Na Tausi Ally
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Ricky Mahalu na mwenzake la kutaka kesi hiyo ifutwe, badala yake imepanga ianze kusikilizwa Januari 28, mwaka huu .
Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi alisema jana kuwa hoja zilizotolewa na upande wa utetezi kutaka kesi hiyo ifutwe haina msingi.
Alisema sheria hailazimishi maelezo ya mlalamikaji kuonyesha kosa kama ulivyodai upande wa utetezi bali kosa huonekana wakati wa upelelezi.
Awali wakili Cathbert Tenga anayemtetea Mahalu na mwenzake aliiomba mahakama ifute hati ya mashitaka akidai kuaw ni ya bandia kwa madai kuwa maelezo ya mlalamikaji yaliyowasilishwa mahakamani hapo haionyeshi kosa.
Alidai maelezo ya mlalamikaji ndiyo msingi wa kuandaa makosa ya kumpeleka mtu mahakamani na yaliyopo mahakamani hayaonyeshi kosa hivyo hati iliyopo mahakamani ni feki.
Hoja ya wakili huyo iliungwa mkono na wakili mwnzake Alex Mgongolwa anayewatetea washitakiwa hao ambaye alisisitiza kuwa ni lazima hati ya mashitaka iandaliwe kwa kutumia maelezo ya malalamikaji.
Mgongolwa alidai kuwa mlalamikaji August Chami anadai kuwa Agosti 3, 2004 akisikiliza redio, alisikia Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akieleza Bungeni kuwa, taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) inaonyesha kwamba alipoenda kukagua ubalozi wetu wa Rome Italia hakukuta hati yoyote inayohusiana na ununuzi wa jengo lililonunuliwa na wizara hiyo.
Alidai kuwa baada ya Chami kusikia mjadala huo alimwandikia kiongozi wake(RCB) na kumweleza wasiwasi wake juu ya kutoonekana kwa hati hizo ndio sababu akafanya uchunguzi.
Pia Mgongolwa aliiomba Mahakama iangalie ripoti ya maswali na majibu ya majadiliano ya kikao cha 39 cha Agosti 3, 2004 cha Bunge kilichoanza saa tatu asubuhi mbele ya aliyekuwa Spika wa Bunge Pius Msekwa ili ijilidhishe.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara serikali ya Euro 2,065,827.60 wakati wakiwa maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Itali na keshi hiyo ilifunguliwa mwaka jana.