Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo amekutana na Rais wa sasa wa Taifa hilo Alassane Ouattara ikiwa ni zaidi ya miaka kumi baada ya vurugu za uchaguzi zilizolizonga Taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mkutano huo uliosubiriwa kwa kiwango kikubwa, unatajwa kuwa ni jaribio la kupunguza mvutano wa kisiasa, ambazo zimekuwepo nchini Ivory Coast tangu kufanyika mkutano wao wa mwisho kwa Viongozi hao zaidi ya muongo mmoja uliopita pale ambapo Ouattara alimshinda Gbagbo katika uchaguzi wa rais.
Baada ya mkutano wao, Ouattara alisema wameona ni muhimu kurejesha hali ya uaminifu baina yao "Tumeamua ni muhimu kujenga hali ya kujiamini na kutafuta njia ya maridhiano ya Waivorycoast, hili ndio jambo la msingi na kuaminiana kwa kila mmoja wetu, matukio yaliopita yalikua na machungu, kulikuwa na vifo vingi, lazima tuyasahau hayo na kutazama hatma, kwa mshikamano na mapatano."
Gbagbo kwa upande wake alisema angependa rais huyo awaachie huru wale waliokuwa wakimuunga mkono ambao kwa sasa wapo magerezani Nchini humo, Gbagbo amerejea Ivory Coast hivi karibuni baada ya Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa ICC, kuyatupilia mbali mashtaka yake ya uhalifu dhidi ya binaadamu ya vurugu za baada ya uchaguzi ambazo zilisababisha watu 3,000 kuuwawa.