Tusilainishwe na tabasamu (2)
MIONGONI mwa wasomaji wa Maswali Magumu waliowasiliana nami wiki hii, yupo mmoja ambaye aliniunga mkono, lakini pia akadokeza:
"Kutoa kashfa binafsi kwa (Jakaya) Kikwete kwa makosa yanayofanywa na mawaziri au maofisa si sawa; ni utovu wa nidhamu na kwenda kinyume cha maandiko uliyonukuu.
Inafahamika anayelikandamiza gazeti la MwanaHALISI na (Saed) Kubenea ni Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni. Kwa nini kashfa zako umpakazie rais?"
Naamini wapo wengine kadhaa wanaofikiri kama Mtanzania mwenzetu huyu. Wana sababu zao. Na wamegawanyika katika makundi kadhaa, lakini makubwa yaliyo dhahiri ni haya matatu.
Kundi la kwanza ni la watu ambao hawataki kabisa kuona wala kusikia rais akihusishwa na uzembe, kashfa, kushindwa, udhaifu au ufisadi wowote katika utendaji wa serikali anayoiongoza. Hawa bado wana imani kwamba rais ni mtu wa pekee na ana uwezo mkubwa na wa pekee, bali wasaidizi wake ndio wana uwezo mdogo. Hivyo, wasaidizi hao ndio wanaoharibu. Na wakiharibu wao, walaumiwe wao; si rais.
Watu wenye fikra hizi ndio wamekuwa wanadai (tuliiona hata kwenye utafiti wa REDET) kwamba umaarufu wa serikali umeshuka kuliko wa rais.
Wanathubutu kumtenga rais na serikali anayoiongoza! Wanajaribu kumtenga na mawaziri wake! Inawezekana? Rais anaongoza serikali ipi, na mawaziri wanaongoza serikali ipi? Kama si kupitia kwa mawaziri na wateule wake wengine, rais anaongozaje nchi?
Kundi la pili ni la wale ambao hawajui kabisa kwamba makosa ya mawaziri na watendaji wengine wa serikali yanamrudia rais.
Hivyo, hawamuoni rais katika wizara za nchi hii na idara zake. Hawamuoni mikoani na wilayani katika matamko na utendaji wa wakuu wa mikoa na wilaya. Nasisitiza: hawajui; si kwamba hawataki. Hawa tutawaelimisha taratibu.
Kundi la tatu ni la wale wanaojua vema uhusiano kati ya rais na wasaidizi wake, lakini bado wamekumbwa na kasumba na ulimbukeni wa kizamani juu ya utukufu na "ufalme" wa rais. Wanaiona taasisi ya urais kama taasisi nyeti isiyopaswa kuguswa – iheshimiwe tu, isiwajibishwe hata inaposhindwa kuonyesha unyeti wake.
Hawa wapo tayari kuswagwa au kuandamana kama kondoo nyuma ya kiongozi ambaye hawajui anaelekea wapi! Utii na ufuasi huu wa kikondoo ndio wanaouita heshima na nidhamu wanayotarajia kila mwananchi awe nayo. Ndiyo maana wanaona kuwa kumhusisha rais na makosa ya mawaziri wake ni kashfa binafsi na utovu wa nidhamu!
Ni bahati mbaya, lakini tunao watu wenye fikra za namna hizi. Tutawakomboaje? Labda tuwahoji kidogo; harakati zao za kupata majibu ya maswali tutakayowapa zinaweza kusaidia kufungua milango yao ya uelewa na ufahamu.
Tutumie mfano wa mwili wa binadamu. Tuseme rais ni kichwa. Mawaziri, wakuu wa mikoa, wakurugenzi mbalimbali kutoka Ikulu hadi idara za wizara, wakuu wa wilaya, wakuu wa vyombo vya usalama, majeshi yote, mabalozi wote nje ya nchi, na wateule wote wa rais tuwafananishe na macho, masikio, midomo, pua, mikono, miguu, na viungo mbalimbali vya mwili.
Kama mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, na wateule wengine wote wa rais ni mikono na miguu yake, tunaweza kujidai tuna akili timamu kwa kuthubutu kuwatenga na rais?
Maana wao ndio mikono anayoitumia kushika; ndiyo miguu anayotembelea; ndiyo macho anayotumia kuona; ndizo pua anazonusia; ndiyo masikio anayotumia kupata habari; na ndiyo midomo yake.
Watu hawa, na vyombo vingine vya dola vinavyomzunguka rais, ndiyo nguvu halisi ya urais wake. Hawa ndio wanaomletea taarifa, ndio wanaomshauri; na baada ya kutafakari taarifa anazopewa nao, anawatuma wale wale na wengine ili kutekeleza makubaliano au hitimisho la ushauri aliopewa. Au anawapuuza.
Ndiyo maana majeshi yamekula kiapo kumtii rais. Mawaziri na wateule wengine wameapa kumtii. Wakuu wa mikoa na wilaya wanaitwa wawakilishi wa rais katika maeneo yao ya utawala. Ndiyo maana kuna Ikulu Ndogo katika maeneo yao ya kazi.
Viapo, utii na mnyororo huu wa kimadaraka kutoka Ikulu hadi vijijini, ndivyo vinamfanya rais awajibike kwa matendo ya wateule wake.
Na kwa sababu ndiye anayewateua kwa mamlaka aliyonayo, na ndiye anayeweza kuwaondoa wasipofanya kazi vizuri, taifa litamwandama yeye anapoendelea kuvumilia makosa yao.
Uchumi ukitetereka, usalama wa nchi ukiwa hatarini, nchi ikikumbwa na njaa, maradhi yakiongezeka na kuhatarisha maisha ya wananchi, elimu ikishuka, walimu na wanafunzi wakinyanyaswa kwa kulalamikia sera au masilahi duni, bei za bidhaa zikipanda hovyo hovyo na kudunisha maisha, miundombinu ikiharibika na kukosa matengenezo, uhusiano wetu na mataifa ya nje ukiharibika, mfumo wa kisheria na kikatiba ukiwa kandamizi, rasilimali za taifa zikiporwa na wageni au wenyeji, zikitungwa sheria mbovu au kandamizi na kama mbaya zilizopo hazifutwi wala kufanyiwa marekebisho, wananchi wakikandamizwa na kunyanyaswa wanapojaribu kuwasiliana, kugoma au kuandamana; anayelaumiwa ni rais.
Sababu kuu ni moja. Ndiye mwenye mamlaka ya juu yanayoendesha taasisi zote kubwa na nyeti; na ndiye anayewateua wasimamizi wa taasisi hizo, washauri wake na waendeshaji wa idara nyeti za serikali.
Ndiye anayepaswa kujenga visheni ya kitaifa, na kwa kushirikiana na wataalamu washauri katika nyanja mbalimbali, kuweka mwelekeo wa kitaifa na kuwatumia watu wenye ujuzi kusimamia na kutekeleza visheni hiyo.
Kama alivyo na mamlaka makubwa ya kuwateua watu hao, ndivyo alivyo na mamlaka makubwa ya kuwaondoa pale wanapodhihirika kushindwa kazi aliyowapa. Wakishindwa akawaondoa, tunaona rais anafanya kazi yake vizuri. Wakishindwa akawavumilia na kufurahia kushindwa kwao, tunaona rais ameshindwa kazi, na anashirikiana na walioshindwa kazi kuhujumu maendeleo ya nchi.
Kama rais asingekuwa na uwezo huu ndani ya utendaji wa wateule wake, basi hata heshima anayopewa isingepaswa kuwapo. Na kama yeye hawajibiki kwa matendo ya wasaidizi na wateule wake – yaani kama wao wana mamlaka yanayoishia kwao, na wanawajibika kwa nafsi zao bila kumhusisha yeye, basi hatuna sababu ya kuwa na rais. Hana umuhimu!
Lakini katiba yetu imemfanya rais kuwa mtu muhimu sana, mwenye mamlaka makubwa sana, kiasi kwamba ingawa maandishi yanasema hakuna mtu aliye juu ya sheria, rais anaishi na kutenda kama mtu aliye nje ya sheria.
Na hii ni sehemu mojawapo ya udhaifu wa katiba yetu ambayo inampa rais mamlaka makubwa mno, kiasi kwamba anafika mahali pa kupuuza na kuviendesha hata vyombo vinavyopaswa kumsimamia na kumwajibisha.
Tazama wabunge wetu wanavyonywea linapofika suala la kujadili makosa kadhaa ya rais! Hivi tujiulize. Kama wabunge wetu wangekuwa hawamwogopi rais, Bunge lingekuwa na msuli wa kuwazuia kujadili hotuba yake aliyoitoa bungeni mwezi Agosti mwaka huu, hotuba iliyoonekana kupwaya na ikabezwa na wengi, wa kwanza akiwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta?
Kwamba hatimaye iliondolewa kabisa katika mjadala wa Bunge, ni dhahiri kwamba mamlaka ya rais yalitumika kudhibiti wabunge wasifukue na kuanika udhaifu wa rais katika hotuba hiyo. Ni udhaifu ulioandaliwa na wasaidizi wake walioandaa hotuba hiyo, lakini pia ni udhaifu wa serikali yenyewe maana hawakuwa na la maana kuliko hilo la kuwaeleza wananchi.
Ndiyo maana licha ya udhaifu wa hotuba hiyo, wale walioiandaa bado wapo Ikulu wanaandaa hotuba nyingine. Rais hana wasiwasi. Ni kazi bure kuwakemea wale kama bosi wao anaona wanafanya kazi nzuri.
Au tujadili kidogo hili la waziri wa habari na MwanaHALISI. Wizara yake ni sehemu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne. Sheria aliyotumia kulifungia gazeti hilo ni sheria halali lakini dhalimu na katili inayotumiwa na Serikali ya Awamu ya Nne.
Na kabla ya waziri kutoa tamko lake, Ikulu ilishatoa mwelekeo kwa kumtumia Mkurugenzi wa Mawasiliano, Salva Rweyemamu, ambaye alikemea habari liyoandikwa na MwanaHALISI.
Na kuna mambo mawili ya kukumbuka juu ya Salva Rweyemamu. Kwanza, amekuwa Rais wa MISA (Taasisi ya Vyombo vya Habari katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, pia katika tawi la Tanzania).
Bado tunakumbuka matamko mazito aliyotoa akiwa rais wa MISA dhidi ya serikali (ya Mkapa) kwa kufungia vyombo vya habari. Ni mwandishi mwandamizi ambaye baadhi yetu tumepata bahati ya kufanya kazi kwa karibu naye, pamoja naye na chini yake.
Tunajua uwezo wake na uelewa wake wa masuala mbalimbali, lakini hasa ya habari na mawasiliano. Si huyu aliyepaswa kutoa tamko (kwa niaba ya Ikulu) ili kulikandamiza gazeti la MwanaHALISI.
Pili, kwa cheo alichonacho sasa, yeye ni mshauri wa rais katika masuala ya habari na mawasiliano. Maana yake ushauri wake ndio unaweka mwelekeo wa uamuzi na utendaji wa serikali katika suala husika. Na kwa kuwa alishatoa kauli kukemea kilichofanywa na MwanaHALISI, ni wazi kuwa alitumwa kutoa kauli hiyo (kama sehemu ya majukumu yake), na kwamba ofisi inayomtuma ni ile iliyomteua. Kwa hiyo, tamko lolote analotoa Salva ni la rais. Salva alikuwa anaisemea Ikulu.
Kwa hiyo, kama Ikulu imeshatoa kauli, halafu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ikahitimisha kwa kuchukua hatua, tunadhani tuko sahihi kusema mbaya wa MwanaHALISI ni waziri, si rais? Au bado tupo pale pale tulipoanzia wiki iliyopita tunalainishwa na tabasamu?
Na kama Salva huyu tunayemjua kwa miaka mingi amegeuka na kuwa msemaji wa rais katika mambo aliyokuwa akiyapinga kwa nguvu zote, basi kuna mawili.
Kwanza, tutasema kwamba hakuwa mkweli tangu awali; yaani hakutetea jambo aliloliamini kwa moyo wake na akili zake zote. Maana haiingii akilini kwamba sheria hizi na matendo haya yalikuwa dhalimu wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, lakini sasa tunayaona kuwa halali na ya kawaida katika utawala wa Rais Kikwete. Vinginevyo, tukubaliane kwamba tumelainishwa na tabasamu.
Pili, wadhifa wake wa sasa unampa fursa ya kuathiri mambo mengi ndani ya serikali katika sekta ya habari na mawasiliano. Ni fursa ya Salva kutekeleza kwa vitendo, tena kwa kasi na ari mpya, harakati alizokuwa anaziendesha kwa makongamano na matamko makali akiwa rais wa MISA au mkurugenzi wa Habari Corporation.
Kama hadi sasa ameshindwa kubadili mwelekeo wa serikali katika masuala nyeti kama hayo, huku akiwa mshauri wa kiongozi mkuu wa nchi ambaye ‘akipiga chafya mawaziri wanaugua mafua,' basi huu ni ushahidi mwingine kwamba nguvu ya bosi wake ni kubwa mno na hashauriki wala habadiliki kwa yale asiyotaka.
Ndiyo maana Salva na waziri wa habari wamejikuta wakiimba wimbo ule ule dhidi ya MwanaHALISI – wimbo wa serikali, wimbo wa bosi wao.
Ni hatari kama wapo wananchi wanaodhani kwamba rais ni mtu siyepaswa kuhusishwa na uamuzi na vitendo kama hivi.
Kama asingehusika, angewakemea Salva na Mkuchika; angebatilisha uamuzi wa wizara kulifungia gazeti; angewachukulia hatua kali wahusika; na kwa mamlaka aliyonayo, tayari angekuwa ameelekeza mabadiliko ya haraka yafanyike kufuta sheria dhalimu na kandamizi. Ni kwa nini tunalainika hovyo hovyo na kushindwa kufikiri kwa kina?
Itaendelea Jumapili ijayo.