Mahakama katika kuboresha mazingira ya biashara nchini

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
21,327
24,232

31 Januari 2023​

KONGAMANO KUJADILI NAFASI YA MAHAKAMA UBORESHAJI MAZINGIRA YA BIASHARA LAFANYIKA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akichukua kumbukumbu muhimu wakati wa Kongamano hilo

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 31 Januari, 2023 amefungua Kongamano la siku moja la wadau lenye lengo la kujadili wajibu na nafasi ya Mahakama katika kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, Jaji Mkuu alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto na vikwazo vya upatikanaji wa haki, ikiwemo ucheleweshwaji wa mfumo wa Mahakama na mlundikano wa mashauri katika ngazi na hatua mbalimbali.

Alisema kuwa hatua hizo zilikuja chini ya awamu ya miaka mitano ya Mpango Mkakati katika uboreshaji wa huduma za Mahakama na Mradi wa Utoaji wa Huduma za haki ambapo Mpango Mkakati wa kwanza wa Mahakama wa Miaka Mitano ulianza 2016 hadi 2021.

“Mpango huu ni mwitikio wa Mahakama kwenye changamoto zinazokabili upatikanaji na utoaji wa haki nchini Tanzania na uliendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025. Kupitia Mpango Mkakati huu, Mahakama ilipanga, kubuni na kutekeleza mfululizo wa mikakati ya maboresho ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ambayo ilitoa huduma za kimahakama zinazozingatia wananchi," alisema.

Jaji Mkuu alibainisha zaidi kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea na awamu yake ya pili ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama (2021-2025), ambao inaendelea kuutekeleza kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama na Utoaji Huduma za Haki kwa Wananchi wa Tanzania.

“Katika Kongamano hili, mtapata baadhi ya vionjo vya yale ambayo Mahakama ya Tanzania imekuwa ikifanya katika kipindi cha miaka minane iliyopita ya kufanya maboresho ya kimahakama,” aliwaambia washiriki wa Kongamano hilo.

Jaji Mkuu alieleza zaidi kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inabainisha uhakika wa upatikanaji wa haki na kuweka jukumu hilo kwa Mahakama kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mtu anayetafuta haki hiyo.

Aliwaambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa licha ya taasisi tofauti za sekta ya umma na binafsi walizotoka, wote wanashiriki mambo mengi yanayowahusu, ikiwemo uwepo wa Mahakama huru ambayo inachangia amani na usalama.

"Sote tunataka Mahakama kulinda haki za kimsingi za watu binafsi, kutatua migogoro ya kibiashara kwa haraka na kusimama imara dhidi ya ufisadi kwa umma na binafsi. Kila mdau ana matarajio kutoka kwa Mahakama, hivyo kutambua maboresho ambayo kila mmoja wetu anafanya ni muhimu kwa matarajio yetu ya pande zote mbili, "alisema.

Jaji Mkuu alieleza zaidi kuwa Mahakama ya Tanzania imeandaa mwongozo kuelekea kwenye mabadiliko ya kielektroniki ya haki ili kuziba pengo la utoaji haki. Alisema kuwa Serikali ya Tanzania imeanzisha Mradi wa Kidijitali Tanzania.

“Mradi wa Kidijitali Tanzania unatambua kwamba uchumi wa kidijitali ni mustakabali wa Tanzania na mapinduzi ya kidijitali yatakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji na ustawi wa Tanzania katika siku zijazo. Ni wakati wa kuboresha programu zetu za kidijitali zinazotumia teknolojia ya kidijitali kubadilisha michakato ya haki na miundo yetu ya utoaji huduma,” alisema.

Awali katika salamu zake za ukaribisho kwa niaba ya kamati ya maandalizi, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alieleza kuwa wanaona ni bahati kuwa wenyeji wa Kongamano hilo la siku moja ambao lengo lake ni kushirikisha na kutafuta mawazo ili kuibua mijadala zaidi, kwani Mahakama iliyopewa dhamana pekee ya kutoa haki inaweza kufanya zaidi na zaidi ili kulainisha magurudumu ya biashara na uwekezaji, hivyo kuboresha mazingira ya biashara nchini.

“Kongamano hili ni ushuhuda wa wazi wa azimio na dhamira ya Mahakama ya kuwashirikisha wadau wakuu katika sekta ya utoaji haki kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama (2021-2025) ili kufikia malengo ya Uboreshaji wa Huduma za Mahakama kwa Wananchi na Mradi wa Utoaji Huduma za Haki katika kuboresha hali ya biashara, "alisema.

Mhe. Dkt. Kihwelo alisisitiza kuwa uchaguzi wa mada, wasimamizi, wazungumzaji na washiriki umefanywa kimkakati ili kupata mafanikio makubwa ndani ya siku moja na walikuwa na matumaini makubwa kutaibua mijadala na washiriki watakuwa huru kuzungumza na kuchangia mawazo yao kwa uwazi.

Ufunguzi wa Kongamano hilo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustepher Siyani, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, maafisa wa Mahakama waliostaafu na walioko kazini pamoja na Mahakama ya Uingereza. Washiriki wengine wa Kongamano hilo ni kutoka taasisi binafsi, taasisi za umma pamoja na wizara mbalimbali.

Jaji Mkuu aliungana na washiriki wa Kongamano hilo lililokuwa linafanyika katika Hoteli ya Morena jijini hapa wakati wa mchana akiwa ameongozana na Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Gerson Mdeme.

Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kushirikiana na wadau kwa mujibu wa matakwa ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2020/21- 2024/25) hususani Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati huo ambayo inasisitiza ushirikishaji wa wadau.

Linafanyika kwa mara ya tatu baada ya Kongamano la kwanza la namna hii kufanyika katika Wiki ya Sheria Februari, 2020 jijini Dar es Salaam na la pili ambalo lilifanyika katika Wiki ya Sheria mwaka 2022 jijini Dodoma, lengo likiwa ni kubadirishana uzoefu na kujadili namna ambavyo Mahakama ya Tanzania inaweza kuchangia ukuaji uchumi nchini pamoja na ustawi wa biashara kupitia utoaji haki kwa wakati.

Katika Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliadiliwa na kutolewa na wawezeshaji mahili wakiwamo wafanyabiashara, wawakilishi wa sekta binafsi pamoja na sekta ya umma lakini pia Majaji kutoka Uingereza na Afrika ya Kusini.

Source : KONGAMANO KUJADILI NAFASI YA MAHAKAMA UBORESHAJI MAZINGIRA YA BIASHARA LAFANYIKA
 
Back
Top Bottom