(a) Hakuna Unyonyaji:
Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi: haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbii za watu: tabaka ya chini ya watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi. Katika nchi ya Ujamaa kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi hufanya kazi, na kila mfanya kazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbali mbali hayapitani mno. Katika nchi ya Ujamaa kamili watu peke yao ambao huishi kwa jasho la wenzao, na ni haki yao kuishi kwa jasho la wenzao ni watoto wadogo, wazee wasiojiweza, vilema na wale ambao, kwa muda, Jumuiya imeshindwa kuwapatia kazi yo yote ya kujipatia riziki kwa nguvu zao wenyewe. Nchi yetu ni nchi ya Wakulima na Wafanya kazi, lakini si nchi ya Ujamaa kamili. Ina misingi ya ubepari na ukabaila na vishawishi vyake. Misingi hii ya ubepari na ukabaila yaweza ikapanuka na kuenea.