Zee la shamba
Member
- Oct 17, 2007
- 55
- 4
- Rais asema watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
- Asema wananchi wakiwaona, wataamini vita inapiganwa
- Viongozi sasa kueleza jinsi walivyopata ukwasi walionao
RAIS Jakaya Kikwete ametoa kauli inayoashiria kwamba siku si nyingi, Watanzania watashuhudia vigogo 38 watuhumiwa wa ufisadi, wakifikishwa mahakamani.
Rais Kikwete ametoa dalili za kuwapo mpango huo, katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaofanyika katika Ukumbi wa Kizota, nje kidogo ya mjini Dodoma, juzi.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alisema vigogo hao 38 wamebainika kuwa na mali yenye thamani kubwa kuliko kipato chao.
Alisema Tume ya Maadili imebainika kuwa viongozi hao wanamiliki mali ambayo maelezo yake ya namna ilivyopatikana, hayalingani na kipato chao.
Alisema baada ya kubainika, taarifa hizo ziliwasilishwa kwa uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambao aliwaita wanaume wa shoka.
Rais alisema TAKUKURU wanafanyia kazi taarifa hizo kabla ya kuwafikisha mahakamani na kujigamba kwamba, mara vigogo hao watakapofikishwa mahakamani, Watanzania ndiyo wataamini kuwa Serikali haina mchezo katika vita dhidi ya rushwa.
Kwa upande wa rushwa, tayari kesi moja iko mahakamani na wakati wowote watapeleka kesi nyingine.
Naamini kesi hizo na nyinginezo zitakapofikishwa mahakamani, ndipo watakapojua kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jambo tulilodhamiria na kwamba hatulisemi idomoni tu, alisema Rais.
Aliwahakikishia wananchi na wadau wote kwamba hakuna jambo linalotajwa kuhusu rushwa, halifuatiliwi.
Hakuna kiongozi anayetajwa ambaye suala lake halifuatiliwi . Kila taarfa hufuatiliwa, iwe imetoka gazetini au katika mkutano wa dhahara au kwa ujumbe wa simu ya mkononi au kwa minongono na uvumi tu, alisema.
Alisema Takukuru imekuwa ikifanya uchunguzi wa kina ili inapokwenda mahakamani, iwe na uhakika wa ushindi.
Kufanya hivyo kunawapan uhakika wa ushindi mahakamani, lakini pia kunazuia watu wasionewe au kuvunjiwa heshima kwa makosa wasiyokuwa nayo. Hata mtuhumiwa ndugu zangu, anastahili kutendewa haki mbele ya vyombo vya sheria.
Mtu hana hatia mpaka pale Mahakama au chombo husika cha sheria kitakapotamka hivyo. Ni kanuni ya msingi sana katika utoaji haki ambayo lazima tuizingatie ipasavyo, alisema.
Alisema anajua vizuri jinsi wananchi wanavyochukia rushwa na wala rushwa, hata hivyo, alitahadharisha kuwa hasira zisiwafikishe mahali wakasahau kutenda haki.
Ni hatari kupuuza msingi huo muhimu kwani tutatoa fursa kwa walio hodari kusema na wenye majukwaa ya kusemea kuwaonea wale wasiokuwa nayo. Tutatoa fursa kwa watu wazushi na wafitini kuwamaliza wenzao wasiokuwa na hatia.
Nawaomba sana wenzangu, tuchukie sana rushwa, lakini tusisahau wala kupuuza kuwatendea watu haki, huo ndiyo msingi wa utawala wa sheria, alisema.
Kuhusu maisha bora kwa kila Mtanzania, Rais Kikwete alisema wapo waliopotosha kwa kudhani kuwa kufumba na kufumbua, Tanzania itakuwa nchi ya maziwa na asali.
Najua maajabu yanawezekana, lakini kwenye maendeleo hayaji ghafla. Yanachukua muda kwa sababu maendeleo ni mchakato unaochukua muda kukamilika.
Alisema maisha bora yanayozungumzwa yana sura mbili, upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii zilizo bora na zinazotosheleza na upatikanaji wa mapato ambayo yakiongezeka, watu watakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kujipatia mahitaji ya maisha.
Rais Kikwete alisema miezi 23 tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani, tathimini ya utekelezaji dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania inapata mafanikio makubwa, licha ya changamoto kadhaa. Pia alisema ajira zaidi ya 300,000 zimepatikana katika kipindi hicho, dalili ambazo zinaonyesha kuwa lengo la kutengeneza ajira mpya milioni moja ifikapo mwaka 2010, litatimia.
Kuhusu Tume ya Maadili, alisema imeanzisha utaratibu wa kuhakiki taarifa za mali zinazotolewa na viongozi kwa mujibu wa sheria.
Kwa ajili hiyo, hufanya ukaguzi wa mali za viongozi kama walivyojaza kwenye fomu ili kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo. Fomu ya tamko imebadilika na kumtaka kiongozi kueleza jinsi alivyoipata mali , tofauti na siku zilizopita ambako alieleza tu mali na madeni aliyo nayo, alisema.
Habari hii imeandaliwa na Waandishi Wetu, Manyerere Jackton kutoka Dodoma na Godfrey Dilunga, aliyeko Dar es Salaam.
Source: Gazeti la Mtanzania