Lindi: Wanachama wanne wa CHADEMA watupwa jela miaka 8

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,010
9,875
MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi, imewahukumu wanachama wanne kati ya sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutumikia kifungo cha miaka nane kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya makosa mbalimbali yakiwamo kuharibu mali zenye thamani ya Sh. milioni 22.2.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Consolata Singano, baada ya kuridhishwa pasipo na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Waliohukumiwa ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Majengo, Rajabu Hassani Mfaume (45) , Dadi Shayo (46), Hamisi Abdallah Seif Maleje (46) na Moshi Hamisi Mbelenje (26) wakazi wa Kata ya Majengo katika Halmashauri ya Mtama.

Kabla ya Hakimu Singano kutoa hukumu katika kesi namba 07/2020, washtakiwa walipewa nafasi ya kujitetea, ambapo kila mmoja kwa wakati wake aliomba aonewe huruma kwa madai ana familia inayomtegemea.

Baada ya utetezi huo, Mwanasheria wa Serikali, Godfrey Mramba, aliulizwa na Hakimu Singano, kama anazo kumbukumbu za makosa ya zamani kwa washtakiwa na kujibu hana, huku akiiomba mahakama kuwapa adhabu kali iwe funzo kwao na wengine wenye tabia za aina hiyo.

Mramba alidai kitendo cha kuharibu mali za umma si cha kiungwana, hakistahili kufumbiwa macho hivyo adhabu kali za kisheria zinahitajika kukomesha tabia ya aina hiyo.

Hakimu Singano akitoa hukumu kupitia vifungu mbalimbali vya kosa la kwanza kuharibu mali kila mmoja alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, la pili kuisababishia hasara taasisi ya umma kulipa faini ya Sh. milioni moja kila mmoja au kwenda jela miaka mitano.

Kosa la tatu na la nne kuharibu mali za watu binafsi aliwataka kulipa faini ya Sh. 500,000, wakati kosa la tano hadi la sita kujeruhi na kusababisha maumivu kwa watu wengine aliwahukumu kifungo cha miaka mitatu kila mmoja, kwa vile adhabu zinaenda kwa pamoja, watatumikia kifungo cha miaka mitano.

Mahakama hiyo pia imewaachia huru washtakiwa wawili, Fatuma Ibrahimu Kumwalu (45) na Fatuma Raphael Protas (45) wakazi wa Kata ya Majengo, Halmashauri ya Mtama, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa yaliyokuwa yanawakabili.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Serikali, Mramba kuwa Oktoba 28, 2020, katika Halmashauri ya Mtama siku ya uchaguzi mkuu, washtakiwa wakitambua wanachofanya ni makosa waliharibu kwa kuchoma moto Ofisi ya Serikali ya Kata Majengo na kusababisha hasara ya Sh. milioni 20.7.

Mramba alidai licha ya ofisi ya kata pia walichoma moto pikipiki moja aina ya Snoley 110 yenye usajili namba MC 600 CCG yenye thamani ya Sh. milioni 1.6 mali ya Arafa Shaha Saidi na kufanya jumla ya Sh. milioni 22.3.

Pia washtakiwa hao walidaiwa kuwajeruhi kwa kuwashambulia kwa mawe na fimbo maeneo mbalimbali ya miili yao watu watatu, akiwamo askari Polisi WP 7657 Ester Kalaminyo, Hamza Hassani Zamea na Haifu Hamisi Abdallah

Chanzo: NIPASHE
 
Mtamsababishia mbowe aendelee ku2mikia jela.

Tatizo la chadema, badala kumaliza tatizo kisha watulie, wanakuja wengine kuanzisha msala
Chadema kama chama ndio iliyowatuma hao kufanya huo uharibifu,au una maana gani kuhiusisha chadema na makosa binafsi ya watu?

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Tanzania ya sasa inahitaji watu jasiri kama nyinyi! Uchaguzi wa 2020 ulijaa upuuzi mwingi sana. Kiuhalisia hata hiyo hukumu ni ya uonevu tu.

Haiwezekani mgombea umeshinda kwa kura nyingi, halafu wakati wa kumtangaza mshindi, anatangazwa aliyeshindwa kutoka ccm huku akilindwa na mapoliccm! Hovyo kabisa.
 
Back
Top Bottom