Maandamano haya yamefanyika jana Jijini DSM kwa wanafunzi wa shule za sekondari na za msingi.
Ni nadra sana kusikia wanafunzi wa shule za sekondari na za msingi wanaandamana kupinga kitu, je?huu ni mwanzo wa enzi mpya Tanzania?
Soma ujumbe wa Mabango yao ni mkali sana , kuna nini kinakuja?
Taarifa ya gazeti la mwananchi,.
Date::8/1/2008
Wanafunzi waandamana kupinga nauli mpya Dar
*Wataka mafisadi wafilisiwe fedha zikanunue magari
Kizitto Noya na Festo Polea
MAMIA ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam jana waliandamana hadi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro kupinga ongezeko la nauli yao kutoka Sh50 hadi Sh100.
Wanafunzi hao walihoji sababu za serikali kuwaongezea nauli wakati imeshindwa kuwafilisi watuhumiwa wa ufisadi na kutumia fedha walizoiba kununua magari kwa ajili yao.
Katika maandamano hayo yaliyoanza majira ya saa 5:00asubuhi wanafunzi hao wakiwa na mabango walipinga kulipa nauli hiyo na kushinikiza serikali iwakubalie waendelee kulipa Sh50.
Baadhi ya mabango yalisomeka: "Wafilisiwe Chenge, Mkapa, Karamagi na Yona tuletewe mabasi ya shule, J.K utawala umekushinda, Tulipe Sh100 kwa lipi uliloboresha?".
Mabango mengine yalisomeka: "Tumegundua Kandoro na askari wake pia mafisadi, Heri Makamba kuliko Kandoro, Bora Mkapa kuliko Jakaya na imekuaje hatuna kazi na tulipe Sh100 huku polisi wanapanda bure"
Mbali na mabango hayo wanafunzi hao walikuwa wakiimba nyingi za hamasa kulaani vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, wakidai kuwa ndivyo vinavyochangia ugumu wa maisha na kupanda kwa nauli.
Baadhi ya nyimbo hizo walizokuwa wanaimba zilikuwa zinasema: "Wawafilisi mafisadi watununulie magari, usiseme Tanzania, sema kaburi la Waafrika, mara kumi Makamba kuliko Kandoro...?"
Kwa zaidi ya nusu saa, polisi wa kawaida walikuwa wakisukumana na wanafunzi hao kuwazuia wasiingie lango kuu la ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambako walitaka kwenda kumwonyesha mabango yao na kumtaka atoe msimamo mbadala kuhusu nauli ya wanafunzi.
Vurugu hizo ziliwafanya askari hao kuomba msaada wa Kikosi cha Kutuliza ghasia (FFU), ndipo zaidi ya askari 30 wakiwa na rungu, bunduki mabomu ya machozi na gari la maji ya kuwasha waliwasili katika eneo hilo saa 5:57 asubuhi.
Hata hivyo askari hao ambao walionekana kujiandaa kupambana nao, waliofika katika eneo hilo kwa magari mengine matatu, hawakuweza kutumia silaha hizo wala kuwafukuza wanafunzi hao kwa nguvu baada ya kuona kuwa hawakuwa wamevunja amani.
Wanafunzi hao waliondoka kwenye lango kuu la ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuziba Barabara ya Kawawa huku wakiendelea kuimba na kunyanyua mabango yao jambo ambalo liliwapa kazi ya ziada askari hao.
Wakati wanafunzi hao wakiendelea kuimba na kuonyesha mabango yao nje ya ofisi za Mkuu wa Mkoa ambako kazi zilisimama , viongozi wao walikuwa ndani wakikutana na maafisa wa ofisi ya RC, kindo ambacho kilitafsiriwa na wanafunzi wenzao kuwa ni batili wakidai kuwa wana njama za kutaka kuwahujumu.
Zaidi ya mara tatu viongozi hao walitoka kwenye mkutano huo na kujaribu kuwatuliza wanafunzi wenzao, lakini ushauri wao ulionekana kugonga mwamba kwa sababu ya kukosa imani nao na kisha wakaamua wawachague wawakilishi wengine wa kuungana na viongozi hao katika mkutano huo.
"Wanafunzi mpo?," aliuliza Desemba Malaki mmoja wa viongozi hao na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Ementi ya Kibamba.
"Tupo," walijibu kwa pamoja.
"Mkuu wa mkoa hayupo ofisini hivyo tunawaomba mrudi shuleni na sisi tunaendelea na mkutano na maafisa wake na makubaliano yoyote tutawangazia leo (jana) jioni kupitia vyombo vya habari," alisema
Nao wakamjibu kwa sauti ya juu: "Hatutoki hapa mpaka kieleweke".
Baada ya tangazo hilo lililotolewa kwa kipaza sauti cha FFU, viongozi hao na wawakilishi wa wanafunzi waliondoka kwa gari la polisi kuendelea na mkutano huo katika shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa.
Kuondoka kwa viongozi hao kuliibua upya fujo baada ya baadhi ya wanafunzi kudandia gari hilo huku wengine wakilizuia kuondoka, wakitaka tamko la kupunguzwa nauli litolewe hapo hapo.
Mpaka tunaondoka katika shule ya Benjamin Mkapa saa 7:00 mchana, mkutano huo ulikuwa haujaanza.
Awali akizungumza na gazeti na hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wa Shule za Sekondari nchini (TASSA), Augustin Matefu, alisema maandamano ya wanafunzi hao sio sahihi kwani tayari mamlaka zinazohusika na nauli zimekubali kufanya mazungumzo nao na kutafuta uwezekano wa kupunguza nauli hizo.
"Sisi juzi (majuzi) jana (juzi) na leo (jana) tulikutana na Kamanda wa kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kujadili suala hilo na tumekuja hapa kuwatuliza wenzetu. Mimi nasema sio sahihi kuandamana, kwani suala hilo liko kwenye mazungumzo," alisema.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alijaribu kuwasihi wanafunzi hao na kuwataka kuchagua viongozi iliwakazungumze na Sumatra kuhudu suala hilo, lakini haikusaidia.
Kwa upande wa Kamanda Kova, aliwataka wanafunzi waliounda umoja wa wanafunzi huo kufuata taratibu za maandamano ili waandamane.
Wanafunzi wakifuata masharti waliyopewa sisi hatuna tatizo kwani kazi yetu ni kuwalinda, lakini sasa hatutoi kibali cha kuandamana, tunataka watimize masharti kwamba maandamano yao yatakuwa ya amani, alisema Kova.