[emoji3578][emoji3578] Shaffih Dauda
Ni kipindi cha usajili wa dirisha dogo, ni wakati wa vijana kuwa makini katika kipindi hiki kwa maslahi mapana ya maisha yao ya soka na vipaji vyao.
Ni kweli kwenye vilabu vya Simba na Yanga wachezaji wanapata angalau maslahi mazuri [maisha mazuri, mshahara mzuri, posho na bonus] lakini vijana wengi wanazika career zao.
Huwezi kupata vitu vyote kwa wakati mmoja hasa kwa vijana wanaokua, lazima uchague kimoja, kuendeleza kipaji au uchague kibunda. Bahati mbaya sana vijana wa kibongo wanachagua vibunda kuliko kuendeleza vipaji vyao.
Niliwahi kuzungumza wakati Salamba anatoka Lipuli kwenda Simba, anatoka kwenye timu aliyokuwa na uhakika wa kucheza kila mara anaenda kwenye timu ambayo eneo lake lina Bocco, Kagere na Okwi unategemea atapata nafasi ya kutosha?
Mifano ipo mingi ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye timu nyingine lakini wakakwama Simba, Yanga, Azam kwa sababu ya kukosa nafasi. Mohamed Rashid, Ilanfia, Waziri Jr si wachezaji wabaya lakini kutokana na mahitaji ya hivi vilabu walishindwa kutoboa.
Kwa hiyo kwa mchezaji ambaye bado kijana, naona kipaumbele ni career yake kuliko pesa. Anatakiwa kuwa sehemu ambayo atacheza mechi za kutosha ili kulinda kipaji na kiwango chake kikue zaidi halafu badae atapata kibunda huku akiwa anapata nafasi ya kucheza.
Lakini ikitokea kijana mdogo anawaza kibunda kwanza, atapata lakini huenda akaingia shimoni halafu kutoka ikawa jambo jingine.
Hivi vilabu pia vinatakiwa kulinda vipaji vya watoto, wanaweza kuona kijana mwenye uwezo wakamsaini halafu wakamwacha kwenye timu ambayo atapata nafasi. Ikifika wakati unamuhitaji unamchukua unamtumia.