Tafasiri Unavyoweza: Jamii Hojaji Haifi Hata Ukinyamaza Wewe
CAG kamaliza uhakiki wake na tuliyoyasikia tumeyasikia. Makusanyo yamekaa vizuri, matumizi yamejaa 'wino damu' (walimu huwa wanatumia kalamu ya wino mwekundu kuonesha kilichowatatiza), matumizi makubwa tu ya serikali hayana vielelezo, kiufupi kama hutaki kujisumbua na utabaki kuwa mkweli ni kuwa mpunga mrefu sana umepigwa na wajanja na siku zote tunamjua mkuu wa serikali ni nani, na kwa maana hiyo mlaji aliyekula hizi hela huhitaji kujifikiria sana au kupoteza muda kuchunguza nani kazipiga hizi hela. Tafasiri unavyoweza.
Ni bahati mbaya sana kama taifa kuna mambo tunayapuuza, kiukweli tumekuwa ni taifa la wapuuzi. Hatuhoji na hata wanaojitokeza kuhoji tunawapuuza na wakati mwingine tunaenda mabli zaidi kwa kuwapa majina ili tupate sababu ya kuwapiga risasi au kuwabambikizia kesi na kuwatesa. Kuhoji ni kutaka kujua, hakuna furaha ya kuwa mjinga au mpuuzi, anayepuuza atapuuziwa na ukikaa kimya usijedhani uko salama.
Tunakoelekea tutafika tu, kujidai kuwa hawa ni bora zaidi ya hawa itatoa majibu muda si mrefu pale watoto wanaozaliwa leo wenye akili za nyoka, wajanja, wanaohoji wanaojua kusoma kabla ya kuingia darasani watakapokaa vifua wazi kuhoji kwanini kuna madhamani tumewaamini kulinda kibubu tunachokichangia lakini wanajiona wao wana haki ya kula na kutudhihaki wote wenye midomo iliyopauka kwa njaa ya kukosa huduma muhimu za msingi tunazostahili kama wana wa nchi hii. Tafasiri unavyoweza