Benki ya NMB imekusanya Sh74.27 bilioni katika mauzo yake ya hatifungani ya Jasiri (NMB Jasiri Bond), ikiwa ni zaidi ya lengo ililojiwekea la kukusanya Sh25 bilioni.
Makusanyo hayo yanayoweka rekodi ya ukubwa Afrika Mashariki, yamebainishwa jana Aprili 28 baada ya benki hiyo kufunga hati fungani na kuiorodhesha hati hiyo rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa hati fungani hiyo, Naibu Katibu Mkuu- Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, amesema fedha hiyo iliyokusanywa itasaidia kutoa mikopo kwa wanawake wanaojishughlisha na biashara.
“Hii sio mara ya kwanza kwa NMB kuja na Hati Fungani na kuvuka lengo la makusanyo, hii ni mara ya nne na kwa hati hii ambayo ni ya kipekee, kama jina lake lilivyo, kumekuwa na ujasiri mkubwa sana, kwani jina Jasiri linaashiria mambo mengi sana," amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema NMB ilipokea maombi 1,630 yaliyowezesha kukusanya kiasi hicho cha fedha badala ya kilichotarajiwa
“Kuaminika kwa NMB katika hili kunathibitishwa na kuwa asilimia 96 ya waliotuma maombi ya kununua Hati Fungani, yamepitia katika matawi yetu, huku asilimia 4 tu yakifanyika kupitia Madalali wa Soko la Hisa waliosajiliwa," amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Nicodemus Mkama, amesema kuorodheshwa kwa hati fungani hiyo katika DSE kunafungua fursa kwa walioshindwa kununua awali, kufanya hivyo kupitia soko hilo.