Mapinduzi ya Zanzibar - Januari 12, 1964

Mshume Kiyate

JF-Expert Member
Feb 27, 2011
6,771
1,195
Wana JF.

Usiku wa tarehe 12 Januari 1964 kundi la watu 300 walikitwaa kisiwa cha Unguja wakiongozwa na mtu asiyekuwa maarufu kipindi hicho, aliyekuwa akiitwa John Okello, John Okello alikuwa akiishi Pemba ambako alitokea Uganda miaka michache tu.

Ndani ya Zanzibar Okello alipata umaarufu kwa vijana majabari, ambao wengi katika wao walikuwa ni makuli na wachukuzi w meli zilizoingia na kutoka bandarini Zanzibar, kundi lake hili John Okello lilikutana kwa siri. Okello aliwapa matumaini ya mabadiliko watu wake hawa, wafuasi, ambao wakifanya kazi pamoja kwa muda mrefu, mara nyingine katika mazingira ya hatari, na tayari kufuata amri za kiongozi yeyote ambaye ataweza kuwalipa. Wao walikuwa waasi wanaotafuta makaazi.Mchafuko wa kisiasa ulikuwa ukiongezeka ndani ya Zanzibar na Pemba tangu kifo cha Sultani Khalifa katika mwaka 1960. Sultani Khalifa alitawala Zanzibar kwa karibu ya miaka 50, tangu mwaka 1911. Baada ya udanganyifu mkubwa kwa majimbo ya uchaguzi na mseto katika chaguzi kuu mbili za mwaka 1961 vyama vikuu vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja.

Waingereza waliondosha majeshi yao kikiwemo kikosi maalumu cha Kiarishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa mji mkongwe mapema mwaka 1963. Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar tarehe 12 Disemba 1963, aliadhimisha uondokaji wa Gavana wa kiingereza Zanzibar na mwisho wa ukoloni Zanzibar.
Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiipa ushindi mdogo wa kura Muungano wa vyama viwili ZNP na (chama cha kizalendo Zanzibar) na ZPPP (Chama cha watu wa Pemba na Unguja).

A.S.P (Chama cha Afro shirazi) kilikuwa kiwe kipo katika Serikali iliyo na chini ya nusu ya wabunge kwa mtindo wa bunge la Kiingereza na Sultani, akiwa kama ni mtawala tu lakini sio mtawala mwenye maamuzi ya mwisho. Taifa hili la Zanzibar ambalo lilikuwa mwanchana kamili wa Jumuia ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.Majadiliano makali ya kisiasa na maandamano yalikuwa ni matukio ya kawaida siku hizo.

Nakumbuka nilikuwa naendesha baskeli kuelekea shuleni kupitia makundi ya watu yaliyokuwa yakiimba na kusifu majina mbalimbali ya viongozi wa kisiasa, huku yakivuka vizuizi vya barabara vilivyokuwa vikilindwa na askari wa kiingereza.

Vikundi mbalimbali vilijadiliana juu ya mambo mbali mbali; mfano Haki dhini ya fursa, Wageni dhidi ya wenyeji wa zamani, Ubepari dhidi ya Ujamaa, Wafanyabiashara dhidi ya wamiliki ardhi, Waunguja dhidi ya Wapemba, Waasia dhidi ya pazia la nyuma la vita baridi na harakati za utaifa na kuondosha ukoloni ambazo zilikuwepo kipindi hiki ndani ya Afrika.John Okello hakuwa na jawabu ya mambo haya nyeti, lakini alikuwa na kipawa cha kutambua kwamba vikundi hivi vinavyoshindana vinatoa nafasi nzuri kwa mtu wa harakati kama yeye Okello.

Hata hivyo, watu kama mia waliojizatiti wangaliwez kutwaa vituo muhimu vya kienyeji vya habari na kambi za Polisi. Mara tu baada ya vituo vya habari na Kambi za polisi pamoja na silaha kudhibitiwa na John Okelo, Ni nani katika visiwa angeweza kumshinda? Jee, wanasiasa wangeliungana na kumshutumu na kumpinga kwa vitendo vyake visivyo halali? Au kama alivyotaraji, wangeendelea kutoaminiana na kutuhumu kwamba kati yao ndio wanaomuunga mkono? Jee, wasingelitaka kukubaliana na yeye, haraka kabla mwengineo hajafanya hivyo? John Okello alichezesha dadu usiku huo wa mwezi wa Januari.

Viongozi wa A.S.P walifadhaishwa na matendo ya Okello (wengi wao, walikuwa hata hawapo visiwani wakati huo). Walikimbilia haraka kuwaunga mkono waasi. Mamia ya wafuasi wa vyama walipigwa na butwaa juu ya wale ambao walikuwa na shuku ya kukata fundo hilo gumu la majadaliano ya kidemokrasia na kukimbilia moja kwa moja kwenye utawala. Hawawalitafuta njia ya kuiandaa jamii kwenda sambamba na kanuni zao. Kanuni siku hizo zilikuwa ni ghali sana kama sarafu ya Marekani. Ubinadamu ulikuwa ni kitu adimu sana.Baadhi ya viongozi wa ASP baada kuona kwamba serikali itakuwa haina udhibiti na uwezo kujilinda na kutokuwa na imani matokeo ya chaguzi huria zilizofanyika, viongozi hawalitafuta njia za haraka za kuhalalisha udhibiti yale ambayo yaliitwa sasa "Mapinduzi". Makundi ya watu wenye fujo yalikuwa huru. Sheria na amani zilikuwa hazipo katika mitaa ya Zanzibar.
Walimiliki ardhi na wafanya biashara waliburutwa kutoka majumbani na madukani mwao, uporaji na mauaji yalienea mji mkongwe mzima. Kwa kweli mji wenyewe uliporwa.

Waarabu na Waasia, waliokuwa wakiunga mkono vyama vyengine waliuliwa kwa makundi. Kwa usiku mmoja maisha ya watu yasiyovika yalipotea na siku nyengine baadae maelfu ya watu waliikimbia nchi pamoja na kila walichoweza kubeba.John Okello mwenyewe alijipachika cheo cha “Jemedari Mkuu“ akishirikiana na bataliani zake zenye fujo walianzisha utawala wa vitisho ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba. John Okello alitangaza vitisho visivyo vya kawaida na ahadi ya kifo kwa wote watakaojaribu kumpinga yeye.

John Okello aliamini alikuwa akipokea maelekezo /dokezo kutoka kwa Mungu na akionyesha uwezo usiokuwa wa kawaida kwa kutumia nambari, kwa mfano tarehe 13 Januari, 1964, alitangaza ujumbe ufuatao:

"Serikali sasa inaendeshwa na sisi ikiwa mtakuwa wakaidi na kukataa kutii amri, Nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua ninazozichukua hivi sasa" na

"Na ikiwa yeyote atashidnwa kutii amri ya kutotoka nje ya nyumba kama walivyofanya wengine.sitokuwa na njia nyengine lakini kutumia silaha nzito. Sisi, ni jeshi lenye nguvu ya 99,099,000".

Vitisho vyake na uwezo wake wa kuvitekeleza viliwatia hofu raia, hasa makundi mbali mbali ya jamii zilizo ndogo. Tarehe 14 Januari, 1964 alitangaza maneno haya ya kufadhaisha:

“Huyu hapa ni Jemedari Mkuu wa Unguja na Pemba; Nafikiria kuelekea kijiji cha Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa hapo hawatafuata amri. Baada ya dakika 40 nitawamaliza nyote hasa Wangazija na kwa vijana wote wa kiarabu wanaoishi Malindi; Nitapita Malindi nikiwa nimesheheni silaha ambazo mimi mwenyewe ndie nizijuazo. Nataka kuona kila mmoja abakie na chupi na kulala chini. Nataka kuwaona wao wanaimba... Baba wa Waafrika. Mungu Mbariki yeye na malengo yake na yale ya Jemedari Mkuu"Wakati unyanyasaji uliposima jamii za tamaduni tofauti za Zanzibar zilikuwa zimeparaganyika. Taifa la chama kimoja lilitangazwa. Lakini bado Taifa hili likihofia uwezekano wa kufufuka upinzani kutoka kwa wapinzani waliokimbia nchi. Wanamapinduzi hawa baadae walijihakikishia udhibiti zaidi baada ya kusaini mkataba wa muungano wa Tanganyika. Hii ingeruhusu maelfu ya marafiki wa kisiasa wa Tanganyika kuingilia kati upinzani wowote wa baadae katika visiwa hivi. Askari polisi wa Zanzibar walibadilishwa kwa askari polisi kutoka Tanganyika ambao ni watiifu kwa chama na pazia la siasa za utengano ziliwakumba wazanzibari ambazo zilitakiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 20.

Leo hii siasa hizi za utengano hazipo tena, kumalizika kwa vita vya baridi na kuelekea kwa uchumi wa kisasa umeweza kuifungulia Zanzibar milango kwa ulimwengu wa nje. Uchaguzi wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995 na mwengine unatarajiwa kufanyika mwaka, 2000. Viongozi wa kweli na wenye kujali hali za watu wameibuka Tanzania na hii imewafanya wakimbizi waliokimbia wakati wa mapinduzi kurejea visiwani. Uvumilivu na amani wa watu wa aina tofauti, ambayo ni tabia ya maisha ya wazanzibari, sasa hivi unajitahidi kurejea katika mitaa ya mji mkongwe.

MCHANGO WA MDAU:
Soma hii makala kutoka kwa Ahmed Rajab.
Licha ya mgeni kutoka Uganda, John Okello (aliyekaa katikati), kuonekana mstari wa mbele katika mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar mwaka 1964, dhima na nguvu yake ilikuwa na nafasi gani katika uhalisia?

SINA tabia ya kusutana, kubishana au hata kujibizana na wasomaji wa makala zangu wenye kutoa maoni tofauti na yangu. Ninaamini kwamba kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yoyote ayatakayo hasa pale maoni hayo yanapokuwa ni ya ufafanuzi au uchanganuzi wa matukio ya kihistoria.

Kufanya ufafanuzi lakini ni tofauti na kuuelezea ukweli hasa ule ukweli wenye kuhusika na tendo ama vitendo fulani.
Nimekuwa nikisubiri kwa shauku kubwa hitimisho la makala za mwandishi mwenzangu wa Raia MwemaJoseph Mihangwa kumhusu John Okello.

Mfululizo huo wake wa makala zake kuhusu Okello na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ulikuwa ni majibu ya maandiko yangu juu ya mada ya Okello. Kwenye sahafu (safu) ya leo nataka kuyajibu baadhi ya yaliyomo kwenye majibu yake.

Kuna baadhi ya Wazanzibari wanaoona kwamba hakuna faida yoyote kujadili yaliyopita hasa sasa wakati wa mchakato wa Katiba mpya. Lakini wanakosea kwani tunaposonga mbele ni lazima tujue si tu hapa tulipo lakini pia tulikotoka. La sivyo tutajikuta tunajikwaa kila tunapopiga hatua.

Kuna tatizo kubwa kumtathmini Okello na dhima yake katika Mapinduzi ya Zanzibar. Sababu yake ni kuwako kwa simulizi zenye kukinzana kuyahusu Mapinduzi hayo na walioshiriki kwenye matukio yaliyoanzia Januari 12, mwaka 1964.

Migongano ya simulizi hizo yanamfanya mtu afikirie kwamba labda mapinduzi hayo yalifanywa na maruhani na kisha ndipo wanaadamu nao wakaingia. Ndio maana wengine chambilecho Sheikh Thabit Kombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Afro-Shirazi Party (ASP), wanaifikiria historia ya Zanzibar yote kuwa ni uongo mtupu.

Lazima niseme hapa kwamba baadhi ya wanaotoa simulizi mbadala huwa hawana nia njema na Zanzibar. Simulizi zao huupotosha ukweli ili ziweze kuwa na mishiko. Mihangwa si miongoni mwao. Yeye ni mwandishi mahiri mwenye kuandika baada ya kuridhika kuwa amefanya uchunguzi wa kina kuhusu mada inayohusika.

Nimekuwa nikiyafuatilia maandishi yake kuhusu Zanzibar kwa muda mrefu na kwa maoni yangu huyu ni mwandishi mwenye kutupenda laisa kiasi sisi wazawa wa Zanzibar.

Lakini kwa vile yeye si mzaliwa wa Zanzibar na wala hajakuwako Visiwani (hasa Unguja) wakati wa Mapinduzi kwa kiwango kikubwa amekuwa akiwategemea wengine kwa masimulizi yake. Pingine hao ndio waliompotosha.
Sitothubutu kusema kwamba ubara wake umeugubika utaalamu wake kwa sababu hakuteleza kuyaeleza ya Zanzibar tu kama alivyomuelezea Othman Sharif kuwa alikuwa Mkomunisti wakati bwana huyo akijulikana kwa chuki zake dhidi ya wenye siasa za mrengo wa kushoto.

Mihangwa ameteleza kwa mengine pia. Kwa mfano, amemuelezea Idi Amin kuwa ni Mlangi, mtu wa kabila la Lango, ilhali tunajua kwamba alikuwa Mnubi wa kabila la Kakwa.

Tukiliacha hili la Okello, ambalo hakika Mihangwa halielewi, maandishi yake mengine kuhusu Zanzibar hayakirihishi kama ya wenzake wengi wa Bara. Mara kadha wa kadha kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar alikuwa akiwavua nguo watawala wa Visiwani kwa kufuata kisiri siri sera za kibaguzi zilizopitishwa na Mkutano Mkuu wa ASP mwaka 1973 kule Pemba.

Kwa kiwango Fulani Mihangwa amesaidia kuwaelimisha Wabara wenzake kuhusu mgongano wa maneno na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Juu ya hayo lazima tumkumbushe Mihangwa kwamba Che Guevara, mzawa wa Argentina, hakwenda Cuba kama mfanyakazi mhamiaji kama alivyokuwa Okello. Che alikuwa msomi aliyeshirikiana na akina Fidel Castro, Raul Castro, Camilo Cianfuegos na Wacuba wengine waliokuwa uhamishoni kwenda Cuba kwa dhamira thabiti ya kufanya Mapinduzi ya kuikomboa nchi hiyo kutokana na udikteta wa Batista.

Wala Che hakuwahi kujaribu kudai na kupora haki ya kutawala na uongozi kama alivyofanya Okello Zanzibar. Wacuba walimtunuku Che nyadhifa za uongozi kwenye serikali yao mpya kwa ridhaa yao na kwa heshima kubwa. Walimfanyia hayo kwa vile walitambua mchango wake adhimu kwenye Mapinduzi yao.

Kiashiria kingine cha mapenzi ya Wacuba kwa Che ni pale Wacuba walipokwenda Bolivia alikouawa Che na kulisaka kaburi lake na kisha kuirejesha Cuba maiti yake kwa mazishi ya kitaifa. Kumfananisha Che na Okello ni kumtukana Che bila ya kiasi.

Okello alionyesha chuki kubwa kwa Wazanzibari na kujisifu kwa kuwaua wengi mbali na kujaribu kupora hatamu za utawala kutoka viongozi wa ASP. Ukweli ni kwamba Okello anafaa kulinganishwa na jamaa yake Joseph Kony wa Lords Resistance Army ya kule Uganda na sio kumweka pamoja na Major Ernesto ‘Che' Guevara.
Laiti Okello angalikuwa hai basi yakini angelijiunga na LRA kwani ni muumini wa dini ya Ukristo uchwara wa kuendesha mauaji ya kikatili sawa na mhalifu Kony.

Okello mwenyewe alizidi kuipotosha historia pale alipolalama kuwa Waafrika wa Zanzibar wamemfukuza baada ya yeye kwenda Visiwani kuwasaidia kuwashinda Waarabu waliokuwa wakiwachinja. Hapo ndipo tatizo linapoanza na hicho ndicho kielelezo au kiashirio cha uzushi unaobatizwa kuwa ‘historia ya nyumbani'.

Kwenye makala yake ya mwisho juu ya kadhia ya Okello, Mihangwa amemalizia kwa kuibua maswali muhimu kuhusu uhasama mkubwa uliojitokeza upande wa baadhi ya wakuu wa ASP dhidi ya Makomredi, yaani wafuasi wa Abdulrahman Babu na chama cha Umma Party.

Hii ni mada nzito lakini lazima tuigusie. Hali ya kutoaminiana kati ya Makomredi na wakereketwa wa ASP imekuwepo wakati wote chini kwa chini tangu kilipoundwa chama cha Umma Party mwaka 1963.

Juu ya kuwepo hali hiyo ilibidi pia wakati ule pawepo na aina ya ushirikiano kati yao katika kukabiliana na wapinzani wao yaani vyama vya Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and Pemba Peoples' Party.

Haja hiyo ndiyo iliyopelekea pawepo umoja uliovishirikisha vyama vya ASP na Umma, vyama vya wafanyakazi pamoja na Jumuiya ya Wanafunzi.

Kiini cha kuwepo hali hiyo ya kutoaminiana ni ule msimamo wa itikadi ya kikabila wa takriban viongozi wote wa ASP wa kuwaepuka kisiasa Wazanzibari wenye asili ya kiarabu sembuse waliotokana na damu ya Hizbu. Mtazamo huu wa aina ya ‘kikaburu' ndio uliokuwa msimamo na unaendelea hivyo hadi leo kwa upande wa wahafidhina wa iliyokuwa ASP.

Wabara wasioitakia kheri Zanzibar wamekuwa wakiipalilia moto hali hii iliwaweze kuidhibiti Zanzibar kwa maslahi yao. Kwa hiyo dhana ya Umma Party ya kuyasuka Mapinduzi ili yawe na mtazamo wa kitabaka pekee badala ya ‘ugozi' (ubaguzi wa kikabila na wa rangi) ilisambaratishwa muda wote tangu kuanzia miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1960 na akina Othman Sharif, Jamal Ramadhan Nasib na Mdungi Usi.

Baadaye usambaratishaji huo uliendelezwa na wanapinduzi kina Seif Bakari, Abdalla Said Natepe na kaumu yote ya ile ijulikanayo kama ‘Kamati ya Watu 14.' Hao ndio waliomshinikiza Sheikh Karume kutowashirikisha Makomredi kwenye uongozi wa nchi.

Siku zote walikuwa wakimtisha Mzee Karume kuwa Makomredi walikuwa na njama na jamaa zao Wakiarabu za kuutokomeza utawala wa Waafrika. Hatimaye walifaulu pale Karume alipowatimua kutoka kwenye serikali kina Badawi Qullateinna Ali Sultan na kubwa lao Babu kudondoshwa na Julius Nyerere.

Kuna siku ambapo Brigadia Yusuf Himidi aliwasikitia baadhi ya wafuasi wa Umma Party waliokuwa naye kwa kuwaambia: "Eh jamaa fitna nyingi zimepita kutugombanisha." Hakumtaja mtu lakini ilikuwa wazi kwamba mafatani walikuwa baadhi ya wahafidhina wa ASP.

Tatizo kubwa la Zanzibar ni kwa Wazanzibari kukubali kuhadaiwa na wanasiasa uchwara kuendelea kuwa wafungwa wa historia ya kisiasa iliyoigawa jamii katika makundi ya kikabila na kinasaba.

Jukumu linalotukabili sasa ni namna ya kutafuta njia za kuuyayusha urathi huu muovu unaoigawa jamii ya Wazanzibari na unaoutia sumu ufahamu au utambuzi wa pamoja wa Wazanzibari.

Okello alifurushwa Zanzibar kwa sababu alikuwa akileta matatizo. Alikuwa ni adha lakini hakuwa kitisho cha kisiasa. Angelikuwa ni kitisho cha kisiasa basi isingekuwa rahisi kumng'oa nchini kama alivyotolewa.

Wala si peke yake kati ya wageni waliokuwa wakifanya fujo aliyefukuzwa Zanzibar. Mwengine alikuwa Engine kutoka Kenya. Naye pia alitimuliwa baada ya kukamatwa huko Maruhubi, kwa amri ya Sheikh Karume, na kikundi cha Makomredi wakiongozwa na Ali Mshangama.

Mwengine aliyekuwa akiitwa Mfarinyaki alikamatwa Chwaka na Komredi Hamed Hilal aliyempeleka gerezani Kiinua Miguu. Amri za kukamatwa Mfarinyaki aliitoa Yusuf Himidi akiwa mkuu wa jeshi. Kwa nini hajawahusisha wanajeshi wengine na wapinduzi wa ASP, haijulikani. Labda Yusuf Himidi alikwishang'amua kwamba wenzake walikosa nidhamu, wakijihusisha zaidi na wizi wa ngawira, wakati Makomredi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Hatujui pia kwa nini Karume alihiyari kuwatumia Makomredi kuwatimua akina Okello, Engine na wapinduzi wengine waliokuwa si wenyeji wa Zanzibar.

Yumkini Karume aliamua kuwatumia Makomredi kumfukuza Okello badala ya kuwahusisha akina Said Washoto, Mohamed Abdalla Kaujore, Seif Bakari, Khamis Darwesh na wengine wa Kamati ya Watu 14 kwa sababu alihisi wangelisitasita na pengine kuibua mgogoro. Said Abdallah Natepe aliwahi kuhadithia kwamba waliwahi kumjadili Okello miongoni mwao na hata pakatolewa wazo la kumuua.

Sheikh Aboud Jumbe amekiri kwenye kitabu chake ‘The Part-nership' kuwa alikuwa hawajui na hakupata kuwaona baadhi ya waliokuwemo kwenye Kamati ya Watu 14, wakiwa pamoja na Okello.

Nakiri kwamba ni taabu kuamini ya kuwa Okello aliibuka ghafla Raha Leo kutoka halaiki ya watu waliokuwa wamekusanyika hapo. Lakini pia tuna uhakika kwamba Okello hakuwa na uwezo wala heshima anayobandikwa nayo na Mihangwa.

Hatusemi hivi kwa sababu Okello hakuwa Mzanzibari. Tunasema hivi kwa sababu huo ni ukweli huku tukikubali kwamba kuna haja ya kuiangalia upya nafasi yake Okello katika mchakato mzima wa maandalizi ya Mapinduzi.

Nimalizie kwa kukumbusha jingine. Nalo ni kwamba kadhia niliyoieleza ya kutimuliwa Okello kutoka Zanzibar haikuwa ya mwanzo ya kufukuzwa Okello. Mara ya kwanza alifukuziwa kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kusindikizwa hadi Nairobi na Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika.
___________________________________________________________
Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 4 Aprili 2012 chini ya kichwa cha habari "Maruhani hawakupindua Zanzibar".
 
Pascal Mayalla

Platinum Member
Sep 22, 2008
37,968
2,000
Mkuu Mshume Kiyate, ahasanta kwa hii ya Mapinduzi Mtukufu ya Zanzibar, Kiukweli umenipreempty hivyo zile mada zangu zilobaki nitaziteremshia kwenye michango yangu ndani ya huu huu uzi wako.

Kiukweli Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yameviletea heshima kubwa Visiwa hivi, kwa kuirejesha Zanzibar kwa wenyewe Wazanzibari, Wazanzibara na Wazenj wa asili baada ya kumtimua Mwarabu mvamizi aso haya aliyetoka zake Arabuni Omani na kuja kuvivamia Visiwa hivyo vya kupendeza kwa kujileta tuu na kuvitwaa hivi hivi kama ameokota koo au Kombe-bahari, baharini na kuvitawala kama vyake!.

Mapinduzi haya matukufu, yaliomfurusha Mwarabu, yanastahili kuenziwa, kuheshimiwa, na kudumishwa milele!.
Mapinduzi Daima!.
Pasco
 
Falconer

JF-Expert Member
Oct 14, 2008
808
500
Waso Haya wana mji wao. Rasimu ya pili imetoka na Tanganyika inarudi. Sijui kama tutakuwa na Tanzania lakini jitayarisheni maana sisi hatutaki tena muungano bandia. Na kura ya maoni ya kujitenga tunaifanyia mipango kabambe.
 
Pascal Mayalla

Platinum Member
Sep 22, 2008
37,968
2,000
Mkuu Mshumi Kiyati, Du hii thread
yako tangu imefunguliwa jana, imepata wachangiaji wawili tuu!. Au kwa vile ilikuwa ni usiku mainzi walikuwa bado wamelala na mpaka saa hizi bado ni mapema mno hayajaamka?!.

Kuna mtu humu anaitwa Mkuu Zomba kuna member amempachika jina la 'muuza utumbo!', akiingia kuchangia humu, ghafla utaona mainzi kibao yanajaa, yanamfuatia nyuma yake!.

Kama vipi tumwite Mkuu Zomba amshtue 'muuza utumbo', thread ichangamshwe?!.
Heri ya Mwaka Mpya.
Pasco
 
Mshume Kiyate

JF-Expert Member
Feb 27, 2011
6,771
1,195
pasco,
Pasco, wala mie sina tatizo na wachagiaji najua watakuja tu, naona unamuogopa sana huyo zomba hauishi kumtaja, hii thread yangu inakaribisha mtu yeyote kinachotakiwa watu wafyonze Ilm, kuna mengi tayaweka humu, karibu sana naona umeikimbia thread yako mwenyewe baada kukumbana na hoja nzito umekuja kujiliwaza hapa.
 
Last edited by a moderator:

Erythrocyte

JF-Expert Member
Nov 6, 2012
79,220
2,000
kumbe ndiyo ilivyokuwa ? Je huyu OKELLO anapewa heshima anayostahili kweli ?
 
TIMING

JF-Expert Member
Apr 12, 2008
22,001
2,000
Waso Haya wana mji wao. Rasimu ya pili imetoka na Tanganyika inarudi. Sijui kama tutakuwa na Tanzania lakini jitayarisheni maana sisi hatutaki tena muungano bandia. Na kura ya maoni ya kujitenga tunaifanyia mipango kabambe.
Bora muungano uvunjike tu
 
Pascal Mayalla

Platinum Member
Sep 22, 2008
37,968
2,000
Pasco, wala mie sina tatizo na wachagiaji najua watakuja tu, naona unamuogopa sana huyo zomba hauishi kumtaja, hii thread yangu inakaribisha mtu yeyote kinachotakiwa watu wafyonze Ilm, kuna mengi tayaweka humu, karibu sana naona umeikimbia thread yako mwenyewe baada kukumbana na hoja nzito umekuja kujiliwaza hapa.

Shukran ahasanta tumekurubia.
Kule sijakimbia hoja ziliisha kitambo ila nakiri miinzi ilizonga sana japo ilichangamsha hadi kufikia post 600 plus!. Sii kawaida yangu!, mimi kama mimi huwa zikizidi sana huweza kufika yapata 50 tuu hivyo 'muuza utumbo ' amesaidia!.
Pasco.
 
Last edited by a moderator:

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,886
2,000
Tujikite katika Serekali yetu ya Tanganyika hivi sasa kwa kuipa meno , hizi kasumba nyengine tuwachie Wazanzibar wenyewe na Serekali yao ya Mapinduzi.

Hivi sasa tutambue zile kelele za kua Serekali ya Tanganyika haipo lakini ya Zanzibar ipo, nazani itakua Warioba kafanya Kazi nzuri , sasa laumuhimu ni kua Tanganyika ni nchi na Zanzibar ni nchi tutakutana katika chirikicho la Muungano kwa Mambo ya Muungano .

Kwa hio Tanganyika tuwe bizi na kutengeneza katiba yetu na mambo yetu ya Tanganyika ili kuipa meno serekali yetu na mambo yetu ,haya ya Wazanzibar @ Mshume Kiyate washie wenyewe Wazanzibar ili mambo ya Goswa ,muachie goswa wenyewe.
 
Bobwe

JF-Expert Member
May 21, 2013
1,239
0
pasco,
Heshima ipi iliyonayo Zanzibr baada ya hayo unayoyaita mapinduzi ya zanzibr,kuiondoa bendera ya zanzibr isipeperuke kule UN ni heshima?
 
Mshume Kiyate

JF-Expert Member
Feb 27, 2011
6,771
1,195
kumbe ndiyo ilivyokuwa ? Je huyu OKELLO anapewa heshima anayostahili kweli ?
YAFUATAYO ni masimulizi mafupi ya kipindi kifupi cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 1964 yaliyoipindua serikali ya ubia ya chama cha Zanzibar Nationalist (maarufu Hizbu) na kile cha Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP). Tunaangazia nini hasa kilitokea usiku wa Jumamosi Januari 11, yaliyojiri siku ya pili yake na mwezi mzima wa Januari, mwaka 1964.

Tumeyakusanya masimulizi haya baada ya kuzungumza na walioshiriki katika Mapinduzi hayo ambao baadaye walisaidia kudhibiti madaraka na kuunda taasisi zilizoziba pengo la Serikali iliyopinduliwa ya Waziri Mkuu, Muhammed Shamte Hamadi.

Usiku wa manane wa Januari 11, makada wapatao 200 wa Umoja wa Vijana wa Afro-Shirazi (Afro-Shirazi Youth League) walielekea kwenye kambi ya polisi ya Ziwani, nje kidogo ya mji huko Unguja.

Wakiongozwa na Yusuf Himid wapinduzi hao hawakukabiliwa na upinzani walipofika Ziwani ila waliikuta ghala ya silaha iko wazi na wakazinyakua silaha na kukimbia nazo hadi kwenye uwanja ulio nje ya jengo la Raha Leo.
Hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache na ndipo wapinduzi walikokuwa wakipewa silaha. Studio za redio ya Serikali pia zilikuwa hapo.

Moja ya sababu zilizoyafanya Mapinduzi yafanikiwe haraka ni uamuzi wa viongozi wa Serikali iliyopinduliwa - Sheikh Muhammed Shamte na Sheikh Ali Muhsin Barwani - kuwataka wafuasi wao wasitumie nguvu kuyapinga.

Hivyo, mbali na mapigano yaliyozuka saa za asubuhi ya Jumapili Januari 12, mbele ya Steshini ya Polisi Malindi, hapajazuka mapigano Unguja kati ya waliopindua na waliopinduliwa. Pemba nako pia hakukuwa na upinzani ijapokuwa kisiwa hicho kilikuwa ngome ya vyama vya ZNP na ZPPP.

Wengi wa wapiganaji waliokuwa kwenye Stesheni ya Polisi ya Malindi walikuwa wakuu wa polisi Wakiingereza. Wakipigana na makada wa Umma Party ambao ndio pia waliouteka uwanja wa ndege, bandari pamoja na kituo cha mawasiliano ya nje cha Cable & Wireless, kilichokuwa kwenye jengo ambalo sasa ni Hoteli ya Serena Mji Mkongwe.
Kwa hakika, kinyume cha baadhi ya watu walivyoandika hapakutokea mauaji ya kimbari. Aliyeanzisha uvumi huo alikuwa John Okello aliyeandika kwenye kitabu chake kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kwamba watu zaidi ya elfu kumi waliuliwa. Okello aliongeza kwamba aliamrishwa na Yesu Kristo kuwakomboa ‘Waafrika' wa Zanzibar kutoka kwa ‘wageni'.

Tutamrejelea Okello na wengine waliokuwa Raha Leo baadaye. Kwanza tukumbushe kwamba mkesha wa Januari 12, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na jeshi. Kulikuwa polisi waliokuwa wakiongozwa na Waingereza. Wengi wa askari polisi walikuwa raia wa Tanganyika. Serikali iliyopinduliwa ilikataa kuandikiana mkataba wa kijeshi na Uingereza kwa sababu ikihisi mkataba kama huo utaonekana kuwa wa kikoloni.

Hatuwezi kusema ni nani hasa aliyepiga risasi ya mwanzo au ya mwisho katika Mapinduzi. Naitoshe tusemapo kwamba kwa vile hakukuwa na upinzani, Serikali iliyokuwa madarakani iliporomoka kama ‘nyumba ya karata'.
Tuwarejelee sasa waliokuwa Raha Leo, makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache. Kwanza tumuangalie Okello ambaye sauti yake ndiyo iliyokuwa ikivuma kwenye Redio Zanzibar.

Hatuna uhakika nani alimpeleka Okello Raha Leo. Wengine wanasema ni Yusuf Himidi. Wengine wanasema ni Seif Bakari aliyetoa rai atumiwe kutoa matangazo kwenye redio kwa vile sauti yake ilikuwa na lafudhi ngeni ya kutisha.
Uhakika tulio nao ni kwamba Okello alipotokea Raha Leo na mabastola yake, Aboud Jumbe alishtuka na akauliza: "Nani huyu? Katokea wapi?"

Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 27 hakujulikana kabla ya Mapinduzi. Alikuwa mtu asiyejua kuandika wala kusoma na akili zake zikimtosha mwenyewe. Hakuwa na sifa za uongozi na wala hakushiriki katika vuguvugu lolote la kisiasa.

Akijibandika cheo cha kijeshi cha Field Marshall ni yeye aliyetangaza kwamba serikali ya ZNP/ZPPP imepinduliwa.
Kwa hakika, kazi hiyo ya kutangaza kufanikiwa kwa Mapinduzi kwanza alipewa Ramadhan Haji, mmoja wa wapinduzi. Lakini alikataa. Jina la Okello lisingelisikika lau Ramadhan Haji angekubali kutangaza kwamba Serikali imepinduliwa na kwamba wapinduzi waliidhibiti nchi.

Waliokuwa wakiongoza mambo Raha Leo tangu Mapinduzi yaanze, hadi Jumatatu Januari 13, walikuwa Aboud Jumbe, mmoja wa viongozi wa chama cha Afro-Shirazi (ASP), Thabit Kombo (Katibu Mkuu wa ASP) na Badawi Qullatein wa Umma Party. Muda wote huo, Sheikh Abeid Amani Karume (kiongozi wa ASP), Abdulrahman Babu (mwenyekiti wa Umma Party) na Abdalla Kassim Hanga (ASP) walikuwa Dar es Salaam.

Mnamo siku hizo hizo liliundwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri lililokuwa na mamlaka kamili ya kuiendesha Zanzibar. Mabaraza hayo mawili yalikuwa taasisi kuu za Serikali ya kimapinduzi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Na sio ile iitwayo ‘Kamati ya Watu Kumi na Nne' ambayo baadhi ya watu wanasema kuwa ndiyo iliyoandaa Mapinduzi.

Okello akipenda kujigamba kwamba ndiye aliyeyapanga na kuyaongoza Mapinduzi. Alikuwa akitoa matamshi ya kushtusha na ya ajabu-ajabu kwenye Redio Zanzibar. Kwa mfano, siku moja alidai kwamba alipwe mshahara mkubwa zaidi ya aliokuwa akilipwa Rais Karume. Siku nyingine akasema kwamba kasri zote alizokuwa akitumia sultani kupumzikia apewe yeye.

Kuna siku aliyotoa hukumu kwamba mzee mmoja wa zaidi ya miaka 60 afungwe kwa miaka 99. Alisema kama huyo bwana atakufa gerezani basi mwanawe afungwe ili kuendeleza kifungo na mwanawe akifa basi mjukuu wake afungwe mpaka itimie miaka 99.

Nyakati nyingine aliwaonya watu wazitie moto familia zao na wao wenyewe mpaka wafe ‘kabla ya majeshi yangu kuja.' Alikuwa akitoa vitisho visivyowahi kamwe kusikika Zanzibar.

Kuna siku alitangaza kwamba wakazi wa eneo moja ambako alikuwa apite, wajipange foleni barabarani wakiwa wamevaa chupi tu.

Okello alikuwa ni adha, kitisho, kichekesho na fedheha kwa Zanzibar. Viongozi wapya wa nchi walichoka naye na wakaamua kumchukulia hatua. Salim Rashid, mmoja wa viongozi wa Umma Party aliyekuwa katibu wa Baraza la Mapinduzi anasema kwamba, kwanza alilizungumza suala la Okello na Sheikh Karume. Halafu akalizungumza na Brigadia Yusuf Himid na mwisho yeye, Yusuf Himid na Kanali Ali Mahfoudh wakalitafutia dawa.

Ilisadifu kuwa siku moja Okello alisafiri kwenda Dar es Salaam akifuatana na Jaha Ubwa, aliyekuwa katibu wake. Walipokuwa wanatarajiwa kurudi Zanzibar, Karume, Yusuf Himid, Salim Rashid na Ali Mahfoudh walikwenda uwanja wa ndege kumsubiri.

Siku hiyo anaikumbuka vizuri Luteni Hashil Seif aliyekuwa ofisa wa zamu kwenye kambi ya jeshi huko Migombani karibu na uwanja wa ndege.

Alipigiwa simu akitakiwa aende kwa haraka uwanja wa ndege. Hakuambiwa anaitiwa nini.
Alipofika ndipo alipoambiwa kwamba kuna ndege ya Shirika la Ndege la Afrika ya Mashariki iliyokuwa inakuja kutoka Dar es Salaam ndani yake wakiwemo pia Okello na Jaha Ubwa.

Akaelezwa kwamba awaruhusu abiria wote pamoja na Ubwa washuke, lakini amzuie Okello asishuke. Halafu amwambie rubani ampeleke Okello Kenya.

Hashil naye akampigia simu komredi mwenzake Luteni Amour Dugheshina kumwita aende uwanja wa ndege amsaidie. Maluteni wote wawili walikuwa na bunduki za aina ya ‘machine gun'.

Ndege ilipotua walipanda ndani ya ndege, wakampokonya silaha Okello na kutekeleza amri waliopewa. Rubani wa ndege alikasirika sana. ‘Uso wake ulighadhibika, utafikiri mnyama aliyekosewa risasi,' alieleza Hashil.
Lakini rubani hakuwa na la kufanya ila kuiwasha ndege na kuelekea Kenya.

Huku nyuma Salim Rashid akampigia simu Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa Kenya, kumuarifu kwamba wamemfukuza Okello na ‘wanamrejesha' Kenya. Alifanya hivyo kwa makosa kwa sababu kutokana na jina lake akifikiri kuwa Okello ni Mjaluo kutoka Kenya.

Kumbe alikuwa mtu wa kabila la Acholi aliyezaliwa Uganda na alikwenda Unguja kabla ya kuhamia Pemba ambako alikuwa mwashi, mtiaji rangi nyumba na mpasuaji mawe.

Swali la kujiuliza hapa ni; je, iwapo kweli Okello alikuwa ‘kiongozi mpendwa wa Mapinduzi' ilikuwaje wafuasi wake na wanamapinduzi wenzake wasimtetee alipoadhiriwa uwanja wa ndege na kufukuzwa nchini? Ilikuwaje akafukuzwa kwa urahisi hivyo?

Kuna uzushi mwingi kuhusu kipindi hiki kifupi cha historia ya Zanzibar. Kwa mfano, kuna filamu ya kubuni ya Wataliana inayoonyesha maiti chungu nzima za watu waliopigwa risasi. Filamu hiyo ilikuwa na lengo moja tu; kuonyesha ‘ukatili na unyama wa Waafrika.'

Hakuna ithibati yoyote kwamba watu waliouawa katika siku za mwanzo za Mapinduzi walifika elfu kumi. Ukweli ni kwamba jumla ya watu waliouawa siku hizo haipindukii 200, katika sehemu za mjini hawazidi 25.

Uzushi mwingine ni kwamba walipelekwa Watanganyika, Zanzibar wakiwa na silaha kwenda kupindua. Na si kweli kwamba Mapinduzi yalikuwa na msisitizo wa kikabila. Katika kipindi cha mwanzo cha Mapinduzi msisitizo ulikuwa wa kitabaka. Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa kwenye Redio Zanzibar zikiwazungumzia ‘wakwezi na wakulima' na wafanyakazi kwa jumla na si makabila.

Mapinduzi ya Zanzibar yalianzisha taasisi mpya za utawala zikiwa pamoja na Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mawaziri na ofisi ya Rais. Taasisi hizo zilikuwa zifanye kazi kwa muda wa mwaka mmoja tu kwa vile ilikwishaamuliwa kwamba Januari 1965 pafanywe uchaguzi wa kulichagua Bunge la Katiba, lililokuwa litunge Katiba ya kudumu ya Zanzibar.

Baraza la Mapinduzi la Zanzibar pamoja na Serikali mpya zilianza kwa ubia baina ya chama cha ASP na Umma Party. Ingawa wanachama wa ASP ndio waliofanya Mapinduzi waliutambua mchango wa wafuasi wa Umma Party na hasa mchango wa makada wao waliopata mafunzo ya kijeshi nchini Cuba.

Vijana hao wa Umma walizitia wasiwasi serikali za Marekani na Uingereza na kuzifanya ziamini kuwa utawala mpya wa Zanzibar ulikuwa wa ‘kikomunisti'. Dhana hiyo ndiyo iliyosababisha kuchukuliwa hatua ya kuyachimba na kuyagandamiza Mapinduzi ya Zanzibar yaliyodumu kutoka Januari 12, hadi 26 Aprili, mwaka 1964.
- See more at: Raia Mwema - Siku Field Marshal John Okello

John Okello, hapa nakumbuka walitoka watu, wametoka watu hapa wakenda Pemba. Kwa hali ya kiuchunguzi. Je, Pemba tunaweza kuwapata wenzetu tukaja kusaidiana hapa? Wakatupa motisha? Kule nakumbuka mtu wa mwanzo aliekwenda kule alikuwa Ibrahim Makungu. Alikwenda na Jaha Ubwa, Mdungi Usi. Watu watatu hao.

Sasa walipokwenda kule, sasa wale Ma Afro-Shirazi magogo wa kule Pemba, wakawauliza, jamani e, vipi tunaweza kumpata kijana mshupavu huku wa kutusaidia hii kazi yetu sisi, au vijana washupavu hivi tunaweza kuwapata? Sasa alikuwepo mzee mmoja Mkoani. Huyu akasema jamani mnajuwa nyinyi?

Hapa yuko Mganda mmoja anachonga mawe huko. Huyu kijana naona kachangamka sana. Kachangamka sana! Sasa hatujuwi utaratibu wake hatuujuwi vipi. Sasa hapo mtu kama huyo sio anaingiwa tu ovyo ovyo. Panataka mbinu. Wakarudi wale kwanza. Kufika huku Mfaranyaki na Washoto wakasema "twende tukachonge mawe."

Wakenda Pemba. Kufika Pemba, wakaanza shughuli ya kuchonga mawe, sasa yule akiwa kama ni fundi wao. Wamechonga mawe pale, wamechonga, wamechonga, ile data wakamuelezea yule. Hii kazi gani hii? Utumwa gani huu? Pangelikuwa na wanaume wa kuipinduwa hii nchi…1

Lengo walilolikusudia ni kumvisha blangeti Okello kwa sababu yeye ni mgeni. Si mwenyeji. Sasa sisi tukitaka kutafuta sababu ya kujifunika tumvishe huyu. Huyu si Mtanganyika huyu. Ni Mganda! Mbali huko. Kwasababu leo Mtanganyika hapa akilizuwa balaa hili lazima atajulikana "Oh! Mwalimu umefanya chokochoko." Lakini huyu, huyu anatoka Uganda huyu. Sasa watu watakuja kumuuliza Obote "vipi mambo haya?" Wewe Obote vipi mtu wako anakuja kufanya machafuko nchini kwetu. Sultani sasa atakuwa atapambana na Obote. Sio na Tanganyika.2

Bwana yule [Okello] kumueleza vile akasema "nyinyi wapumbavu, sisi tunazo dawa tunaweza kwenda kuzichukuwa hapo kwa Mau Mau, tukafanya mambo hapa yakajulikana yakawa kweli." "Ah ewe bwana huwezi bwana. Mambo gani hayo? Unatufanyia kitu masihara tu bwana." Akasema "bwana e hayo mambo yapo, tunaweza kuyafanya." "Kweli?" "Kweli." "Hebu fanya." Akatoka Okello, akenda Nairobi. Kufika Nairobi akakutana na Mau Mau, wakampa dawa.

Bwana eh, mnaweza kulifanya hili nyie lakini dawa hizi shote wote watakaoshiriki kwenye mapinduzi dawa hii sote mmoja mmoja uwapake. Unavowapaka dawa hizi, ina maana nyinyi mnawapumbaza wale watu wasijuwe. Japo kama watajuwa watadharau. Watadharau dharau. Okello akarudi Pemba. Kurudi Pemba kamkuta Washoto kaja Unguja. Kule kamkuta Mfaranyaki, vipi? Nimeleta. Umeleta nini? Hizi hapa. Dawa. Akamwambia sasa bwana wewe inabidi sasa tuondoke mimi na wewe twende Unguja. Wakaondoka, wakaja zao hapa. Okello akakaa na mzee mmmoja sehemu za Bambi huku, pamoja na dawa zake. Kutwa nzima humkuti na mazungumzo na watu. Imekwenda kwenda ikabidi, akina Sefu Bakari, akina Natepe, akina Ingine, ndio wakaanza kusema, unajuwa nyie, sisi tumeshapata mtu wa kumfunika blangeti bwanaa! Vipi? Huyu hapa. Tumpeni cheo huyu. Tukimpa cheo huyu kwani iwe nini? Mambo yetu yakikaa sawa si basi! Si tunamwambia "chukua chako hichi, kwaheri."

Okello sogea, vipi bwana wewe, masuala ya huyu Washoto na huyu Mfaranyaki. Mmekubaliana vipi nyie? Nimewaambia hakuna uzito. Lakini mimi nimewaambia, ngojeni mimi nikachukuwe dawa. Mimi nimechukuwa dawa. Zipo. Dawa hizi masharti yake? Akasema hizi dawa bwana, hizi dawa zinako-rogwa kwenye maji, wale watu siku ile khasa ya mapambano, wanamwagiwa mwagiwa hawa, wanajipakaa pakaa, tayari, halafu kuna dawa moja watu wanakunywa, wakishakunywa hiyo, suala limekwisha. Watu wanaondoka wanakwenda kwenye mapambano. Washakingika. Lakini shoti mfanye ngoma. Ngoma tunaweza kufanya fete, kubabaisha. Watakapokuja watu mjini kutoka mashamba watakuwa hawajulikani. Watakuwa wanaonekana wanakwenda kwenye sherehe, starehe na furaha.
Baada ya kupitishwa watu kuja kunako fete, hapo sasa ndo Kisasi na Okello, Mfaranyaki, huyu Kassim Hanga pamoja na Hasnu Makame waliambiwa "kaeni pembeni kabisa! Pembeni kabisa nyinyi. Msiingie huku, tuwachieni sisi kwa sababu nyinyi ndo chimbuko."

Suala hili aliyekuwa akilishughulikia Kaujore. Kumalizika "jamani tumeshamaliza." Sasa katika hao mmoja ile dawa akawa hakuipata, kama utaskia habari za chinichini, yuko mmoja alitoka Bomani akakimbia moja kwa moja mpaka Ndagaa akenda akasema "jamani huko mjini serikali imekwisha pinduliwa." Ile dawa kwa sababu hakuipata. Lakini aliepata dawa bwana, hakupepesa hapa na pale. Hakupepesa hapa na pale. Khofu hamna. Mtakuwa khofu hamna. Hamuogopi kitu chochote. Hamuogopi kitu chochote. Na kwa kweli bwana. Leo we ufikirie, kweli tizama, mtu kuvunja mlango wa nyuma wa Bomani. Yule Kamanda yuko pale, watu wanapita pale, Kamanda yuko pale, hakuna anayemuona, mpaka kuja kumkabili sentry [askari wa zamu]. Si mchezo. Hapa kiinimacho hiki kilipita kikubwa sana. Hata ikabidi mambo yakaja yakaingia sura.

[Kwa upande wa Umma Party] Hanga ilikuwa kama ni kitu geresha kwa Abrahmani Babu. Siasa za Babu zilikuwa za Kikoministi za Kichina. Juu ya kuwa Mkoministi na siasa zake za Kichina, Hanga alisema, huyu vyovote itakavokuwa, wale ni wenzake. Kwa vyovyote itakavokuwa, damu nzito kuliko maji.3 Alisema hivo. Usifikiriye kama leo huyu Babu apigwe, Waarabu hawakubali. Hawatokubali, kwa sababu itakuwa aibu kwao. Watasema "ala! kwanini Mwarabu apigwe? Kaasi tu huyu chama cha Hizbu, anapigiwa kwanini. Hapana." Hilo suala kwanza ndoto ya kumueleza Babu hamna. Asielezwe kwanza huyu. Babu, Ali Mahfudhi, na wenzao, hakuna suala namna hilo. Hii yote mambo ya Manamba, walikuwa hawayaelewi. Katika vikao vyote vilivopita hakuna mmoja aloshiriki katika Makomred. Hata sku moja.

Kwa sababu Komred siku ya Jumapili ndipo alivochukuwa bunduki kuumiza wenzake kujificha macho. Kujionyesha yeye kwa Mzee Karume au kwa Afro-Shirazi, yeye yuko bega kwa bega na Afro-Shirazi. Kujiaminisha. Kujikubalisha.

Kwamba mimi hawa Waarabu sina imani nao. Na aliwaumiza kweli Babu. Jumapili bwana ndipo wale walipojuwa, mimi nikifanya hivi madam ile serikali imeshapinduka, wadhifa ntapewa na mzee Karume. Huyu anafaa kupewa posti [cheo] kwa sababu aligombana na Hizbu na ataweza kutumika kuwazuwia kina Hanga na Othman Sharifu.

Kilichokuwa kinatendeka mpaka Jumamosi usiku walikuwa hawakijuwi. Kabisa. Komred hakijuwi kabisa kwa sababu Hanga alizungumza "bwana, mtu damu nzito kuliko maji." Sasa ukija ukitizama, Babu, Ali Mahfudhi, Badawi, nk, hawa wamezaliwa mshipa wa Kiarabu. Wazee wao Waarabu.

Sasa leo mkija kuwazungumzia watakuwa na fikra hawa wawaze "je, wanotaka kupinduliwa hawa Waarabu. Sasa vita vikitokezea vitakuwa va Waarabu. Je, sisi tutanusurika?" Ikabidi pakafunikwa hapo. Wasiambiwe. Jumapili, kweli Komred walikuja Raha Leo kifua mbele.
 
Mshume Kiyate

JF-Expert Member
Feb 27, 2011
6,771
1,195
Tujikite katika Serekali yetu ya Tanganyika hivi sasa kwa kuipa meno , hizi kasumba nyengine tuwachie Wazanzibar wenyewe na Serekali yao ya Mapinduzi.

Hivi sasa tutambue zile kelele za kua Serekali ya Tanganyika haipo lakini ya Zanzibar ipo, nazani itakua Warioba kafanya Kazi nzuri , sasa laumuhimu ni kua Tanganyika ni nchi na Zanzibar ni nchi tutakutana katika chirikicho la Muungano kwa Mambo ya Muungano .

Kwa hio Tanganyika tuwe bizi na kutengeneza katiba yetu na mambo yetu ya Tanganyika ili kuipa meno serekali yetu na mambo yetu ,haya ya Wazanzibar @ Mshume Kiyate washie wenyewe Wazanzibar ili mambo ya Goswa ,muachie goswa wenyewe.
Soma hii makala kutoka kwa Ahmed Rajab.
Licha ya mgeni kutoka Uganda, John Okello (aliyekaa katikati), kuonekana mstari wa mbele katika mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar mwaka 1964, dhima na nguvu yake ilikuwa na nafasi gani katika uhalisia?

SINA tabia ya kusutana, kubishana au hata kujibizana na wasomaji wa makala zangu wenye kutoa maoni tofauti na yangu. Ninaamini kwamba kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yoyote ayatakayo hasa pale maoni hayo yanapokuwa ni ya ufafanuzi au uchanganuzi wa matukio ya kihistoria.

Kufanya ufafanuzi lakini ni tofauti na kuuelezea ukweli hasa ule ukweli wenye kuhusika na tendo ama vitendo fulani.
Nimekuwa nikisubiri kwa shauku kubwa hitimisho la makala za mwandishi mwenzangu wa Raia MwemaJoseph Mihangwa kumhusu John Okello.

Mfululizo huo wake wa makala zake kuhusu Okello na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ulikuwa ni majibu ya maandiko yangu juu ya mada ya Okello. Kwenye sahafu (safu) ya leo nataka kuyajibu baadhi ya yaliyomo kwenye majibu yake.

Kuna baadhi ya Wazanzibari wanaoona kwamba hakuna faida yoyote kujadili yaliyopita hasa sasa wakati wa mchakato wa Katiba mpya. Lakini wanakosea kwani tunaposonga mbele ni lazima tujue si tu hapa tulipo lakini pia tulikotoka. La sivyo tutajikuta tunajikwaa kila tunapopiga hatua.

Kuna tatizo kubwa kumtathmini Okello na dhima yake katika Mapinduzi ya Zanzibar. Sababu yake ni kuwako kwa simulizi zenye kukinzana kuyahusu Mapinduzi hayo na walioshiriki kwenye matukio yaliyoanzia Januari 12, mwaka 1964.

Migongano ya simulizi hizo yanamfanya mtu afikirie kwamba labda mapinduzi hayo yalifanywa na maruhani na kisha ndipo wanaadamu nao wakaingia. Ndio maana wengine chambilecho Sheikh Thabit Kombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Afro-Shirazi Party (ASP), wanaifikiria historia ya Zanzibar yote kuwa ni uongo mtupu.

Lazima niseme hapa kwamba baadhi ya wanaotoa simulizi mbadala huwa hawana nia njema na Zanzibar. Simulizi zao huupotosha ukweli ili ziweze kuwa na mishiko. Mihangwa si miongoni mwao. Yeye ni mwandishi mahiri mwenye kuandika baada ya kuridhika kuwa amefanya uchunguzi wa kina kuhusu mada inayohusika.

Nimekuwa nikiyafuatilia maandishi yake kuhusu Zanzibar kwa muda mrefu na kwa maoni yangu huyu ni mwandishi mwenye kutupenda laisa kiasi sisi wazawa wa Zanzibar.

Lakini kwa vile yeye si mzaliwa wa Zanzibar na wala hajakuwako Visiwani (hasa Unguja) wakati wa Mapinduzi kwa kiwango kikubwa amekuwa akiwategemea wengine kwa masimulizi yake. Pingine hao ndio waliompotosha.
Sitothubutu kusema kwamba ubara wake umeugubika utaalamu wake kwa sababu hakuteleza kuyaeleza ya Zanzibar tu kama alivyomuelezea Othman Sharif kuwa alikuwa Mkomunisti wakati bwana huyo akijulikana kwa chuki zake dhidi ya wenye siasa za mrengo wa kushoto.

Mihangwa ameteleza kwa mengine pia. Kwa mfano, amemuelezea Idi Amin kuwa ni Mlangi, mtu wa kabila la Lango, ilhali tunajua kwamba alikuwa Mnubi wa kabila la Kakwa.

Tukiliacha hili la Okello, ambalo hakika Mihangwa halielewi, maandishi yake mengine kuhusu Zanzibar hayakirihishi kama ya wenzake wengi wa Bara. Mara kadha wa kadha kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar alikuwa akiwavua nguo watawala wa Visiwani kwa kufuata kisiri siri sera za kibaguzi zilizopitishwa na Mkutano Mkuu wa ASP mwaka 1973 kule Pemba.

Kwa kiwango Fulani Mihangwa amesaidia kuwaelimisha Wabara wenzake kuhusu mgongano wa maneno na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Juu ya hayo lazima tumkumbushe Mihangwa kwamba Che Guevara, mzawa wa Argentina, hakwenda Cuba kama mfanyakazi mhamiaji kama alivyokuwa Okello. Che alikuwa msomi aliyeshirikiana na akina Fidel Castro, Raul Castro, Camilo Cianfuegos na Wacuba wengine waliokuwa uhamishoni kwenda Cuba kwa dhamira thabiti ya kufanya Mapinduzi ya kuikomboa nchi hiyo kutokana na udikteta wa Batista.

Wala Che hakuwahi kujaribu kudai na kupora haki ya kutawala na uongozi kama alivyofanya Okello Zanzibar. Wacuba walimtunuku Che nyadhifa za uongozi kwenye serikali yao mpya kwa ridhaa yao na kwa heshima kubwa. Walimfanyia hayo kwa vile walitambua mchango wake adhimu kwenye Mapinduzi yao.

Kiashiria kingine cha mapenzi ya Wacuba kwa Che ni pale Wacuba walipokwenda Bolivia alikouawa Che na kulisaka kaburi lake na kisha kuirejesha Cuba maiti yake kwa mazishi ya kitaifa. Kumfananisha Che na Okello ni kumtukana Che bila ya kiasi.

Okello alionyesha chuki kubwa kwa Wazanzibari na kujisifu kwa kuwaua wengi mbali na kujaribu kupora hatamu za utawala kutoka viongozi wa ASP. Ukweli ni kwamba Okello anafaa kulinganishwa na jamaa yake Joseph Kony wa Lords Resistance Army ya kule Uganda na sio kumweka pamoja na Major Ernesto ‘Che' Guevara.
Laiti Okello angalikuwa hai basi yakini angelijiunga na LRA kwani ni muumini wa dini ya Ukristo uchwara wa kuendesha mauaji ya kikatili sawa na mhalifu Kony.

Okello mwenyewe alizidi kuipotosha historia pale alipolalama kuwa Waafrika wa Zanzibar wamemfukuza baada ya yeye kwenda Visiwani kuwasaidia kuwashinda Waarabu waliokuwa wakiwachinja. Hapo ndipo tatizo linapoanza na hicho ndicho kielelezo au kiashirio cha uzushi unaobatizwa kuwa ‘historia ya nyumbani'.

Kwenye makala yake ya mwisho juu ya kadhia ya Okello, Mihangwa amemalizia kwa kuibua maswali muhimu kuhusu uhasama mkubwa uliojitokeza upande wa baadhi ya wakuu wa ASP dhidi ya Makomredi, yaani wafuasi wa Abdulrahman Babu na chama cha Umma Party.

Hii ni mada nzito lakini lazima tuigusie. Hali ya kutoaminiana kati ya Makomredi na wakereketwa wa ASP imekuwepo wakati wote chini kwa chini tangu kilipoundwa chama cha Umma Party mwaka 1963.

Juu ya kuwepo hali hiyo ilibidi pia wakati ule pawepo na aina ya ushirikiano kati yao katika kukabiliana na wapinzani wao yaani vyama vya Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and Pemba Peoples' Party.

Haja hiyo ndiyo iliyopelekea pawepo umoja uliovishirikisha vyama vya ASP na Umma, vyama vya wafanyakazi pamoja na Jumuiya ya Wanafunzi.

Kiini cha kuwepo hali hiyo ya kutoaminiana ni ule msimamo wa itikadi ya kikabila wa takriban viongozi wote wa ASP wa kuwaepuka kisiasa Wazanzibari wenye asili ya kiarabu sembuse waliotokana na damu ya Hizbu. Mtazamo huu wa aina ya ‘kikaburu' ndio uliokuwa msimamo na unaendelea hivyo hadi leo kwa upande wa wahafidhina wa iliyokuwa ASP.

Wabara wasioitakia kheri Zanzibar wamekuwa wakiipalilia moto hali hii iliwaweze kuidhibiti Zanzibar kwa maslahi yao. Kwa hiyo dhana ya Umma Party ya kuyasuka Mapinduzi ili yawe na mtazamo wa kitabaka pekee badala ya ‘ugozi' (ubaguzi wa kikabila na wa rangi) ilisambaratishwa muda wote tangu kuanzia miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1960 na akina Othman Sharif, Jamal Ramadhan Nasib na Mdungi Usi.

Baadaye usambaratishaji huo uliendelezwa na wanapinduzi kina Seif Bakari, Abdalla Said Natepe na kaumu yote ya ile ijulikanayo kama ‘Kamati ya Watu 14.' Hao ndio waliomshinikiza Sheikh Karume kutowashirikisha Makomredi kwenye uongozi wa nchi.

Siku zote walikuwa wakimtisha Mzee Karume kuwa Makomredi walikuwa na njama na jamaa zao Wakiarabu za kuutokomeza utawala wa Waafrika. Hatimaye walifaulu pale Karume alipowatimua kutoka kwenye serikali kina Badawi Qullateinna Ali Sultan na kubwa lao Babu kudondoshwa na Julius Nyerere.

Kuna siku ambapo Brigadia Yusuf Himidi aliwasikitia baadhi ya wafuasi wa Umma Party waliokuwa naye kwa kuwaambia: "Eh jamaa fitna nyingi zimepita kutugombanisha." Hakumtaja mtu lakini ilikuwa wazi kwamba mafatani walikuwa baadhi ya wahafidhina wa ASP.

Tatizo kubwa la Zanzibar ni kwa Wazanzibari kukubali kuhadaiwa na wanasiasa uchwara kuendelea kuwa wafungwa wa historia ya kisiasa iliyoigawa jamii katika makundi ya kikabila na kinasaba.

Jukumu linalotukabili sasa ni namna ya kutafuta njia za kuuyayusha urathi huu muovu unaoigawa jamii ya Wazanzibari na unaoutia sumu ufahamu au utambuzi wa pamoja wa Wazanzibari.

Okello alifurushwa Zanzibar kwa sababu alikuwa akileta matatizo. Alikuwa ni adha lakini hakuwa kitisho cha kisiasa. Angelikuwa ni kitisho cha kisiasa basi isingekuwa rahisi kumng'oa nchini kama alivyotolewa.

Wala si peke yake kati ya wageni waliokuwa wakifanya fujo aliyefukuzwa Zanzibar. Mwengine alikuwa Engine kutoka Kenya. Naye pia alitimuliwa baada ya kukamatwa huko Maruhubi, kwa amri ya Sheikh Karume, na kikundi cha Makomredi wakiongozwa na Ali Mshangama.

Mwengine aliyekuwa akiitwa Mfarinyaki alikamatwa Chwaka na Komredi Hamed Hilal aliyempeleka gerezani Kiinua Miguu. Amri za kukamatwa Mfarinyaki aliitoa Yusuf Himidi akiwa mkuu wa jeshi. Kwa nini hajawahusisha wanajeshi wengine na wapinduzi wa ASP, haijulikani. Labda Yusuf Himidi alikwishang'amua kwamba wenzake walikosa nidhamu, wakijihusisha zaidi na wizi wa ngawira, wakati Makomredi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Hatujui pia kwa nini Karume alihiyari kuwatumia Makomredi kuwatimua akina Okello, Engine na wapinduzi wengine waliokuwa si wenyeji wa Zanzibar.

Yumkini Karume aliamua kuwatumia Makomredi kumfukuza Okello badala ya kuwahusisha akina Said Washoto, Mohamed Abdalla Kaujore, Seif Bakari, Khamis Darwesh na wengine wa Kamati ya Watu 14 kwa sababu alihisi wangelisitasita na pengine kuibua mgogoro. Said Abdallah Natepe aliwahi kuhadithia kwamba waliwahi kumjadili Okello miongoni mwao na hata pakatolewa wazo la kumuua.

Sheikh Aboud Jumbe amekiri kwenye kitabu chake ‘The Part-nership' kuwa alikuwa hawajui na hakupata kuwaona baadhi ya waliokuwemo kwenye Kamati ya Watu 14, wakiwa pamoja na Okello.

Nakiri kwamba ni taabu kuamini ya kuwa Okello aliibuka ghafla Raha Leo kutoka halaiki ya watu waliokuwa wamekusanyika hapo. Lakini pia tuna uhakika kwamba Okello hakuwa na uwezo wala heshima anayobandikwa nayo na Mihangwa.

Hatusemi hivi kwa sababu Okello hakuwa Mzanzibari. Tunasema hivi kwa sababu huo ni ukweli huku tukikubali kwamba kuna haja ya kuiangalia upya nafasi yake Okello katika mchakato mzima wa maandalizi ya Mapinduzi.

Nimalizie kwa kukumbusha jingine. Nalo ni kwamba kadhia niliyoieleza ya kutimuliwa Okello kutoka Zanzibar haikuwa ya mwanzo ya kufukuzwa Okello. Mara ya kwanza alifukuziwa kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kusindikizwa hadi Nairobi na Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika.
___________________________________________________________
Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 4 Aprili 2012 chini ya kichwa cha habari "Maruhani hawakupindua Zanzibar".
 
Kichangan

Member
Sep 3, 2013
36
0
Wambie kakke ila hiyo sio historia ya mapinduzi okelo hajapindua aliepindua ni ZPPP na Nyerere hawo wengine ni washirikishwaj tu
 
kajirita

JF-Expert Member
Jul 27, 2013
1,575
1,225
Wakuu,
Kwanza nimefurahi sana kuisoma habari hii siku chache kabla ya sikukuu ya mapinduzi kuwadia.

Nimesikitishwa sana na negative comments dhidi ya John Gidion Okello,wala sijawahi kusikia popote pale katika historia jamii Fulani inayosema mabaya kwa mtu au kundi lililowasaidia kufanya na kufanikisha mapinduzi matukufu.
Hii inaonyesha ni jinsi gani baadhi ya watu wa Zanzibar walivyokosa shukrani kwa yote aliyowatendea mwanamapinduzi huyu!Eti wengine wanafika mahala wanasema alikuwa mganda hivyo hakuwa na chake baada ya mapinduzi!?Ni nani asiyejua idadi kubwa ya wazanzibar ni zao la watumwa kutoka nje ya Zanzibar na walikuja Zanzibar kutoka sehemu mbalimbali za bara(ikiwemo Karume)?Ni nani anayeweza kusema Zanzibar ni ya kwao ikiwa hata Sultani alivyokuja Zanzibar hakukuta mwenyeji?Huu ni ubaguzi wa hali ya juu kabisa kutokea!Sio mzungu ,sio muarabu ni muafrika mwenzenu halafu anafukuzwa kama mbwa!

Labda tujiulize maswali kadhaa kabla ya kutoa conclusive arguments!

Je,ni vipi John Okello alipata nguvu ya kuunda baraza la kwanza la mawaziri baada ya mapinduzi?

Je,ni kwa nini John Okello ndio alikuwa akitoa hotuba pale Raha leo baada ya mapinduzi matukufu?

Je,ni kwa nini yeye ndie aliyemchagua rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Karume alipokimbilia Dar es Salaam siku yalipotokea mapinduzi hayo labda kwa kuogopa au kwenda kumpa taarifa JK Nyerere(kama alivyodai) na kumuita kwa mamlaka "popote ulipo urudi kuchukua nafasi yako ya urais"?

Je,ni kwa nini kwenye hotuba ya kwanza ya Mzee Karume alisema wazanzibar wamtambue John Okelo kama mtu muhimu sana aliyesaidia kufanyika na kufanikisha kwa mapinduzi hayo(rejea records)?

Ukijaribu kusoma kitabu cha John Okello kiitwacho Revolution in Zanzibar, anadai kuna vitisho kadha wa kadha alivyopata kupitia barua iliyoandikwa kwa kiswahili ambavyo anaamini vilitoka ZNP kumtuhumu kuwa ana siku chache madarakani !

Kwa mfano tarehe 24 Januari 1964, Okello alipata ujumbe uliosomeka(nanukuu) “Field Marshal John Okello, your behaviors is inconsistent with the requirement of the indigenous people. You are the only person boasting of having the power in the revolutionary government. You must realize that, you do not belong to the Muslim religion and you are leading Muslims even though you are a Christian. Also your activities led to the death of many people in the Island most of whom are Muslims. So start counting your days for a time will come when Muslims will unite to expel you from the Island”

Na pia tarehe 8 Februari 1964 alipata ujumbe unaosema(nanukuu) “Field Marshal John Okello we are telling you that, you will not last for ever on this Island. You will soon find yourself outside and unable to return. Remember Karume himself is a Muslim and you may be certain he loved the Arabs killed during the Revolution more than he loves you”.

Kwa hiyo ukijaribu kuiangalia hii issue kwa jicho la tatu unagundua kuwa Okello alifukuzwa Zanzibar kwa sababu Mzee Karume aliona ni tishio kwa utawala wake!Na njia nyepesi kuitumia ilikuwa ni dini ya Okello na u-Uganda wake!Hakukumbuka tena kuwa huyo ndiye mtu aliyempa madaraka baada ya mapinduzi na hayo hayakupaswa kuwa malipo yake!

Huwa ninashangaa sana hivi huwa mnajisikiaje hasa mnapomtaja mtu ambaye hakushiriki hata kwenye mapinduzi hayo(Abeid Karume) kuwa ndiye aliyefanikisha mapinduzi hayo?Huu ni uposhaji wa hali ya juu!Umefika wakati sasa wa kumkumbuka mwanamapinduzi huyu kama ndiye aliyefanikisha mapinduzi matukufu ya Zanzibar na kutomkumbuka ni sawa na kuipotosha historia nzima ya Zanzibar.

Asante sana
 
gombesugu

JF-Expert Member
Apr 4, 2013
1,485
0
kumbe ndiyo ilivyokuwa ? Je huyu OKELLO anapewa heshima anayostahili kweli ?

Mkuu,

Kutaka kumpa hishma huyo maluuni muuaji,haramia Okello...itakuwa si tafauti tu na wale Neo-Nazis wanavyomuabudu Shetani Hitler!

Pana khabar za uhakika ziliwahi kuletwa humu-JF na Mag3 nafikiri,yakuwa family ya yule muuaji haramia Kenge Okello...hvi sasa inaishi kwa taabu ilokubuhu,madhila,njaa kubwa mno na maradhi yalowasheheni...yaani wapo mwituni/vichakani wanaishia kula matunda kama ndege maskini!? Dah!

Ahsanta.
 
gombesugu

JF-Expert Member
Apr 4, 2013
1,485
0
kajirita,
Naona umemwaga povu jingi mno,lakini bakhti mbaya yaani kwa kusoma kitabu kimoja tu cha Huyo muuaji,haramia kenge aso fadhila Okello!? Duh! Teeh! Teeh! Teeh!

Hivi pana ushahidi upi yakinifu yakuwa yale maneno/maandishi mle kitabuni yaliandikwa na haramia Okello mwenyewe!?...bila hata chembe ya upotoshwaji wa hali khalis wakti huo!?

Hivi unafahmu yakuwa huyo Okello wenu alojiita ati "Field Marshal" katika moja ya vituko vyake vingi mno...alikua hajui hata kusoma wala kuandika/Illiterate!? Yaani kama sisi watoto wa Madrassa! Dah! Teeh! Teeh! Teeh!

Sasa embu jiulize madhumuni/lengo la huyo Mwandishi khalis wa hicho kitabu,nani walokua ndo wadhamini wa hicho kitabu,na pia nini malengo yao au ulokua msukumo wao/nafasi zao katika ile Zanzibary and/or Afrikan Politics as a whole!?

Nafikiri wafahamu yakuwa yule pundaka Okello...yaani alikua ni fundi mchundo,mpanga/mchoma matofali,tena kwa hao hao muwaitao ati "Waarabu" mnaowachukia nyinyi na pia mpiga lipu!

Yaani kwa kifupi shughuli zake zalikua hazina tafauti asilan na za kama yule Yeriko Yohana Msambila ajiitae pia ati ndo Yericko Nyerere! Dah!

Sasa kwa kuwa labda wewe ndo "msomi" wa hali ya juu,embu jiulize japo kiduchu...mtu mchovu wa maisha kama yule Yeriko,anawezaje hata ati hata kuthubutu kupanga/kuratibu na kuleta Mapinduzi japo kwenye kijiji,Tarafa au Wilaya,sembuse Taifa/nchi nzima!? Duh! Hapa nakhis jibule ni kwamba hili haliwezakani,asilan abadan! Teeh! Teeh! Teeh!

Sasa kwa mfano huo mwepesi kwako hapo juu,ndo yalazimu turejee kwenye masuali "magumu" japo kiduchu!

Ni akina nani khasa walokua waandalizi/waratibu,wadhamini wa mipango ya mauaji/"mapinduzi" yale ya 1964!?

Je ni kweli malengo na madhumuni yao ilikua ni kwa manufaa ya Zanzibar/Wazanzibary woote bila ya kujali urangi,dini,ukabila,na tafauti zao za kisiasa!?

Nafahamu fika,wewe binafsi huna majibu yoyote ya maana utakayoleta...lakini siku hizi "nshazoea" kiduchu,maana ndo "mambo ya JF" haya,au sio Mkuu!? Teeh! Teeh! Teeh!

Ahsanta.
 
Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom