Leo siku ya mashujaa tuwakumbuke mashujaa hawa wa siku za mwanzo za TANU

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,263
LEO SIKU YA MASHUJAA​

Mwaka jana nilipokea picha hiyo hapo chini ya kwanza kutoka Maktaba ya Ally Sykes.
Picha hii nilikuwanayo kwa miaka mingi lakini ubora wake ulikuwa hafifu.

Nilipoipata picha hii yenye ubora wa kuridhisha nikaiweka hapa.

Leo tunaadhimisha Sikukuu ya Mashujaa na nimeona niiweke picha hii ya hawa mashujaa watano wa TANU na niwaadhimishe kwa historia zao katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Katika kufanya hivi nikaona nitumie fursa hii kuwaadhimisha pia mashujaa wengine wanawake waliokuwa mstari wa mbele na Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Katika picha hiyo ya kwanza kulia ni Haruna Iddi Taratibu muasisi wa TANU Dodoma.
Haruna Taratibu alikuwa mfanyakazi wa Public Work Department (PWD) Dodoma akifanyakazi kama muashi.

Haruna Taratibu ana historia ya kusisimua katika kupigania uhuru.
Saadan Abdul Kandoro halikadhalika historia yake ni nzito sana.

Saadan Abdu Kandoro ni kati ya wazalendo 17 walioasisi TANU mwaka wa 1954.

Saadan Abdu Kandoro yeye ndiye mwanaTANU wa kwanza kuandika historia ya TANU na historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kitabu chake ''Mwito wa Uhuru,'' kilichapwa mwaka wa 1961 na inasikitisha kuwa kitabu hiki hakijachapwa tena toka hapo.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere haitaji kutambulishwa.
Historia nzima ya uhuru kaibeba yeye peke yake bila msaidizi na hakuna asiyeijua historia yake.

Baada ya Baba wa Taifa ni Sheikh Mohamed Ramiyya wa Bagamoyo, Khalifa wa Tariqa Quadirriya.

Mchango wake kwa TANU na ulimongezea nguvu kubwa Mwalimu Nyerere katika kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja.

Huyo wa mwisho hapo kushoto ni Iddi Faiz Mafungo binamu yake Sheikh Mohamed Ramiyya na ndiye aliyempeleka Nyerere Bagamoyo kumjulisha kwa Sheikh Ramiyya akiwa ameongozana katika safari hiyo na ndugu yake, Iddi Tosiri.

Kadi ya TANU ya Iddi Faiz Mafungo ni no. 24 na ni kati ya watu wasiozidi 20 waliohudhuria mkutano wa kwanza wa TANU Ukumbi wa Arnautoglu August 1954.

Iddi Faiz Mafungo alikuwa Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyy fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) na alikuwa pia Mweka Hazina wa TANU.

Iddi Faizi Mafungo ndiye alikuwa mkusanyaji wa fedha za safari ya kwanza UNO ya Rais wa TANU Julius Nyerere mwaka wa 1955.

Iddi Faiz Mafungo alikamatwa na Special Branch Turiani wakati anatoka Tanga kuchukua fedha za safari ya Nyerere UNO kutoka kwa Mwalimu Kihere.

Hiki ni kisa kinahitaji muda kukieleza chote.

Hawa wote wana historia za kusisimua zinazoonyesha matatizo na shida walizopata wakati wakipigania uhuru wa Tanganyika.

Inasikitisha kuwa hii leo hakuna anaewatambua mashujaa hawa ambao leo ndiyo siku yao ya kukumbukwa.

Kama si kuwa na picha hizi ambazo zinatuthibitishia kuwa mashujaa hawa walikuwapo ingekuwa tabu sana historia zao kuaminika.

Picha ya pili ilipigwa Uwanja wa Ndege wanaTANU wakimsindikiza Nyerere safari ya kwanza UNO mwaka wa 1955.

Aliyesimama mkono wa kulia wa Julius Nyerere Rais wa TANU ni Mweka Hazina wa TANU Iddi Faiz Mafungo aliyevaa kanzu, koti na tarbush.

Wanaofuatia ni Zuberi Mtemmvu, Robert Makange na Rashid Sisso.
Kushoto kwa Nyerere ni John Rupia na Bi. Titi Mohamed.

Lakini iko picha nyingine ya siku hii hiyo hapo chini.

Kulia ni Bi. Chiku bint Said Kisusa, maarufu Mama Sakina, Bi. Titi Mohamed, kushoto wa kwanza ni Bi. Tatu bint Mzee na Julius Nyerere yuko katikati.

Hawa akina mama wana historia kubwa katika kuwakusanya wanawake wa Dar es Salaam kuja katika mikutano ya kwanza ya TANU Mnazi Mmoja kuichangamsha kwa vigelegele na nyimbo zao za lelemama.

Nchi hii ina deni kubwa kwa mashujaa hawa wake kwa waume.
Iweje picha hizi hazionekani katika kuta za ofisi za CCM?

1690291991004.png

Kushoto Iddi Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu, Dodoma 1955.
1690292105611.png

Kushoto Rashid Sisso, Robert Makange, Zuberi Mtemvu, Iddi Faiz Mafungo, Julius Nyerere, John Rupia, Bi. Titi Mohamed wanamsindikiza Julius Nyerere safari ya kwanza UNO 1955.
1690292199011.png

Kushoto Bi. Tatu bint Mzee, Kulia Bi. Chiku bint Said Kisusa (mke wa Shariff Abdallah Attas) kati Julius Nyerere wanamsindikiza safari ya kwanza UNO 1955.​
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom