Mambo nyeti kuzingatiwa majadiliano ya gesi

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
Na Mwandishi Wetu

NI miaka kadhaa imepita kutoka majadiliano ya uchakataji wa gesi nchini Tanzania yaanze. Mara kadhaa majadiliano hayo yamesitishwa kutokana na makampuni ya kimataifa ya nishati kuwa na matakwa hasi kwa maslahi ya nchi.

Kila kukicha makampuni ya kimataifa ya nishati yamekuwa yakibadilisha mbinu na kuleta masharti mapya ili mradi malengo yao ya kutorosha faida yafanikiwe. Mbinu hizi zimetumika katika nchi mbalimbali na kulalamikiwa sana.

Bahati nzuri Tanzania inafanya majadiliano wakati nchi kadhaa zimepata mafunzo kutokana na matokeo hasi yaliyotokea kwa kutozingatia namna bora ya kulinda maslahi ya nchi.

Pia nchi nyingine zililazimika kutunga sheria ili kudhibiti masharti hasi katika mikataba ya gesi. Mifano halisi ni Pamoja nan chi za Algeria,Angola, Uganda, Ghana, Trinidad na Tobago, Azerbaijan, Kazakhstan na Peru. Nyingine ni Urusi, Malaysia, Brazil India, Guyana na Msumbiji.

Kwa kiwango kikubwa Indonesia ni nchi iliyolazimika kuchukua misimamo mikali katika kutengeneza mikataba ya mafuta na gesi (PSAs). Kuna nchi ambazo tayari zina nguvu sana katika majadiliano ya mikataba hiyo kama Qatar, Iran na Saudi Arabia. Hivyo kuna mifano lukuki ya kujifunza namna ya kupambana na mbinu ninazotumiwa na makampuni ya kimataifa ya nishati katika majadiliano ya mikataba.

Ningependa kujadili mbinu kadhaa ambazo Serikali inapaswa kuziwekea wigo wa kuzizuia. Benki Kuu ya Urusi ililazimika kutoa andiko la vitu vinavyotakiwa kuangaliwa kama tahadhari. Indonesia ina sheria mahsusi ya kudhibiti mikataba ya aina hii. Vilevile Algeria.

Mambo ambayo makampuni ya kimataifa ya nishati yamekuwa yakidai na kuyatumia kujipatia faida kubwa na kuzinyima nchi zenye rasilimali hiyo kufaidi mgao halali wa faida ni kama ifuatavyo-

Kuondoa Matumizi ya Sheria za Nchi Mwenyeji

Makampuni ya kimataifa ya nishati hupenda kudai yasiwe chini ya sheria za nchi ambako miradi inaanzishwa. Hutaka zitungwe sheria ya pekee ili yasiwajibike kwa mamlaka zozote ndani ya nchi.

Sheria ya Mradi au “Project Law” hudai zitungwe ili kuondoa matumizi ya sheria za nchi, kwa mfano, sheria za uhamiaji, kodi, forodha, ulinzi na usalama, ardhi, na kadhalika.

Bahati nzuri, ukiacha Western Australia, nchi nyingi zimekataa matumizi ya sheria za mradi. Sheria hizi zinakinzana na “sovereignty” ya nchi na zinadhalilisha kwa kuwa ni tamko kuwa sheria za nchi hazina ubora na siyo za haki. Hayo ni matusi kwa nchi huru.

Kupinga Mamlaka za Udhibiti za Nchi

Makampuni haya pia hudai mamlaka za udhibiti zisiwe na madaraka juu ya mradi. Kwa mfano mamlaka inayosimamia sekta ya petroli, mamlaka za kodi, mamlaka zinazosimamia fedha za kigeni, mamlaka za forodha, na kadhalika. Hudai uhuru wa kujisimamia wenyewe. Hii inawawezesha kuinyima Serikali taarifa mbalimbali muhimu na kudhibiti mwenendo wa utekelezaji mradi hata pale ambapo ni dhahiri kuwa mradi unaweza kuwa na athari kubwa kwa nchi kama uharibiwa wa mazingira, uchumi, afya na usalama wa raia, na hata kuwanyima wazawa fursa za kiuchumi.

Kuna wakati wamediriki hata kudai kuwa wafanyakazi wao wa kigeni wasidhibitiwe na vyombo vya usalama eti kwa sababu havina ubora wa kutenda haki. Kutaka Maeneo ya Mradi yawena Hadhi ya Nchi ndani ya Nchi

Makampuni ya kimataifa ya nishati katika nchi mbalimbali yamekuwa yakidai yapewe umiliki usio na ukomo wa maeneo ya mradi na yapewe uwezo wa kufanya lolote katika maeneo hayo bila udhibiti wa Serikali.

Kwa mfano, hupenda masuala ya ulinzi na usalama yawe chini yao ambapo mamlaka za nchi haziwezi kuingia maeneo hayo bila ruhusa yao hata kama kuna taarifa kuwa kuna uvunjaji wa sheria za nchi. Hii inalenga kutengeneza nchi ndani ya nchi na kudhalilisha utaifa wa nchi.

Usiwe chanzo cha mapato kwa Serikali Imekuwa ni kawaida kwa makampuni ya kimataifa ya nishati kutotaka kulipa kodi, mrabaha au kuwepo na mgawayo wa haki wa faida na mapato ya mradi.

Kutotumia taasisi za fedha za ndani

Makampuni ya kimataifa ya nishati hupenda kutoa sababu mbalimbali ili yaruhusiwe kutunza fedha zinazopatikana kutokana na mauzo zitunzwe nje ya nchi.

Lengo ni kuzinyima fursa benki za ndani ya nchi kupata fedha za kigeni. Pia ni kuinyima nchi haki ya kuongea akiba ya fedha za kigeni. Hivyo mradi uliopo Tanzania hutumika kujenga akiba ya fedha za kigeni kwa nchi nyingine hasa “tax havens”.

Mara nyingi hutolewa shutuma zisizo na msingi kuwa serikali katika nchi zinazoendelea ni kigeugeu na hazipaswi kuaminika. Hii ni Pamoja na ukweli kuwa kuna kampuni kubwa za nje zenye uwekezaji ndani ya nchi na ambazo hazijadhurika na shutuma zinazotolewa. Ni kawaida kwa kampuni za kimataifa za nishati kuonyesha dharau kubwa kwa Serikali na mifumo ya nchi.

Fedha zinazotengwa

Ni kawaida kwa makampuni ya madini, mafuta na gesi kutakiwa kudunduliza fedha kwa ajili ya kurekebisha mazingira pindi mradi unapokoma.

Hili ni takwa la kisheria ili mradi unapokoma Serikali iwe na uhakika kuwa fedha za kutosha zimetengwa kurekebisha mazingira na kwamba kampuni husika haiwezi kutoroka bila kutekeleza jukumu hilo.

Makampuni ya kimataifa ya nishati yamekuwa yakisisitiza kuwa fedha zinazotengwa zisihifadhiwe ndani ya nchi. Kuna malengo kadhaa ya kusisitiza hivyo. Moja ni kuyawezesha kutoroka bila kutekeleza jukumu hilo.

Kuna nchi ambako makampuni hayo yametumia viongozi wasio waadilifu kutekeleza lengo hilo ovu. Pili, ni kutaka kuinyima Serikali fursa ya kuweka fedha hiyo katika uwekezaje salama ili kukuza mfuko maalum wa kurekebisha mazingira.

Kwa vile fedha hizo huwekwa katika fedha za kigeni na huhifadhiwa kwa miaka mingi ifikayo 30 mpaka 50, hutoa fursa nzuri ya kukuza akiba ya fedha za kigeni nchini.

Tatu, makampuni hayo yanataka yaachiwe fedha hizo kwa uwekezaji wao nje ya nchi. Ni dhahiri kuwa hizo ni fedha ambazo zinapaswa kuwepo katika mikono ya Serikali ili zitumike pindi mradi unapokoma bila kuwepo na uwezekano wa makampuni hayo kutoroka.

Mfumo wa kugawana faida

Imekuwa ni utamaduni toka miaka ya 1950 kuwa mikataba ya ubia katika uchimbaji mafuta na gesi, yaani, “Production Sharing Agreements” huwa katika misingi muhimu inayohusisha kuwepo kwa mafuta ya kulipa mrabaha; mafuta ya kulipa gharama za mradi, yaani, “cost oil”; mafuta ya kugawana faida, yaani, “profit oil”.

Ina maana kuwa mradi wenyewe hujilipia gharama na mrabaha, halafu wabia hugawana faida kwa kugawana mafuta ili kila mbia akauze anakotaka. Hii huzuia mmoja wa wabia au kundi la wabia kubandika gharama ili kufuta faida na kuzuia mgawanyo wa faida.

Hivi karibuni makampuni haya yameanza kubadili mfumo wa mgawanyo kwa kutaka mgawanyo ufanyike baada ya mauzo na pia kwa vigezo ambavyo ni hasi kama matumizi ya “internal rate of return”, “netback value” na vigezo vingine ambavyo vinahamisha faida kwenda kwao na kuiacha Serikali isiwe na mgao kabisa au ipate mgao kiduchu. Hivi ni vigezo ambavyo nchi nyingi vimekataa, kwa mfano Algeria.

Athari za Kibiashara kwa Serikali

Katika miradi ya mafuta na gesi athari za kibiashara lazima zibebwe na yule anayefanya ile biashara. Moja ya athari kubwa ni bei ya mafuta na gesi kushuka. Kama mgawanyo wa mafuta unafanyika ipasavyo kila anayeenda kuuza sokoni lazima abebe athari zake.

Serikali haipaswi kubebeshwa athari hizo kwa namna yoyote ile. Moja ya njia zinazotumika kuibebesha Serikali mzigo ni pale makampuni haya yanapopendekeza kuinyima Serikali mgao kwa kubadilisha mfumo wa mgawanyo, kutaka kusiwepo mgawanyo wa mafuta badala yake mapato ya mauzo yatumike kama kigezo baada ya kufidia gharama na wakati mwingine kutaka Serikali isipata mgao pindi bei inashuka sokoni, ikiwemo kutokusanya kodi.

Kuhusu mrabaha

Mrahaba siyo kodi na siyo sehemu za gharama za uendeshaji wa mradi. Haya ni malipo ya kuruhusiwa kuvuna maliasili kama mafuta, gesi, madini na nyinginezo.

Hulipwa kwa Serikali kama asilimia ya thamani ya maliasili iliyovunwa. Baada ya hapo hufanyika mgawanyo wa mafuta au gesi ya kulipia gharama yaani “cost gas” na gesi ya mgawanyo wa faida, yaani “profit gas”.

Makampuni haya huwa yanataka mrabaha utambulike kama moja ya gharama za uendeshaji mradi ili kupunguza pato la Serikali litokanalo na ukusanyaji kodi. Katika mfumo ambao mrabaha sio kodi na haukusanywi kwa misingi ya kikodi kama ilivyo nchini Tanzania, madai hayo hayana msingi. Mfumo huu hutambulika kimataifa na hukubalika isipokuwa pale tu ambapo mrabaha ni sehemu ya mfumo wa kodi. Hata hivyo, wabia wan je hawawezi kutaka mrabaha utumike kukokotoa kodi wanazopaswa kulipa kwa sababu sio wao ambao hulipa mrabaha.

Kuminya ushiriki wa serikali

Miradi ya mafuta na gesi hutegemea sana fedha za utekelezaji kupatikana kutoka kwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa hizo duniani.

Serikali huwezesha hilo kufanyika kwa kutoa leseni kwa ubia wa uchimbaji ambayo hutolewa kwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta au Gesi, yaani, “National Oil Company” au kifupi NOC. Kwa hiyo mwenye mali katika mradi huo ni NOC kwa niaba ya Serikali.

Makampuni ya kimataifa ya nishati mara nyingi hayataki kutambua kuwa hisa za Serikali na NOC zipo pia katika kuruhusu mali yake iwezeshe kupata fedha za uwekezaji. Hudai kuwa Serikali lazima iwekeze fedha taslimu kwenye mradi.

Kwa kuwa Serikali huwa haina fedha za uwekezaji ambazo hufanywa kuwa nyingi sana na waliobuni mradi ili Serikali ishindwe huwa kunakuwa na majadiliano ya Serikali kumiliki hisa ambazo zitalipiwa kadiri rasilimali inavyovunwa na yenyewe kupata gawio la “profit oil/gas”. Makampuni haya hutaka kuweka masharti magumu na onevu ili kuminya ushiriki wa Serikali katika mradi japokuwa kwa kawaida mwenye hisa nyingi ni NOC na Serikali kwa pamoja.

Gesi yote iuzwe nje ya nchi

Kumekuwa na tabia ya makampuni ya kimataifa ya nishati kutaka mafuta au gesi yote inayopatikana iuzwe nje ya nchi bila kuangalia mahitaji ya matumizi ya ndani ya nchi.

Hii mara nyingi huleta migongano na mwenye mali ambaye ni Serikali ambayo pia ina mipango yake ya matumizi ya mafuta na gesi ili kukuza uchumi. Serikali ina haki ya kupata gawio la mafuta na gesi na kuamua namna ya kuitumia.

Ni kawaida kwa mikataba hii kuweka viwango vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya gesi ndani ya nchi pamoja na ukanda ilimo nchi kama vile Afrika Mashariki.

Haya ni baadhi tu ya mambo ya kuzingatiwa kutokana na mafunzo yanayopatikana kutoka nchi ambazo zimekuwa na mikataba ya aina hiyo. Ni muhimu kwa Serikali kupitia timu ya majadiliano kuhakikisha nchi haipotezi maslahi yake kwa kuachia makampuni ya kimataifa ya nishati kupenyeza masharti hasi katika mikataba inayojadiliwa.

Endapo kuna masharti ambayo ni muhimu yakubalike basi kuwepo na makubaliano thabiti ya tahadhari, yaani, “safeguards” ili kuzuia masharti hayo kutokutumika visivyo na kuiletea nchi athari.

Kwa vile mikataba hii imefanyika sehemu nyingi duniani nchi yetu haipaswi kugundua upya gurudumu. Ni vizuri kuwa imara ili kutokubali vitisho vitumike kuingia katika mikataba yenye athari badala ya kujadili kwa kina faida na athari ya kila linalopendekezwa

*Source: Raia Mwema la Jumatano hii, Toleo namba 1224; Machi 27– Aprili 2, 2024*t
IMG-20240327-WA0013.jpg
 
Back
Top Bottom