MAHALI FULANI HUKO BAGAMOYO
PORI LOTE LILIONEKANA TUPU, ni miti ileile ya kila siku ilibaki mahala pake, kutokana na miti hiyo kuwa mbalimbali kiasi iliwezekana kiumbe chochote kutembea bila kupata shida sana. Utulivu na mvumo wa upepo wa wastani vilifanya mlio kama mluzi kila mara, ukipanda na kushuka. Ndege wa porini kama dudumizi na wengine wengi walikuwa wakitoa sauti zao kuashiria jioni imekaribia, wengine walionekana angani wakirudi kwenye viota vyao makundi makundi. Ndani ya pori hili lenye miti mikubwa na midogo na mimea yenye mfano wa kamba kamba ambazo zilitoa upinza kwa binadamu kutembea kwa kuwa si mazingira yake kulikuwamo na watu watatu waliokuwa kama wakitafuta kitu, mwanaume mmoja na wanawake wawili.
“Una uhakika Chiba kuwa ni eneo hili?” Gina akauliza
“Ndio ni eneo hili, maana kila nikiangalia kwenye kifaa change hapa, signal inaishia hapa,” Chiba akajibu wakati huo Daktari Jasmine akiwa ameketi juu ya mzizi wa mti mkubwa. Gina akachukua kile kifaa kutoka katika mkono wa Chiba na kukitazama; juu katika kioo chake kulionekana mchoro kama wa ramani iliyopigwa picha kwa satellite na kitu kama doti nyekundu ilikuwa ikiwakawaka kwa kufifia.
“Mbona hii signal kama inafifia?”
“Betri inkwisha muda si mrefu, kumbuka tangu asubuhi inafanya kazi,” Chiba akajibu na kufungua chupa yake ya maji. Jasho lilikuwa likimtiririka bila mafanikio ya kile anachokitafuta. Jasmine akiwa na begi lake mgongoni lenye vifaa vyake vya kazi alikuwa akisikiliza tu hakujua nini cha kuongea.
“Lakini Chiba, uelekeo ndio huu, tuko sahihi?” Jasmine aliuliza kwa taabu kidogo kutokana na uchovu uliomkabili.
Watu hawa watatu walikuwa katika mapori hayo katikati ya Bagamoyo na Mbegani kwa operesheni maalum ambayo ilikwishawachukua siku mbili katika eneo hilo na isioneshe mafanikio.
“Yaani kiukweli kabisa eneo hasa ni hili, tatizo ni wapi kwa maana signal yangu inaishia hapa na haiendelei kuonesha kama kuna eneo linguine, hatuna budi kupiga kambi hapa na kulala usiku huu,” Chiba aliwaeleza wenzake.
“Ha, nani alale hapa porini?” Jasmine aling’aka huku akiwa kapata nguvu ya kusimama.
“Wote lazima tulale hapa,” Chiba akasisitiza.
“Hakuna kulala hapa ni mpaka tupate jibu na kutoka ndani ya pori hili,” Gina naye akasisitiza kwa kuongezea sentensi nyingine.
“Enhe! Hilo ndilo nilikuwa nalisubiri kwa muda mrefu sana, nilifikiri mmechoka kumbe bado mna nguvu,” Chiba aliwaeleza.
Wakapeana moyo na kuendelea kutafuta humo porini kwenya vichaka na juu ya miti huku jua likichwea na kagiza kuanza kuingia taratibu.
† † †
GIZA LILIKUWA juu ya uso wan chi wakati Gina, Jasmine na Chiba wakiwa wametawanyika kila mtu upande wake, wakiendelea kuwasiliana kwa walkie talkie zao ambazo ziliunganishwa kwa mtambo mdogo uliobebwa katika begi la Gina.
Majira kama ya saa nne usiku hivi ndipo Gina alipoona kitu kilichomshtua.
“Shiiit!” akang’aka na kuwaita wenzake kwa kutumia chombo hicho.
Dakika nne baadae wote waliungana wakimulika eneo hilo na tochi zilizofungwa vichwani mwao, zote tatu zikamulika mahala pale.
“Hii ni simu ya Scoba!” Chiba akawaambia kisha akasimama wima na kuwa kama anayeangalia kitu katika vichaka hivyo huku akihema kwa nguvu.
“Vipi?” Gina akauliza.
“Kwa vyovyote hapa ni eneo la tukio”.
Jasmine akaiokota ile simu kwa mkono wenye gloves na kuiweka ndani ya mfuko wa plastiki kisha wakaanza kupita vichakani polepole huku wakiangalia kwa makini. Saa moja baadae Gina akakutana na kitu kingine, mkufu, wakauokota na kuuweka kwenye mfuko mwingine wa plastiki. Wakati msako huo ukiendelea Gina alikuwa akijawa na machozi lakini alijaribu kujibana asilie kwa sauti, moyo wake ulipoteza matumaini.
Saa sita usiku, ukimya ukiwa mkubwa katika mapori hayo, Jasmine alijikwaa vibaya na kuangukia kitu kama binadamu.
“Oh, Shiit!” akang’aka kwa ukulele huku akijiinua kutoka pale alipoanguka. Kurunzi yake iakamulika mwili wa binadamu uliolala kimya ukiwa na damu iliyoganda katika nguo yake iliyofanana na ovaroli la kijani cha mgomba.
“Scoba! Aiyaaaa!!!” Chiba alijikuta akichanganyikiwa alipouona mwili wa Scoba na kuutambua kwa ile beji yake iliyobanwa katika mkanda wake wa kiunoni. Alikuwa amelala kimya akiwa katapakaa nyasi kila mahali na parachute lake likiwa kando juu ya miti midogo midogo.
Jasmine harakaharaka, akashusha begi lake na kutoa kifaa cha kupima mapigo ya moyo ‘Stethoscope’ na kuipachika masikioni mwake huku tayari Chiba amekwishafungua jaketi la juu la Scoba na kumwacha kifua wazi. Jasmine baada ya kupachika masikioni mwake kile chombo, upande wa pili akauweka juu ya kifua cha Scoba upande wa kushoto na kutulia kimya huku akikihamisha hamisha lakini eneo lile lile. Wote walibaki kimya wakiweka matumaini yao kwa mwanadada huyo daktari. Baada ya kusikiliza kwa makini mkubwa huku akifinya sura na kuiachia akachukua kitu kingine na kumfunga katia kiungo cha sehemu ya juu ya mkono na ile ya chini, kile chombo kilikuwa kama mpira Fulani wenye kitu kama saa upande mmoja, kisha akapachika kile kidubwasha cha kwanza pale upande wa juu wa kiwiko na kufanya kama anajaza upepo kwa kuminyaminya kitufe kingine na mara ule mpira ukajaa upepo na kubana sawia mkono wa Scoba, Jasmine akawa akiangalia kile kitu kama saa huku akiusoma ule mshale wake uliokuwa ukitikisikatikisika huku ukirudi chini. Aliporidhika akauachia ule upepo na kutoa ile mashine.
“Vipi?” Chiba akawahi kuuliza.
“Mzima, ila mapigo ya moyo yako chini sana,” Jasmine akajibu huku akichukua kitu kingine ndani ya begi lake, akatoa chupa ya maji ‘drip’ na kumpa Chiba aishike kwa juu kwa mtindo wa kuinging’iniza kisha akachukua sindano na kutoboa moja ya mishipa ya Scoba katika mkono wake na kupachika ule mpira, akachezea kidubwasha Fulani na kisha akasimama akiwa kajishika kiuno. Akitazama huku na huko.
“Tumsogeze hapo kwenye hako kamti,” akasema na kisha Chiba akampa Gina ile chupa aendelee kuishika wakati yeye na Jasmine wakimsogeza Scoba mpaja walipopataka na kumuweka vizuri.
“Piga kambi mwanaume, tufungue zahanati,” Jasmine akamwambia Chiba ambaye tayari alitoa katika begi lake aina ya kitambaa kigumu kisichopitisha maji, akakibana kwa vyuma Fulani alivyovito humohumo na kisha akafyatua kitu kama mwamvuli mkubwa na kukifunika mahali hapo, wote wakawa ndani ya kijumba kidogo kilichoweza kuwahifadhi.
“Atapona?” Chiba aliuliza.
“Bila shaka,” akajibiwa na Jasmine.
“Sasa Amata atakuwa wapi? Au inawezekana akawa jirani hapa hapa?” Gina aliuliza kwa dukuduku.
“Nafikiri ni maeneo haya haya kama alifamikiwa kuruka kama mwenzake, maana Scoba inaonekana aliruka na hapa anaonekana ameumia sehemu ya nyuma ya shingo kwa kuwa ndiyo inayoonesha uvimbe,” Jasmine alieleza.
“Tuendelee kumtafuta maana bibi yake huko aliko kila dakika anapiga simu mpaka kero,” Chiba aliwaambia wenzake.
“Na anavyompenda, yaani leo halali, na bila kumzuia angekuja huku porini,” Gina akaongeza.
“Eeh jamani huko mbali, kwani sisi hatupendi?” Jasmine akauliza kwa shaka.
“Sijasema hivyo, wote anatupenda kama watoto wake, ni jambo zuri sana”.
Wakiwa katika kuongea mara wakasikia michakacho ya watu au wanyama, hawakujua ni kitu gani, Chiba akanyanyuka na kukamata shotgun yake mkononi tayari kwa lolote na wakati huohuo Gina naye alikuwa tayari upande wa pili wa kibanda kile naye shotgun ikiwa mkononi inasubiri amri tu.
Ndani ya kile kibanda Jasmine naye alikuwa tayari na bastola mkononi.
Kutoka katika kile kichaka wakaibuka vijana wane wakiwa na mbwa watatu, mikononi mwao walikuwa wameshikilia mavisu makubwa na mikono yao ikiwa imelowa damu.
“Amani jamani!” mmoja wa wale vijana akasema.
“Amani kwa wote,” Chiba akajibu wakati huo Gina alikwishasimama pembeni na bunduki yake ilikuwa ikwaelekea vijana hao.
“Vipi porini hapa na usiku huu? Hamuogopi? Hili pori sio zuri kabisa ndugu zangu, fanyeni hima muondoke,” mmoja wa wale vijana aliyekuwa kifua wazi aliwaeleza Chiba na wenzake.
“Tupo kazini kijana,” Chiba akajibu.
“Najua lakini hili eneo lina mambo ya ajabu, watu wengi hupotea humu na hawajulikani wanakokwenda, vitu vya ajabu hunekana na kukipambazuka huwa tunashuhudia mabaki ya miili ya binadamu,” mwingine akaeleza.
“Hapa ndio Mlingotini, wakiwakamata watawatoa sadaka,” Yule wa kwanza akaeleza.
“Nimewaelewa, nisikilizeni, mnamwona huyu?” Chiba akawafunulia kile kihema na wale jamaa wakamwona Scoba aliyekuwa amelala kimya na ile drip ya maji ikiendelea kushuka na kuingia mwilini mwake.
Wale jamaa wakatazamana na kisha kurudisha macho kwa Chiba.
“Huyu ni nani?” wakauliza.
“Rafiki yangu, nimekuja kumtafuta huku tangu jana asubuhi haonekani,” Chiba akaeleza.
“Hamjaona mwingine kama huyu?” Gina akadakia swali.
“Hapana ila jana kuna kitu cha ajabu kimetokea huko baharini, tuliona kama ndege sijui ikiwaka moto anagani kisha ikaanguka baharini nafikiri, kwani tulipokuja kutazama hatukuona chochote,” wakeleza.
Ikawa zamu ya Gina na Chiba kuangaliana.
“Eneo gani mlipoona huo moto au mlipuko?”
“Huku, usawa wa baharini, halafu ule moto ukaangukia huko huko,” wakajibu huku wakionesha uelekeo wa tukio lile kwa vidole vyao.
Chiba akamtazama Gina kisha wote wakatikisa vichwa vyao kuashiria wameelewa jambo.
“Tunafanyaje?” Gina akauliza.
Chiba akabaki kimya akifikiri jambo.
“Jamani twendeni kijijini hapa mahala si pazuri hata kidogo,” mmoja wa wale watu akatoa ombi na kisha msafara ukaanza kwa kumbeba Scoba huku na huku kwa kutumia miti iliyofanywa kama machela.
“Tukiwa kijijini tutawaonesha vizuri kule ambako tuliona tukio hilo,” mwingine akaeleza huku msafara ukiendelea katika mapori na usiku wa giza nene.
† † †
SIKU ILIYOFUATA
MADAM S aliliweka sawa pazia la dirisha lake ofisini na kisha kurudi kitini kukaa kama mwanzo huku kichwa chake kikiwa hakijatulia hata kidogo. Aliitazama saa yake ya ukutani na kurudisha macho yake mezani kwa mara nyingine kabla hajagutuliwa na mlio mkali wa kengele ya simu.
“Ndiyo, Chiba…” akaitikia namna hiyo huku uso wake ukijawa na shauku ya kujua kilichojiri.
“Operesheni imefanikiwa kwa asilimia hamsini, tumempata Scoba katika hali mbaya lakini sasa anaendelea vyema…”
“…Endelea…”
“…bado hatujampata Kamanda Amata na pia hatuna fununu yoyote juu yake,” Chiba akajibu na kutulia kimya.
“kwa hiyo nini kimewakuta hasa kwa maelezo ya Scoba?”
“Scoba bado hawezi kuongea, ila tunafanya utaratibu wa kumfikisha hospitalini kwa matiobabu zaidi, ila kwa haraka haraka tumegundua kuwa ndege waliyokuwa wakitumia ama imepata hitilafu na kuanguka au imetunguliwa…”
“Mungu wangu! Mmeona mabaki yoyote ya ndege au imekuwaje?”
“Hapana Madam, hakuna mabaki ya ndege tuliyoyaona ila kwa uchunguzi tulioufanya inaonekana ndege hiyo imeangukia baharini…”
“Sawa, kwa hiyo tunahitajika kugeuka samaki sivyo?” Madam akauliza kwa lugha tata.
“Ndiyo Madam, inabidi iwe hivyo,” Chiba akajibu.
“Sawa, aaaaaaa… nipe dakika kadhaa kisha nitakupigia,”
“Copy!” Chiba akakata simu.
Madam S alitulia akituliza akili yake na kuizungusha huku na kule, kisha akapiga ngumi mezani na kuinua simu yake akaiweka sikioni na kubofya tarakimu kadhaa. Upande wa pili ukaitikia.
“Hello!” sauti nzito ikalipenya sikio la mwanamama huyo.
“Msaada wa haraka tafadhali…”
“Wapi?” ile sauti ikauliza.
“Nyumba ya samaki,”
“Copy!” ile simu ikakatwa. Madam S akatoka ofisini na kuvaa koti lake la suti alilokuwa amelitundika kwenye kining’inizio kilichochongwa kwa fimbo ya mpingo, akatoka na kuubana mlango nyuma yake.
† † †
KURASINI
NDANI YA MELI MBOVU iliyotelekezwa kwa miaka mingi katika eneo hilo watu wawili walikutana kwa mazungumzo ya dakika zisizozidi tano.
Madam S alikuwa akitazamana na Inspekta Simbeye katika mkutano huo wa dharula.
“Ndiyo Madam!” Simbeye alianza namna hiyo mara tu baada ya kuingia katika meli hiyo chakavu ilizama nusu na kubaki nje nusu ilihali ndani yake kuna mitambo ya kuchunguza usalama wa baharini kama rada ambazo huweza kuona kitu chochote kisicho samaki kikiwa zaidi ya maili mia moja chini ya maji. Vijana wanaoijua kazi hiyo wa jeshi la polisi na lile la wananchi JW walikuwa wakifanya kazi humo usiku na mchana; hakuna aliyewaona wakiingia wala wakitoka, na hakuna aliyewahi kujua kama meli hilo linalozidi kuoza kwa nje kwa nini lilikuwa halihamishwi mahala hapo.
“Njiwa wangu amepigwa manati, kadondoka majini, alikuwa na mayai mawili, moja nimelipata lakini linguine mpaka sasa sijalipata wala kuliona…” Madam alimwambia Simbeye.
“Oh, pole sana, nilipata taarifa ila sikujua mayai ya nani! Sasa unatakaje?” akauliza Simbeye.
“Nahitaji samaki, japo wawili tu wakaangalie kule chini?”
“Umesomeka Madam,” Simbeye akajibu kisha akaagana na Madam S na kuondoka zake kutoka ndani ya meli hilo.
Dakika mbili baadae, boti iendayo kasi inayojulikana kwa jina la ‘GHOST’ inayoweza kupita juu na chini ya maji ilichomoka ndani ya meli hiyo ikiwa na vijana watatu waliovalia tayari kwa kuendesha maisha majini. Safari kuelekea katika bahari ya Bagamoyo ilikuwa imewiva. Wakati huohuo Madam S aliondoka na gari helkopta ya polisi kuelekea upande huo ili kutoa msaada zaidi.
† † †
Simu ya Chiba akafurukuta mfukoni akainyanyua na kiuiweka sikioni.
“Tuko njiani!”
“Copy!” kisha ile simu ikakatwa. Chiba akawatazama wenzake.
“Madam yuko njiani!” akawaambia.
Wakaitikia kwa vichwa huku wakiwa tuli wakiangalia huku na kule kwa vifaa vyao maalum, pia wakitumia kompyuta kumtafuta Kamanda Amata kwa picha za satellite wakijaribu ku-ping tarakimu za utambulisho wake lakini haikuonekana hata dalili za mtu huyo kuonekana. Chiba alimtazama Jasmine aliyekuwa na Gina muda huo.
“Dokta, vipi mgonjwa?” akamuuliza.
“Yuko poa, naona sasa anaweza kuongea japo si kwa ufanisi sana,” Jasmine akajibu na kisha wote wakarudi kwenye ile hema yao ambayo sasa walikuwa wameijenga tena kijijini pembezonin kidogo. Nukta hiyo hiyo kifaa cha mawasiliano mgongoni mwa Gina kikakoroma, akaukwanyua mkonga wa chombo hicho na kuupachika sikioni.
“Unasomeka,” akitikia.
“Nipe uelekeo tafadhali…”
“ Nyuzi 278 Kaskazini kwa kipimo wima na 120.56 Mashariki kwa kipimo ulalo,” Gina akajaribu kujibu kwa kutumia vipimo vya ardhini kuielekeza helkopta hiyo ya polisi kufika eneo lile bila tabu.
Haikuchukua muda lile helkopta liliwasili eneo hilo na kutafuta eneo wazi ili litue a kufanikiwa kutua katika uwanja wa shule. Chiba, Gina na Jasmine sasa wakisaidiwa na vijana wa pale kijijini walimbeba Scoba hadi kwenye dege hilo na kumpakia kisha wakaondoka zao bila kuchelewa.
“Poleni kwa kazi vijana,” madam aliwapa pole.
“Asante lakini kazi haijaisha,” Gina akawa wa kwanza kujibu.
“Najua msijali, mnaweza kutazma chini?” akawauliza. Kisha wote wakajaribu kuangalia kwa kupiti kioo kikubwa kilicho chini ya dege hilo.
“Nini kile?” Gina akauliza.
“Vijana washafika wanajaribu kutazama kama Kamanda atakuwa kabaki huko au vipi, wamekuja na boti inayopita ndani ya maji,”
“Waoh!” Gina akashangaa.
“Lakini sina uhakika kama Amata atakuwa huko kwenye maji, maana kama yuko huko basi amekwishakufa,” Jasmine akaeleza dukuduku lake.
“Usiseme hivo Jasmine,” Chiba alimkata kauli.
“Kamanda hawezi kufa kijinga hivyo!” Scoba alijibu kwa tabu kidogo, wote wakageuka kumtazama kutoka pale alipolala.
“Naona ana nguvu sasa, anaweza kuongea” Dkt Jasmine alimweleza Madam S.
“Yeah, ila ngoja tufike mahala salama,” akaeleza Madam na wote wakahafiki.
† † †
Wale vijana watatu wakiwa chini ya maji waliweza kufika eneo ambalo ndege ile iliangukia, vilikuwa vipande vichache vilivyonasa katika miamba na mapango ya baharini, haikuwa ndege kamili au vile vipande havikukamilika. Waliendelea kuchunguza haa na pale ndipo wakagundu kuwa ndege ile ilidunguliwa kutokana na alama kubwa nyuma kabisa upande wa chini, kipande hiko hakikuathiriwa na mlipuko ule.
Walifanya juu chini na kufanikiwa kupata kisanduku cheusi (black box) ambacho kazi yake ni kurekodi mwenendo mzima wa ndege ikiwa angani. Walipokipata na kukihifadhi kazi iliyobaki ilikuwa ni kutafuta binadamu wa pili kama ataonekana. Saa nzima ilipita hawakufanikiwa, walipekuwa kila kona ya mwamba na pango lakini hakukuwamo mtu yeyote wala mabaki yake. Walipokamilisha awamu hiyo ya zoezi wakaondoka zao na kurudi kwenye boti yao. Wakiwa ndani ya boti hiyo ya kisasa ‘GHOST’ walitoa taarifa kwa Simbeye na wakatakiwa kurudi mara moja.
† † †
SHAMBA (Safe HOUSE)
SCOBA ALIKETI KIMYA JUU YA KITI cha vono, mbele yake kulikuwa na Madam S na Jasmine.
“Nina uhakika Kamanda hajafa, ama ameangukia mbali au yuko mahala, kwa sababu yeye alikuwa wa kwanza kutoka kwa parachute,” Scoba alieleza.
“Kwani nini hasa kimewatokea?” Madam alisaili
“Tumedunguliwa lakini hatujui hata kombola limetokea upande gani, sasa inakuwa ngumu kueleza, mi nilmestuka kitu kimeshafika mkiani, kilichofuatia sikuwa na jinsi zaidi yaku – evacuate. Mwamvuli wa Amata ulikuwa wa kwanza kufyatuka na kumtoa nje na mimi ulifuatia,” akaeleza. Madam S akabaki kimya kabisa akiwa hajui la kusema, baadae akarudisha uso kwa Gina.
“Huyu ni mwanaharamu, na lazima apatikane,” Madam S akasema kisha akamgeukia Scoba.
“Lakini kuna mlichogundua?”
“Kiukweli bado, pale tulikuwa tunakiona kijiji cha Kaole na vile vya pembezoni zaidi ni mapaori mpaka Mbegani”.
“Sasa nani kawatungua?”
“Inawezekana kabisa ni wanajeshi wa kambi ya Mlingotini kwani tulipita pande hizo hatukuwa na ruhusa yoyote,” Scoba akaeleza na Madam S akatikisa kichwa. Kisha akatoka na kuwaacha Jasmine na Scoba yeye akatokomea katika chumba kingine.
Dakika kama tano baadae akarudi na taarifa nyingine kwa Scoba kuwa kambi ya jeshi ya Mlingotini hawajadungua ndege yoyote eneo hilo kwani wao hawawezi kudungua ndege bila idhini ya mkuu wa kikosi.
“Basi, kutakuwa na kambi ya siri eneo hilo, hili ndio tatizo la serikali kuuza viwanja kiholela, hata mnayemuuzia hamumjui wengine magaidi hawa,” Scoba akazungumza huku akisimama.
Madam S alimtazama Scoba kwa tuo na kisha kumtupia swali.
“Hatujamuona kamanda kabisa hata kwenye mitambo yetu haonekani, kama hajafa atakuwa wapi?”
“Kamanda hawezi kufa, tuendelee kumtafuta,” Scoba akajib