Mauaji yaliyojaa utata

Spider

JF-Expert Member
Feb 13, 2011
1,604
1,500
Asanteni jamani tunaendelea

NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA

Sehemu ya Ishirini na Saba.

Wanaume watatu wenye uchu wa fedha walikuwa wamekaa sebuleni, chupa kubwa za pombe zilikuwa mezani na walikuwa wakinywa mfululizo, maisha yao yalionekana kubadilika kwani kitu walichokuwa wakikitaka, walikipata na kazi moja tu ndiyo iliyokuwa ikisubiriwa, kumuua mtu ambaye waliambiwa wamuue.
Mbele yao hakukuwa na kazi kubwa, kazi kubwa ambayo walikuwa nayo ni kumtafuta mtu huyo, baada ya kumpata, hakukuwa na kazi nyingine yoyote ile kwani kitendo cha kumuua, wala hakikuwa kazi kubwa, ilikuwa nyepesi sana, kama kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima Kitonga.
Walipokuwa wakiendelea kunywa pombe kali, ndipo waliposikia kelele kutoka katika chumba walichomuhifadhi David, walikumbuka kwamba walimsiba mdomo kwa kutumia gundi hivyo wakajua kwamba kijana huyo alileta ubishi na hatimaye kutoa gundi hiyo mdomoni.
Hilo liliwakasirisha sana, wawili wakamwambia mwenzao achukue bastola na kuelekea huko chumbani ili amtulize David, baada ya kunywa pombe ndipo wamuue kwa kumtumbukiza ndani ya pipa la tindikali.
“Kamtulize, akileta ubishi, mzimishe kwa muda,” alisema Cobra.
“Ila mnanionea sana, tunakunywa na kufurahia maisha, mnaanza kunituma,” alisema jamaa huyo aliyejulikana kwa jina la Amazon.
“Wewe nenda, kwanza wewe si ndiye mdogo, hatumalizi pombe zote,” alisema Cobra huku akimwangalia Amazon kwa jicho lililomtaka kufanya kile alichomwambia.
Huku akionekana kukasirika, Amazon akainuka, akachukua bunduki na tochi kisha kwenda katika chumba kile alichoambiwa aende. David hakunyamaza, aliendelea kuzungumza maneno yaleyale ya kuwatia hasira kwa kudai kwamba waliogopa kumuua.
Alipoufikia mlango ule, akawasha tochi na kuingia ndani, alipomulika, mtu aliyemuona akiwa amelala, hakumuona vizuri, alimuona kwa nyuma tu, kutokana na mavazi aliyokuwa nayo, aliamini kwamba alikuwa David, akaanza kumfuata pale chini.
Alipomfikia na kumwangalia vizuri, nywele nyingi alizokuwa nazo zilimshtua, alipotaka kugeuka tu, akashtukia akipigwa nondo ya kichwa, hapohapo akaanguka chini na kupoteza fahamu.
“Inuka...inuka Vivian,” alisema David huku akimuinua Vivian.
Vivian akainuka, David akachukua bastola ile na kumwambia Vivian amfuate, wakaanza kuelekea sebuleni. Walipofika huko, wakamkuta Cobra na mwenzake wakinywa pombe kali, hapohapo wakawaweka chini ya ulinzi.
“Ukitingishika tu, nakumwaga ubongo,” alisema David huku akionekana kuwa na hasira.
Wote wakatulia, kwa jinsi David alivyoonekana, alionekana kuwa na hasira nyingi ambaye hakutaka kabisa kufanyiwa mchezo. Walibaki wakiwa wametulia na kufanya kile ambacho David alitaka wakifanye.
Alichowaambia ni kwamba wachukue simu na kumpigia mtu ambaye aliwatuma na kumwambia kwamba kazi ilikuwa imekamilika, yaani yeye na Vivian walikuwa wamekufa.
Hakukuwa na aliyeleta ubishi kwani walijua kwamba kijana huyo hakuwa na masihara hata kidogo hivyo wakachukua simu na kumpigia Dracula. Simu iliita kwa muda mchache tu, ikapokelewa.
“Mmekamilisha?” ilisikika sauti ya Dracula kutoka upande wa pili.
“Kila kitu tayari! Tumewaua wote,” alisema Cobra.
“Safi sana! Ngoja niwasiliane na mzee, kiasi kilichobaki kitatumwa katika akaunti zenu,” alisema Dracula kisha Cobra kukata simu.
Hiyo wala haikutosha, alichoagiza David ni kwamba Vivian awafunge kamba na kisha waondoke, hilo wala halikuwa tatizo, Vivvian akarudi chumbani kule ambapo alimkuta Amazon akiwa hoi chini huku damu zikimtoka kichwani, akachukua kamba na kurudi sebuleni ambapo akawafunga vijana hao na wao kuondoka huku wakiufunga mlango kwa nje.
****
Dracula alikuwa akizungumza na Bwana Seppy katika kituo cha polisi, muda wote uso wa mzee huyo ulionyesha tabasamu pana kwani hakuamini kile alichokisikia kwamba mtu aliyekuwa akimsumbua kwa wakati huo alikuwa marehemu.
Hiyo ilimaanisha kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye angemtisha katika kesi hiyo kwani kama shahidi aliyekuwa akimtegemea Benjamin alikuwa mmoja tu, David ambaye mpaka katika kipindi hicho alipewa taarifa kwamba alikuwa marehemu.
“Una uhakika wamefanikiwa?” aliuliza Bwana Seppy.
“Ndiyo! Wamenipa taarifa, huwa wanafanya hivi kila siku,” alisema Dracula.
“Asante Mungu!”
Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumshukuru Mungu tu, kwake ulionekana kuwa kama muujiza mkubwa kwani kwa kipindi hicho alihitaji sana David auawe kuliko kitu chochote kile.
Alibaki akiiangalia saa yake, aliona muda ukikawia kwenda kwani alitamani kusimama kizimbani na kuiambia mahakama kwamba hakuwa amefanya mauaji na kama wanabisha walete shahidi kitu ambacho ingekuwa ngumu kwa Benjamin na watu wake kufanya hivyo.
Upande wa pili ulikuwa ni kilio tu, taarifa zilianza kusambaa kwamba David alikuwa ameuawa, hakukuwa na siri tena, kwa Benjamin, tayari alikata tamaa, muda wote alionekana kuwa na huzuni tele kwani kwa namna moja au nyingine lazima mahakama ingemhukumu kifo au hata kufungwa kifungo cha maisha gerezani.
Alizungumza na mwanasheria wake, Donald na kumwambia wazi kwamba alikuwa na hofu moyoni mwake, kama ilivyokuwa kwa Benjamin, hata kwa Donald ilikuwa hivyohivyo kwani aliamini kwamba David aliuawa lakini napo ilikuwa ngumu kusema kwamba Bwana Seppy ndiye alikuwa amehusika kwani wangeulizwa kama wana ushahidi kitu ambacho kingewapa wakati mgumu.
“Kwa hiyo tufanye nini?” aliulizaDonald.
“Duh! Yaani siwezi kuamini kama David ameuawa, na FBI wanasemaje?” aliuliza Benjamin huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Wamejaribu kumtafuta...”
“Ikawaje?”
“Nao wakamkosa.”
“Hata mwili wake?”
“Nao wameukosa pia,” alijibu Donald.
Benjamin akaona huo ndiyo mwisho wake, alipoambiwa hivyo na Donald, hakutaka kuendelea kuzungumza naye, akaomba kuondoka kwani kichwa chake kilichanganyikiwa mno.
Siku hiyo haikuwa nzuri katika maisha yake, alipagawa kwa sababu mtu pekee ambaye alibaki, aliyekuwa tegemeo lake alikuwa David tu ambaye mpaka muda huo tetesi zilisema kwamba aliuawa kwani hakuwepo nyumbani na wala hakuonekana sehemu yoyote ile.
“Mungu nisaidie!” alisema Benjamin huku akiwa amepiga magoti, alionekana kukata tamaa kwa asilimia mia moja.
****
Siku hazikumsubiri mtu, ziliendelea kukatika, Moyo wa Benjamin ulikuwa kwenye maumivu makali mno hasa baada ya kugundua kwamba mshikaji wake aliyekuwa na ushahirdi wote, David alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Hakukaa kimya, aliwaambia wazazi wake juu ya hofu aliyokuwa nayo moyoni mwake, aliwaambia wazi kwamba kila siku alikuwa mtu wa mawazo na hakujua kama ingetokea siku yoyote ile angeweza kupata furaha aliyokuwa nayo kabla kama tu huyo David asingepatikana.
“I don’t know what I should do but the world must know that I killed nobody,” (Sijui ninachotakiwa kufanya lakini lazima dunia ijue sijamuua mtu yeyote yule) alisema Benjamin huku akiwa ameuinamisha uso wake.
“Everybody knows you killed nobody, but we have to look for the evidence to set you free,” (Kila mtu anajua hujamuua mtu yeyote yule lakini ni lazima tuutafute ushahidi) alisema baba yake.
“Nobody knows where David is by now, they killed him, why? When I come back, I’ve to tell the world about what happened although David disappeared” (Hakuna anayejua mahali David alipo kwa sasa, watakuwa wamemuua, kwa nini? Nitakaporudi, nitatakiwa kuiambia dunia kila kitu kilichotokea hata kama David amepotea) alisema Benjamin huku machozi yakianza kumtoka.
Hakukuwa na kilichobadilika, bado Benjamin alitakiwa kukaa jela mpaka pale ambapo angeitwa tena mahakamani. Ushahidi mwingine ukakusanywa na hivyo kilichokuwa kikitakiwa ni siku ya mahakama ifike na kila kitu kuwekwa wazi.
Siku ilipofika, tayari watu wengi walikwishakusanyika ndani ya mahakama hiyo. Hali ilikuwa tofauti na kipindi cha nyuma. Watu walibadilika, hawakutaka tena kuona Benjamin akifungwa bali Bwana Seppy ndiye alitakiwa kufungwa kutokana na kile alichokifanya.
Waandishi wa habari walikuwa ndani ya mahakama hiyo, walitaka kuandika kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Mwana huo wa 2011, hakukuwa na kesi iliyovuta hisia za watu wengi kama hiyo.
Kila mtu duniani alitegesha masikio yake kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea katika mahakama hiyo huko nchini Marekani. Jaji yuleyule, McRegan ndiye aliyetakiwa kusikiliza kesi hiyo na kutoa hukumu.
Mahakama ilijaza watu, hakukuwa na nafasi ya watu wengine na hata wale waliokuwa wamechelewa ambao walikuwa ni zaidi ya watu elfu kumi walitakiwa kubaki nje na kufuatilia kesi ile kupitia televisheni kubwa iliyowekwa tayari nje ya mahakama hiyo.
Haukupita muda mrefu, basi kubwa lililobeba watuhumiwa likaanza kuingia ndani ya eneo la mahakama hiyo. Waandishi wa habari ambao walikuwa nje wakalisogelea gari hilo na kuanza kulipiga picha.
Basi liliposimama, mahabusu kadhaa wakaanza kuteremka huku wakiwa na pingu mikononi mwao. Miongoni mwa mahabusu hao alikuwa Benjamin na Bwana Seppy ambaye muda wote uso wake ulikuwa na tabasamu pana.
Alichokuwa akifahamu, David alikuwa ameuawa kama alivyoambiwa na Dracula, alijua kwamba Benjamin hakuwa na ushahidi wowote ule ambao ungemuweka matatani.
Aliwapungia watu mikono, watu wengi walikuwa wakimzomea lakini hakuonekana kujali mpaka alipoingia ndani ya mahakama. Watu walitaka kuisikiliza kesi hiyo na hukumu kutolewa siku hiyohiyo, hakukuwa na mtu aliyefika mahali hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi nyingine yoyote ile.
Wakati Jaji McRegan anaingia ndani ya mahakama hiyo, watu wote wakasimama kama ishara ya heshima, jaji akatembea mpaka mbele ambapo akakaa katika kiti chake kisha kuwaruhusu watu kukaa kwa kupiga nyundo yake.
Muda wote Benjamin alikuwa amekiinamisha kichwa chake chini, alionekana kuwa na majonzi mazito na muda wote machozi yalikuwa yakimtoka tu. Wakili wake, Donald ndiye aliyekuwa akimsimamia siku hiyo, mbali na huyo, pia kulikuwa na wakili wa upande wa Bwana Seppy, wakili huyu aliitwa Tedd, mwanaume mrefu ambaye muda wote alivalia miwani.
Zilianza kusikiliza kesi nyingine ambazo zilichukua masaa mawili na ndipo Benjamin akatakiwa kupanda kizimbani. Watu walikuwa wakimwangalia tu, alionekana kuwa na maumivu makali moyoni mwake kiasi kwamba hata watu wengine wote wakaanza kumuonea huruma.
“Unaitwa nani?” aliuliza Donald.
“Naitwa Benjamin Saunders.”
“Unajua kwa nini upo hapa?”
“Ndiyo! Ni kwa sababu mahakama inanihusisha na mauaji yaliyotokea,” alijibu Benjamin.
“Mnamo tarehe ishirini mwezi wa sita mwaka jana, kulikuwa na mauaji yaliyotokea, mwanamuziki, Carter Phillip alikutwa amekufa katika chumba kimoja huko Southampton nchini Uingereza, polisi walifanya kazi yao na kugundua kwamba alama zako za vidole zilikutwa katika mwili wa marehemu, na si kwenye mwili tu bali hata katika sehemu nyingine chumbani humo, unalizungumziaje hilo?” alisema Donald na kuuliza swali.
“Kitu cha kwanza ambacho mahakama hii inatakiwa kufahamu ni kwamba sikuwahi kuua katika maisha yangu. Nilimfahamu Carter kama mwanamuziki chipukizi. Mnamo tarehe tano mwezi wa saba nilipokea simu ya kuhitajika sehemu fulani, huko nilipokwenda, nilikutana na Bwana Seppy ambaye alinipa kazi ya kufanya mauaji ya Carter Phillip. Sikujua sababu ila nilimkatalia kwa kuwa sikuwahi kuua,” alisema Benjamin.
“Unahisi kwa nini alikuchukua wewe?”
“Mimi ni mtaalamu wa kompyuta, aliamini kwamba kama ningeifanya kazi yake ingekuwa nyepesi na hata kugundulika ingekuwa ngumu. Kwa kweli nilikataa kabisa,” alisema.
Huo ulikuwa ni muda wa maswali kutoka kwa wakili wake, maswali yake yalikuwa ya kumpa nafasi ya kuelekezea kile kilichokuwa kimetokea, wakili Donald alichukua dakika kumi, alipomaliza maswali yake, akakaa chini na wakili wa Bwana Seppy kusimama.

Je, nini kitaendelea?

Tukutane Jumamosi.
sehemu ya kwanza au ya pili nadhani,ilielekeza kuwa,benjamini ni mwanafunzi wa masomo ya sayansi ya utabibu,yaani udaktari,hii ya leo inasema yeye ni mtaalamu wa kompyuta...marekebisho tafadhali
 

Madame S

JF-Expert Member
Mar 4, 2015
15,817
2,000
NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA

Sehemu ya Ishirini na Nane.

Maswali yake yalikuwa magumu lakini Benjamin alijitahidi kujibu kwa uelewa mkubwa, baada ya kuulizwa maswali hayo na kumaliza, hapo ndipo akakaa, watu wote wakata kuona Bwana Seppy naye akiulizwa maswali.
Hilo halikuwa tatizo, akasimama na kuelekea kizimbani. Mtu wa kwanza kabisa kumuuliza maswali alikuwa wakili wake, maswali aliyoulizwa yalikuwa mepesi na yale ya kumuweka katika wakati mzuri wa kushinda kesi, wakili huyo alipomaliza, akasimama na Donald kusimama.
“Unaitwa nani?” aliuliza Donald huku akimwangalia Bwana Seppy usoni mwake.
“Naitwa David Seppy...”
“Sawa. Una akili?” aliuliza Donald.
“Unasemaje?”
“Una akili?” alirudia swali lake.
“Ndiyo nina akili!”
“Unajua kwa nini upo hapa?”
“Ndiyo mheshimiwa! Nipo hapa kwa sababu nimesingiziwa kwamba nimeua,” alisema Bwana Seppy.
“Umesingiziwa au umeua kweli?”
“Nimesingiziwa kwa kuwa kama ningekuwa nimeua, basi hata alama za vidole vyangu zingeonekana,” alijitetea.
“Mshtakiwa ambaye ni Benjamin anasema kwamba wewe ndiye uliyehusika katika mauaji hayo na wewe ndiye uliyemuita na kumpa kazi hiyo ili akaue, ni kweli?” aliuliza Donald.
“Si kweli!”
“Unamjua Benjamin? Ushawahi kuonana naye kabla?” aliuliza Donald.
“Hapana! Sikuwahi kuonana naye kabla.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Tarehe kumi na mbili mwezi wa sita, simu yako ilitumika kutuma ujumbe mfupi kwenda namba +56 890 672 88 ambayo inamilikiwa na mtu anayejulikana kwa jina la Petterson Edward ambaye ulikuwa ukimuita kwa jina la Dracula, ujumbe huo uliuandika kwamba kulikuwa na mtu ambaye alitakiwa kuuawa mara moja, huyo si mwingine bali ni Carter, ni kweli?” aliuliza Donald.
“Si kweli!” alijibu Bwana Seppy baada ya kukaa kimya kwa muda.
“Mheshimiwa hakimu, naomba niwekewe televisheni na kompyuta kwa ajili ya kuletea ushahidi ulioshiba kabla ya shahidi wa mwisho kabisa ambaye ni David kuja na kuthibitisha yote yaliyotokea,” alisema Donald.
Bwana Seppy alipolisikia jina la David, akayapeleka macho yake kwa Dracula ambaye alikuwa ndani mahakama ile, alichanganyikiwa kwani taarifa ya mwisho ilisema kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa, je, ni David yupi ambaye alikuwa akizungumziwa mahali hapo.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka televisheni ikaletwa mahali hapo, laptop ikaunganishwa na simu simu aina ya iPhone aliyokuwa nayo Donald na kisha kuanza kuonyesha ushahidi wa kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“Kama nilivyosema, ushahidi umeonyesha kufanya mawasiliano hayo kama inavyoonekana, ujumbe huo ulitumwa kutoka namba hii, naomba kuuliza, je, hii namba ni yako au si yako?” aliuliza Donald huku akimuonyeshea namba Bwana Seppy katika televisheni.
“Ni yangu!”
“Kuna mtu aliwahi kuishika simu yako na kutuma ujumbe pasipo kujua?” aliuliza.
“Hapana!”
“Sawa. Mnamo tarehe kumi na tisa mwezi wa tisa, ujumbe wa mauaji ulitumwa kutoka katika simu yako kwenda katika namba ileile na ulisema kwamba ni lazima Todd Lewis auawe kwa sababu alikataa kuweka mkataba na wewe ambao ungemlipa kiasi kidogo cha fedha, hivyo kama kisasi ukaamua kumuua kwa kutuma watu, je, ni kweli?” aliuliza Donald, Bwana Seppy akabaki kimya, alianza kuweweseka huku akiangalia huku na kule.
“Uliidanganya dunia kwamba Benjamin ndiye aliyekuwa akifanya mauaji. Hiyo haikutosha, pia ulitumia njia hizohizo kuwaua watu wengine na kumfanya Benjamin kuingia matatani. Na kwa faida ya mahakama ni kwamba ulikuwa ukiweka noti kila sehemu uliyoua ili iwe vigumu kugundulika ila noti hizo zilikuwa na maana kubwa.
“Ile noti ya Dola, alama yake ambayo inawakilisha S, ile Euro ambayo inawakilisha fedha ya Ulaya, ile Paundi iliyowakilishwa na P, na mwisho ile Yuen iliyowakilishwa na Y, inaunganisha jina lako la SEPPY, je, bado unataka kubisha hapo?” aliuliza Donald huku akimwangalia mzee huyo usoni. Bwana Seppy akabaki kimya.
“Wiki kadhaa zilizopita, kulikuwa na mauaji ya msichana Stacie, mauaji hayo yalifanyika jijini Los Angeles mnamo majira ya saa nne usiku huku alama za vidole zikionyesha kwamba ni Benjamin ndiye aliyehusika, saa tano usiku kupitia kamera za CCTV zilizokuwa Boston zilimuona Benjamin na hivyo polisi kwenda kumkamata.
“Swali langu ni hili! Kama ni Benjamin ndiye aliyekuwa amefanya mauaji ya Stacie, je, alitumia usafiri gani kutoka Los Angeles mpaka Boston na wakati kutoka sehemu hizo kwenda nyingine hutumia muda wa saa tatu kwa usafiri wa treni na saa mbili na nusu kwa usafiri wa ndege? Wewe ndiye uliyefanya mauaji hayo, na bahati mbaya sana ulishindwa kujipanga kwa kutumia saa yako,” alisema Donald huku akiifunga faili lake.
Bwana Seppy alibaki kimya, alikuwa akitetemeka mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo, alimwangalia Donald huku akionekana kuchanganyikiwa.
Minong’ono ilianza kusikika hapo mahakamani, kesi ilionekana kuwa nyepesi mno kwa upande wa Benjamin. Wakati Donald akilifunga faili lake, hapohapo akamuomba mheshimiwa jaji kumruhusu kumleta shahidi wa mwisho, huyo shahidi wa mwisho akaruhusiwa kuingia hapo mahakamani, kitu kilichomshtua Bwana Seppy, ni David na msichana Vivian wakaingia.
“Aliuawa, nini kinaendelea?” alijiuliza Bwana Seppy, hapohapo akaona huo ndiyo mwisho wake.
“Mheshimiwa jaji, naomba tumpe nafasi shahidi, hii ni kesi nzito ambayo inahitaji ushahidi wa kutosha kwani kama shahidi hatotoa ushahidi wake hapa mahakamani sasa hivi, anaweza kuuawa kwani hata alipotajwa kwamba yeye ni shahidi, alitekwa,” alisema Donald na kumuomba hakimu, hapohapo David akapanda kizimbani na kuanza kutoa ushahidi wake.
“Mheshimiwa jaji, mara baada ya rafiki yangu Benjamin kupata tatizo, aliniomba nimsaidie ili kujua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia, ilikuwa kazi kubwa na nzito lakini kwa kutumia kompyuta yangu, niliweza kufanikiwa kunasa ushahidi wote ambao niliukabidhi kwa Donald.
“Kwa kifupi ni kwamba Bwana Seppy amehusika katika mauaji. Baada ya kujua kwamba mimi ndiye shahidi kwa kuwa data zote ninazo, akawatuma watu waje kuniteka, wakaniteka na kunipeleka katika jumba moja lipo sehemu fulani.
“Huko nikakutana na huyu msichana, Vivian ambaye ni mpenzi wa Benjamin, alinihadithia kilichotokea baada ya kutoroka. Tulipotoroka, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtafuta Donald ambaye akatupeleka katika jengo la FBI ambapo tulipewa hifadhi kwani bila kufanya hivyo, tungeuawa.
“Ila mbali na kufanya mauaji ya watu hao, nadhani pia anatakiwa kushtakiwa kwa kufanya mauaji ya maofisa wa FBI kwani wakati amewatuma vijana wake kumteka Benjamin, waliua maofisa wa FBI na kumteka Vivian,” alisema David.
David alizungumza mambo mengi yaliyokuwa yametokea, kila alipokuwa akizungumza, watu walikuwa kimya wakimwangalia tu, jaji McRegan alikuwa akiandika kila kitu kilichokuwa kikihitajika kuandikwa. Mpaka David ananyamaza, alikuwa ameridhika na ushahidi.
Jaji akabaki kimya, watu wote walikuwa wakimsikilizia yeye ni kitu gani angezungumza baada ya kupewa ushahidi uliojitosheleza. Hakutaka kutoa hukumu moja kwa moja, alichokifanya ni kuliita jopo la wazee wa baraza, wakaomba muda wa dakika ishirini kwa ajili ya kuijadili kesi hiyo.
Minong’ono haikuisha hapo mahakamani, kila mtu alikuwa akiongea lake huku wakimtaka jaji amuhukumu Bwana Seppy kifungo cha maisha gerezani au hata kumnyonga kutokana na kile alichokifanya.
Jopo hilo la wazee wa baraza na jaji lilichukua dakika kumi na tisa, likarudi mahakamani. Kabla ya kuzungumza kitu chochote kile, jaji akaanza kuwaangalia watu waliokusanyika ndani ya mahakama hiyo kisha kuyapeleka macho yake kwa Bwana Seppy.
Mwanaume aliyekuwa bilionea, aliyewatetemesha watu wengi kwa ajili ya ubilionea wake, leo hii alikuwa kizimbani huku akituhumiwa kuua watu kwa tamaa zake za fedha.
Mbali na yeye, pia kulikuwa na familia yake, muda wote mke wake alikuwa akilia, hakuwa akiamini kile kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo. Watoto wake waliokuwa na miaka kumi na tisa nao walikuwa pamoja nao, kitendo cha baba yao kufikishwa mahakamani tu kisa aliua kiwahuzunisha wote na hawakutegemea kama kitu kama kile kingetokea.
“Mahakama imejiridhisha kwa kila kitu kilichotokea, ushahidi umekamilika na kila kitu kilichozungumzwa. Hivyo kwa kupitia kifungu namba 113B kilichowekwa mwaka 1893, mahakama haikumkuta Benjamin na hatia hivyo inamuachia huru ila kwa mauaji aliyoyafanya David Seppy, amekutwa na hatia hivyo atahukumiwa kifo kwa kuchomwa sindano ya cyanide mpaka kifo.
“Hii itakuwa fundisho na pia kwa kupitia maofisa wa FBI, imebainika kwamba mmoja wa watu wake ambao walikuwa wakifanya mauaji ajulikanaye kwa jina la Petterson Edward ‘Dracula’ yupo hapa mahakamani akifuatilia kila kitu, hivyo naye atachukuliwa na kujumuishwa katika adhabu hii,” alisema jaji, hakutaka kuendelea sana, akapiga nyundo yake, akasimama na kutoka katika kiti kile.
Mahakama nzima ilikuwa shangwe, watu hawakuamini kama kweli kile walichokisikia ndicho kilichokuwa uamuzi wa mahakama ile. Benjamin hakutaka kusubiri, hapohapo akachomoka na kuwafuata wazazi wake na kuwakumbatia, kwake, ilikuwa furaha tele.
Kwa Bwana Seppy ilikuwa ni kilio kikubwa, hakuamini kile ambacho mahakama ilikiamua, akabaki akilia pale alipokuwa. Hata kabla watu hawajawanyika, tayari maofisa wa FBI walimfikia Dracula na hapohapo kumpiga pingu na kuondoka naye.
Siku iliyofuata, magazeti yote nchini Marekani yalitawaliwa na habari hiyo, kifo cha Bwana Seppy ambaye katika kipindi hicho ndiyo alitakiwa kuanza maandalizi ya kuiaga familia yake kabla ya kutekelezwa adhabu kali ya kifo ambayo ilikuwa mbele yake.
Alilia na kuhuzunika sana lakini hakuweza kubadilisha kitu chochote kile, hukumu ilikuwa palepale kwamba ni lazima afe kama hukumu ilivyosomwa mahakamani.
Benjamin akabadilika na kuwa shujaa, yule mtu aliyekuwa akitafutwa usiku na mchana, akawa mtu aliyekuwa akipendwa na kuzungumziwa kila kona, kila mtu alitamani kuwa karibu naye japo kupiga picha naye kwani hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa shujaa kama alivyokuwa yeye.
Alichokifanya ni kuendelea na masomo yake chuoni na baada ya miaka miwili, akakamilisha miaka yake mitano ya kusomea masuala ya kitabibu na hivyo kuwa daktari katika Hospitali ya St. Monica iliyokuwa Ohio nchini Marekani.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yake, hakumuacha mpenzi wake, Vivian, baada ya miaka miwili kukatika, akamuoa kwa harusi kubwa na iliyohudhuriwa na watu wengi maarufu.
Kilichoendelea baada ya hapo, kilikuwa ni historia tu.

MWISHO
 

iron2012

JF-Expert Member
Feb 16, 2012
481
250
Madam S ndiyo maana nakupenda sana Ahsante kwa kumaliza MAUAJI YALIYOJAA UTATA, kwa kweli wengine waige mfano wako ukianzisha riwaya/Hadithi/Simulizi ni mwanzo mwisho Ubarikiwe sana mama
 

Madame S

JF-Expert Member
Mar 4, 2015
15,817
2,000
Asante sana sana sana jaman nimefarijika mno na comment yako, tubarikiwe sote pia
Madam S ndiyo maana nakupenda sana Ahsante kwa kumaliza MAUAJI YALIYOJAA UTATA, kwa kweli wengine waige mfano wako ukianzisha riwaya/Hadithi/Simulizi ni mwanzo mwisho Ubarikiwe sana mama
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Similar Discussions

Top Bottom