Leo Spika anakera, kesho CAG, baadaye walalahoi! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Leo Spika anakera, kesho CAG, baadaye walalahoi!

Discussion in 'Tech, Gadgets & Science Forum' started by Pdidy, Aug 29, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Aug 29, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,136
  Likes Received: 5,571
  Trophy Points: 280
  Leo Spika anakera, kesho CAG, baadaye walalahoi!

  Godfrey Dilunga Agosti 26, 2009
  GWIJI wa kupigania uhuru wa maoni FranÁois-Marie Arouet, maarufu kama Voltaire aliyefariki 1778 akiwa na miaka 84, aliwahi kusema; "I do not agree with a word that you say, but I will defend to the death your right to say it." Kauli ya Voltaire ambaye aliwahi kutoroka Ufaransa kwenda Uingereza, ni ya kishujaa uliwenguni.

  Kwamba; tetea haki ya kuzungumza, hata kama hukubaliani na kinachosemwa.

  Kwa mantiki ya Voltaire, nimebaini mafisadi ni dhaifu mbele ya umma wa Watanzania wakiongozwa na makamanda wao. Udhaifu huo unajidhihirisha katika juhudi zao za kuziba midomo wapinga ufisadi, si kwa njia haramu kama ilivyozoeleka, bali kwa kutoa matamko kupitia taasisi zenye makuwadi wao.

  Hawana chembe ya ushujaa kama Voltaire, hawavumilii na hawatetei haki ya wengine kuzungumza. Kwa lugha ya mtaani mafisadi “hawajai mkononi” mbele ya nguvu za Watanzania wazalendo, ni wepesi. Siku zao zinahesabika na baadhi yao watakimbia nchi, siku na wakati utakapowadia.

  Lakini pia upo msemo (methali) maarufu wa Kiingereza; "It is not the size of the dog in the fight, it is the size of the fight in the dog" (kwenye mapambano (vita) cha muhimu si ukubwa wa mbwa, bali uwezo wake wa kupambana.

  Kwa mantiki hiyo, CCM ni chama kikubwa, lakini dhahiri hakiwezi kuongoza vita ya ufisadi. Kitaweza kufanya hivyo baada ya kung’olewa kwa sekretariati ya sasa, inayoongozwa na Yusuf Makamba, ambaye ni mtuhumiwa pia.

  Mwenendo wa CCM unadhihirisha ni chama kilichotiwa mfukoni na kuzingirwa. Kimezoea kupumua na kuvuta hewa ya ufisadi, ni vigumu kujiachia huru. Sehemu ya viongozi wake waandamizi ni watuhumiwa sugu wa ufisadi.

  Nitajadili njama za NEC-CCM kutaka Bunge liongozwe kwa maslahi ya mafisadi, kwa kutaka mijadala ya ufisadi isiachiwe kuumbua mafisadi.

  Kwa kuzingatia uamuzi wa NEC-CCM kuhusu Spika, maana yake maslahi ya mafisadi ni maslahi ya chama, kuwaumbua mafisadi ni kukiumbua chama na serikali. Vishindo vya wabunge dhidi ya watuhumiwa wa Richmond, ni kugusa maslahi ya chama hicho. Nitajidili hali hiyo kama ifuatavyo.

  Nafasi ya Bunge nchini

  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuhimiza kuongoza nchi kwa kuzingatia sheria. Akaonya; hatutaki kiongozi anayelala na mkewe nyumbani na kesho anafanya mabadiliko nchini. Mantiki hapa, ni nchi iongozwe kwa Katiba.

  Hasira au maslahi ya NEC-CCM bila kujali ni maslahi yenye uhusiano wa kifisadi, hayana uhalali wa kuvunja Katiba au kula njama kuhujumu Bunge. Kutoa tamko nje ya Bunge, ili kudhibiti mijadala bungeni ni kuvunja Katiba.

  Kutaka mijadala ya ufisadi iendeshwe kwa unyenyekevu, tabasamu, upole na upendo ni maelekezo (amri) yanayoingilia uhuru wa Bunge (contempt of parliament). Ingawa inachekesha, lakini labda siku moja NEC-CCM itataka wananchi mitaani wamkimbize mwizi au kibaka sugu kimya kimya. Watataka iwe hivyo, ili wakazi wengi zaidi wasiungane kumkamata mwizi wakisingizia kulinda haki zake (mwizi).

  Inashangaza viongozi hawataki kukubali ukweli kwamba; Uchaguzi Mkuu unapokwisha, chama tawala kinapoteza sehemu ya mabavu yake mbele ya Bunge na Serikali (vyombo vya umma). Kwamba, mfumo wa sheria za nchi ndiyo unaobaki kudhibiti vyombo hivyo, pamoja na viongozi wake. Ni mfumo wa sheria na si hasira au matakwa ya CCM.

  Ndani ya mfumo wa vyama vingi, viongozi waliopigiwa kura wanabaki kuwa wa umma, wanapepea bendera za Taifa, si za chama. Wameapa kuilinda Katiba ya Tanzania. Katiba inayohifadhi maslahi ya mwana-CCM, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, Yanga, Simba, Mtibwa au Kagera Sugar.

  Mwalimu Nyerere aliwahi kusema; “Tumekuchagua, tutakuapisha kwa Katiba, usipoitii tutakutambua kuwa ni msaliti.” Wasioilinda Katiba ni wasaliti. Tutafakari, NEC – CCM ina nguvu gani kwa mujibu wa Katiba, kiasi cha kuliamuru Bunge badala ya kulishauri.

  NEC haitambuliki ndani ya Katiba, na kwa mantiki hiyo haina ubavu wa kuamuru mihimili ya taifa (dola), likiwamo Bunge, ingawa inaweza kushauri. Nguvu za Bunge ni zaidi ya CCM, hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi. Kutumia chama, kutishia vyombo vya dola ni kuvunja Katiba.

  Nguvu za Bunge zinatamkwa hata wakati wa vita, lakini nguvu za NEC-CCM hazina nafasi katika Katiba iwe wakati wa amani au vita. Naandika kuonyesha kama kuna uhalali kikatiba, NEC-CCM kuamuru Bunge, badala ya kushauri. Mfano, Ibara ya 32 ya Katiba inaeleza mamlaka ya Rais kutangaza hali ya hatari.

  Kifungu cha tatu, katika Ibara hiyo kinaeleza Bunge linavyopaswa kushirikiana na Rais. Maana yake, vyombo hivi ni vya umma, vinawajibika kwa umma kama kipaumbele, wakati wa amani hata vita. Mbele ya umma, CCM inalinda maslahi ya wachache, lakini Bunge linalinda maslahi ya Watanzania wote.

  Spika na Bunge wanaongozwa kwa Katiba, na kanuni za Bunge, sio maelekezo au matakwa ya NEC-CCM. Katika Bunge, kuna kanuni za majadiliano, adhabu, kupitisha hoja, kumwondoa Spika, kumwondoa Rais au Waziri Mkuu na nyinginezo. Bunge limejitosheleza na kama kuna upungufu kanuni hurekebishwa.

  Mfano mwingine wa kupima ubavu wa Bunge na NEC-CCM mbele ya Watanzania, ni kifungu cha nne, ibara ya 32 ya Katiba, kinachotoa mamlaka kwa Bunge kumwongezea muda wa kubaki madarakani Rais, baada ya miaka mitano kwisha.

  Kifungu kinasema; “Iwapo Jamhuri ya Muungano inapigana vita dhidi ya adui na Rais anaona kuwa haiwezekani kufanya uchaguzi, Bunge laweza mara kwa mara kupitisha azimio la kuongeza muda wa miaka mitano… isipokuwa kwamba muda wowote utakaoongezwa kila mara hautazidi miezi sita.”

  Hivyo basi, utabaini si NEC-CCM, CHADEMA, CUF, TLP au NCCR-Mageuzi au kundi lolote nchini lenye nguvu za kumtisha au kumuamuru Spika na wabunge kutangulisha maslahi yake dhidi ya umma. Kinyume chake, Spika na Bunge wanashauriwa ili watende kwa kuzingatia sheria na kanuni.

  Spika na wabunge wanadhibitiwa kwa kanuni za Bunge, sio hasira au uamuzi wa NEC-CCM. Spika kama ilivyo kwa Rais, hata kama anatoka chama fulani, akishachaguliwa kuwa Spika au Rais anakuwa kiongozi wa umma. Kama hawafai zipo njia za kuwaondoa kisheria, si majungu au rushwa.

  Athari za uroho wa NEC-CCM

  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuzungumzia dhambi ya ubaguzi, akaonya; ukianza kuitenda hautaacha, utaendelea ni sawa na kula nyama ya mtu. Nitazingatia mantiki hiyo kujadili athari za uamuzi wa NEC-CCM kwa taifa.

  Kwa kuwa hatua hiyo ya NEC-CCM kula njama ili kudhibiti majadiliano bungeni ni ya kuvunja Katiba, chama hicho kitanogewa, kitasonga mbele. Kitasaka mchawi mwingine. Baada ya Spika na Bunge, mchawi atakayefuata ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

  CAG kama ilivyo kwa Spika na Bunge, anatambuliwa na Katiba. Kazi yake ni kuibua uozo wa ki-mahesabu serikalini na hata Ikulu, na taarifa yake hujadiliwa bungeni. Hivyo basi, NEC-CCM inapokerwa na mijadala ya ufisadi sambamba na wabunge wanaoivalia njuga, ni wazi baada ya kuwaziba midomo itaelekeza vitisho vinavyotokana na nguvu za bandia mbele ya sheria, kwa CAG.

  Watakula njama ili kumdhibiti CAG aliyekagua hesabu za malipo kwa Richmond na Dowans, akabaini wametoroka na fedha za Watanzania. CAG anayebaini ufisadi wizarani na mashirika ya umma, ikiwamo mkopo wa mabilioni NSSF kwa Kampuni ya Kiwira, ambao haujalipwa.

  Mchawi anayefuata lazima awe CAG aliyeshirikiana na kampuni ya Ernst & Young, kuthibitisha ufisadi wa bilioni 133 Benki Kuu ya Tanzania. CAG aliyebaini kati ya wezi ni Kampuni ya Kagoda. Watamwona CAG ni kero, kidomodomo, hana maslahi kwao.

  Watamwita vikaoni, watamkaripia na kumuaru cha kufanya, kama walivyoliamuru Bunge. Wataendeleza ari ya kuvunja Katiba, ibara ya 143, kifungu cha kwanza inayomtambua CAG, na uhuru wake. Hawataridhika, dhambi ya kuvunja Katiba itaendelea. Wameshakula nyama ya mtu.

  Watabaini kero nyingine ni walalahoi wa Manzese, Buguruni, Kaliua, Igunga na Monduli, ambao haki zao zinalindwa kikatiba. Watadhihirika walalahoi hao ni kero kwao kama Spika na Bunge.

  Kwa kuwa walalahoi hao hawana kadi za CCM, mikakati ya kuteka uamuzi wao wakati wa kupiga kura itawekwa. Mgombea wanayemtaka ataporwa ushindi na kupewa mgombea mlinda maslahi yao. Walalahoi hawatakubali, watadai haki kwa upanga. Nchi itanuka damu.

  NEC-CCM imejikoroga

  Ibara ya 143 ya Katiba, kifungu cha nne kinasema; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa (ya ukaguzi wa ufisadi)…

  “…Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.

  Tutafakari, NEC-CCM imetoa tamko mijadala ya ufisadi na mafisadi iendeshwe bungeni bila kuigharimu serikali (mafisadi serikalini) Wakati huohuo, taarifa ya CAG inayofichua ufisadi inapaswa ijadiliwe bungeni. Je, hapa kuna juhudi za kutokomeza ufisadi au ni kuwalinda mafisadi?

  Hata hivyo, kwa kuwa vyama vya siasa vinatambulika kikatiba, angalau uamuzi huo wa NEC-CCM kumdhibiti Spika na Bunge ungeweza kumega kidogo busara za wana-CCM wa kawaida kama ungeridhiwa na mkutano mkuu wa chama hicho. Vinginevyo, nina uhakika wapo wana-CCM wengi wanaoshangazwa na viongozi wao sasa.

  Nini kifanyike?

  Kabla ya kusema cha kufanya, nizungumzie kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kwamba chama chake kina jeuri ya kumwita Spika. Nakubaliana na Makamba, si chama hicho tu, Spika anaweza hata kuitwa na familia yake, mke au wanawe. Anaweza kupewa masharti yoyote na chama, familia yake na hata rafiki zake.

  Hata hivyo, tahadhari hapo ni kwamba, masharti hayo kama yanagusa utendaji wake wa kazi yanageuka kuwa ushauri au maoni ili kutoa fursa kwa Katiba, sheria na kanuni kumlazimisha au kumwelekeza Spika namna ya kutenda kazi yake.

  Kitendo cha kulazimisha masharti ya CCM yawe mwongozo kwa Bunge na Spika, ni sawa na kuruhusu siku moja masharti ya familia ya Spika yawe mwongozo kwa Spika kutimiza majukumu yake. Matakwa ya busara yanaelekeza, kundi lolote zaidi ya Bunge, linabaki kutoa ushauri au maoni tu kwa chombo hicho na viongozi wake na kiongozi mhusika huzingatia maoni hayo kama yanajenga taifa.

  Sasa nirejee juu ya nini cha kufanya. Hatua ya kwanza; Ibara ya 30 ya Katiba, kifungu cha tatu kinaeleza; Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu.

  Hatua ya pili: viongozi walioapa kutetea Katiba na wanakusudia kujiheshimu wazingatie msimamo wa Mark Twain, Mwanahabari wa Marekani aliyezaliwa Novemba 30, 1835 na kufariki Aprili 21, 1910.

  Mark Twain alisema; "Always do right. This will gratify some people and astonish the rest." Kwamba; unaweza kuwaridhisha baadhi ya watu na kuwashangaza waliosalia, daima unapotenda kwa usahihi. Daima tuzingatie, anayefanya mambo sahihi atafanikiwa kwa kuwa atakuwa amewaridhisha baadhi na kushangaza wengine kwa kufanikiwa ghafla.

  Natoa wito kwa viongozi wa CCM kukumbuka msemo wa Kiingereza; Life is hard. It’s even harder if you’re stupid; Kwamba maisha ni magumu zaidi unapokuwa ‘si makini.’
   
Loading...