[h=3][/h]
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, amewahimiza wananchi visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni juu ya Katiba mpya na kkuwa huru kueleza aina ya Muungano wanaoutaka.
Akiwa katika ziara ya siku moja ya kukagua uhai wa chama chake kisiwani Pemba jana, Maalim Seif, alisema fursa ya kutoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni adimu na itakuwa si jambo la busara kwa wananchi kutoitumia vema kwa maslahi ya Zanzibar.
Aliwaambia wananchi kutoka majimbo ya uchaguzi ya Mgogoni na Micheweni waliokusanyika huko Mapofu Wingwi, mkoa wa Kaskazini Pemba kuwa, katika miaka 48 ya muungano wananchi hawajapata fursa kama hiyo, hivyo wasikubali kuitupa, kwani inaweza isitokee tena katika muda ujao wa uhai wao.
Kwa mtazamo wangu ajenda kuu kwa Wazanzibari katika mchakato wa kuandika Katika mpya ni muungano, kwa sababu Zanzibar inayo Katiba yake ya mwaka 1984, alisema Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Aliwakumbusha wananchi kwamba, Katiba ya Zanzibar inajumuisha mambo mengi yanayogusa maslahi ya Wazanzibari, kama vile haki za binaadamu na mgawanyo wa madaraka.
Mwakilishi wa Mgogoni, Abubakar Khamis Bakary kwa upande wake aliwataka wananchi kuwa na imani na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema wananchi wawe na imani kwa sababu kisheria tume hiyo itaheshimu maoni yao na kwamba hakuna namna utendaji wa chombo hicho unaweza kuruhusu udanganyifu.
Source: Nipashe