Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 673
Ripoti mpya ya Furaha Duniani (World Happiness Report) ya mwaka 2026 iliyotolewa Machi 19, 2026, imeendelea kuiweka Tanzania katika orodha ya mataifa yasiyo na furaha.
Katika utafiti huo uliohusisha nchi 147, Tanzania imeshika nafasi ya 138, ikiingia kwenye kundi la nchi 10 zisizo na furaha zaidi duniani. Licha ya kuwepo kwa ongezeko dogo la alama za tathmini ya maisha (Life Evaluation) kufikia 39.02, hatua hiyo haijatosha kuiondoa nchi hiyo kwenye lindi la majonzi ya kitakwimu.
Tanzania imeonekana kusuasua ikilinganishwa na majirani zake wa Ukanda wa Afrika Mashariki. Ripoti hiyo inaonesha kuwa mataifa ya Kenya, Uganda, na Ethiopia yamepiga hatua kubwa zaidi, yakiorodheshwa juu ya Tanzania katika vigezo vya ustawi wa jamii na kuridhika na maisha.
Matokeo ya utafiti huu yalitarajiwa kwa kipindi hiki na ni kipimo cha utendaji wa CCM kwa wananchi. Kwamba CCM imelifikisha Taifa kuwa miongoni mwa nchi 10 za watu wasio na fursaha.
Mataifa mengine yaliyopo kwenye orodha hiyo ni pamoja na Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lebanon, Yemen, Botswana, Zimbabwe, Malawi, Sierra Leone na Afghanistan.
Ukiangalia mataifa hayo, utaona mengine yamekuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na vita vya nje kwa muda mrefu, kama DR Congo, Yemen, Sierra Leone na Afghanistan. Zimbabwe imekuwa kwenye vikwazo vya kiuchumi kwa muda mrefu.
Kwa nini Watanzania hawana furaha?
Kwa nini Watanzania hawana furaha, ilihali nchi yao ina utajiri wa madini, uwepo vyanzo vingi vya maji, ardhi yenye rutuba, misitu, wanyamapori, eneo kubwa la bahari? Kwa nini?
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, ili nchi iendelee, inahitaji mambo makuu manne: Watu, Ardhi, Siasa Safi, na Uongozi Bora. Katika hayo mahitaji, Tanzania imekosa Siasa safi na uongozi bora.
Japo kwa mrefu Tanzania imeonekana kuwa nchi yenye Amani na utulivu, lakini ukweli ni kwamba kuna utulivu unaolazimishwa kwa mtutu wa bunduki, hakuna amani wala furaha. Watu wana majonzi ya ndani kwa ndani, myoyo inavuja damu.
Yaliyotokea Oktoba 29, 2025 ndiyo yamedhihirisha kwamba Watanzania hawana furaha na ndiyo maana licha ya vitisho vya kijeshi, wananchi walitoka kuandamana siku ya uchaguzi. Watanzania wana kiu ya siasa safi na uongozi bora.
Ripoti za waaangalizi wa uchaguzi zimeonyesha kuwa, Oktoba 29, kwanza idadi ya wapiga kura ilikuwa ndogo sana na ilipofika saa 5 asubuhi, maandamano yalilipuka katika miji mikubwa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na baadaye yakaambukiza kwenye mikoa ya Dodoma, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi na mingineyo.
Wananchi walieleza waziwazi kutokubaliana na mfumo wa uchaguzi na kwamba wanataka mabadiliko ya Katiba. Wengine kwa kuonyesha hasira zao waliharibu miundombinu ya Serikali na ya watu binafsi.
Maandamano hayo yalikabiliwa vikali na vyombo vya ulinzi na usalama na kusababisha mauaji, majeruhi, watu kupotea na wengine hawakupata maiti za wapendwa wao hadi leo. Askari waliokuwa na silaha za moto waliingia mitaani na kuwashambulia hata watu ambao walikuwa hawaandamani na kuwafyatulia risasi. Baadhi ya watu waliohojiwa na Tume ya Jaji Mohamed Othman Chande wamesimulia hayo.
CCM sikio la kufa
Malalamiko kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kuwa na mfumo bora wa uchaguzi hayakuanza leo, yamekuwepo tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa miaka 35 iliyopita.
Tume ya Jaji Francis Nyalali ilitoa mapendekezo kuhudu mfumo bora wa vyama vingi, lakini mapendekezo mengi hayakutekelezwa likiwa la kufanyika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Kwa hiyo CCM iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi ikiwa bado ni chama Dola, huku vyama vingine vilivyoanzishwa vikiwa havina nguvu ya Dola wala havina rasilimali kama ilivyokuwa CCM.
Matokeo yake kila uchaguzi mkuu CCM ilikuwa inaviburuza tu vyama ya upinzani, kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye mwenyekiti wa CCM na ndiye anayeteua uongozi wote wa Tume ya Uchaguzi na watendaji wote wa Serikali wakiwamo wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, ambao ndiyo wanaosimamia chaguzi kwa njia moja au nyingine. Sasa unategemea CCM itashindwaje uchaguzi?
Kwa hiyo kilio hicho cha mabadiliko ya Katiba na mfumo bora wa uchaguzi kimeendelea kuwepo vifuani mwa Watanzania, mpaka yalipoibuka maandamano ya Oktoba 29, 2025. Watu walishauri sana CCM ikubali kufanya mabadiliko, lakini waliziba masikio.
Wataalamu walishauri kwamba, ni heri kufanya mabadiliko kwa njia ya Amani, kuliko kusubiri kumwaga damu, lakini CCM ilipuuza. Sikio la kufa halisikii dawa.
Walau mwaka 2012, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, lakini pia rasimu ya tume hiyo ilipofikishwa bungeni, ilichakachuliwa na kuundwa Katiba inayopendekezwa.
Baada ya Hayati Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, alipuuzilia mbali mabadiliko ya Katiba akisema hayakuwa kipaumbele chake.
Rais Magufuli aliona kama mabadiliko ya Katiba na mfumo bora wa uchaguzi vitachelewesha maendeleo aliyokusudia. Hivyo alizuia hata utendaji wa vyama vya upinzani, alipiga maprufuku mikutano ya hadhara na maandamano. Wakosoaji wengi walikipata cha mtema kuni, wengine walikamatwa na kupewa kesi, wengine walipotea.
Baada ya kifo chake Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alirithi nafasi yake akileta matumaini makubwa kwa wananchi. Aliondoa makatazo yote ya vyama vya upinzani yaliyowekwa na mtangulizi wake na kuanza mazungumzo ya maridhiano na vyama vya upinzani.
Lakini baadaye alionekana kupiga danadana mabadiliko ya Katiba na hata baada ya ripoti ya Kikosi kazi alichokiunda, suala la Katiba mpya lilisogezwa hadi baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Mpaka uchaguzi mkuu unakaribia mwaka 2025, shinikizo la madai ya Katiba mpya na mfumo bora wa uchaguzi liliendelea kupamba moto. Matokeo yake ndiyo maandamano ya Oktoba 299, 2025 na damu ikamwagika.
Yale yale yaliyokuwa yakisemwa awali, kwamba CCM isisubiri damu imwagike ndipo wafanye mabadiliko ya Katiba, sasa damu imemwagika, mpaka wanaona aibu hata kutaja idadi ya watu waliokufa katika vurugu za kuanzia Oktoba 29 hadi 30, 2025.
Pamoja na Rais Samia Kuunda Tume ya Uchunguzi wa Uvunjifu wa Amani kabla na baada ya Oktoba 29, bado swali la idadi ya watu waliokufa linagionga vichwa. Je, wataitaja hiyo idadi au watakaa kimya? Hata wakikaa kimya, inajulikana watu waliuawa na wengine miili yao haijawahi kuonekana tena mpaka leo.
La kuvunda halina ubani, hata wakificha hadi lini, ukweli huwa haufichwi, ipo siku tu utajidhihirisha. Lakini yote hii ni aibu waliyokuwa wakiitaka CCM. Ni ubinafsi wa kutaka kukumbatia madaraka yote, wakati wananchi wengi wakiogelea kwenye lindi la umasikini.
Ripoti ya hali ya furaha duniani imedhihirisha kuwa Watanzania wengi hawana furaha, hawana Amani, wanataka mabadiliko ya kweli yatakayowaletea furaha myoyoni mwao. Endapo CCM itaendelea kukaidi, hali itakuwa mbaya Zaidi siku za usoni.