hivi kama hakuwa na sifa, zisingebainika? alihoji Chiligati na kuongeza Hayo ni maneno ya hovyo tu na majungu ambayo tukiyafuatilia yatatupotezea tu muda,
Shirika hilo kwa sasa linajipanga kujiingiza kwenye biashara ya kujenga nyumba katika mikoa yote na kuziuza kwa mkopo nafuu kwa Watanzania wa kipato cha chini na kati.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI