Mama Yangu Adui Yangu -29-
ILIPOISHIA:
Maneno aliyosema mganga na aliyosema Beka yanafanana lazima niseme ukweli nimechanganyikiwa sana ninaposhindwa kumjua mbaya wangu.
Mdogo wangu yote hayo yataisha, kwanza mshukuru Mungu umeachwa na Beka lakini hivi sasa una maisha mazuri. Wengine wakiharibikiwa huwa wanachanganyikiwa na kukata tamaa ya maisha kwani huwa wanaandamwa na mikosi.
Mmh! Sawa.
Basi usiyape sana nafasi mawazo yanayoumiza, sisi tusingekuwa hapa.
Lakini nani kanifanyia hivi?
Mwaija hebu kwanza kaoge ili tuwahi kwa mganga.
SASA ENDELEA...
Sawa.
Nilinyanyuka kitandani na kwenda kuoga harakaharaka na kutoka kumuwahi da Suzy. Sikutaka hata kufungua kinywa kwa vile nilikuwa nyuma ya muda tuliokubaliana kufika kwa mganga.
Dada chai tayari, msichana wa kazi alinishtua aliponiona naondoka bila ya kufungua kinywa.
Mmh! Mdogo wangu kuna sehemu nimechelewa nitakunywa nikirudi.
Sawa dada lakini ungekunywa hata nusu kikombe cha maziwa ya moto?
Nisamehe mpenzi nimechelewa sana.
Sawa dada.
Nilitoka hadi barabarani na kukodi teksi mpaka Changombe kwa Da Suzy, niliyempitia kuelekea kwa mtaalam Mbagala Maji Matitu. Kabla ya kufika tulisimama sehemu na kununua doti mbili za kanga mpya nilizoagizwa na mganga.
Tulipokelewa na mganga aliyekuwa na wateja wengi zaidi ya jana yake.
Nilijikuta nikijawa na mawazo mengi kichwani na kujiuliza uwepo wa watu wengi pale ulitokana na nini!.
Nilipomuuliza da Suzy aliniambia ukiona watu wengi ujue ni ubora wa tiba zake umewavuta.
Yule dada alipotuona alitukaribisha kwa furaha kwani siku zote uso wake ulijaa ucheshi. Baada ya kutukaribisha mganga alituchukua na kutupeleka katika chumba kimoja kilichokuwa kimejengwa peke yake ndani ya uzio wa nyumba yake na kutueleza:
Jamani nisubirini hapa kila kitu nimekiandaa kwa kazi yenu. Ngoja nikaandae kisha nitawaita.
Hakuna tatizo.
Mganga aliondoka na kutuacha tukiwa tumekaa kwenye kochi la mbao lililokuwa halina mito tulilolikuta nyuma ya nyumba.
Baada ya muda aliniita, nikaingia ndani ambapo yule mganga aliniambia niingie chumbani.
Nilipoingia alinieleza nivue nguo zote kisha nijifunge upande mmoja wa kanga na mwingine nijifunge kichwani kama kilemba.
Baada ya kufanya hivyo, alinipeleka kwenye bafu lililokuwa pale uani na kunieleza nikae kwenye stuli.
Pembeni ya stuli kulikuwa na beseni lililokuwa na maji na kamba za ukindu saba zilizofungwa na dawa ya unga kama aliyonipa jana yake nikaweke kwenye maji ya kuoga.
Tukiwa bafuni, alisimama nyuma yangu na kunishika katikati ya kichwa na kuzungumza maneno anayojua, lakini yote yakiwa kumuomba Mungu kunifungua katika matatizo yangu na kuisafisha nyota yangu iliyofifia.
Nyota yangu Ilikuwa imeingia ukungu na kushindwa kutoa mwanga wake halisi.
Baada ya kusema kwa muda maneno hayo, alitoa mkono kichwani mwangu na kunimwagia maji kwa kutumia kata kuanzia kichwani huku akisema maneno kisha mikononi na kumalizia miguuni.
Alinimwagia juu ya kanga niliyokuwa nimejifunika kisha mwili wote.
Baada ya kunimwagia maji mwili mzima kwa kumwagia juu ya kanga nilizojifunga aliiondoa kanga ya kichwani na kuchukua ukindu mmojammoja uliofungwa na kuzungusha kwenye mikono na kuufyatua.
Alifanya vile kwa sehemu za viungo vya mwili ambavyo wanasema ndimo watu wanatumia kuingiza uchawi wao kama kwenye magoti, kifuani na kiunoni.
Kufungua kamba za ukindu alikuwa akifungua vifungo mwilini mwangu. Baada kumaliza zoezi lile alinieleza nioge maji yaliyobaki mwili mzima bila nguo kisha yeye alitoka nje.
Niliondoa nguo mwilini na kuoga mwili nzima, wakati huo alikuwa amekwenda ndani kisha alirudi akiwa na kanga nyingine mpya na kunieleza nikimaliza nivae zile na nilizoogea alinieleza nizianike bila kuzikamua.
Nilifanya kama alivyonieleza na kutoka nje nikiwa nimejifunga kanga mpya, kisha niliingia kilingeni. Nilielezwa nivae nguo zangu.
Nilifanya vile na kukaa kwenye mkeka na kupata dua, nilipewa makombe ya kunywa na kuoga kwa siku tatu na miti ya kuchemsha kwa ajili ya kukifungua kizazi na dawa ya kunawa kabla ya kukutana na mwenzangu.
Nilitoa kiasi alichonieleza huku nikimuahidi nikishika ujauzito nitampa zawadi kubwa sana.
Mdogo wangu tumuombe Mungu kila kitu kitakwenda vizuri.
Niliagana na mganga na kumpitia da Suzy aliyekuwa bado nyuma ya nyumba ameegemea ukutani na kushikwa na usingizi.
Da Suzy, nilimwita huku nikimtikisa.
Abee, vipi tayari? alishtuka usingizini na kufikicha macho huku akipiga miayo.
Ndiyo twende zetu.
Mmh! Usingizi ulianza kuninyemelea.
Basi twende zetu.
Mmh! alinyanyuka na kujinyoosha kisha akasema:
Acha nikamuage mama Amina, mama Amina lilikuwa jina la mganga.
Kabla hatujaenda mgang alikuja na kusema alisahau kitu.
Samahani kuna kitu muhimu nilitaka kukisahau kukuelezea.
Kitu gani? Nilimuuliza.
Ukishika ujauzito njoo mara moja tufunge ili usiweze kutoka.
Sawa dada nimekuelewa nitafanya hivyo.
Tuliagana na mganga na kwenda kutafuta usafiri. Kwa vile tulikuwa hatujala tulitafuta sehemu ya kupata kifungua kinywa kisha nilimpeleka da Suzy kwake na kurudi zangu kwangu.
Kutokana na uchovu nilipofika nyumbani nilipanda kitandani na usingizi mzito ulinichukua.
***
Nilitumia zile dawa kwa siku tatu kwa umakini mkubwa na kumaliza. Baada ya kumaliza kutumia makombe na dawa za kunywa nilikaa kusubiri matokeo ya dawa zile japokuwa sikuwa na uhakika wa kushika ujauzito kama nilivyoahidiwa na mganga.
Baada ya siku nne mzee Sambi alirudi, niliamini ule ulikuwa muda muhimu kutega mtoto.
Usiku kabla ya kukutana naye, nilifanya kama nilivyoelekezwa na mganga.
Nilifanya vile kisha tulikutana na mwenzangu, niliendelea kufanya zoezi hilo kwa wiki nzima huku nikiwa na matumaini madogo ya kushika ujauzito.
Mwezi ulikatika huku duka langu likiwa tayari limejazwa vitu vyote vya muhimu na kuanza kulifanyia matangazo kwenye magazeti na kwenye baadhi ya redio.
***
Kupitiliza kuziona siku zangu kulinishtua lakini bado sikuamini kwa kuwa hali kama hiyo ilishawahi kunitokea hata nilipokuwa na mume wangu kwa kupitiliza miezi miwili, lakini mwezi wa tatu niliziona siku zangu na ziliendelea kama kawaida.
Mabadiliko ya hali yangu yalinishtua kidogo, nilimweleza mwenzangu ambaye alinishauri twende hospitali kuangalia afya yangu.
Tulikwenda kufanya vipimo, baada ya daktari kuangalia majibu alisema:
Vipimo vinaonesha upo sawa, ila...
Alishusha pumzi na kututazama usoni na kutabasamu kitu kilichonifanya nijiulize mbona anatabasamu ameona nini.
Ila nini dokta...? mzee Sambi aliuliza wakati huo nilikuwa nimemuegemea begani.
Hongereni.
Itaendelea Jumamosi ijayo....