Mabadiliko ya Profesa Kabudi kwenye sheria ya madini yanalitesa Taifa. Nini kifanyike?

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,519
41,024
Katika awamu hii kuna sekta nyingi zimeharibiwa badala ya kuboreshwa ili ziwe na mchango chanya kwenye uchumi na maisha ya Wananchi.

Kusipofanyika mabadiliko ya haraka, kadiri tutakavyoenda, kila mwananchi, hata mwenye mwenye akili ya kawaida kabisa, atapata jibu kama tupo kwenye njia sahihi au tunaelekea shimoni.

Kati ya sekta zilizoharibiwa sana ni sekta ya madini. Hii sekta kabla ya uharibifu ilikuwa inaongoza kwa ukuuaji na uingizaji wa fedha za kigeni. Sekta hii iliharibiwa zaidi na mabadiliko ya sheria ya madini yaliyoandaliwa na kusukumwa kwa kiasi kikubwa na Prof. Kabudi, ambayo aliyafanya bila ya kushirikisha wadau wa sekta na wataalam wa Wizara ya madini kikamilifu.

Kabla sijaenda kwenye makosa yaliyofanyika, napenda nieleze wazi kuwa mimi ni mtaalam mwanasayansi kwenye sekta hii ya madini wa kiwango cha kimataifa ambaye nimekuwa nikijishughulika na usimamizi, uendeshaji, upatikanaji wa miradi ya madini katika nchi nyingi. Lakini pia nimekuwa nikishiriki kwenye upatikanaji wa mitaji kutoka soko la mitaji la Australian Securities Exchange (ASX) kwaajili ya uwekezaji kwenye miradi ya madini. ASX ndiyo soko kubwa kabisa Duniani kwaajili ya upatikanaji wa fedha za kuwekeza kwenye miradi ya madini. Ni kwa kupitia soko hili, matajiri wa mataifa kama Singapore, Hong Kong, Japan na Malaysia, huweza kuwekeza katika miradi ya madini iliyopo Afrika. Kwa hiyo ukilikosa soko la Hisa la Australia, utakuwa umekosa mitaji kutoka mataifa mengi, na siyo Australia pekee yake.

Madini yapo mataifa mengi Duniani. Na kila wakati madini hugundulika. Leo hii hata mataifa ambayo hapo awali hayakuwahi kufikiriwa kuwa na dhahabu, kutokana na teknolojia kukua ugunduzi wa migodi mipya umekuwa ukipatikana katika mataifa hayo.

Tanzania hatuna madini ya aina yoyote ambayo hayapatikani mahali pengine Duniani. Madini pekee ambayo tumekuwa tukizungumzia kuwepo Tanzania tu ni Tanzanite lakini kitaalam huwezi kusema kuwa madini ya Tanzanite hayapo mahali pengine Duniani. Tanzanite ni sapphire ambayo tofauti na sapphire nyingine, yenyewe ndani yake ina vanadium. Na wala Tanzania, katika uzalishaji wa dhahabu, hatuyakaribii mataifa kama ya China, Australia, South Africa, Peru, Mexico, Brazil, US, Russia au Indonesia. Nimeyasema haya ili Watanzania, na watu wengine kama akina Prof. Kabudi wajue kuwa hatupo pekee yetu Duniani wenye madini, na wala Dunia haiwezi kusimama kwa sababu hawatapata madini toka Tanzania.

Kutokana na uwepo wa madini katika mataifa mbalimbali Duniani, mataifa yote yamekuwa yakinyang'anyana wawekezaji wale wale wakubwa waliopo Duniani - New mont, Barrick, Anglogold, Kinross, Newcrest, Freeport, Polyus na Goldcorp. Ili uweze kuijenga sekta yako ya madini, kama Taifa, ni lazima uwe na wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya madini, na hawa kwa Dunia nzima hawazidi makampuni 15 hivi. Utafiti ni gharama kubwa, na risk ya kupoteza pesa ni zaidi ya 95%. Ni hawa wenye mitaji mikubwa tu ndio wanaoweza kugharamia utafiti. Hawa ndio hufanya utafiti, na pale wanapopata resources ndogo, huziacha kwaajili ya makampuni madogo, na kwa hapa Tanzania maeneo hayo mara nyingi huvamiwa na wachimbaji wadogo.

Kuna watu kutokana na kukosa uelewa wa sekta hii, hudiriki hata kusema kuwa makampuni yamekuwa yakiwafuata wachimbaji wadogo, wakati ukweli ni kinyume chake. Huwa hawaujui ukweli kwa sababu huwa hawajui makampuni yalianza utafiti kwenye maeneo husika wakati gani. Na kwa vile mchimbaji mdogo anapovamia tu huanza kuchimba, watu humtazama anayechimba bila ya kumtazama aliyetafiti alianza lini. Kwa hiyo usipokuwa na makampuni makubwa, makampuni madogo hufa, na sekta ya uchimbaji mdogo nayo hufifia kabisa maana wao hawafanyi utafiti, na hawatapata mahali pa kuvamia.

Makosa aliyoyafanya Kabudi Kwenye Mabadiliko ya Sheria:

1) Masharti Magumu ya Kufanya Utafiti
Utafiti ni risk kubwa. ndiyo maana dunia nzima anayefanya utafiti wa madini hubembelezwa na siyo kumburuza. Kabudi kwenye mabadiliko ya sheria ameweka utaratibu wa kutosafirisha sampuli za madini kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine bila ya kibali cha afisa wa madini mkazi. Maabara ya madini inayotambulika Tanzania ipo moja tu kwa sasa, SGS. Mara ya kwanza maabara za madini zilikuwa kama 4 hivi, na zote zilikuwa Mwanza. Zote kwa sasa zimeondoka, imebakia 1. Unapofanya utafiti kama wa drilling, unahitaji activities continuity, na hivyo samples hutakiwa kupelekwa maabara wakati wote, usiku na mchana. Kuisimamisha rig kusubiria majibu ya maabara, gharama yake huwa ni dola 400 kwa saa. Kabudi anataka usipeleke samples maabara usiku wala siku za mapumziko kwa sababu huwezi kupata kibali. Maana yake ulipe zaidi ya dola 9,000 kwa siku kwa kusimamisha rig. Lakini hiyo sheria ililenga nini? Najua yeye alifikiria kuwa madini yanaibiwa kupitia samples. Jambo ambalo kwa mtu anayejua kinachofanyika, fikra hizo ni za kijinga kabisa maana ni jambo lisilowezekana. Ufafanuzi wake unaweza kuwa makala nyingine.

2) Kufuta Reetention Licenses
Kufuta Retention licenses, nao ulikuwa ni upuuzi wa hali ya juu. Serikali iliweka aina hii ya leseni ili kuyapa nafasi makampuni ambayo yamefanya utafiti na kufikia muda wa kuanza kujenga migodi lakini muda wa leseni zao au umeisha au ni mfupi kiasi cha kutotosheleza kufanya taratibu za kupata leseni ya uchimbaji. Leseni hizi zilitolewa kwa kipindi cha miaka 2 tu na ziliweza kurudiwa kwa kipindi kimoja tu, baada ya hapo ni ama unaanzisha mgodi au unalirudisha eneo serikalini. Serikali ilipendelea zaidi kutoa leseni hizi kuliko kutoa extension kwa sababu annual rent ya leseni hii ilikuwa dola 2,000 kwa kila square kilometre kwa mwaka, ukilinganisha na dola 100 kwa square kilometre kwa mwaka kwa leseni za utafiti. Leseni nyingi za retention zilikuwa na ukubwa wa kati ya square kilometre 10 - 30. Hivyo makampuni yalikuwa yakilipa kati ya dola 20,000 - 60,000 kwa mwaka kwaajili ya leseni tu. Mwekezaji amepewa leseni ya awali, ametumia mamilioni ya dola kufanya utafiti, umempa Retention License, tena mara nyingi kwa kumshahwishi, amekuwa akilipa ada zote, wengine walibakiza miezi tu Retention Licenses zao ziishe, ghafla unafuta leseni ambazo zilikuwepo kwa mujibu wa sheria yenu, unawanyang'anya haki yao uliowapa, na kwa mujibu wa sheria yako hawajavunja sheria yoyote - hiki ni nini, kama siyo ujambazi katika biashara na uwekezaji? Kutokana na tendo la kuwanyang'anya wawekezaji leseni zao bila haki yoyote, na kuzuia usafirishaji wa makinikia kwa sababu za uwongo kuwa kulikuwa na dhahabu inayoibiwa, Tanzania kwenye soko la hisa la ASX, ilitajwa rasmi kama siyo mahali salama kwa uwekezaji wa mitaji ya nje. Leo hii huwezi kupata fedha kwenye masoko makubwa ya fedha Duniani kwaajili ya kuja kuwekeza Tanzania. Unaweza kupata fedha kidogo kutoka kwa matajiri binafsi lakini siyo kutoka kwenye masoko ya fedha.

3) Utaratibu Sumbufu wa Kupeleka Sampuli Maabara za Nje
Kabudi kwenye sheria mpya, aliondoa utarattibu wa zamani ambao maabara za maandalizi zilikuwa zikiandaa sampuli zinazotakiwa kwenda nje ya nchi na kufuata taratibu za customs kwaajili ya kuzipeleka nje. Kwa sasa, ni lazima kwanza zipitie GST halafu ziende customs. Hizi samples, zile kwaajili ya Fire Assay au Aqua Regia (sample pulps) kila moja huwa na uzito wa 50 - 100gm; na zile kwaajili ya MET huwa kati ya 2 - 20kg kila moja. Lakini kwa nini uweke huo utaratibu mgumu? Maana kila ukiritimba unaouweka unaongeza business cost. Sababu ni ujinga ule ule kuamini kuwa kuna wizi wa madini unafanyika kupitia sampuli za madini. Ni fikra za kijinga kabisa za mtu asiyejua nini huwa kinafanyika kwenye suala la samples. Ni mada nyingine, kuna wakati nitaelezea.

4) Kodi za Ajabu
Hapo awali tulikuwa tunatoza mrabaha wa 3%, corporate tax ya 30%. Kikwete alikuja kuongeza mrabaha kwa kupitia majadiliano rafiki, mpaka kufikia 4%. Kabudi akapandisha kwa ubabe bila majadiliano mpaka 7%. Kwa nini alifanya hivyo? Nadhani aliamini kuwa 4% ni ndogo mno. Lakini nchi nyingine zinatoza nini? Mataifa karibu yote Mineral Royalty ni 0 - 5% tu. Ni Zimbabwe pekee yake ndiyo inayotoza 7%. Na hii inatozwa kwenye gross production value, haijalishi umepata faida au hasara. Kama mataifa mengine yanatoza kati ya 0 - 5%, kwa nini sisi tuliokuwa tunatoza 4% tuone kuwa tumekuwa tunaibiwa? Kwenye corporate tax, nchi nyingi zinatoza 20 - 30%. Zimbabwe wanatoza 28%. Kwa nini sisi tuliokuwa tunatoza 30% tuone kuwa tulikuwa tunaonewa? Naamini tuliongozwa na ujinga zaidi kuliko weledi.

5) Kufuta Usafirishaji wa Makinikia (Mineral Concentrate)
Kabudi kwenye mabadiliko ya sheria alifuta usafirishaji wa concentrates. Kwa nini alifuta? Naamini pia ni kwa sababu ya ujinga na kutotaka kushirikisha wataalam wa sekta hii. Kwanza hakuna kampuni inayopenda kusafirisha concentrates. Aina ya ore material, hasa inapokuwa na sulphides, humlazimisha mchimbaji kutafuta njia ya kuchenjua dhahabu inayokuwa imebanwa kwenye sulphides, na ambayo haitoki kwa njia za kawaida zilizozoeleka. Unatoa dhahabu huru (free gold), na ile iliyokuwa locked in, unafanya floatation kwa nia ya kutengeneza concetrates zitakazokuwa na dhahabu nyingi (mara nyingi ni kati ya 100 - 300g/ton, na siyo ule upuuzi walioutaja watu wa bandari kuwa concetrates zilikuwa na dhahabu 90%). Hiki ni kitu kinachofanyika Duniani kote. Zambia, Canada, Indonesia, Australia, Mali, Ghana, Brazil, etc, wote wanapeleka concentrates zao, hasa Japan. Kama hawa wote wanasafirisha concentrates, ni sababu gani inayotufanya sisi pekee yetu tuamini kuwa hawa wengine wote hawaibiwi isipokuwa sisi tu? Athari ya sheria ile mbaya ya Kabudi, deposits zote zenye refractory gold hazitaweza kuja kuwa migodi. Siku zote, kazi ya serikali inayoongozwa na watu wenye hekima ni kujenga mifumo na kuweka taratibu zinazorahisisha na kupunguza gharama za uwkezaji na biashara huku ikiangalia faida pana ya wadau wote.

6) Data Zote za Utafiti Kupelekwa Serikalini
Kabudi kwenye sheria yake ya mabadiliko, anayalazimisha makampuni yote yanayofanya utafiti nchini, kupeleka data za utafiti GST. Jambo hili halipo Duniani kote. Utafiti ni risk kubwa na ni gharama kubwa, na pia ni confidential information. Kampuni ya utafiti wa madini, asset yake kubwa ni data za utafiti. Ni hizo data ndiyo zimeifanya kampuni kutumia mamilioni ya dola. Wewe unasema wafanye utafiti, data wakupe wewe!! Haijawahi kusikika. Utaratibu uliopo mataifa mengi Duniani, kampuni hufanya utafiti, wakiamua kuanzisha mgodi, data zinaendelea kuwa zao, Wakiamua kulirudisha eneo serikalini, wanarudisha eneo, na wanaipatia serikali data zote. Kuyataka makampuni kukabidhi GST raw data ni kati ya hitaji la ovyo kabisa kuwahi kuwepo katika ulimwengu huu.

Makosa haya makubwa yaliyofanywa na Prof. Kabudi yana athari zifuatazo:

1) Taswira Mbaya ya Mazingira ya Uwekezaji ya Nchi Yetu
Leo huwezi kuwapata wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza Tanzania. Katika kipindi chote cha awamu hii, hakuna mwekezaji mkubwa (>U$500m), aliyeweza kuwekeza Tanzania, awe wa ndani au wa nje.

2) Kifo cha Makampuni
Makampuni yote ya madini yaliyowekeza Tanzania na ambayo yanafanya biashara kwenye masoko makubwa ya fedha, kutokana na mabadiliko yale ya Kabudi yalipoteza kati ya 30 - 60% kwenye capitalization ya makampuni kwa sababu yamewekeza kwenye mazingira hatarishi ya mitaji. Kupoteza capitalization ya kiasi hicho ni kuua kampuni. Makamuni haya yote, kwa kiasi kikubwa yameondoka Tanzania na mengine yamebakia tu kwenye vitabu vya serikali lakini kiuhalisia yameondoka na hayafanyi chochote nchini

3) Kulipa Fidia
Makampuni yote yaliyonyang'anywa maeneo kwa kufutiwa Retention Licenses zao, karibia yote yatataka kulipwa fidia na serikali au kufungua kesi za fidia kwenye mahakama za kimataifa. Tayari makampuni mawili yameipelekea notice serikali. Hata kwa mimi nisiye mwanasheria, nina uhakika wa over 99% kuwa serikali itashindwa katika kesi zote zitakazofunguliwa, na hivyo kutakiwa kulipa fidia

4) Kupungua kwa Mapato ya Serikali
Makampuni makubwa yanayochimba dhahabu kwa sasa, yataendelea kuwa hayo hayo. Lakini makampuni hayo yana uwezekano mkubwa wa kufunga migodi yao mapema zaidi kuliko muda uliotarajiwa kutokana na kuongezeka kwa gharama. Makampuni haya imebidi kuweka cutoff grades mpya ili kuendana na gharama za uzalishaji zinazochangiwa na kodi na tozo kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa. Na wala hakutakuja kuwa na miradi mikubwa mipya.

5) Kudumaa kwa Technology Transfer
Ujio wa makampuni makubwa kabisa yanayotumia teknolojia za kisasa kama Barrick na Anglogold, ulifanya watanzania wengi kupata teknolojia ya juu na ya kisasa kabisa Duniani. Leo hii, nchi zinazoongoza katika utaalam wa madini Afrika, ni South Africa, Ghana kisha Tanzania. Leo hii Watanzania wapo kwenye nafasi za juu kwenye miradi ya madini katika mataifa mbalimbali. Kuondoka kwa makampuni haya makubwa, kutalifanya Taifa kwenda kwenye udumavu wa maarifa kama ilivyokuwa zamani. Katika utaalam, wataalam wa Tanzania kwenye sekta hii, wapo juu maradufu kuzidi wataalam kutoka mataifa kama vile China. Mimi binafsi nimekuwa nikizunguka, pamoja na kazi nyingine, lakini nimekuwa nikitoa mafunzo kwa wataalam wa sekta hii. Wakati mmoja nilipokuwa nikitoa mafunzo kwenye mgodi mmoja wa Waingereza, nilikuwa na wanafunzi 84, na kati ya hao Waafrika walikuwa 29, Waingereza 34, Wairan 2, Waaustralia 2, Wacanada 3, Wachina 3, Wavietinam 5, Waindonesia 6

6) Athari nyinginezo
Nyingine ni zile za kawaida ambazo kila mwenye ABC ya uchumi anazijua - kama vile kupungua kwa ajira, business interactions, na uchangamshashaji wa uchumi, kupungua kwa fedha za kigeni (sekta hii na ya utalii ndizo zinazoingiza fedha za kigeni nyingi kuliko sekta nyingine zote)

NINI KIFANYIKE
1) Kufutwa kwa Mabadiliko
Sheria ile mpya ya Kabudi ifutwe. Na kama kuna haja ya kufanya mabadiliko, yafanyike kwa kushirikisha wadau wote, na yafanyike kwa njia ya maelewano

2) Retention Licenses Zirudishwe
Wamiliki wa Retention Licenses warudishiwe, na wapewe muda wa ama kujenga migodi au kuyarudisha maeneo wanayoyamiliki kwa serikali. Hata wauaji hupelekwa mahakamani kujitetea, lakini Retention License holders, walinyang'anywa rights zao bila ya kupewa sababu, kupewa nafasi ya kurekebisha, kama kweli kulikuwa na makosa.

3) Majadiliano Rafiki
Wamiliki wa Retention Licenses wanaokusudia kuifikisha serikali/nchi kwenye mahakama za usuluhishi za kimataifa ili kulipwa fidia waalikwe kwenye mazungumzo ili wasifanye wanachotarajia kukifanya. Serikali ikiri ilifanya kosa, na iombe ikubaliwe kutolipa fidia yoyote kwa wawekezaji walioathirika na uamuzi wa kuwanyang'anya leseni zao kinyume cha sheria.

4) Wadau Wataalam Watoe Muongozo
Kama nilivyoeleza, sekta hii ina Watanzania wataalam waliobobea, na walioenea Duniani kote, wao kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara, watoe mwongozo kwa serikali namna ya kuihuisha sekta hii baada ya kuidumaza kwa miaka hii minne kutokana na mabadiliko Kabudi. Wataalam hawa watumike kufikisha kwenye masoko ya fedha Duniani na taasisi mbalimbali za kimataifa, kufutwa kwa mabadiliko yaliyoiharibu sekta. Jambo hili siyo geni. Huko Australia, kuna Waziri mkuu mmoja alianzisha Mining Super Profit Tax. Mwanzoni wananchi walimshangilia. Baadaye madhara yalipoanza, wananchi walimchukia Waziri Mkuu na kumwondoa madarakani. Waziri Mkuu mpya akaifuta hiyo kodi, na baada ya muda sekta ya madini ilirejea kwenye utengamano.

JUMUISHO

1) Kuwa msikivu na hekima, siyo unyonge au udhaifu, sawa kama ilivyo, kuwa katili siyo ushujaa

2) Hakuna nchi hata moja iliyowahi kuendelea kwa kuwategemea watu wake tu. Mchangamano wa watu, makampuni na taasisi za mataifa mbalimbali ndiyo hujenga Taifa ka kasi. Mfano mzuri wa karibu ni Dubai, South Africa, Nigeria, Botswana. Kwa upande mwingine, tujifunze toka China. China chini ya kiongozi wao Mao, na mfumo wao wa Maoism, uchumi wao ulikuwa wa kujifungia. Miaka yote waliendelea kuwa Taifa duni, hata nguo wakivaa zenye viraka magotini na makalioni. Mwishoni walirejewa na akili, wakaufungua uchumi wao kwa Dunia. Makampuni ya America na Ulaya, yakawekeza huko kupindukia, hata kuufanya uchumi wa China kupaa. Ni uwekezaji huo ndio ulioingia na teknolojia ambayo Wachina mpaka leo wamekuwa wakiiga kwa kasi kubwa. Japo makampuni makubwa yaliyopo China hayamilikiwi na Wachina, lakini makampuni hayo yameifanya China kukua kwa kasi kiuchumi na kitekinolojia.
 
Bams,
Hongera Mleta Mada. Hizi ndo thread zinazotakiwa kuwepo humu sio mapambio ya kusifu na kuabudu.

Ushauri wangu kwa Mzee Magu- angalia sana mawazo ya wasomi ya namna hii. Mtu anayekushauri tena kwa id isiyotambulisha yeye ni nani ni mtu mzuri zaidi kwa sababu hatarajii fadhila kuliko yule anayekushauri kwa kujionesha ili mkono uende kinywani.
 
Mbona mageuzi ya sharia hii yameleta neema au mimi naona opposite?

 
Hongera Mleta Mada. Hizi ndo thread zinazotakiwa kuwepo humu sio mapambio ya kusifu na kuabudu.

Ushauri wangu kwa Mzee Magu- angalia sana mawazo ya wasomi ya namna hii. Mtu anayekushauri tena kwa id isiyotambulisha yeye ni nani ni mtu mzuri zaidi kwa sababu hatarajii fadhila kuliko yule anayekushauri kwa kujionesha ili mkono uende kinywani.
Mwajitekenya na kucheka wenyewe, mtapata taabu sana vibaraka vya wanyonyaji, zoeeni tu, waambieni wazoee, hakuna mali ya Tanzania itavunwa kivile tena na tuko tiari kupay the price "wapumbavu" nyie mlotusababishia, tumefunga mikanda.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mwajitekenya na kucheka wenyewe, mtapata taabu sana vibaraka vya wanyonyaji, zoeeni tu, waambieni wazoee, hakuna mali ya Tanzania itavunwa kivile tena na tuko tiari kupay the price "wapumbavu" nyie mlotusababishia, tumefunga mikanda.

Sent using Jamii Forums mobile app
Asante ndugu. Kuna kesi mbili tayari zinatarajiwa kufunguliwa. Natumai hela zitakazolipwa zitakuwa sio za watanzania.

Sidhani kama upeo wako wa kifikiri uko sawa. Samahani sana
 
Hakuna kipya ulichoandika kwa sisi tunaoijua sekta hiyo vilivyo.

Bandiko Limekaa kiushabiki sana..

ili update balance nzuri ungeleta takwimu za mapato ya serikali kabla na baada ya mabadiliko ya sheria.

Acheni kutumika ovyo Vijana..
 
Kijana wangu, mimi siyo kijana. Nipo kwenye sekta hii katika ngazi ya kimataifa kwa miaka 23 sasa. Na mimi kama mtu binafsi sidhuriki na mabadiliko yaliyofanywa. Watakaodhurika ni Watanzania, wengi wao ni wale wasiojua hata kinachoendelea. Unaweza kuwa na mawazo tofauti, ukawa sahihi au vinginevyo lakini ni vizuri kuongozwa na weledi kuliko ushabiki.
Hakuna kipya ulichoandika kwa sisi tunaoijua sekta hiyo vilivyo.

Bandiko Limekaa kiushabiki sana..

ili update balance nzuri ungeleta takwimu za mapato ya serikali kabla na baada ya mabadiliko ya sheria.

Acheni kutumika ovyo Vijana..
 
Mleta mada alikua wapi wakati tunapigwa na utaalam wake. Wazungu walikua na mahesabu ya aina mbili, moja ya kuwasilisha TRA, nyingine za kuwasilisha London stock exchange.

Hizo za Lse ndio sahihi, TRA wakazidaka huyo mtaalam wa miamba hakusema kitu Inazlishwa kilo 100,imaandikwa kilo 10,mtaalam hakufungua thread Mchanga unasafirishwa,tumaambiwa hauna kitu,umekamatwa ukapimwa wote umeonekana ni mali tupu

Imebidi tubadili sheria tulinde rasilimali zetu,na bado wawekezaji wanakuja wakiwemo Barrick,lakini bwana mtaalam wa miamba anatuletea upupu.

Hakuna anaelazimishwa kuwekeza,madini hayaozi watayakuta wajukuu zetu
 
Umeandika maelezo mengi lakini umeshindwa kuweka takwimu kabla ya mabadiliko ya sharia, sekta ya madini ilikuwa inaliingizia taifa kiasi gani cha fedha za kigeni na mara baada ya mabadiliko hayo ya sharia ya madini taifa limeingiza kias gani cha fedha.

Uko sahihi katika hoja yako, sasa tuangalie unachokisema. Kuna uwezekano mapato yakaongezeka kwa muda mfupi kwakuwa kuna rafu zimefanyika, lakini ndani ya muda mrefu tukaendelea kurudi nyuma kwani hatuna technology na hiyo iliyokuwepo itaondoka.

Naomba nikupe mfano halisi ulionitokea mimi. Nilikodi nyumba kwa mtu mmoja nikawa nafanya biashara ya vinywaji, nyama choma na chakula. Mwenye nyumba mbali ya kodi niliyokuwa namlipa, kwenye nyumba yake akawa anaendesha biashara ya guest. Kadiri siku zilivyokuwa zinaenda mwenye nyumba akawa anapata wivu kuwa napata sana, ikabidi awe anapandisha kodi tofauti na makubaliano ya awali. Na tatizo hasa ilikuwa anaona napata sana. Yeye na familia yake wakakaa wakashauriana kwamba nalipa kodi kidogo, hivyo niongeze au niachie nyumba yao. Baada ya mahesabu nikaona hailipi naikachia nyumba yao. Basi mwenye nyumba na familia yake wakaendelea na biashara niliyoiacha. Ni kweli siku za mwanzo walipata kuliko nilichokuwa nawalipa maana bado jina langu lilikuwepo. Lakini baada ya muda biashara ikaanza kuwashinda, wateja wakakimbia, hata kile nilichokuwa nawalipa wakawa hawapati. Wakajaribu kuniita lakini niligoma.

Tuache hayo ya hadithi binafsi, ni kweli ndani ya huu muda mfupi tunaweza kuona tumepata mapato fulani, lakini ndani ya muda mrefu tunawezaje kuendelea kuinua hiyo sekta? Tuna nguvu za kweli kuwekeza katika sekta hiyo? Kama bado tunapambana na kuwaelimisha watu kutumia vyoo na kunawa mikono baada ya kutoka chooni, tutaweza kuwekeza vyema kwenye sekta hiyo? Hatukatai kulinda rasilimali zetu, lakini mbinu tunazotumia ni sahihi kupata tunachotaka?
 
Back
Top Bottom