[emoji3578][emoji3578] Habibu Anga (2)
Akiwa anaendelea kuongea kwa hasira kwenye hiyo video, Ramon ‘Hushpuppi’ eidha kwa bahati mbaya au kutokana na hasira, aliongea jambo ambalo wengi tulikuwa tunalitamani kulijua kwa muda mrefu sana.. ‘trigger’ ambayo ilitokea kwenye maisha yake na kumfanya awe namna alivyo.
Ramon aliongea kwamba, mama yake anatokea eneo la Niger Delta, eneo ambalo ndilo lenye rasilimali ya mafuta pale Nigeria.
Ramon akaeleza kwamba licha ya mama yake kutokea eneo hilo lenye utajiri mkubwa lakini wananchi karibia wote wa eneo hilo wanaishi kwenye umasikini uliokithiri.
Ramon akatoa mfano hai wa mama yake, ambaye ambaye ana umri wa zaidi ya miaka sitini lakini maisha yake yote hajawahi kunufaika hata kwa kupata dola moja kutokana na jimbo lao kuwa na rasilimali ya mafuta.
Ramon akaeleza kwamba licha ya jimbo lao kuwa na utajiri mkubwa huo wa mafuta, lakini wakiwa wadogo mama yao aliwalelea kwa kuchuuza mikate barabarani na waliishi kwenye umasikini mkubwa.
Ramon akaenda mbali zaidi na kueleza kwamba akiwa mdogo alishuhudia dada yake akipoteza maisha kwa kuugua typhoid kutokana na familia yao kukosa fedha za matibabu.
Ramon akabainisha kwamba matukio hayo yote yalimuathiri sana kisaikolojia akiwa mtoto na hata sasa bado yangali yakimuumiza hasa kifo cha dada yake.
Marafiki wa utotoni wa Ramon wanabainisha kwamba, kifo cha dada yake kwa kuugua typhoid pengine ndio ilikuwa ‘trigger’ ya kumfanya Ramon “Hushpuppi’ kuwa namna alivyo leo hii.
Marafiki zake wanadai kwamba baada ya kifo cha dada yake, Ramon alibadilika kabisa.
Watu wanaomfahamu wanamueleza Ramon alikuwa ni kijana mpole mno na ambaye hakuwa na matukio yoyote ya ajabu mtaani.
Enzi hizo mtaani kwao Hushpuppi watu walikuwa wamembatiza jina wanamuita “Ramoni” kutokana na kupenda sana mitindo ya mavazi.
Sasa, kwenye kipindi hiki, yaani mwanzoni mwa miaka ya 2000’s ndipo pia kulikuwa kumeibuka wimbi la “internent cafes” Africa nzima.
Upepo huu pia ulipitia kwenye mitaa ya Oworo jijini Lagos ambako Hushpuppi na wazazi wake walikuwa wakiishi……