Majukumu yanayomsubiri Mwana FA Wizara ya Sanaa

Aug 31, 2022
54
99
Siku moja baada ya kuapishwa kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, wadau wametaja mambo yanayomkabili ikiwamo yale aliyokuwa akiyapigania bungeni.

Miongoni mwa mambo ambayo Mwinjuma ambaye pia ni mbunge wa Muheza aliyokuwa akiyapigania bungeni ni suala mirabaha kwenye kazi za sanaa, tozo kwenye blank tape zinapoingia nchini na kutaka sheria iliyounda Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) iondolewe na kuwe na chombo kingine cha kulea wasanii nchini.

Akizungumzia uteuzi wa kiongozi huyo, Joachim Kimaryo maarufu ‘Master Jay’ alisema ni mtu sahihi kwenye eneo hilo, ila apewe muda wa kutekeleza majukumu hayo.

“Tofauti yake na wengi waliopita, yeye ametoka kwenye tasnia yetu, changamoto zote anazijua, alianza akiwa chipukizi hadi kuwa msanii mkubwa si tu Tanzania hadi Afrika Mashariki.

“Akishindwa sasa yeye ndio tutammaliza sababu changamoto zote anazifahamu, tumefurahi tumepata mtu wetu,” alisema Master Jay.

Kwa upande wake, mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime alisema Mwana FA hapaswi kuangalia idara moja, kwani ile ni wizara inayohusisha masuala mbalimbali ya utamaduni, sanaa na michezo.

“Huwa tunasahau sana kwenye utamaduni ambako ndiko asili ya nchi, asimamie kote na sanaa si Dar es Salaam, ni kote nchini atupie jicho, huyu ni mtu sahihi ambaye anaijua vema tasnia,” alisema Kitime.

Makamu wa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau alisema, “tumpe muda, wizara imeletewa watu sahihi, wana jukumu la kukabiliana na changamoto zilizopo, wengi wakisikia michezo wanahisi ni rahisi, lakini inajumuisha diplomasia, biashara, afya na vitu vingine vingi,” alisema.

Msanii G Nako alisema kiongozi huyo anafahamu matatizo ya tasnia hiyo na mahitaji ya wasanii, hivyo ana imani atayafanyia kazi kwa haraka.

“Kwenye mirabaha yeye yupo kwenye kamati, hivyo tunaamini Rais ametuletea mtu sahihi wa kuisaidia tasnia,” alisema.

Mwanamuziki Afande Sele alisema iwapo Mwana FA ataendelea na utashi aliokuwa nao awali, atawasaidia, kwani ni miongoni mwa mwanamuziki waliopitia changamoto za sanaa.

Msanii wa Bongo Muvi, Yvonne Cherrie ‘Monalisa’ alisema wizara hiyo imepata mtu anayeijua vema, hivyo wanatarajia kitu cha tofauti.

MWANANCHI
 
John kitime, alichosema ni sawa kabisa,maana nchi hii kuna watu wanaona bongo fleva bongo movie
Ndiyo wanatakiwa kusikilizwa zaidi.

Wakati kuna sanaa nyingi tu

Ova
 
Back
Top Bottom