Madame S huyu nyemo hajatukumbuka tu sisi wasomaji wake jamani
NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA
Sehemu ya Ishirini na Tano.
“Wewe ni muuaji,” alisema polisi mmoja aliyekuwa na koti lililoandikwa BPD yaani Boston Police Department.
“Hapana! Mimi si muuaji,” alisema Benjamin huku akimwangalia mwanaume huyo usoni, hakuwa peke yake, alikuwa na wanaume wengine, wote walikuwa polisi.
Walimkamata Benjamin kwa kuwa walihisi kwamba yeye ndiye aliyekuwa akifanya mauaji ya watu wote waliokuwa wameuawa vyumbani mwao, walikuwa na uhakika kwa sababu alama za vidole vyake zilikutwa katika miili ya maiti hizo na baadhi ya vitu ndani ya chumba hicho.
Benjamin alikuwa akilia huku akiendelea kujitetea kwamba hakuwa muuaji, hakuwahi kuua kama dunia ilivyokuwa ikijua bali kulikuwa na mtu nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kukamatwa kwake ilikuwa siri kubwa, hakupewa mwandishi wa habari yeyote yule, waliwaacha Wamarekani waendelee kuwalaumu lakini walitaka kufanya vitu vyao kwa mpangilio kwani kama taarifa zingetoka na kusema kwamba walimkamata Benjamin, wangeweza kuharibu kila kitu.
“Tunajua kwamba hujafanya mauaji Benjamin japokuwa alama za vidole vyako zimekutwa katika maiti zilizokuwa katika vyumba,” alisema polisi mmoja.
“Kweli sijafanya mauaji.”
“Sawa! Ila kama hukufanya, nani alifanya?” aliuliza mwanaume huyo.
Hapo ndipo Benjamin akaanza kusimulia kila kitu kilichotokea tangu siku ya kwanza alipopigiwa simu na Bwana Seppy na kuambiwa kazi kubwa ya kufanya mauaji iliyokuwa mbele yake, aliwaambia wazi kwamba alikataa hivyo kumteka yeye na mpenzi wake, wakamtisha lakini pamoja na hayo yote, alikataa kufanya mauaji hayo.
“Ikawaje?”
“Walinipa simu ya iPhone, nilipoishika, nafikiri ndipo walipata alama za vidole vyangu ambazo wamekuwa wakiziweka kila kona,” alisema Benjamin.
“Una chochote cha kushikilia dhidi ya Bwana Seppy?’ aliuliza polisi mmoja.
“Ndiyo! Nina rafiki yangu ambaye amekuwa akizifuatilia meseji na simu za mzee huyu kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kwa maana hiyo ushahidi upo wote,” alisema Benjamin.
Polisi wale hawakutaka kuzungumza kitu chochote, walitaka kufahamu kama kulikuwa na ushahidi kwani kumfikisha mahakamani mtu mzito kama Bwana Seppy haikuwa rahisi, ilikuwa ni lazima ujikamilishe kwa kila kitu.
Mara baada ya kukata walichokitaka, hapohapo polisi hao wakatoka ndani ya chumba kile. Benjamin akabaki kimya, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.
Hapo ndipo mawazo juu ya mpenzi wake, Vivian yalipomjia kichwani mwake, hakujua alikuwa wapi baada ya kutekwa, kabla ya kufanya kitu chochote ilikuwa ni lazima ajue mahali alipokuwa.
Wakati akiwa kwenye mawazo lukuki, hapohapo mlango ukafunguliwa na wanaume wawili waliokuwa na makoti yaliyosomeka FBI wakaingia na kukaa katika viti vilivyokuwa chumbani humo.
Mwanaume wa kwanza alijitambulisha kwa jina la Brett Phillip na mwingine Ryan Cashman. Watu hao walifika mahali hapo kwa kuwa walitaka kumuhoji maswali kadhaa juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
“Sikuwahi kuua, nililazimishwa kufanya hivyo ila nikakataa,” alisema Benjamin huku akiwaangalia wanaume hao usoni, tena kwa zamu.
“Kama hukuua, nani aliua?” aliuliza Brett.
Kama alivyowaambia polisi wale ndivyo alivyowaambia hata maofisa hao wa FBI kwamba hakuhusika katika mauaji hayo bali kulikuwa na mtu mwingine ambaye ni bilionea ndiye aliyehusika katika mauaji yote yaliyotokea.
“Bwana Seppy! Haiwezekani,” alisema Brett.
“Ndiyo hivyo! Ushahidi upo tayari, kama hamuamini, natumaini kuna siku mtaamini, hasa tutakapokwenda mahakamani,” alisema Benjamin.
****
Taarifa za ndani kabisa zilisema kwamba yule muuaji aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, Benjamin alikuwa amekamatwa jijini Boston na hivyo kushikiliwa na polisi.
Kila aliyezisikia taarifa zile, hakuamini masikio yake kama kweli muuaji huyo aliyekuwa akichukiwa kila kona alikuwa amekamatwa na polisi. Taarifa hizo zilisambaa kwa kasi kubwa kama moto wa kifuu, kwenye mitandao ya kijamii, taarifa hizo zilisambazwa kila kona kiasi kwamba watu wengine wakahisi kwamba hazikuwa na ukweli wowote ule.
Hapo ndipo watu walipoamua kutaka kumuona huyo Benjamin. Wengi wakahisi kwamba zilikuwa taarifa za uongo ambazo zilitengenezwa na polisi ili waweze kujisafisha kutokana na uchafu waliokuwa nao wa kushindwa kumtafuta Benjamin na kumkamata.
Polisi hawakutaka kuzungumzia lolote lile, walikuwa na msemaji ambaye yeye ndiye aliyehusika kutoa taarifa kwa wananchi, kwa kuwa taarifa hizo zilivuja, hawakutaka kuthibitisha juu ya hilo.
Baada ya taarifa hizo kusambaa kila kona, siku mbili baadaye ndipo polisi walipothibitisha kukamatwa kwa Benjamin na hivyo kuwaambia wananchi kwamba mua wowote ule kuanzia kipindi hicho angefikishwa mahakamani kusomewa mashitaka kwa kile alichokuwa amekifanya.
Hicho ndicho kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa, watu wakaandaa mabango yao na kuandika jumbe nzito kwamba mahakama isilete masihara katika kesi hiyo, ilikuwa ni lazima kumhukumu Benjamin kwa kosa la mauaji kwa kile alichokuwa amekifanya.
“Just hung him,” (Mnyonge) liliandikwa bango moja.
Watu hawakuishia kuandika mabango hayo tu bali siku iliyofuata wakaanza kuandamana kuitaka mahakama imuhukumu kifo Benjamin kwa kile kilichotokea.
Muda wote wakati hayo yakiendelea, Benjamin alikuwa sero, huko hakutakiwa kuzungumza na mtu yeyote yule, alitakiwa kukaa hivyohivyo mpaka pale kesi ingeanza kusikilizwa.
Mtu pekee aliyeruhisiwa kuingia na kuzungumza naye alikuwa mwanasheria wake ambaye alimhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea na kwamba hakuhusika katika mauaji hayo yaliyokuwa yametokea.
“Kwa hiyo unamaanisha Bwana Seppy ndiye aliyefanya mauaji?” aliuliza mwanasheria wake, Bwana Donald Gilphin.
“Ndiyo! Ushahidi upo wa mawasiliano yake aliyokuwa akiyafanya,” alisema Benjamin.
“Kama yapo, hakuna tatizo, hapo ndipo ninapopataka,” alisema mwanasheria.
Mitaani hakukukalika hata mara moja, kila kona, watu walikuwa wakiandama huku wakiishinikiza mahakama kumuhukumu kifo Benjamin kwa kile kilichokuwa kimetokea kwa kuua watu wengi ambao walitabiriwa kuwa mastaa wakubwa hapo baadaye.
Maandamano hayo yalikusanya watu wengi, si hapo Boston tu bali katika sehemu mbalimbali nchini Marekani watu walizidi kuandamana kila siku. Kama kuanza, walianza hapo Boston, wakaitikia Texas, New Orleans, New York, Washington na sehemu nyingine nyingi, kote huko walitaka kushuhudia Benjamin akihukumiwa kifo tu.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya siku kadhaa, Benjamin akachukuliwa na kufikishwa mahakamani. Siku hiyo ilikuwa ni hatari mitaani, watu walikuwa na mabango yaliyoitaka mahakama imuhukumu kifo Benjamin kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Moyo wake uliumia sana kwani alijua kwamba hakuua na wala hakuwahi kuua lakini hilo watu hawakulielewa, alitamani sana kuwaambia watu wote ukweli juu ya kilichokuwa kimetokea lakini hakupata muda huo, hasa siku ya kwanza kusikiliza kesi.
Siku hiyo, alisomewa mashitaka tu na kisha kesi yake kupangwa kusikilizwa baada ya wiki mbili, baada ya hapo alitakiwa kuwasubiri watu wengine na kisha safari ya kuelekea rumande kuanza. Pale alipokuwa, hakuwa na amani kabisa, watu walitaka kuona akihukumiwa kifo tu na si vinginevyo.
Waandishi wa habari hawakuwa nyuma, wakati yeye na watu wengine wakipelekwa katika basi kubwa la gereza, wakaanza kupiga picha kwani kwa kipindi hicho, Benjamin alikuwa biashara kubwa sana mitaani.
“I hate him...” (ninamchukia) alisikika mwanamke mmoja aliyekuwa mahakamani hapo.
“I hate him too, he is not supposed to live,” (hata mimi namchukia, hastahili kuishi) alisikika mwanamke mwingine.
Hicho ndicho kilichokuwa ndani ya mioyo ya Wamarekani, hawakumpenda kabisa Benjamin, walimchukia kwa kuwa waliamini kwamba yeye ndiye aliyehusika katika mauaji yote yaliyokuwa yametokea.
Moyo wake haukuacha kuuma, kila siku maumivu yalikuwa ni sehemu ya maisha yake. Kwa sababu kitu kilichokuwa kikisubiriwa ni kujitetea mahakamani kutokana na yale yaliyokuwa yametokea, hivyo wazazi wake na baadhi ya ndugu zake wakaruhusiwa kuzungumza naye tena huku akiwa chini ya ulinzi mkali.
“Ni kweli uliua mwanangu?’ aliuliza baba yake.
“Hapana baba! Sijaua, niliambiwa niue lakini nikakataa.”
“Nani alikwambia?”
“Bwana Seppy! Sijajua kwa nini alitaka kuua kipindi hicho ila yeye ndiye aliyehusika katika mauaji yote na kuacha alama za vidole vyangu,” alijitetea Benjamin.
“Ilikuwaje hapo?”
Hapo ndipo Benjamin alipoanza kuhadithia kila kitu, hakutaka kuficha kitu chochote kile kwani aliamini kupitia wazazi wake na baadhi ya ndugu waliokuwepo hapo alipokuwa wangeweza kuibadilisha mioyo ya watu wote duniani ambao walikuwa wakiamini kwamba aliua kumbe hakufanya hivyo.
“Nitasimama kidete mpaka kijana wenu ashinde, hii kesi haina nguvu tena,” alisema mwanasheria wake ambaye naye alisimama kama wakili wake, Donald.
Siku ziliendelea kukatika mpaka ilipofika siku ya kupandishwa tena mahakamani. Kama kawaida watu wengi walikusanyika mahakamani hapo, walitaka kushuhudia kile ambacho kingeendelea na Benjamin angejitetea vipi juu ya yale mauaji aliyokuwa ameyafanya.
Wakati akiingia mahakamani, watu walianza kuzomea, hawakutaka kabisa kumuona katika uso wa dunia, walitaka kuona akihukumiwa kifo kwani hata kama angefungwa kifungo cha maisha gerezani bado watu wasingeridhika kabisa kutokana na mauaji aliyokuwa ameyafanya.
Maofisa wa FBI walikuwepo mahakamani hapo, walikuwa wakifuatilia kila kitu, waliufahamu ukweli uliokuwa umejificha, walimwangalia Benjamin, walimuonea huruma kwani hakuwa ameua kama dunia ilivyokuwa ikiamini.
Baada ya dakika kadhaa, hakimu ambaye alitakiwa kusikiliza kesi hiyo akaanza kuingia ndani ya mahakama hiyo, watu wote waliokuwa humo ndani wakasimama kama kumpa heshima, walipomwangalia, wakagundua kwamba alikuwa McRegan, miongonimwa mahakimu waliokuwa na rekodi kubwa ya kuwahukumu watu vifo.
Kidogo mioyo yao ikaridhika, kitendo cha kumuona McRegan akiingia mioyo yao ilikuwa na furaha tele kwa kuona kwamba hatimaye kilio chao kilisikika na mambo yangekwenda vizuri kabisa kama walivyotaka iwe mioyoni mwao.
Baada ya hakimu kukaa, watu wote hapo mahakamani wakakaa na kuanza kusikiliza. Kesi kwanza ikaanza kusikilizwa kwa muda kisha kupewa nafasi upande wa mshtaki ambaye ni Jamhuri ya Marekani, wakili wake, Bwana Peters akasimama na kuanza kumuuliza maswali Benjamin.
“Bila shaka unaitwa Benjamin Saunders,” alisema Peters.
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Unajua kwa nini upo hapa?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Upo hapa kwa kosa la mauaji, ni kweli?”
“Ni kweli mheshimiwa.”
“Ni kweli uliua?”
“Hapana!”
“Sasa kama hukuua, kwa nini upo hapa?”
“Kwa sababu nimesingiziwa kuua.”
“Ila alama za vidole vyako vilikutwa katika kila mwili wa marehemu, unalizungumziaje hilo? Tuna majibu ya vipimo vyote, picha zako zilibandikwa kila kona, kila mtu anajua kwamba wewe ni muuaji, unakataa pia?’ aliuliza Peters.
“Ndiyo mheshimiwa. Ninakataa kwa sababu sikuua!”
“Kama kweli hukuua, kwa nini ulikuwa uunajificha baada ya kugundua kwamba unatafutwa?” aliuliza Peters.
“Nilikuwa najificha si kwa sababu niliua, ila nilikuwa najificha kwa sababu nilitakiwa kuuawa muda wowote ule,” alisema Benjamin.
“Ulitakiwa kuuawa! Na nani?”
“Bwana Seppy, huyu bilionea,” alijibu Benjamin, minong’ono ikaanza kusikika humo mahakamani.
“Kwa nini alitaka kukuua?”
“Kwa sababu nilikataa kuua.”
“Kumuua nani?”
“Wote nilioambiwa kwamba nimeua.”
“Kivipi?”
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake, hakutaka kuchelewa, akaanza kuhadithia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, alianzia tangu siku ya kwanza kabisa alipopigiwa siku wakati alipokuwa jijini Washington, kipindi ambacho yeye na Wamarekani wengine walitaka kumsikiliza rais katika hotuba ambayo alitakiwa kuitoa katika siku hiyo ya uhuru wa Marekani.
Hakuishia hapo, alizungumzia namna alivyopigiwa simu na mtu asiyemfahamu ambaye alimtaka kuonana naye sehemu fulani, alitii kwani kama asingefanya hivyo mpenzi wake angeuawa.
Ilikuwa ni simulizi iliyochukua zaidi ya dakika ishirini, mahakama ilikuwa kimya ikimsikiliza. Alisimulia huku akionekana kuumizwa sana na muda wote alikuwa akilia tu.
Aliiambia mahakama kwamba hakuua bali Bwana Seppy ndiye aliyeua na hata alama za vidole vyake zilitengenezwa baada ya kupewa simu ya iPhone kwa ajili ya mawasiliano, kitendo cha kuishika simu ile tu, akawa ameacha alama za vidole vyake.
“Mheshimiwa hakimu, kwa mamlaka ya mahakama, naomba Bwana Seppy akamatwe na kufikishwa mahakamani kwani tumegundua kwamba mteja wetu hana hatia,” aliingilia wakili wake, Bwana Donald japokuwa haikuwa ikiruhusiwa.
Hakimu hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutoa amri Bwana Seppy afikishwe mahakamani kwani kwenye kesi ile na yeye alitajwa kama mhusika katika mauaji yale. Mahakama ikawa kimya, mpaka katika kipindi ambacho Benjamin alikuwa akishuka kizimbani, watu walibaki wakimwangalia kwa huruma kubwa.
Kila kitu kikabadilika, chuki walizokuwa nazo watu dhidi yake zikaanza kupotea mioyoni mwao baada ya kugundua kwamba hakuwa muuaji bali aliambiwa aue lakini akakataa na hivyo ujanja kufanyika kwa ajili ya kumuingiza matatani.
“Hii kesi utashinda. Ila ushahidi unao?” aliuliza Bwana Donald.
“Upo! Ni lazima tumtafute David, ana ushahidi wote, kama hatutompata, tutashindwa,” alisema Benjamin.
“Basi sawa. Nitawasiliana na polisi ili waweze kuwasiliana naye, baada ya wiki mbili, ushahidi uwe tayari,” alisema Donald.
“Nitashukuru.
****
Bwana Seppy alikuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Dracula aliyekuwa mahakamani kazi yake kubwa ilikuwa ni kumtumia ujumbe mfupi juu ya kila kitu kilichokuwa kikijiri huko.
Moyo wake ulikuwa na hofu kubwa baada ya Benjamin kupinga kufanya mauaji hayo na mwisho wa siku kulitaja jina lake. Aliiona dunia ikiwa imemuangukia, kila mtu mbele yake alikuwa akimzomea na mbaya zaidi aliiona milango ya gerezani ikifunga na yeye kuchukuliwa na kuingizwa humo.
Alisikitika mno, alijuta na wakati mwingine alikuwa akijiulaumu juu ya sababu iliyomfanya kufanya mauaji yale na wakati alikuwa na uwezo wa kukaa kimya na maisha kuendelea kama kawaida.
Siku hiyohiyo akafuatwa na maofisa wa FBI ambao walimtaka kuondoka naye kutoka hapo New York alipokuwa akiishi na kuelekea jijini Boston. Alijifanya kutokujua kitu chochote kile, wakamwambia kwamba angepewa taarifa juu ya kilichokuwa kikiendelea mara baada ya kufika katika kituo cha polisi.
Kipindi hicho polisi hawakuhusika, walijua kwamba mtu huyo alikuwa na jina kubwa hivyo ingekuwa rahisi kwake kutengeneza watu wake katika vituo mbalimbali vya polisi na ndiyo maana hata kwenye kumkamata, walikwenda maofisa wa FBI na si polisi kama ilivyotakiwa iwe.
“Benjamin amekutaja kwamba umehusika katika mauaji, ni kweli?” aliuliza ofisa wa FBI huku wakiwa wamemuweka ndani ya chumba kilichokuwa na kioo katika upande mmoja wa ukuta, hakujibu kitu, akabaki kimya.
“Kuna ukweli?” ofisa huyo akauliza tena swali.
“Siwezi kuzungumza kitu chochote kile, namtaka mwanasheria wangu awe hapa,” alisema Bwana Seppy.
Hilo halikuwa tatizo, walichokifanya ni kumpa simu yake na kumwambia awasiliane na mwanasheria wake ambaye ndani ya dakika ishirini, alikuwa katika kituo hicho.
Alitajwa na mtuhumiwa wa mauaji kwamba yeye ndiye aliyehusika katika mauaji hayo, hivyo alitakiwa kujipanga kwani naye angepanda mahakamani na kujibu kesi iliyokuwa ikimkabili.
“Unaona kama tunaweza kushinda kesi hii?” aliuliza Bwana Seppy, yeye mwenyewe alikuwa na hofu.
“Kesi tunaweza kushinda kama huo ushahidi hautoweza kupatikana mahakamani,” alijibu mwanasheria wake ambaye angemfanya kuwa wakili wake hapo baadaye.
“Kwa hiyo huo ushahidi inabidi upotee?”
“Ndiyo hivyo!”
Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu Benjamin alisema kwamba kulikuwa na ushahidi, Dracula na wenzake wakaanza kufuatilia na mwisho wa siku kujua kwamba kulikuwa na mtu ambaye alifahamu kila kitu na ndiye ambaye alikuwa na ushahidi, huyu alikuwa David Belshaaz, mmoja wa marafiki wa Benjamin aliyekuwa akiishi hapo Boston na alikuwa akisomea masomo ya kompyuta katika Chuo cha Harvard.
“Inabidi mmuue haraka iwezekanavyo,” alisema Bwana Seppy.
“Hakuna tatizo.”
Alichokifanya Dracula ni kuwatuma vijana wake waelekee katika Chuo Kikuu cha Harvard kwa ajili ya kumtafuta huyo David. Vijana hao hawakutaka kupoteza muda, harakaharaka wakaondoka kuelekea huko chuo ambapo baada ya kuulizia, wakaambiwa kwamba kijana huyo alikuwa akiishi West Mania, mtaa uliokuwa na wahuni wengi hapo Boston.
Je, nini kitaendelea?