Tafasiri Unavyoweza: Waziri Na Mimba Ya Rushwa
...waziri wa mambo ya ndani kabeba mimba ya rushwa, na ni muda si mrefu mimba itazaa. Ndiyo, usijedhani naandika kumdhalilisha waziri wa mambo ya ndani, waziri ambaye badala ya kukaa chini na kuangalia namna nzuri ya kuboresha sera za usalama wa raia na mali zao amekuwa ni mtu wa kutangatanga, huku na kule, kama kala miguu ya kuku au miguu yake imelambwa na mbwa. Hatulii aseme ya msingi, hakai chini kusema ya kusaidia serikali inayojinasibisha kupambana na rushwa. Hajifungii ndani kuteta na wasaidizi wake namna ya kulifanya jeshi la polisi na idara zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi kwa ufanisi, tija na weledi. Matamko ya kukatisha tamaa, matamko ya kutisha, matamko ya kuua na kutoa matumbo eti 'watapata tabu sana' ujinga na ulevi wa madaraka na mimba anayojitungia itahitaji mkunga wa tofauti, mkunga wa kuhakikisha mimba ya rushwa aliyoibeba haikui. tafasiri unavyoweza.
Angalia matamko anayoyatoa, mara kumuita Lugumi ofisini kwake, tangu lini serikali inajadiliana na wahujumu (kama kweli Lugumi and co) wamehujumu kiukweli? Tangu lini waziri anasimama kadinda kabisa, tumbo mbele kwamba hakuna kibali cha mtu kusafiri nje ya nchi kwenda kutafuta ajira halali! Waziri asiyejua tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wanaohangaika kila kukicha kutafuta kazi nje ndani, vijana waliosoma na kumaliza masomo yao ila waliofaulu ni watoto wa vigogo. Tafasiri unavyoweza.
Ninakuandikia wewe unayechekelea mimba ya waziri, wewe unayedhani uko salama kisa tumbo la waziri liko karibu na wewe linakupa kivuli, mkunga anakuja na sio wa kutumbua majibu bali kutumbua mimba za rushwa. tafasiri unavyoweza