TOKYO, JAPAN - Shirika la Anga la Japan (JAXA) kwa kushirikiana na vyuo vikuu vikuu nchini humo limefanikiwa kufanya jaribio la kwanza la injini ya ndege inayokwenda kwa kasi ya sauti (hypersonic), hatua inayotajwa kuwa mapinduzi makubwa yatakayobadilisha sekta ya usafiri wa anga duniani kote.
Jaribio hilo la kihistoria lilifanyika katika Kituo cha Anga cha Kakuda mkoani Miyagi, lilihusisha mfano wa ndege hiyo yenye urefu wa mita mbili ikiwa imeunganishwa moja kwa moja na injini maalum inayotumia nishati ya haidrojeni.
Wakati wa jaribio hilo, wataalamu walifanikiwa kuchoma nishati hiyo kwa ufanisi mkubwa katika kasi iliyoiga mwendo wa Mach 5, ambayo ni sawa na kilomita 6,115 kwa saa au mara tano ya kasi ya sauti.
Kasi hii ina maana kwamba safari kati ya miji ya Tokyo na New York ambayo sasa huchukua takriban saa 12 itaweza kukamilika kwa chini ya saa 2 tu.
Changamoto kubwa ya usafiri wa kasi hii ni joto kali linalotokana na msuguano wa hewa, ambalo hufikia hadi nyuzi joto 1,000 na linaweza kuyeyusha vyuma vya kawaida.
Ili kukabiliana na hali hiyo, wanasayansi wa Japan walitengeneza ngao maalum ya kuzuia joto ambayo ilifanya kazi kwa mafanikio makubwa na kulinda mifumo ya ndani ya ndege hiyo kubaki katika kiwango cha joto cha kawaida.
Licha ya mafanikio haya makubwa, teknolojia hii bado ipo katika hatua za awali za utafiti ambapo hatua inayofuata itakuwa ni kurusha injini hiyo angani kwa kutumia roketi ili kuona uwezo wake halisi nje ya maabara.
Wataalamu wanakadiria kuwa itachukua takriban miaka 20 ya maboresho kabla ya ndege za kwanza za abiria kuanza kutumika rasmi, huku wakilenga miaka ya 2040 kuleta mabadiliko haya ya kudumu katika namna binadamu anavyosafiri duniani.