Mbunge Stanslaus Nyongo Asema MSD Iwezeshwe Mtaji Ili Ifikie Malengo

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,900
944

MBUNGE STANSLAUS NYONGO ASEMA MSD IWEZESHWE KIMTAJI ILI IFIKIE MALENGO NA KUTOA HUDUMA NZURI KWA WANANCHI

Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo tarehe 12 Mei, 2023 amechangia hotuba ya Bajeti Wizara ya Afya Bungeni jijini Dodoma iliyosomwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.

"Tunatambua, Maadui wakubwa ni hatujawasahau; Maradhi, Umasikini na Ujinga. Hawa ndiyo maadui zetu wakubwa katika nchi yetu. Maadui hawa ni Maadui wa Afrika nzima." - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki

"Miaka ya nyuma Viongozi wetu walikaa Abuja wakatafakari wakasema kwamba kila nchi inapoandaa bajeti itengwe angalau asilimia 15 ya bajeti ya nchi iende ikahudumie masuala ya Afya. Mpaka sasa tuna asilimia 2.8 inayotengwa kwa ajili ya huduma ya Afya. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya kupeleka huduma za afya" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja kuhakikisha afya za watanzania linakuwa jambo la kipaumbele. Kila mtanzania anapopata shida aende apate tiba ya uhakika, tiba nzuri ya hali ya juu" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Kwa sababu maradhi ni adui mkubwa ni lazima tuwe na mkakati wa kutenga fedha kwa ajili ya kuhudumia wananchi. Bima kwa watu wote. Tanzania kupitia Serikali imefanya kazi kubwa kupitia Universal Health Coverage (Kila nchi lazima ipeleke huduma ya afya kwa wananchi wake). Tumejenga vituo vya afya, Zahanati, Hospitali za Rufaa (Mkoa) na Hospitali za Kanda" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Kupitia Universal Health Coverage miundombinu ya afya imejengwa kwa sababu lazima tupeleke Matibabu, Huduma za Kinga, Chanjo. Changamoto iliyopo huduma imeshasogezwa Kijijini huyu mwananchi anakwenda vipi kulipia huduma katika kituo ambacho ameletewa. Ndiyo tunapiga debe tuwe na Universal Health Coverage" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Hali iliyopo, mifuko ya bima inapata shida (Suffocate) kwa upungufu wa fedha. Toto Afya Kadi imefutwa, mimi nilishangaa. Njia iliyopo ni kutafuta njia nyingine mbadala ya kuhakikisha watoto wanapata huduma za bima. Bima iwe ni watoto wanaingia kwenye Package za Wazazi na Shule zetu zihakikishe watoto wanakuwa na Bima ya Afya" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Naishauri Serikali tuhakikishe mfuko Maalum kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kupitia Bima zao. Tuna asilimia 28 ya watanzania ni masikini. Ni lazima Serikali iwahudumie kwa kuwapatia Bima. Serikali inaingia gharama kubwa kuwasafirisha wananchi kwenda nje kwa ajili ya matibabu ya kibingwa" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Tumeona Hospitali za Mikoa na Kanda zinatoa misamaha kwa wananchi zaidi ya Bilioni 600 wanatoa msamaha kwa mwaka mmoja. Ni lazima tuwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba tunatoa fedha kwa ajili ya Bima kwa wananchi" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"MSD amekuwa mtu anayepokea fedha kwenda kununua dawa. Tunaomba tuipatie MSD mtaji iliyoomba inataka Bilioni 592 kwa ajili ya kununua dawa, kujenga maghala na kuanzisha viwanda vya dawa ili kuwawezesha watu binafsi kujenga na kuzalisha dawa kwa ajili ya matumizi ya watanzania na kwenda kuziuza nje ya nchi" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Tunaomba Wizara ya Fedha muwasilikilize MSD, msipowasikiliza tatizo la upungufu wa dawa kwa wananchi wetu litaendelea kujitokeza. Leo MSD akisema apeleke madawa atumie fedha zote atakuwa na upungufu wa zaidi ya billion 133. Ni lazima tufanye jambo kuhakikisha MSD anapata mtaji aweze kufanya kazi zake ambazo amepangiwa" - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo

"Huduma za afya Wizara ya Afya inafanya vizuri. Tunaona Hospitali za Mikoa na Kanda zinafanya vizuri. Kule chini kwenye Hospitali za Wilaya, Zahanati na Vituo vya Afya bado tunaona kuna tatizo. Aliyeshikilia sera ya afya ashikilie hivyo hivyo mpaka kwenye Zahanati na vituo vya afya' - Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo
 

Attachments

  • WhatsApp Image 2023-05-15 at 18.16.54(1).jpeg
    WhatsApp Image 2023-05-15 at 18.16.54(1).jpeg
    59.5 KB · Views: 5
Back
Top Bottom