Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema afariki dunia, chama hicho kimeanza mchakato wa kujaza nafasi yake.
Tayari imetangaza Ijumaa, Septemba 9, 2022, kikao cha sekretarieti kitafanyika ili kumpata atakayekaimu nafasi hiyo wakati mkutano mkuu ukiandaliwa.
Mwenyekiti mpya atapatikana kwenye mkutano mkuu baada ya kupigiwa kura na wajumbe wengi wa mkutano huo. Tarehe ya mkutano huo itatangazwa baadaye baada ya sekretarieti kufanya maandalizi.
Mrema alifariki Jumapili, Agost 21, 2022, saa 12.15 asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Amekuwa mwenyekiti wa chama hicho tangu alipojiunga nacho mwaka 1999 akitokea NCCR Mageuzi.
Akizungumzia mchakato huo leo Jumatatu, Septemba 5, 2022, Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo amesema mwenyekiti mpya atapatikana kwenye mkutano mkuu lakini sasa ameitisha kikao cha sekretarieti kwa ajili ya kukaimisha nafasi hiyo.