Usipotoshe, jisomee halafu tuonesha hayo usemayo yako wapi?, hotuba mbona ipo karibu:
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani 127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Miaka minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO walishauri Shirika hilo lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi 50,000 badala ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1.
Wakati wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika kulipa madai hayo. Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja. Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji. Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme (energy charges) TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili husika hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji ulisimama katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi 8,020,522,330.37; Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000 na Dola za Marekani 22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi bilioni 202.9.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8. Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa riba ya asilimia mbili ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6.
Ni matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na sahihi kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.