Kyela: Ubadhirifu na ufisadi chama cha ushirika KYECU

nokwenumuya

JF-Expert Member
Jun 29, 2019
810
2,851
UBADHIRIFU CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KYELA (KYECU), NA UVUNJAJI NA UKIUKAJI WA MIONGOZO YA VYAMA VYA USHIRIKA



Mimi ni mdau na Mkulima wa Kakao katika Wilaya yetu Kyela, Mkoani Mbeya. Kutokana na ushiriki wangu katika kilimo hadi mauzo, kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanatukwanza kama wana Ushirika na nimeamua kuyaweka bayana ili tuweze kupata msaada kwa Viongozi wa Serikali na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa Vyama Vya Ushirika.

Mambo haya nimeyaweka katika mafungu matatu na nitaeleza japo kwa ufupi kama ifuatavyo;

  • Mapato na matumizi
  • Manunuzi (Rushwa)
  • Mfumo wa Mauzo na Bei za kakao

Mapato na matumizi

Sisi wakulima tumekuwa na mashaka juu ya mapato na matumizi ya Chama chetu cha Ushirika, ukiachia mbali ripoti ya mwisho ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya UShirika (COASCO), ambapo KYECU tulipata Hati Mbaya, bado mapato na matumizi yanatia shaka, yaani hakuna uwajibikaji.

Hii inatokana na sababu nyingi, na ikumbukwe mnamo July 2022, Mh. Mkuu wa Mkoa, Mh. Juma Homera alipofanya ziara Kyela aliuliza KYECU mna akiba ya kiasi gani Benki?, ndipo Kaimu Meneja akajibu hawana akiba yoyote, Mh. Mkuu wa Mkoa akashangaa inakuwaje hamna akiba ina maana fedha yote mnayoingiza mnatumia bila kubakiza akiba yoyote?, Ukizingatia kila wiki KYECU inapata mamilioni ya pesa za kitanzania kutokana na ushuru wa mauzo ya kakao, sasa inawezekanaje kila wakati akiba katika akaunti zake ni shilingi 0?



Na hayo yanafanyika huku hatuoni juhudi zao katika kutoa huduma kwa wakulima kama: usambazaji wa miche ya kakao iliyoboreshwa kwa wingi, pembejeo, elimu ya usindikaji na uboreshaji wa thamani ya zao letu.

Tuna mashaka makubwa na uzalendo wa watendaji wa Chama Kikuu Cha UShirika – KYECU, kuwa wapo kwa ajili ya maslahi yao na sio uboreshaji wa zao letu la muhimu la Kakao.

Hivyo suala la mapato na matumizi kutoka vyanzo mbalimbali zikiwemo tozo za watoa huduma zifuatiliwe zinafanyaje kazi? Tunaomba Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama Vya Ushrika (COASCO) lifanye Ukaguzi Maalum katika Chama Chetu Cha Ushirika (KYECU) sababu kuna ubadhirifu mkubwa sana unaofanyika.

Manunuzi



Utangulizi

Hapa katika manunuzi, ndio sehemu iliyoghubikwa na ubadhirifu mkubwa sana katika kupata wazabuni wenye sifa na weledi, wanaotambulika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi;

Naomba kurejea mchakato wa mwaka 2021 wa kumpata msimamizi wa ghala, na msafirishaji uliolazimika kurejewa upya baada ya Serikali kuingilia kati baada ya baadhi ya wazabuni kupeleka Malalamiko yao katika Taasisi ya Kupambana Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) juu ya mchakato ulivyokuwa unaendeshwa. Ndipo Mh. Juma Homera, Mkuu wa Mkoa, kupitia kwa Mh. Mkuu wa Wilaya kupitia TAKUKURU wakaagiza mchakato huo urudiwe na wao kuusimamia ili kuhakikisha haki inatendeka.

Mnamo September 2021, KYECU ilitangaza Zabuni za Mtunza Ghala na Msafirishaji. Wazabuni walipeleka Zabuni zao na kusubiri kuitwa siku ya ufunguzi. Kabla ya siku hiyo husika, Mtendaji mmoja wa KYECU alifungua zabuni zote ili kuwaeleza wazabuni aliowakusudia jinsi washindani wao walivyojaza, ili waweze rekebisha zabuni zao na hatimaye waweze kushinda.

Wazabuni wengine walipata taarifa hizo za hujuma na kutoa taarifa TAKUKURU, hatimaye Serikali iliingilia kati na kuwataka Watendaji wa KYECU kuitisha zabuni hizo upya, na TAKUKURU ilihakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria. Tunamshukuru sana Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kyela, kwa kudhibiti rushwa katika mchakato huo na kutenda haki, Hatimaye tukapata makampuni yenye uwezo na weledi, yasiyopatikana kwa njia ya rushwa.



Zabuni ya Ghala la Ipinda (2022-2023)



Hii ni skendo iliyomuondoa Meneja wa Kyecu aliyekuwepo, aliondolewa Mwezi Mei 2022 baada ya kujulikana kuwa alichukua jukumu la kumuongezea msimamizi wa Ghala la Ipinda mkataba wa mwaka mmoja bila kufuata muongozo wa manunuzi wa vyama vya Ushirika.

Ilipofika Mwezi April 2022, muda ambao Bodi ilitaka kutangaza Zabuni hiyo, kampuni inayosimamia Ghala hilo ilienda mahakamani kuzuia mchakato huo sababu inao mkataba tayari wa kusimamia Ghala hilo hadi mwaka 2023.

Baada ya Meneja Mkuu kupata wito wa Mahakama, aliamua kutafuta mwanasheria bila kuitaarifu Bodi na akaanza kusimamia kesi hiyo. Baada ya Taarifa kuifikia Bodi na Mkuu wa Wilaya ndipo maagizo yakatoka kwa Mh. Mkuu wa Mkoa ya kumfuta kazi Meneja Mkuu aliyekupo, na kumpa Meneja Shughuli aliyekuwepo kuwa ndio Kaimu Meneja wa Chama Kikuu Cha Ushirika Kyela (KYECU).

Na tunajua hakuna jinsi mtu anaweza ongeza mkataba kwa mzabuni bila Baraka za Bodi na bila kufuata muongozo wa manunuzi wa vyama vya ushirika bila kuwa na Ushawishi wa maslahi binafsi.



Zabuni za Usambazaji wa Magunia (Vifungashio)

January 2022, Kampuni ya ANDRE AND ROSS CO. LTD, ilishinda Zabuni ya kusambaza gunia mpya (Jute Bags), kwa ajili ya kuhifadhia kakao, tayari kwenda ghalani kwa ajili ya mauzo.

Kufikia March 2022, kulikuwa na malalamiko kuwa kampuni hiyo inasambaza mchanganyiko wa magunia yaliyotumika na mapya. Malalamiko hayo yalitoka kwa Wanunuzi wa kakao kwani kutumia magunia yaliyotumika kwenye mazao kama mahindi, kahawa na Korosho kunabadili AROMA ya kakao, na kuharibu ubora wake. Hivyo kuliweka zao hili katika hatari ya kukosa wanunuzi wa kimataifa.

Ndipo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Ruswa, kupitia Kamanda wa TAKUKURU wa Wilaya ya Kyela ikawakamata mtendaji wa Kampuni hiyo, na pia ikawakamata baadhi ya Watendaji wa Chama Kikuu Cha Ushirika KYECU. Kampuni ilikamatwa kwa kusambaza magunia yaliyotumika kinyume na mkataba waliopewa. Na viongozi wa KYECU walikamatwa kwa nini wanapokea magunia yaliyotumika wakati mkataba unataka magunia yawe mapya ili kutoharibu ubora wa kakao.

Ndipo mwezi April 2022, mkataba wa usambazaji wa magunia kati ya KYECU na ANDRE AND ROSS CO. LTD ukavunjwa sababu ya usambazaji wa magunia yaliyokwishatumika kwa bei ya shilingi elfu tano mia nne na sitini (5460 Tshs).

Baada ya kuvunjwa mkataba huo, Chama Kikuu Cha Ushirika Kyela (KYECU), chini ya Kaimu Meneja aliyepo kwa sasa kilipaswa kutangaza Zabuni hiyo ili kupata Kampuni mpya inayoweza kusambaza magunia mapya kwa ajili ya kuhifadhia kakao.

Kinyume chake, na kinyume na muongozo wa manunuzi wa Vyama Vya Ushirika, na kinyume na sheria ya manunuzi ya Umma. Kaimu Meneja aliyepo akaamua sasa kukigeuza Chama Cha Ushirika kuwa ndio muuzaji wa magunia ya kufungia kakao, toka muda huo hadi sasa.

Jambo la kusitaajabisha ni kuwa, KYECU ilivunja mkataba na ANDRE AND ROSS CO. LTD, kuwa wanasambaza gunia ambazo zimetumika. Na sasa KYECU, kinyume na sheria na miongozo ya manunuzi wao ndio wasambazaji wa gunia, na wanasambaza gunia hizo hizo ambazo zimetumika sehemu nyingine. Na anauza kwa bei ile ile ya 5460.

Rushwa/Wizi katika haya magunia ambayo Meneja ananunua hivi sasa

Taarifa ambayo ninayo na ya Hakika ni kuwa, hivi sasa Kaimu Meneja, Ndugu Julius Mwankenja, amefanya makubaliano binafsi na mtu anayemuuzia hizo gunia zilizokwisha tumika (mtumba/chakavu), ambapo huwa wanazikung’uta kuondoa vumbi na kisha kuzichapa upya, na ukitazama gunia hizo nyingine huwa zimechapwa mara mbili, yaani zilipotoka nan a chapa ya Kyela (pichani chini nimeweka picha ya gunia hizo).


Sisi tunafahamu magunia hayo yaliyotumika mengi yanatoka ZAMBIA na ZIMBABWE, hadi kufika Tunduma huwa tunanunua kwa shilingi 1700 hadi 1900 za Kitanzania.

Kaimu Meneja (Julius Mwankenja) katika kufanikisha biashara yake haramu na ya rushwa kupitia Chama Cha Ushirika haya ndio makubaliano aliyofanya na anayemuuzia magunia (kinyume na muongozo wa manunuzi).

Kwamba huyu anayemuuzia gunia walikubaliana kuwa yeye atamuuzia gunia moja kwa shilingi elfu nne na mia nne hamsini (4450/- Tshs). Lakini yeye atasema kuwa kila gunia ananunua kwa Shilingi Elfu Tano (5000/- Tshs). Katika malipo itaandikwa hundi ya bei ya 5000 kwa kila gunia, kisha muuzaji wa hayo magunia akishachukua hundi, anaenda kutoa pesa na kumpa Kaimu Meneja (Julius Mwankenja) shilingi 550 kwa kila gunia.

Ukizidisha toka aanze kununua gunia kwa mfumo huu mnamo mwezi mei hadi sasa ndipo utapata kiasi cha mamilioni ambayo huyu Kaimu Meneja, anajiingizia kinyume cha sheria kwa kuvunja kwake kwa wazi muongozo manunuzi wa vyama vya Ushirika.

Katika hili tunaiomba Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa iweze kumkamata Kaimu Meneja, Bwana Julius, na muuzaji wa magunia kwa kufanya biashara kinyume na muongozo wa manunuzi wa vyama vya Ushirika, na kupanga njama za wizi kama nilivyoeleza hapo. Maana mmoja ni mtoa rushwa na mwingine ni mpokeaji wa hiyo Rushwa.



Lakini ukiachilia mbali bei ya kununua na anayouza kuna maswali ya kujiuliza:

  • Kama alivunja mkataba na ANDRE AND ROSS sababu anasambaza gunia ambazo zimetumika, mbona yeye ananunua gunia zilizotumika na kuziuza? Ina maana hapa tatizo sio gunia zilizotumika bali alitaka afanye biashara ndani ya ajira yake kinyume na sheria.
  • Je muongozo wa Manunuzi wa Vyama Vya Ushirika vinakiruhusu Chama Kikuu Cha Ushirika kufanya biashara ya kuwauzia wakulima/wanunuzi vifungashio?
  • Je Kaimu Meneja ana mamlaka ya kuamua kufanya manunuzi yanayozidi milioni hamsini kwa mwaka (50,000,000 Tshs) bila kutangaza Zabuni?
  • Je hayo magunia ambayo KYECU inayauza anawauzia? Walimpataje bila kutangaza zabuni?
  • Je sheria ya vyama vya Ushirika, muongozo wa manunuzi wa vyama vya Ushirika vinaruhusu Chama Kikuu Cha Ushirika kufanya biashara ya kujiuzia Bidhaa au Huduma?
  • Hii faida wanayopata kwa kuuza magunia nani anaijua na inaenda wapi?
  • Chama Kikuu Cha Ushirika kina Leseni ya Biashara ya Huduma au Bidhaa? Inalipa kodi kwa hizo gunia ambazo wamekuwa wanauza hadi sasa?



Kiufupi anachokifanya Kaimu Meneja wa KYECU aliyepo kwa sasa, hakina tofauti na alichokifanya Meneja Mkuu aliyekuwepo kabla yake katika manunuzi. Na kwa kuwa alikuwepo ina maana hii ni tabia ambazo wamekuwa wakifanya na kinachofanyika ni muendelezo tu.

Anachokifanya ni kuacha majumuku makuu ya Chama Cha Ushirika na kufanya biashara zake binafsi yeye na washirika wenzake kupitia Chama kikuu Cha Ushirika, kwa kutotangaza Zabuni mbalimbali ili yeye na washirika wake wafanye biashara kupitia jukwaa la Ushirika Kinyume na Muongozo wa Manunuzi wa Vyama Vya Ushirika.



Mfumo wa Mauzo na Bei za Kakao.

Tunaishukuru Serikali. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani toka umeboreshwa kwetu sisi umekuwa na mafanikio makubwa, Bei za zao letu zilipanda na tumekuwa kwa wakati mwingi tunapata wanunuzi bila wasiwasi.

Pamoja na mafaniko hayo kuna changamoto ambazo tunazipitia, na tunamshukuru Mh. Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, na Mh. Mlawa, Mkuu wa Wilaya Kyela wamekuwa karibu nasi nyakati za changamoto za wanunuzi, bei na masuala yote yanayohusiana na zao la kakao.

Kuanzia June 2022 kulikuwa na changamoto ya kushuka kwa bei ya kakao ghafi katika soko la dunia. Wanunuzi wengi walikuja na ofa ya bei ya kununua ambayo ni chini ya bei elekezi ya Serikali ya Shilingi Elfu nne na mia mbili (4,200 Tshs) kwa kilogramu moja ya kakao.

Baada ya Vikao vya Majadiliano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa tulikubaliana kuuza chini ya bei hiyo huku tukitazamia bei ya soko la dunia ikipanda basi tutarejea katika bei elekezi au zaidi iliyowekwa na serikali.

Toka kipindi hicho hadi sasa ambapo bei katika soko la dunia imepanda bado wanunuzi wanakuja na ofa ya chini ya bei elekezi ya serikali, ambapo huja na bei kati ya 3900 hadi 4070 Shilingi, Hapa ni kwa kakao yetu ya Kyela.

Lakini kakao inayouzwa Mvomero Mkoani Morogoro, wao wamefanikiwa kuuza kwa bei ya juu siku za hivi karibuni kwa sababu wanauza kupitia kampuni ya UMMA ya Tanzania Mercantile Exchange Plc (TMX). Kupitia TMX, kakao ya Mvomero hivi sasa inazuwa kwa zaidi ya shilingi 4440 kwa kilo moja.

Mfumo wa TMX unafanyika mubashara na mnunuzi yeyote aliyejiunga anaweza kununua kokote alipo duniani, hivyo inaongeza ushindani wa bei na hatimaye Mkulima anapata bei kubwa. Mfano ukichukulia bei ya Mvomero ya hivi karibuni (4441 Tshs), ukatoa ya Kyela (4050 Tshs), unapata tofauti ni shilingi 391 kwa kila kilo. Ukizidisha mara kilo 392,350 (Catalogue 21 & 22) iliyouzwa kyela katika mnada wa Tarehe 24 october 2022, unapata kiasi ambacho kimepotea kwa kutouza kupitia TMX ni Shilingi za Kitanzania milioni mia moja hamsini na tatu, laki nne, elfu nane na mia nane hamsini (153,408,850/- Tshs). Pesa ambazo zingeingia kwenye akaunti za Wakulima. Na haya ni mapato ambayo yamepotea ndani ya wiki moja.

Waziri wa Kilimo, Mh. Hussein Bashe amewahi kutoa maagizo mara kadhaa kwa Watendaji wa KYECU kuhakikisha kakao ya Kyela inauzwa kwa mnada kwa njia ya TMX, sio kwa njia ya Boksi ambayo haina ushindani, na wanunuzi ni wale wale, wanabadilishana na kupangiana bei.



Ni sababu zipi zinasababisha KAKAO YA KYELA, isiuzwe kupitia TMX?



  • UONGOZI WA KYECU
  • WANUNUZI



UONGOZI WA KYECU

Viongozi wa Kyecu walipokea maagizo ya Mh. Hussein Bashe, ya kuwataka kuuza kakao kupitia TMX. Wamekuwa wazito kutekeleza kwa sababu kadhaa, moja kubwa ni kuwa ili uweze kununua mazao kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani lazima uweke Amana/Dhamana ya Shilingi Milioni Hamsini (50,000,000/- Tshs.).

Sasa ili hawa wanunuzi waweze kununua kupitia TMX, inabidi dhamana zao zihamishiwe TMX kutoka KYECU. Jambo hilo linakuwa gumu kwao kwa sababu kuna tuhuma kuwa hizo dhamana za 50,000,000/- za kila kampuni iliyoweka hazipo. Kwa kifupi dhamana za wanunuzi zimeliwa na wajanja wa pale KUECU. Hivyo inawawia vigumu kusema mnada wahamishie TMX kwa sababu hawana pesa za kuwarejeshea wanunuzi, pesa ambazo kimsingi hawatakiwi kuzitumia wala kuzigusa kwa sababu muda wowote mnunuzi akijitoa kushiriki kununua inabidi arejeshewe pesa zake.



WANUNUZI

Kupitia mfumo wa mnada kwa boksi, ambao kiufupi unaondoa mantiki yote ya mnada, kwa maana ya washiriki kupandishiana bei. Kila mnunuzi anaandika bei na kutumbukiza kwenye boksi siku ya mnada. Viongozi wanafungua na kusoma bei ya kila mnunuzi. Inayokuwa juu basi Wakulima wanaulizwa kama wako tayari kununua au la. Sasa hiyo inaondoa maana ya mnada kwa sababu mnunuzi haruhusiwi kuongeza bei, sasa huo sio mnada bali ni usanii tu.

Mfumo huu unawasaidia wanunuzi kupanga bei na kufaidika na kupata bei chini, maana kwanza ni wachache na wanafahamiana. Hivyo wanaungana ili kupata unafuu wa bei.

Na kwa sababu mfumo huu unawasaidia wao, kuna namna wanashirikiana na baadhi ya viongozi wa KYECU ili kuhakikisha mfumo unabaki huu huu ili kutoongeza wanunuzi wengine ambapo wakija bei ya kakao ya Kyela lazima itapanda zaidi.



JE, MFUMO WA TMX HAUJAWAHI JARIBIWA KYELA?

Kuna wakati Viongozi wa KYECU walitakiwa kuuza kupitia TMX, wakaomba minada ifanyike kwa njia zote mbili, njia ya Boksi na Mtandao (Online- TMX).

Kwa kushirikiana na wanunuzi wakawa na mbinu ifuatayo, siku ya mnada ukawa ukaanza mnada wa TMX (Online), na mnada huo unafungwa saa 5 kamili asubuhi, na wao wanakuwa wameona na kushiriki.

Kisha mnada wa boksi unaanza saa 6 hadi saa 7. Kwa kuwa tayari wanakuwa na bei ya TMX basi wanunuzi wa Boksi wanaweka bei juu zaidi ya TMX. Wakafanya hivyo kwa wiki mbili kisha wakasema bei ya boksi ni kubwa kuliko TMX, hivyo wakasema bora waendelee kuuza kupitia TMX.



JE WANUNUZI WA KYELA KWA BOKSI, HAWANUNUI KWINGINE KWA NJIA YA TMX?

Hao wanunuzi wanaonunua kakao ya KYELA kwa shilingi 4050, pia wanashiriki minada ya TMX, na wananunua kakao ya Mvomero kwa shilingi 4440 hadi 4700 na zaidi. Hivyo hao wanunuzi wako tayari kununua kakao ya Kyela kupitia TMX, hata hivyo wanafurahia kununua kupitia boksi sababu ni rahisi kupata kwa bei ya chini zaidi.

NB: Hivyo tatizo la bei ya kakao kushuka na kuendelea kuuzwa chini ya bei elekezi ya serikali ni tatizo la kimfumo, na udhaifu wa watendaji wa KYECU, ambao wameshindwa kufanya kazi yao ya kupanua wigo wa wanunuzi, kupitia mifumo madhubuti iliyowekwa na Serikali yetu.





HITIMISHO

Tunawaomba Viongozi na Taasisi zifuatazo zifanye Uchunguzi kuhusu madai haya:

  • Mh. Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo.
  • Mh. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha.
  • Mh. Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
  • Kamanda wa TAKUKURU – Wilaya ya Kyekla.
  • Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya.
  • Afisa Ushirika.
  • Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama Vya Ushirika (COASCO)
  • Tume ya Maendeleo ya Vyama Vya Ushirika (TCDC)



OMBI MAALUM

Vyama Vya Ushirika Nchi nzima vikifanya kazi kwa Weledi na Ubora na kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo iliyoweka itaweza kuondoa umasikini kwa kiwango kikubwa na kuboresha maisha ya Wakulima.

Watendaji wengi wa hivi vyama haswa kwenye eneo la manunuzi wanavitumia kwa maslahi yao binafsi na zaidi wanafanya kazi na kampuni zisizo na uwezo na vigezo vya kisheria kufanya kazi hizo. Mathalani mtu anaweza kuwa na kampuni ya ujenzi na leseni ya ujenzi na akapewa kazi ya kuwa mwendesha ghala, msambaza vifungashio au msafirishaji au mtoa huduma na muuza bidhaa tofauti na Leseni zake.

Tunashauri Vyama Vyote Vikuu Vya Ushirika vifanye mchakato wake wa Manunuzi kupitia mfumo wa Manunuzi wa Kielektroniki wa Tanzania (TANEPS). Kupitia mfumo huu ubadhirifu mwingi unaofanywa na Watendaji wasio waaminifu wa Vyama Vya Ushirika utapungua kwa kasi sana, na pia serikali itaongeza washiriki na wazabuni hivyo mapato ya serikali yataongezeka kwa wingi sana.

Vyama vya Ushirika vinafanya manunuzi ya Mabilioni ya fedha kila mwaka. Vinapaswa kusimamiwa na kuratibiwa vizuri kupitia sheria, miongozi na mifumo iliyowekwa na Serikali yetu ili kuwe na uwazi, uwajibikaji na ufanisi.



VIAMBATANISHO KATIKA TAARIFA HII

  • MUONGOZO WA MANUNUZI KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA (FIRST EDITION, APRIL 2022).
  • RIPOTI YA UJUMLA YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA ULIOFANYWA NA COASCO KWA MWAKA 2019/2020 (OKTOBA 2020)
  • MWONGOZO WA UWEKEZAJI (FIRST EDITION APRILI, 2022)

RIPOTI: IFUATAYO NI SEHEMU YA RIPOTI YA COASCO YA MWAKA 2019/20, ILIYOPELEKEA KYECU KUPATA HATI MBAYA.



SHIRIKA LA UKAGUZI NA USIMAMIZI WA VYAMA VYA USHIRIKA (COASCO)

RIPOTI YA UJUMLA YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA ULIOFANYWA NA COASCO KWA MWAKA 2019/2020

UKURASA 42 & 43




  • KYELA COOPERATIVE UNION (KYECU) LTD UKAGUZI WA MWAKA 2018/2019



Hoja zilizosababisha kupata hati mbaya:

  • Malipo ya manunuzi ya Kakao (cocoa) ambayo hayakulipwa na wanunuzi Tshs 67,460,050 kutokubainishwa kwenye taarifa za fedha.

  • Tulibaini kwamba kulikuwa na mauzo ya kakao kwa jumla ya Tshs 686,398,564 na malipo yaliyofanyika kwa mauzo hayo yalikuwa Tshs 618,938,514 lakini kiasi kilichobaki cha Tshs 67,460,050 hakikuwasilishwa kwenye taarifa za fedha hapo tarehe 31.03.2019. Kutokana na kukosekana kwa maelezo kuhusu malipo hayo na kwakuwa hayakuwasiliswa kwenye taarifa za fedha, hesabu za wadaiwa imepotoshwa kwa kiwango hicho.



  • Makusanyo ya Tshs 50,812,070 na Tshs 66,015,344 kwa ajili ya wasafirishaji na Mrajis hayakuwasilishwa mahala husika na hayajaonyeshwa kwenye taarifa za fedha.

  • Union ilifanya makusanyo kutoka kwenye mauzo ya COCOA kwa ajili ya wasafirishaji wa COCOA pamoja na mfuko wa Mrajis lakini makusanyo ya Tshs 50,812,070 ya wasafirishaji pamoja na Tshs 66,015,344 ya Mfuko wa Mrajis hayakulipwa na pia hayakuonyeshwa kwenye taarifa za fedha. Mchanganuo wa makusanyo na malipo ya fedha hizo na kiasi kilichobaki bila maelezo ni kama ifuatavyo:





    • Maelezo
    • Kiwango (KGS)
    • Makusanyo ya Mrajis
    • Kiwango (KGS)
    • Makusanyo ya Wasafirishaji (Jenifer transporter)
    • 4,447,566
    • 20
    • 88,951,320
    • 40
    • 177,902,640
    • Malipo kwa wahusika
    • 22,935,976
    • 127,090,570
    • Salio lisilo na maelezo
    • 66,015,344
    • 50,812,070

    • Kutokana na kukosekana kwa maelezo ya hesabu hizo pamoja na kutokuwasilishwa kwenye taarifa za fedha, hesabu ya wadai imepotoshwa kwa kiwango hicho.


    • Kukosekana kwa maelezo na vielelezo vya matumizi ya mkopo wa Tshs 400,000,000 toka benki ya CRDB

    • Union imeonyesha kuwa imekopa Tshs 400,000,000 toka benki ya CRDB lakini hatukupata vielelezo vya matumizi ya fedha hizo. Hali hiyo imetokana na barua iliyopatikana ambayo Union inaeleza kuwa itailipa benki ya CRDB Tshs 279,850,754.37 lakini mkopo huo haukuonekana kwenye taarifa za benki na pia hakuna maelezo ya lini mkopo huo ulipokelewa na matumzi yake hayakuwekwa bayana.


    • Kutokuwepo kwa magari na matrekta chamani pamoja na kutokuandika daftari la fedha

    • Wakati wa ukaguzi tumebaini kwamba Union haikuandika daftari la mali za kudumu. Lakini pia tukabaini kuwa baadhi ya magari yaliyopokelewa kutoka iliyokuwa Union ya Kyela –Rungwe hayapo chamani. Hali hii inatia shaka kuhusu uwepo wa magari hayo kama ifuatavyo:-

      • Malori
      • Magari madogo
      • Matrekta
      • Iveco truck TZ98378
      • L/Rover s/wagon TZ 98516
      • Fiat tractor MB 3871
      • Scania truck TZ 80902
      • Suzuki TZC 5567
      • Fiat tractor MB 3864
      • Fiat truck TZ 80769
      • Toyota Stout TZ 80142
      • Trailer of tractor MB 3817
      • Gorica Trailer TZ 92238
      • Toyota Hilux TZ 8429
      • Trailer of tractor MB 3876
      • Trailer chassis 000136
      • Trailer plat form
 

Attachments

  • KYECU UBADHIRIFU NA UKIUKWAJI WA MIONGOZO YA USHIRIKA.pdf
    721.5 KB · Views: 9
  • COASCO_AUDIT_RPORT_2019-2020.pdf
    9.8 MB · Views: 10
  • MWONGOZO_WA_MANUNUZI.pdf
    369.6 KB · Views: 8
  • MWONGOZO_WA_UWEKEZAJI.pdf
    367.2 KB · Views: 6
Back
Top Bottom