Rais Samia Suluhu Hassan amesema upatikanaji wa maji katika eneo la Chalinze haukuwa rahisi kwa sababu kulikuwa na mvutano mkali baina ya viongozi ambao uliolenga kujenga.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Machi 22, 2022 mara baada ya kuzindua mradi wa maji Mlandizi Chalinze – Mboga ulioanza Julai 2019 na kukamilika Novemba 2021.
“Nakumbuka wakati wa kampeni tulipokuwa tunapita kuomba ridhaa ya wananchi kuongoza Serikali kupitia CCM, nilijionea mwenyewe changamoto za maji nchi nzima ikiwemo mkoani Pwani, hasa hapa Chalinze baada ya kampeni nilikuja kwa tukio jingine.
“Ndiyo hiyo siku nilimuona mwanangu Ridhiwan akifoka moto mdomoni unatoka akimfokea Injinia Luhemeja kwamba usipoleta maji hapa nakushtaki kwa wananchi lakini leo nimeshuhudia kila mmoja kamuomba radhi mwenzake kwa matamshi makali lakini maji yamepatikana Chalinze leo tunavyofurahia safari ilikuwa ndefu na ngumu,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali imeipa upekee mkubwa mkoa wa Pwani na maeneo mengine kwa kuwa ina dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani.