Mama UZA UZA: Nyumbani tuna kilio, msiba umetufika

Father of All

JF-Expert Member
Feb 26, 2012
6,376
6,720

Nyumbani tuna kilio, msiba umetufika,

Twahaha kupiga mbio, jawabu tunalisaka,
Tumepatwa na kilio, kilozungukwa na shaka,
Mama yetu uza uza, mbona kaacha kilio.

Jama sie wakulima, watoto wa Mlamali,
Kwa kila tunachochuma, ghalani huenda fuli,
Hata tunavyovilima, au kuhemea mbali,
Huvitunza kwenye ghala, ili vifae baadaye.


Tuna kunde na ufuta, mbaazi hata nyonyo,
Hugawana tukipata, hugawa bila uchoyo,
Sasa roho zatukuta, kwa hali tuliyo nayo,
Mama anosimamia, ameuza kila kitu.

Walikuja wachuuzi, mama walimhadaa,
Kwa mbinu zile na hizi, walimtia tamaa,
Mama kawa mpuuzi, tokana na mnanaa,
Alifanya uamuzi, vitu vyote ameuza.

Ameuza hata nazi, tena kwa pesa kichele!
Pia na kauza na mbuzi, farasira za mchele,
Aliongea kihunzi, tulipopiga kelele,
Sasa yemeshatukuta, kaka ajiinamia.

Watoto walia njaa, ghalani hamna kitu,
Watu watunyanyapaa, atusema kila mtu,
Kaka wanamkungwaa, kapoteza hata utu,
Jamani yametukuta, wenye bongo zingatia.


Jifunzeni toka kwetu, kwa yale yanotusibu,
Si kila mtu ni mtu, wengi ni sawa na dubu,
Wameuza utu wetu, bure wametusulubu,
Sisi yameshatukuta, weledi tia akili.

Walonunua wacheka, wanatuona majuha,
Wanacho walichotaka, tumeambua fedheha,
Kaya imeshaumbuka, kweli fedha ni fedheha,
Mama yetu uza uza, yupo kajiinamia.

Alikodisha na shamba, kwa bei anayojua,
Mihogo watu wachimba, siye njaa yatuua,
Viazi wanavisomba, na miti imepungua,
Sisi tumeshanyolewa, walobaki tia maji.

Baba alifua chuma, kaka kiwanda kauza,
Hata nyuzi alifuma, pia nacho ameuza,
Lile dimbwi pale nyuma, samaki wanapokuza,
Nalo pia ameuza, tunauziwa samaki!

Lile gari la mizigo, nalo kaka ameuza,
Tulionya kawa mbogo, sasa huyo ajiliza!
Amegeuka mzigo, heshima amepoteza,
Mama yetu uza uza, na yeye amejiuza.

Baba naye marehemu, katangulia kuzimu,
Twatamani kula sumu, tumfuate kuzimu,
Tumpatie salamu, kaka ametudhulumu,
Hatunao umuhimu, na maisha ni magumu.

Kidogo alichochuma, anakula na mkewe,
Tumeambua dhuluma, hatunao mfanowe,
Kwa wakweze anatuma, amridhi mkewe,
Sisi yatuua njaa, Mama yetu ni hasara.

Uskani tumempoka, tumepa mdogowe,
Yupo anahangaika, auponye uozawe,
Lini tutanusurika, japo na sisi tupoe,
Bora tumuombe Mungu, akatuvushe salama.

Enda kwa walokodisha, afanya mazungumzo,
Mrabaha kuushusha, lau tupate punguzo,
Ni wagumu si mzaha, nalo bado ni tatizo,
Yule aliyetuuza, eti sasa ajiliza!

Hayo ndiyo masahibu, yake mama uzauza,
Yake mambo ya ajabu, mwenyewe amejiuza,
Hata vipi angetubu, ameisha tuumiza,
Huo ndiyo upuuzi, wa mametu uza uza.

Ardhi tunakodishwa, aliyoiacha baba,
Bure tunalanguliwa, kisa ni akili haba,
Kama si kubinafsishwa, tungeishi kwa haiba,
Jamani tahadharini, mlo nao Uzauza.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom