Mfahamu Floyd Mayweather Jr Bondia anayeamini mwanaume anapaswa kuwa na wanawake wengi.
Floyd Joy Mayweather Jr. amestaafu kutoka masumbwi na sasa anamiliki kampuni yake ya kusimamia mchezo huo wa masumbwi ama ndondi inayoitwa Mayweather Promotions.
Ni baba wa watoto watano, mkubwa ni Koraun, ana miaka 21, anayefuata ni binti yake Iyanna mwenye miaka 20, Zion kijana wa miaka 19 na binti yake wa mwisho ana miaka 16 anaitwa Jirah.
Devion Cromwell, mtoto wa mpenzi wake wa zamani Melissa Brim, anamtaja kama mtoto wake aliyemuasili, licha ya taratibu zingine ambazo hazikuwa zimekamilika.
Koraun, Zion na Jirah amezaa na Josie Harris wakati Iyanna amezaa na muigizaji, mfanyabiashara na mtangazaji wa TV, Melissa Brim.
Floyd Joy Mayweather Jr. alizaliwa Februari 24, 1977 huko Michigan Marekani katika familia ya wanamasumbwi.
Baba yake, Mayweather Sr. alishawahi hata kupambana na bondia mkali, Sugar Ray Leonard.
Baba zake wadogo Jeff na Roger Mayweather, walikuwa mabondia pia wakulipwa.