Lula wa Ndali Mwananzela: Katiba yetu inawapa haki Mashoga, je hili tunalijua? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Lula wa Ndali Mwananzela: Katiba yetu inawapa haki Mashoga, je hili tunalijua?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Adolf Hitler, Nov 11, 2011.

 1. A

  Adolf Hitler Member

  #1
  Nov 11, 2011
  Joined: Nov 4, 2011
  Messages: 50
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mwandishi mahiri wa safu ya HOJA YANGU katika gazeti la Raia Mwema Lula wa Ndali Mwananzela ameibuka na hoja fikirishi kuhusu ushoga nchini Tanzania huku akipangua hoja uchwara za akina Membe na Kikwete na kuweka bayana kuwa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inawapa haki mashoga.....SOMA MAKALA KAMILI HAPA

  [h=1]Sheria ipo, tumewahi kuwashitaki mashoga?[/h]
  Lula wa Ndali Mwananzela


  ANGALIZO: Makala hii imekusudiwa hasa kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 au zaidi. Tafadhali kama ni mzazi au mlezi angalia kama ni sahihi kwa mtoto wako kuisoma - Mhariri
  Kwa kweli wakati mwingine ukisikiliza majibu ya viongozi wetu na hata wananchi wengine unaweza kuona jinsi tulivyo na kazi kubwa sana ya kuweza kujenga hoja zenye ushawishi.
  Baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kusema kitu ambacho kimetafsiriwa kama kufunga misaada ya nchi hiyo na ‘haki’ za mashoga nilitarajia Serikali yetu ingejenga hoja ya uhakika ya kumjibu Cameron. Nilitaraji jibu ambalo lingevuta fikara, kutupilia mbali mapendekezo ya Cameron na vile vile kuonesha kuwa Tanzania ni nchi yenye uvumilivu mkubwa.
  Badala yake lilitolewa jibu la kihisia lakini vile vile ambalo halikuwa linaelezea kabisa kuwa nchi yetu ni nchi ambayo inalinda haki za kibinadamu bila kubagua jinsia zao, rangi zao, au mvuto wa kijinsia.


  Ni makusudio yangu katika mjadala kuchangia mawazo machache ambayo yatawasaidia watu wengine vile vile wanapoangalia suala hili la ushoga katika jamii yetu ili tunapozungumza tuzungumze kama watu ambao wana ujasiri wa kuuita ukweli ukweli na tusizungumze kama tulioshtukizwa na hivyo kupoteza ule uthabiti wa kiakili ambao tumejaliwa na Mwenyezi Mungu.
  Mjadala juu ya ushoga hauepukiki na hauishi kwa kuupuzia. Wengi wetu tumekerwa sana na kauli ya Cameron na hata ufafanuzi wake wa baadaye ambao alionekana kutaka kutumia uombaomba wetu kama njia ya kulazimisha Taifa zima tukubaliane na kile ambacho wengi tumekitafsiri kama ‘kukubali ushoga’.


  Uamuzi wa Tanzania kutambua au kutotambua ‘haki’ za mashoga ni uamuzi wetu sisi kama taifa. Hatuwezi kuamuliwa au kushurutishwa na watu wengine. Hili hata hivyo ni rahisi sana kulisema kuliko kulitekeleza kwani kuna mambo mengi Serikali hii imefanya tayari kwa mashinikizo ya nchi za nje.
  Tuangalie kwanza mambo yafuatayo ili tuweze kujenga msingi mzuri wa kujua ni nini tunakikataa na kwa nini tunakikataa na vile vile kuweza kuona sisi wenyewe ni vitu gani tunaweza kujadiliana bila kulazimishwa na taifa jingine.


  Ushoga upo na mashoga wapo
  Tunaweza tusipende kutambua ukweli huo. Labda kwa sababu tunaombea kuwa ushoga utoweke, tunaona ushoga ni kinyaa na uchafu mkubwa na labda kwa sababu tunaamini kabisa mioyoni mwetu kuwa ni kinyume cha maumbile na makusudio ya Mungu.
  Hayo yote yaweza kabisa kuwa sahihi. Lakini hayaondoi ukweli kuwa ushoga upo. Ushoga upo siyo Tanzania tu lakini karibu nchi zote duniani. Na hivyo tukisema mashoga wapo hatusemi kitu cha ajabu.
  Wengi tu tunawajua, tunawacheka mitaani na wakati mwingine tumewazoea na kuwatunzia siri zao. Ndio sababu hata sheria zetu zinakataza vitendo vya ushoga kwa sababu inatambua kuwa vyaweza kufanyika. Vile vile watu wanaona vingi kupitia mitandao, filamu, luninga na hata kwenye burudani mbalimbali watu wanaona vitendo vya kishoga.
  Kwa hiyo jambo la kwanza ambalo sisi sote tulitambue – hata kama hatupendi kukiri – ni kuwa ushoga upo na mashoga wapo. Ili tuweze kuwajibu vizuri watu kama kina Cameron na vile vile kuelewa wenyewe jamii yetu ni lazima tukiri ukweli huo – USHOGA UPO na MASHOGA WAPO. Hili la kwanza.


  Ushoga ni kuvutiwa kingono watu wa jinsia moja
  Kuna watu wanafikiria ushoga ni mwonekano wa nje (physical appearance). Hivyo mwanamume ambaye anaonekana ‘laini laini’ au anazungumza kwa upole sana anaweza kudhaniwa kuwa ni ‘shoga’ au mwanamke ambaye anaonekana amegangamala kama mwanamume anaweza kudhaniwa ni ‘shoga’. Kuna watu wamewahi kushangazwa sana kuwa yule waliyemdhania shoga kumbe siye na yule waliyemdhania kuwa ni aliyenyoka ‘straight’ kumbe siye.
  Ushoga siyo jinsi mtu anavyozungumza, siyo mtu anavyovaa, anavyocheka au hata jinsi anavyotembea. Wapo watu ambao kutokana na kuzaliwa kwao wanachukua ‘sifa’ –traits- nyingi za kike (wanafanana na dada zao au hata mama yao) na wanaonekana wako ‘wa kike’ lakini hawavutwi na wanaume bali wanavutwa na wanawake.
  Hili pia ni kweli kwa wanawake ambao wanaonekana wamechukua sifa za kiume zaidi lakini kijinsia wanavutiwa na wanaume vile vile na wanajitambua kuwa ni wanawake.


  Ushoga ni kuvutiwa kijinsia au kingono na watu wa jinsia ile ile. Hapa ndipo ulipo msingi wa neno homosexual. Neno ‘homo’ linatoka kwenye Kigiriki likimaanisha ‘kufanana” na ni tofauti na neno ‘homo’ linalotumika katika Kilatini ambalo lina maana ya ‘mtu’.
  Hivyo jamii ya binadamu inaitwa “homo erectus” maana yake “mtu mwenda wima” au “homo sapiens” yaani “Mtu mwenye akili, ufahamu”. Hivyo ‘homo’ ambayo inatumika kuelezea ushoga inahusiana hasa na mvuto wa watu wa jinsia moja.
  Hii ina maana ya kwamba wale wanaovutiwa kimwili na watu wa jinsia zao na wakaenda mbele na kujihusisha na vitendo vya kingono na watu wa jinsia zao hao ni mashoga. Kwa Tanzania na sehemu yetu ya Afrika Mashariki labda na sehemu kubwa ya Afrika tunafikiria mashoga ni wale wanaume wanaoingiliwa na wanaume wenzao tu, lakini wale wanaowaingilia si mashoga. Hii si kweli.
  Yeyote ambaye anatafuta kujamiiana na watu wa jinsia yake huyo ni shoga haijalishi anaonekana kama mwanamke au ana misuli; haijalishi kama ameoa au kuolewa, haijalishi anavaa suti au kaptula! Hili la pili


  Shoga shoga au shoga shosti?
  Kwa upande wa dada zetu mambo ni hivyo hivyo. Wapo wanaovutiwa na wanawake wenzao na wengine wameenda mbele na kuvitekeleza vitendo hivyo. Hawa nao ni mashoga. Huu ni ushoga ule wa kuvutiwa na mtu wa jinsia yako. Na hawa vile vile haijalishi kama wameoolewa au hawajaolewa, wasomi au si wasomi, wana watoto au hawana alimradi wamejitambua kuwa matamanio yao ya kimwili ni kwa wanawake wenzao.
  Bahati nzuri (au mbaya) ni kuwa neno shoga kwa msingi kabisa linahusiana na urafiki wa karibu sana. Ni urafiki wa kina dada katika kusaidiana, kuheshimiana na kuwa pamoja. Hivyo mara nyingi watu hawashtuki wakisikia mtu kasema “naenda kwa shoga wangu” kwani maana yake ya kawaida ni kuwa anaenda kwa rafiki wa kike wa karibu bila kumaanisha suala la kuvutiwa kijinsia.
  Sijui kama neno hili litaendelea sana hivi – nadhani pole pole limeanza kubadilishwa na neno “shosti” na labda itakuja kupaswa hivyo ili neno ‘shoga’ lichukuliwe na kutafsiri neno ‘gay’ la Kiingereza kumaanisha mashoga kama watu wale wanaovutiwa na watu wa jinsia zao.


  Wapo mashoga Watanzania
  Sasa baada ya kusema hayo hapo juu jambo jingine la kulisema ambalo ni kweli ni kuwa wapo mashoga Watanzania. Sasa hili silisemi kama tusi na hii si siri. Watu wote wazima ambao mnanisoma hapa mnajua ninachosema ni cha kweli. Wapo mashoga Watanzania.
  Kwa vile hakuna chombo ambacho kinaweza kuweka takwimu wazi za mashoga kwa mbali tunaweza kuona linapokuja suala la virusi vya ukimwi na ukimwi ambapo mojawapo ya tabia ambazo zinachangia kuenea kwa virusi vya ukimwi ni vitendo vya wanaume ‘wanaolala’ na wanaume wenzao (mashoga). Na ukiondoa hilo bado tunajua wapo mashoga Watanzania.
  Na ninaposema “wapo” simaanishi mitaani tu; wapo maofisini, kwenye wizara, walimu, wanajeshi na hata kwenye siasa. Wengine ndio wale wale wanaopinga sana ushoga hadharani lakini kwa siri ni hao hao. Wapo hata watu wenye madaraka makubwa tu ambao wana mashoga sehemu na mitaani watu wanajua! Hili la tatu.


  Sasa haya mambo matatu ni mambo ya msingi kuyaangalia na yanaweza kabisa kuzua mjadala wa kutosha tu. Lakini hakuna ubishi kuwa ushoga upo, mashoga wapo na wapo mashoga Watanzania. Tunaweza tusipende au hata kukubali ukweli huu lakini ni ukweli wa jamii yetu ni ukweli wa nchi yetu. Hatuhitaji David Cameron au Barrack Obama au mtu mwingine yeyote kutuambia ukweli huu. Sasa kama hayo matatu tunakubaliana tuangalie mengine yanayofuatia.


  Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu
  Tanzania imeridhia Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la 1948. Tanzania kama zilivyo nchi nyingi duniani, tumeridhia Azimio la Umoja wa Mataifa ambalo ni msingi wa Katiba nyingi duniani hasa linapokuja suala la “haki”.
  Hapa ni lazima tutofautishe kile kinachoitwa “haki za binadamu” na “haki za raia” yaani “human rights” na “civil rights”. Tunapozungumzia haki za binadamu tunamaanisha tu kuwa mtu anazo hizo haki kwa sababu ni binadamu na popote anaposafiri haki hizo huambatana nazo. Ni haki ambazo nchi haiwezi kuzivunja ikabakia ikitambuliwa ni ya kidemokrasia au ina utu.
  Katika hotuba yake ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa siku tano tu baada ya kupata uhuru, Mwalimu Julius Nyerere, alisema kuwa “tutatumia Azimio lile kama msingi wa sera zetu za ndani na nje”.
  Na anaendelea kusema na hapa ninukuu kauli yake ya Kiingereza; “That Declaration confirms the right of every individual to many things, which we cannot yet provide for the citizens of our own country. In that respect this document, the Universal Declaration of Human Rights, represent our goal rather than something that we have already achieved”.
  Na akaendelea kusema “We accept without question as a basis, a basic article of faith that every individual has an equal right to inherit the earth, to partake of its joys and its sorrows and to contribute to the building of the sort of society which he desires for himself and also for his children”.  Ni kutoka hapo Nyerere akasema kitu ambacho ni muhimu leo hii miaka hamsini baadaye tujiulize – hasa katika mwanga wa haya tunayoyazungumza – kina ukweli kiasi gani. Alisema; “any apparent deviation from the articles of this Declaration will be an honest attempt on our part to balance conflicting interests while preserving the major principle itself. It will be in the light of this principle that we shall try at all times to determine our stand on every international issue which we shall be called upon to consider in this Assembly or elsewhere”.
  Kwa ufupi Nyerere alikuwa anaweka msingi kuwa kwenye suala la haki za binadamu na mara zote katika sera na mipango yetu mbalimbali tutaangalia haki hizi na pale tunapoona kuwa zinapingana na kanuni nyingine basi tutachukua lililo bora na hivyo kuacha sehemu ya kanuni za Azimio hilo. Hiyo siyo maana ya kudharau bali kuonesha kuwa kuna kanuni kubwa zaidi ya kuilinda.


  Kila Mtanzania ana haki sawa Kikatiba
  Katiba yetu katika fungu la tatu imeweka kile kinachojulikana kama “haki na wajibu muhimu”. Kimsingi ni katika kifungu hicho Watanzania wanalindwa si tu kwa sababu ni binadamu lakini vile vile kwa sababu ni raia wa Tanzania. Zipo haki mbalimbali zinazoanishwa kuanzia ibara ya 12 ya Katiba yetu hadi Ibara ya 32. Haki hizi wanazo Watanzania “wote”.
  Ninaposema wote nina maana ya kwamba kwa kuangalia Katiba wanawake, wanaume, wajane, walezi, wazinzi, waongo, matajiri, masikini, Waislamu, Wakristu na Wapagani. Wote wanalindwa sawa katika Katiba hii. Maana yake ni kwamba kwanza kabisa kutokana na ubinadamu wao na kutokana na uraia wao basi wanazo haki za msingi kabisa ambazo hawawezi kunyang’anywa kiholela.
  Baadhi ya haki ni usawa mbele ya sheria, haki ya kuishi, haki ya uhuru wa maoni, haki ya faragha na usalama wa mtu, haki ya kwenda mtu atakako na haki ya kuamini dini yoyote. Haki nyingine ni uhuru wa kushirikiana na wengine, uhuru wa kushiriki shughuli za umma, kufanya kazi, kumiliki mali na kupata ujira wa haki.


  Sasa hizi zote ni haki ambazo kila Mtanzania anazo. Hii ina maana ya kwamba shoga wa Tanzania anayo haki kama aliyonayo asiye shoga. Anaweza kwenda popote, kufanya kazi yoyote, kusoma popote, kupata mikopo na kumiliki mali. Tanzania haijaondoa haki hizi kwa Watanzania mashoga.
  Hili ni jibu letu la kwanza kwa wale wanaotaka kuionesha Tanzania kuwa haiheshimu haki za mashoga. Mashoga wanazo haki zile zile walizonazo Watanzania kwani zinalindwa kwenye Katiba.
  Leo shoga akipigwa anayo haki ya kwenda kushtaki, akiibiwa anayo haki ya kuita polisi, akiuawa kifo chake ni lazima kichunguzwe kwani kuwa shoga hakumuondolei Utanzania wake au utu wake.


  Sasa tatizo ni nini?
  Kama ukinisoma unaweza kuona kuwa yote hayo niliyoyasema yangekuwa ni rahisi sana kutekelezeka. Kama mashoga wangekuwa wanazo haki kama za Watanzania wengine mjadala uko wapi?
  Unaweza ukafikiria nilichokisema kuwa Watanzania wote wana haki sawa ndivyo ilivyo. Lakini ukweli ni kwamba Watanzania wengi wanaona kuwa hawana usawa japo kisheria usawa huo umehakikishwa. Kuna matatizo makubwa mawili naamini na haya nitayaacha wengine wayajadili na kama nilivyosema awali hatuhitaji mzungu kutuambia tufanye nini.


  Mashoga kuoana? – ah wapi!
  Hakuna mwamko wa wanaotaka mashoga wa Tanzania wawe na haki ya kuoana. Na hata hao Waingereza hawawezi kutuambia au kutushauri kitu kama hicho kwani hata wao katika nchi yao kama zilivyo nchi nyingi duniani hakuna haki kama hiyo.
  Jamii nyingi zinatambua kuwa haki ya kuoana ni haki inayoendana na kuwa na familia. Jamii ya Kiafrika – na ya Kitanzania – inaakisi kanuni ya asili ya ulimwengu yenye kutambua kuwa ndoa ni mahusiano kati ya mume na mke. Ndoa si tu makubaliano ya watu kuwa pamoja alimradi wakitaka. Ndio maana haturuhusu ndoa ya mtu na kaka yake au mzazi na mwanae.
  Jamii ndio inatambua ndoa katika mazingira yake. Kwa mfano jamii yetu inatambua ndoa ya wake wengi wakati jamii za Kimagharibi nyingi hazitambui hilo. Je wanaweza kuja kutuambia kuwa ili tupewe misaada ni lazima watu wote wawe na mke mmoja na mume mmoja?
  Hivyo, mojawapo ya changamoto za Katiba yetu mpya ni kuifafanua familia ni nini. Ninaamini ni jukumu letu sisi wenyewe kama jamii kutambua na kuweka maana ya familia jinsi ambavyo sisi wenyewe tunaamini sawasawa.


  Na sidhani kuna mtu yeyote ambaye ni shoga Tanzania ambaye anataka “ndoa” ipewe maana mpya maana hapo atakuwa anajaribu kuingilia msingi wa familia. Ukirejea ile hotuba ya Nyerere ya Umoja wa Mataifa ni kuwa kanuni ya msingi ya kati ya familia na haki za mashoga kama jamii itachagua familia na katika kufanya hivyo tunakuwa tumechagua kanuni ya msingi zaidi. Hili la ndoa za mashoga halina hoja katika Tanzania na sidhani kama kuna kiongozi wa nchi yeyote anayeweza kuiambia jamii nyingine maana ya ndoa ni nini.


  Sheria za kukataza ushoga zifutwe?
  Baada ya kuweka haya yote niliyoyasema ninaamini hoja pekee ambayo ipo na inatakiwa kujibiwa na Watanzania ni je, sheria zinazokataza vitendo vya ushoga zifutwe? Ikumbukwe hatuzungumzii “ulawiti au ubakaji” tunazungumzia vitendo vya hiari vya watu wawili wenye akili timamu na havimdhuru mtu mwingine.
  Sheria hizi zipo vitabuni tangu enzi za Waingereza lakini sijui ni mara ngapi watu wameshtakiwa kwa kuzizingatia. Wengi wanaoshtakiwa ni kwa makosa ya kulawiti lakini si makosa ya kuwa shoga.


  Ni sheria ambazo hazitekelezeki. Leo hii mtu akikutwa na kosa la ushoga anatakiwa kupewa kifungo cha angalau miaka 14 jela. Hivi kweli tuko tayari kuwafunga wanawake na wanaume ambao wanajihusisha na vitendo hivi na kuwagharimia jela?
  Yaani katika mambo yote yanayolisumbua taifa letu leo hii kweli suala la ushoga tunaweza kuliweka kama ajenda kubwa namna hii? Na tutathibitisha vipi mtu ni shoga? Kwa kumuona anavyovaa? Au anavyoangalia au itabidi tuweke kamera kwenye ‘vyumba’ Tanzania kuwakamata “wahalifu” hawa wakati tumeshindwa kuzuia uhalifu mwingine wa kawaida tu?
  Na tunaposema mtu ‘shoga’ na amefanya ‘uhalifu’ huo itakuwaje kwa wale wanaume ambao wanawaingilia wanawake zao kinyume cha maumbile – kitu ambacho nacho ni kosa – tutawakamata?


  Hivyo swali kubwa ambalo naamini linahitaji mjadala wa kiakili tu ni kwa namna gani tuzitupilie mbali sheria hizo zisizotekelezeka ili tubakie na sheria ambazo tunajua tunaweza kuzisimamia na ambazo tumeshaonesha kuwa tunaweza kuzisimamia.
  Lakini kama hatutaki kuzifuta kwa sababu tutaonekana tunahalalisha vitendo vya kishoga inakuwaje kama hatuwakamati ‘mashoga’ na hivyo kuonekana bado tunahalalisha vitendo hivyo hivyo?
  Je, tukifuta sheria hizi ambazo hazitekelezeki na kuacha suala hilo kuwa ni la watu binafsi tutakuwa tumetambua haki za Watanzania hao kuwa na faragha na usalama wa maisha yao?
  Kweli tunahitaji wazungu kutusaidia kuona hili?
   
 2. zumbemkuu

  zumbemkuu JF Bronze Member

  #2
  Nov 11, 2011
  Joined: Sep 11, 2010
  Messages: 9,004
  Likes Received: 586
  Trophy Points: 280
  mmmmmh! haya bwana, mjadala wa aina yake, nawasubiri wenye nguvu waje wajadili.
   
 3. p

  punainen-red JF-Expert Member

  #3
  Nov 11, 2011
  Joined: Nov 18, 2010
  Messages: 1,735
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Makala ya kufikirisha kweli...
  Pamoja na kuwa siungi mkono ushoga, nimeuliza mara kadhaa; Hawa akina membe, kikwete, serikali na jamii kwa ujumla imechukua hatua gani kukabiliana na ushoga hadi leo hii wawe na nguvu ya kuwabwatukia wageni wanaowapa changamoto ktk suala hili?!
   
 4. Tony Almeda

  Tony Almeda JF-Expert Member

  #4
  Nov 11, 2011
  Joined: Sep 18, 2011
  Messages: 397
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Huyu Membe anatafuta umaarufu tu, nchi ina matatizo lukuki, mafuta bei juu, shillingi imeshuka thamani, maisha yamekuwa magumu na matatizo chungu nzima. wanashindwa kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakela watanzania, wanakomalia starehe za watu.
  Mtu ameamua kujidhalilisha mwenyewe utu wake shauri yake, maadamu asilifanye hadharani.
   
 5. JamboJema

  JamboJema JF-Expert Member

  #5
  Nov 11, 2011
  Joined: Jun 14, 2011
  Messages: 1,148
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 145
  Nimestuka! Nilidhani Lula anatuambia katiba yetu inatambua mashoga... Kumbe kuwapa haki tu kama watanzania...That's fine. Hii ni sawa na jambazi alivyo na haki ndani ya katiba. Si haki ya kuwa jambazi. Uhhhh! Asante, nimeelewa...USHOGA UBAKIE HIVOHIVO KIMYAKIMYA SIO MTUTANGAZIE USHOGA WENU!
   
 6. Kiby

  Kiby JF-Expert Member

  #6
  Nov 11, 2011
  Joined: Nov 16, 2009
  Messages: 5,209
  Likes Received: 1,012
  Trophy Points: 280
  Kwanza ili niseje sahau naanza na kulijibu swali lako la ikiwa sheria zinazokataza vitendo vya ushoga zifutwe? Mi nasema zisifutwe, na kama kuna uwezekano zitiliwe mkazo zaidi. Katika makala yako nimekufuatilia sikuweza kuona kitu ulichokiona ambacho serikali haikukiona wakatika ilipopingana na kauli ya kameruni. Maana umesema kwa habari za kuoana mashoga sii kitu cha kuunga mkono, maana jamii inafahamu fika kwamba familia ni matokeo ya ndoa ya mke na mume. Hiyo pointi ndio iliyokuwa main pointi ya tamko la serikali kupitia Membe. Haki za binadamu ni kweli zinatambuliwa kama ilivyoainishwa katika katiba, na ndio maana hujaona katika vyombo vya seria (kutoa haki) wakibaguliwa, walevi, wazinzi, mabuya unga, malaya, mashoga na kadhalika. Kinachopingwa hapa ni kule kujaribu kuhalalisha magonjwa ya tabia kuwa haki ya kikatiba na kwa maana hiyo watu wa jinsia moja wawe na haki ya kufunga ndoa hadharani na haki hii itambuliwe na kila mtu wa taifa na hata watoto wetu huko shuleni wafundishwe kuijua katiba yao ikiwa ni pamoja na haki ya watu wa jinsia moja kuoana. Mahusiano ya jinsia moja ni miongoni mwa magonjwa ya tabia na sana sana huambukiza watu kwa kuona vitendo hivyo vya kinyume na maumbile vikifanywa na watu waliokwisha kuharibika akili na wasio waadilifu kimaumbile. Tatizo hili limechukua kasi wakati huu kwa sababu ya utandawazi. Na ndio maana hata ukienda katika upande wa dini utakuta Mungu alikuwa anakataa mfumo wa utandawazi kwa nia ya kuwalinda wale waadilifu dhidi ya ushetani. Ref. Kisa cha mnara wa babel. Sasa ikiwa serikali haitasimama kulinda haki ya watoto wa nchi yake kwa kisingizio cha wachache walioadhirika kiakili, ni nani atawalinda? Sasa tukija kwa huyu mtu mume anaemwingilia mme mwenzie nae mnataka kusema kaumbwa na maumbile ya kutamani uani? Hii sii asili acheni kuyafanyia vurugu maumbile. Jambo hili la ushoga linainjectiwa na watu wenye akili nyingi sana, tena wenye ushawishi. Ni mfano wa yule mwerevu na mtanashati na mjuzi wa bustani ya Eden aliyemwangusha hawa kwa kisingizio cha kumuelevusha. Ninyi nyote mnatambua ni nani huyu. Sisi kama taifa sasa tunachopaswa kufanya ni kujielekeza katika kufanya kazi zaidi na kukwepa kuwa tegemezi, hali inayopelekea kupewa masharti ya misaada kama mwanamke anaebembwa. Ukoloni tulishaushinda na privatization haina maana ya msaada zaidi ya makubaliano ya kibiashara kwa manufaa ya wawili waliokubaliana.
  MWISHO NISEME HIVI MAGONJWA YA TABIA SII HATA SIKU MOJA NI HAKI YA MTU.
  .
   
Loading...