SoC03 Maboresho katika mfumo wa vitambulisho kwa ufanisi zaidi na maendeleo ya taifa

Stories of Change - 2023 Competition

Black Opal

Senior Member
Jan 22, 2023
199
257
UTANGULIZI
Kumekuwa na usumbufu mkubwa linapokuja suala la kupata vitambulisho vya taifa, hakuna sababu za msingi za kwanini inachukua mpaka miaka 4 mtu anakuwa anafatilia kitambulisho hiko bila mafanikio. Tatizo ni nini? Lakini pia Serikali imefanya jambo hili la watu kuwa na vitambulisho kuonekana kama ni muhimu pekee kwa wananchi, wakati kwa upande wa pili wao wanafaidika zaidi na zoezi hili kwakuwa wao ndio wachakataji wa kubwa wa taarifa za watu. Pia kumekuwa na usumbufu mkubwa unaoambatana na kuombwa rushwa kupata vyeti vingine kama vile cheti cha kuzaliwa (hasa ukiwa umepoteza ulichokuwanacho) pamoja na cheti cha kifo. Kutokana na hayo napendekeza maboresho yafuayatayo katika mfumo wa utoaji vitambulisho ambayo naamini yataongeza ufanisi na kuchangia maendeleo katika sekta nyingine.

Kwanza kabisa hakuna haja ya kuwa vyombo viwili vinavyoshughulikia utoaji wa vitambulisho kwa wananchi, yaani RITA kwa upande mmoja inayoshughulika na usajili wa mambo ya kijamii kama taarifa kuzaliwa, vifo, vyeti vya ndoa na talaka na upande mwingine NIDA ambao wanashughulika na vitambulisho vya taifa. Chombo kimoja kinatosha kushughulikia mambo yote yanayohusisha kusajili taarifa hizo ili kupunguza urasimu ambao hauna ulazima lakini pia kupunguza matumizi ya rasilimali ambazo zinaweza kutumika katika mambo mengine ya maendeleo.

Kwenye maboresho haya, matumizi ya alama za vidole pamoja na vitambulisho yataendelea (pamoja na maboresho kidogo upande wa watoto), lakini mtu atakuwa na kitambusho kimoja tu ambacho atakuwa anakitumia sehemu mbalimbali. Twende taratibu kuanzia usajili hadi jinsi utakavyokuwa unafanya kazi.

USAJILI
Kwa upande wa watoto, mzazi ndio atakuwa chanzo wa taarifa hizo, ambapo akifikisha umri wa miaka 18 yeye ndio atawajibika kwa taarifa zake na sio mzazi tena.

Usajili wa vitambulisho hivi utaanzia pale mtu (mtoto) anapozaliwa, ambapo atapewa namba maalum ya utambulisho atakayoitumia maisha yake yote. Ili kuongeza visaidizi vya utambuzi kwa upande watoto wenye miaka 0 – 3, utambuzi wao utajumuisha pia alama za nyayo pamoja na viganja, kila mtoto ana alama pekee kwenye nyayo na viganja ambazo zinaweza kuwatofautisha. Hii itasaidia utambuzi wa mtoto kirahisi kwenye hali mbalimbali mfano; ikiwa ametupwa, amepotea au amepatikana kwenye ajali.

Mtoto akifikisha umri wa miaka 3 atatakiwa kusajiliwa kwenye mfumo wa alama za vidole kwakuwa hapa tayari vidole vimeshatengeneza alama ya utambuzi na anaweza kusajiliwa. Kufikia hapa taarifa zake zitaboreshwa pia kama kuna kitu kitakuwa kimebadilika.

Usajili huu wa alama ya vidole utakuwa unaboreshwa kila baada ya miaka mitano (au jinsi sheria za nchi zitakavyoamua) sababu mtoto anakua na mwili wake kuendelea kubadilika hivyo alama za vidole zinaweza kubadilika. Usasishaji huo utaendelea mpaka mtoto akifikia umri wa miaka 18 akiwa mtu mzima. Hapa sasa mtu huyu atakuwa anastahili kupata kitambulisho chake cha taifa ambacho ndio kitakuwa kitambulisho pekee anachohitaji kuwa nacho katika huduma zote nchini isipokuwa kwenye pasi ya kusafiria na huduma za kibenki ambazo zinahusisha mataifa mengine.

Kufikia hapa usasishaji wa taarifa utategemea kama mtu amepata ajali ikatokea vidole vyake vikaathirika vibaya na kadhalika.

Mtu akifikisha tu miaka 18 atatakiwa kufika kwenye mamlaka husika na kuchukua kitambulisho chake ambapo atakipata kitambulisho hicho ndani ya siku tano tu sababu taarifa zilikuwa zinasasishwa muda mwingi, safari hii akiwa ametimiza miaka 18 atamalizia kuweka picha yake ya sasa ambayo atapiga siku akienda kutoa taarifa ya kufuata kitambulisho.

Katika kipindi chote cha kusasisha taarifa kwa watoto na watu wazima, mtu atapewa mwezi mmoja tu baada ya kufikisha umri husika wa kufanya zoezi hilo. Muda utaongezwa kwa wataokuwa na dharula pekee.

KUBORESHA NA KUSASISHA TAARIFA
Kabla ya mtoto kufikisha miaka 18 mzazi ndio atawajibika kusimamia taarifa hizo. Kila mtoto atasajiliwa kwa namba yake kwenye mfumo, mfumo utaruhusu usajili wa akaunti ya mtoto kwa taarifa zake na kutakuwa na utaratibu wa akaunti ya mtandaoni wenye taarifa hizo. Taarifa hizo zitakuwa zinasasishwa na mamlaka (automatically) kila mtoto akipata huduma sehemu mbalimbali. Mzazi atakuwa na uwezo wa kuona taarifa hizo bila kubadilisha, na kutaarifu mamlaka kwa kutuma ujumbe na vithibisho endapo kutakuwa na taarifa iliyokosewa ili kuhakikisha taarifa zote zipo sawia. Utaratibu huu utakuwa sawa kwa watu wazima, tofauti itakuwa kwenye usimamizi pekee.

JINSI VYOMBO VINGINE VITAKAVYOWEZA KUPATA TAARIFA KWA AJILI YA USAJILI NA MATUMIZI MENGINE
Ili vyombo vingine kama hospitali, shule, leseni na kadhalika viweze kupata taarifa husika za mtu vitatakiwa kwanza kuwa na usajili maalumu wa kuwawezesha kupata taarifa husika. Kutokana na huduma ambayo chombo hiko kinatoa kitaingiza ‘code’ maalumu na kuwawezesha kupata taarifa za mtu husika kutoka kwenye namba au kitambulisho cha muhusika. Taarifa yoyote itakayorekodiwa hapo (kutokana na huduma anayopatiwa) itaingia moja kwa moja kwenye mfumo mkuu na kusasisha taarifa zake kwenye kipengele hicho.

FAIDA ZA MABORESHO HAYO
  • Kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa na chombo kimoja fanisi kinachotoa huduma za vitambulisho.
  • Kupunguza udanganyifu kwa anayetoa na kukusanya taarifa, sababu mamlaka itakayoweza kusasisha taarifa hizo ni moja na mtu anauwezo wa kuripoti muda wowote kama kuna taarifa haiko sawa.
  • Kupunguza na kumaliza kabisa matumizi mabaya ya taarifa za watu pamoja na wizi sababu kwanza, utahitaji ‘code’ maalum kupata taarifa hizo, na ukitumia taarifa hizo tofauti na ulivyosajiliwa taarifa zitakwenda moja kwa moja kwenye mfumo mkuu na kuripoti kitendo hiko kama tatizo.
  • Kurahisisha utambuzi wa watu ikitokea mtu amepotea na hawezi kujieleza, kwenye matukio ya ajali ikitokea mtu amefariki, lakini pia kwenye hali inayotokea kwenye hospitali za kuhifadhia maiti ambapo serikali huwa inazika watu kwa kukosa ndugu waliowatambua; hili litakuwa sio tatizo tena. Utambuzi utakuwa rahisi sana na hivyo kuongeza ufanisi kwenye jambo hili.
  • Watu hawatakuwa na haja ya kubeba vitambulisho vingi kwa wakati mmoja ambayo inafanya kuwa rahisi mtu kupoteza kitambulisho chake.
  • Kufanya zoezi la sensa kuwa rahisi sababu chombo hiki kitakuwa na taarifa zilizo sahihi kila wakati na hivyo kuongeza ufanisi za zoesi hilo kwa kiasi kikubwa.
  • Kurahisisha kwenye kutoa huduma na kupanga mipango ya maendeleo katika makundi mbalimbali kutokana na kuwa na taarifa zinazoenda na wakati muda wote, na hivyo kuokoa muda na fedha nyingi ambazo zingehitajika kufanya utambuzi wa makundi haya.

HITIMISHO
Naamini maboresho haya yatasiadia sehemu kubwa kuondoa usumbufu unaojitokeza katika mfumo uliopo sasa na kumaliza matatizo mengi yanayosababisha hasara na kuzorotesha juhudi za maendeleo kuanzia NIDA kwenyewe na kwenye taasisi zinazotegema taarifa kutoka NIDA.
 
Wale mliokuwa mnasubiri nondo zangu, hizo hapo.:):):) Karibuni kwa maoni mdondoshe na kura hizo... andiko jingine naweka sasa hivi karibuni na kwenye hilo pia
 
UTANGULIZI
Kumekuwa na usumbufu mkubwa linapokuja suala la kupata vitambulisho vya taifa, hakuna sababu za msingi za kwanini inachukua mpaka miaka 4 mtu anakuwa anafatilia kitambulisho...
Vema mkuu.
Tuna vitambulisho vingi sana. Unakuta mtu wallet imejaa vitambulisho wakati kitambulisho cha uraia kingeweza kubeba taarifa zote.
 
Watoe vitambulisho, hizi process zoote na longolongo tumezichoka!
Bila ya kuwa na utaratibu mzuri ndio hizo longo longo na urasimu suiokuwa na maana unakuwa mwingi, ingekuaje ukienda nida kuprocess kitambulisho unakipata ndani ya siku 5 tu?
 
Back
Top Bottom