MAYAHUDI KUSEMA MANENO YA DHAMBI.
Mwenyezi Mungu S.W.T. aliwahadharisha sana Mayahudi na akawaonya wasiseme maneno ya dhambi. Na hasa Wanavyuoni wao aliwalaumu sana kwa kule kuacha kukataza ule msemo wa maneno ya dhambi. Kama alivyotueleza Mwenyezi Mungu S.W.T. katika suratil Maaida aya ya 63,
"
"Mbona Wanavyuoni na Makuhani wao hawawakatazi maneno yao ya dhambi, na ulaji wao wa haramu? Ni maovu mno hayo wayafanyayo!"
Lakini Mayahudi waliendelea na huo msemo wao wa dhambi. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu S.W.T. akawalipa malipo ya kama waliyoyachuma. Kama alivyotusimulia katika Suratil An`aam aya ya 120,
"Na acheni dhambi zilizodhahiri na zilizofichikana. Hakika wanaochuma dhambi watalipwa kwa waliyokuwa wakiyachuma."
Na hayakuwa hayo maneno ya dhambi ila ni kumuudhi Mwenyezi Mungu S.W.T. na Mitume Yake. Kwa hali hiyo wakastahili laana ya Mola Mtukufu na ghadhabu Yake katika dunia na Akhera. Na Allah S.W.T. ametuhakikishia haya katika Qurani tukufu, kasema katika Suratil Ahzaab aya ya 57,
"
"Kwa yakini wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (S.A.W.), Mwenyezi Mungu amewalaani katika dunia na Akhera, na amewaandalia adhabu ifedheheshayo."
Na hapa chini nitataja moja moja yale maneno ya dhambi waliyoyasema Mayahudi kama ifuatavyo:-
1.KUSEMA "MKONO WA MWENYEZI MUNGU UMEFUMBA.
Mayahudi walisema maneno chungu nzima ya dhambi na kwa sababu hiyo wakalaaniwa. Na moja ya neno hilo lilikuwa "Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Maaida aya ya 64,
"Na Mayahudi walisema: "Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyoyasema. Bali mikono Yake iwazi. Hutoa apendavyo..."
Na katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas R.A.A. kasema,
"
"Kasema mwanamume mmoja miongoni mwa Mayahudi aitwaye Shaas bin Qais: "Hakika Mola wako bakhili hatoi." Mwenyezi Mungu akateremsha [Na Mayahudi walisema: "Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyoyasema. Bali mikono Yake iwazi. Hutoa apendavyo.]"
Inasemekana Mwenyezi Mungu S.W.T. aliwaneemesha sana Mayahudi kwa mali nyingi wakawa ni watu matajiri sana. Lakini walipomuasi Mola Mtukufu kwa sababu ya kumkufuru Mtume Muhammad S.A.W. na kuukadhibisha ujumbe wake. Akawanyang`anya ile mali aliyowapa. Kwa sababu hiyo Mayahudi wakasema: "Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." Na Mola Mtukufu akalipizia kisasi kwa hilo neno lao baya kwa kuwafanya wawe mabakhili na maskini na wakaidi.
Na Mwenyezi Mungu S.W.T. akawahakikishia katika aya hiyo hiyo ya Suratil Maaida aya ya 64 kuwa,
"Mikono Yake iwazi. Hutoa apendavyo."
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu kasema katika aya nyingine katika Qurani tukufu kwamba kawafadhilisha binadamu kwa neema zisizohesabika. Kasema katika Surat Ibrahim aya ya 34, "
"Na akakupeni kila mlichomwomba (na msichomwomba). Na kama mkihesabu neema za Mwenyezi Mungu, hamtaweza kuzihesabu. Bila shaka mwanadamu ni dhalimu mkubwa asiye na shukurani (mwizi wa fadhila)."
Na kama ilivyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na L-Bukhari, Mtume S.A.W. kasema,
"Hakika mkono wa kuumeni wa Mwenyezi Mungu umejaa haupungui kutoa unatoa kwa wingi usiku na mchana. Jee! Hamuoni ulivyotoa tokeya kuumbwa mbingu na ardhi. Kwa hakika haupungui uliyo kuumeni Kwake. Kasema: "Na arshi Yake juu ya maji. Na mkono Wake mwingine unakamata. Unapandisha na kupunguza."
2.KUSEMA "MWENYEZI MUNGU NI FAKIRI NA SISI NI MATAJIRI.
Mayahudi walisema neno lingine la dhambi kumwambia Allah S.W.T. kwamba: "Yeye ni fakiri na wao ni matajiri." Na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu S.W.T. amewaandalia huko Akhera adhabu ya Moto wa Jahannam. Kama alivyotusimulia katika Suratil Aali-`Imraan aya ya 181 na ya 182,
"Mwenyezi Mungu amekwishasikia kauli ya waliosema: "Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri." Tumeyaandika waliyoyasema, na pia kuwauwa kwao Manabii bila haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: "Onjeni adhabu ya kuungua." Haya ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yenu, na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja."
3.KUMSINGIZIA BIBI MARYAM KUWA KAMZAA NABII ISSA (YESU) KWA KUZINI.
Mayahudi walizidisha maneno yao ya dhambi na wakafikia hadi kumsingizia Bibi Maryam ati kamzaa Nabii Issa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kuzini na mtu mwema aliyeitwa Yuusuf Najjaar. Na neno lao hilo la uwongo la kutisha na la dhambi hawakuwa na dalili nalo na wala hoja yoyote ile. Na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu S.W.T. aliwalaani mpaka siku ya Kiyama, kasema kutubainishia katika Suratin Nisaa aya 156,
"…Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu uwongo mkubwa."
Mwenyezi Mungu S.W.T. atambebesha dhulma kubwa na dhambi yule mtu atakayemsingizia mwingine bila yule aliyesingiziwa kufanya kitendo kile. Kama alivyoelezea katika Suratil Ahzaab aya ya 58,
"Na wale wanaowaudhi Waislamu wanaume na Waislamu wanawake pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri."
4.KUSEMA "NYOYO ZETU ZIMEFUNIKWA."
Na katika neno lao la dhambi Mayahudi walisema: "Nyoyo zetu zimefunikwa." Na sababu ya kusema kwao hivyo walidai kwamba ati nyoyo zao zimejaa elimu walioletewa katika kitabu cha Taurati kwa hivyo hawahitajii ile elimu aliyokuja nayo Mtume Muhammad S.A.W. kuwafundisha. Na lau kama kweli walikuwa na elimu nyingi lakini hata hivyo hawakufahamu wala hawakutumia akili zao kuhusu mambo aliyokuwa akiwaelezea Mtume S.A.W.. Na kwa sababu hiyo wakastahili laana ya Mola Mtukufu. Na Mwenyezi Mungu S.W.T. amelielezea neno hili ndani ya Qurani tukufu, kasema katika Suratil Baqarah aya ya 88,
"Na walisema: "Nyoyo zetu zimefunikwa." Bali Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayoyaamini."
Na katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Said L-Khudriyy R.A.A. na iliyotolewa na Ahmad, Mtume S.A.W. kasema,
"(Aina za) nyoyo ni nne:…Na ama moyo wenye (kufunikwa na) kifuniko ni moyo wa kafiri…"
Na kauli ya Mayahudi ya kusema: "Nyoyo zetu zimefunikwa," imefananishwa sana na kauli waliyosema makafiri wa Kiarabu wakati Mtume S.A.W.alipokuwa akiwaita katika Uislamu. Kwani daima fikira za makafiri ni sawa.
Kama alivyotufahamisha Mwenyezi Mungu S.W.T. ndani ya Qurani tukufu, kasema katika Surat Fusilat (Ha-Mym-Sajdah) aya ya 5,
"Na wakasema: "Nyoyo zetu zi katika vifuniko kwa yale unayotuitia; na katika masikio yetu mna uzito; na baina yetu na baina yako kuna pazia; basi fanya (yako), na sisi tunafanya (yetu; kila mtu asimuingilie mwenziwe.)"
5.KUSEMA "MBONA MWENYEZI MUNGU HASEMI NA SISI."
Mayahudi waliendelea kusema maneno yao ya dhambi na moja ya neno lile walilosema lilikuwa:
"Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi."
Kama alivyotuhadithia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqarah aya ya 118,
"Na walisema wale wasiojua kitu: "Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara." Vivyo hivyo walisema wale waliokuwa kabla yao, mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini."
Na Mwenyezi Mungu S.W.T. aliwajibu Mayahudi ndani ya Qurani katika Surat Sh-shuura aya ya 51,
"Na haikuwa kwa mtu kwamba Mwenyezi Mungu anasema naye ila kwa ilhamu (anayotiwa moyoni mwake) au kwa nyuma ya pazia (la kumsikilizisha sauti inayotokana na Mwenyezi Mungu pasina kumuona Mwenyewe) au humtuma Mjumbe (Jibril A.S.), naye humfunulia (humletea Wahyi) kiasi anachotaka kwa idhini Yake; bila shaka Yeye Ndiye Aliye juu, Mwenye hekima."
6.KUSEMA "HUTUTAAMINI MPAKA TUMUONE MWENYEZI MUNGU."
Mayahudi haikuwatosha kusema kwa matamanio yao kuwa:
"Tunataka tuseme na Mwenyezi Mungu Mtukufu,"
bali walifikia hata kuomba wamuone Mwenyezi Mungu Mtukufu Yeye Mwenyewe kwa macho yao ndio waamini baada ya kuwaijia Ishara zote na dalili za ukweli. Na Qurani tukufu imeleta dalili ya neno hilo:
"Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi."
Yakawa matokeo ya maombi haya ni kuwapatisha adhabu ya Mola Mtukufu. Aliwapiga radi ikawauwa wote nao wanaangalia kwa macho yao. Kisha baada ya hapo Mwenyezi Mungu S.W.T. akawahuisha ili wapate kushukuru neema Zake. Kama alivyotuhadithia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqarah aya ya 55 na ya 56,
"Na mliposema: "Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi." Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru."
7.KUSEMA "`UZEIR MWANA WA MWENYEZI MUNGU."
Mayahudi walimuitakidi `Uzeir ni mwana wa Mungu na hawakujua kuwa neno hilo lilikuwa ni la dhambi kubwa sana kumfanya Mola wa walimwengu wote kazaa mtoto. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Tawba aya ya 30,
"Na Mayahudi wanasema: `Uzeir ni mwana wa Mwenyezi Mungu; Na Manasara (Wakristo) wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu; haya ndio wasemayo kwa vinywa vyao (pasi na kuyapima). Wanayaiga maneno ya wale waliokufuru kabla yao, Mwenyezi Mungu awaangamize. Wanageuzwa namna gani hawa."
Na `Uzeir A.S. alikuwa ni Mtume katika Mitume walioletewa Mayahudi. Na inasemekana mfalme aitwaye Bukht-Nasr aliwauwa Wanavyuoni wote wa Kiyahudi na akabomoa majumba yao kisha akawachukua mateka wa Kiyahudi kuwapeleka Baabil (Hivi sasa ni nchi ya Iraq). Na wakati ule `Uzeir A.S. alikuwa bado kijana mdogo wakamwacha hai hawakumuua kwa sababu ya umri wake mdogo. Mayahudi waliporejea Baitil Muqaddas hawakupata mtu anayeweza kusoma Taurati. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu S.W.T. akamtuma `Uzeir A.S. awe akiwafundisha Taurati na pia awe muujiza kwao baada ya Mola Mtukufu kumfisha miaka mia na kumhuisha.
Aliporejea kwa Mayahudi aliwaambia:
"Mimi ni `Uzeir," wakamkadhibisha wakasema: "Ikiwa kweli kama unavyodai basi tusomee Taurati."
Alipokwishaisoma Taurati wakasema baadhi yao:
"Mwenyezi Mungu S.W.T. hakumwekea Taurati moyoni mwake ila kwa sababu ni mtoto wake."
Na kisa cha Nabii `Uzeir A.S. kimetajwa ndani ya Qurani tukufu, Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Baqarah aya ya 259,
"Au kama yule aliyepita karibu na mji uliokuwa umekufa akasema: "Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu (na watu wake) baada ya kufa kwake?" Basi Mwenyezi Mungu alimfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua akamuuliza: "Umekaa muda gani?" Akasema: "Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku." (Mwenyezi Mungu) Akasema: "Bali umekaa miaka mia; nawe tazama chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na mtazame punda wako (amekuwa mifupa mitupu iliyolikalika). Na ili tukufanye uwe hoja kwa watu (ndio tumekufufua hivi). Na itazame mifupa (ya punda wako jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama." Basi yalipombainikia (haya yule aliefufuliwa) alisema: "Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu."