Ni wajimbo gani huyu Jamani? RIP Mh!
RIP Silima
Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi (CCM), Maalim Mussa Silima, amepata ajali na mkewe, Mwanaheri Alli, amefariki dunia baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongana na gari ya mizigo eneo la Nzuguni mkoani Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Uzini, Muhammed Seif Khatib, alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11:00 jioni na marehemu alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Alisema Mbunge huyo ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, alikuwa akitokea jijini Dar es Salaam akiwa amefuatana na mkewe akiwahi kikao cha Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa kifanyike jana pamoja na kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano.
"Marehemu anatarajiwa kuzikwa katika kijiji cha Kiboje Mkoa wa Kusini Unguja," alisema Khatib na kuongeza kuwa Mwakilishi huyo alisafirishwa kwa ndege kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Kitengo cha Mifupa (MOI).
Alisema baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Dodoma, madaktari walishauri ahamishiwe MNH kutokana na maumivu aliyoyapata sehemu ya uti wa mgongo na paja.
Alisema gari ya mbunge huyo ilikuwa ikiendeshwa na dereva wake, Chizani Sembonga, alipokuwa akijaribu kuikwepa gari iliyokuwa mbele yake alikutana na gari lingine na kugongana nalo.
"Ujumbe wa wabunge tisa umeteuliwa kuwakilisha Bunge katika mazishi wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Dole, Juma Nhunga," alisema Khatib. Mwakilishi huyo alichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwa mara ya kwanza baada ya kumuangusha katika kura za maoni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Tafana Kassim Mzee.