Idimi
JF-Expert Member
- Mar 18, 2007
- 14,601
- 9,780
Ndimara Tegambwage
Polisi, vitisho na Stella wa Msewe
SITAKI polisi wa Tanzania wasahau kwamba ni kwa matendo yao au kwa kutotenda kwao, wanaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Na hivyo ndivyo itakavyokuwa. Hili likitokea. Ile dhana ya 'polisi ni usalama wa raia' itakuwa imetoweka. Hakuna atakayewaheshimu kama ambavyo hakuna atakayeweza kurejesha imani ya wananchi kwa polisi.
Ni wiki ya pili sasa tangu mwanamke mmoja wa Kijiji cha Msewe, Ubungo, Dar es Salaam, ahame nyumba yake kwa woga wa kushambuliwa na hata kuuawa.
Ni Stella Kajuna. Mfupi, mwembamba, hajai kwenye kiganja; lakini ni mama mmoja jasiri aliyetoa tuhuma dhidi ya mwanaume anayedaiwa kufanya ngono na wanafunzi wa kike katika Kijiji cha Msewe.
Stella anataja jina la kijana wa kiume anayehusika. Anataja majina ya wazazi wake. Anataja jina la mwanafunzi mhusika. Anataja jina la mwanafunzi mwingine; na mwingine.
Stella anataja majina ya wazee kijijini waliobughudhiwa na mtuhumiwa. Ana ujasiri wa kweli. Ni mwanamke. Lakini tangu alipotoa hadharani jina la mtuhumiwa, badala ya polisi kufuatilia mtuhumiwa wa uhalifu, wamekuwa wakimfuatilia Stella.
Kama hiyo haitoshi, mama wa mtuhumiwa anadaiwa kufungua mashitaka Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Yusufu kwamba Stella ametishia kumuua.
Licha ya tuhuma za 'kuharibu wanafunzi wa kike,' kijijini Msewe, kuna madai ya ujambazi unaofanywa na kufumbiwa macho na utawala wa kijiji. Kuna madai pia ya polisi wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu kushirikiana na watuhumiwa.
Je, baada ya Chato (Biharamulo) na Singida, wananchi walikojichukulia hatua ya kuvamia vituo vya polisi wakivituhumu kutotenda kazi zake, Mbezi kwa Yusufu imesalia wapi?
Je ni kwa kuwa Mbezi kwa Yusufu ni Dar es Salaam? Kwa kuwa kituo kipo karibu na Ikulu? Kwa kuwa ni langoni kwa Inspekta Jenerali ya Polisi (IGP), Said Mwema? Kwa kuwa watawala hawa hawasikii au wanawalinda wadogo zao Mbezi?
Watawala wamekuwa wakitaka wananchi watoe ushahidi kuhusiana na tuhuma wanazotoa. Polisi nao wamekuwa wakihimiza wananchi kutoa ushirikiano katika kukabili uhalifu na kutoa taarifa za kuwawezesha kufuatilia.
Ingawa ukweli ni kwamba ushahidi sharti utolewe mahakamani, lakini Stella ametoboa kila kitu alichonacho - nini kimefanyika, nani amefanya, nani kafanyiwa, wapi watuhumiwa wanaishi, mazingira ya Msewe na mengi mengine.
Lo! Zawadi ya Stella kwa kutoa taarifa za kufichua uhalifu imekuwa kusakamwa kwa vitisho, kutungiwa tuhuma za kutaka kuua na kunyemelewa kama mhalifu.
Stella angekuwa na uwezo wa kutamka neno 'kuua,' hakika asingetoa taarifa za uhalifu; angekuwa ametishia au ameua mapema. Kilio cha Stella ni haki kwa watoto wake na jamii. Inaonekana bado ana imani na utawala.
Sasa Stella, kila kukicha, ni kiguu na njia. Yuko kwa Kamanda wa Polisi Kinondoni; yuko Ofisi ya Makamu wa Rais; kwa Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia; kwa Mpelelezi Mkuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam anakosema alihojiwa kwa saa tano.
Stella anamtuhumu kijana wa kiume kubaka wanafunzi. Anawatuhumu polisi kutomtendea haki na kutotenda. Yote yanachunguzika. Vitisho kwa mama huyu vinatoka wapi?
Stella ana kila sababu ya kuwa na woga. Vijana Hija Shaha Saleh na Mine Chomba wako wapi? Wanasadikiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi Dar es Salaam. Wako wapi wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathias Lukombe wa Mahenge, mkoani Morogoro; na dereva wao Juma Ndungu. Inadaiwa maisha yao yalisitishwa wakiwa mikononi mwa polisi Dar es Salaam.
Katika hili la Stella, na jinsi anavyosumbuliwa, sharti Rais, Waziri Bakari Mwapachu, IGP, Watanzania wote na dunia nzima, wajue kwamba hapa hakuna utawala bora.
Kwa nini polisi na serikali wasubiri wananchi wa Msewe na viunga vya Dar es Salaam kumrejesha Stella nyumbani kwake kwa maandamano, huku wakipita Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Yusufu na kuwavuta mashavu polisi?
Hilo likitendeka, wakuu wa polisi watalalamika kwamba wananchi wamejichukulia sheria mikononi. Lakini wamsubiri nani, kama wa mwisho aliyetegemewa, ama amekuwa mshiriki wa watuhumiwa au amelala fofofo?
Stella hana uhuru tena. Lakini kurejea kwa uhuru wake kwaweza kuepusha janga na aibu kwa utawala, polisi na taifa. Na bado polisi wanaweza kumaliza hili kwa sekunde tu. IGP Mwema unasemaje?
Wavamia polisi na kuua mtuhumiwa
2007-10-22 08:47:45
Na Elisante John, PST, Singida
Mamia ya wananchi wenye ghadhabu wamevunja mahabusu ya kituo cha polisi cha Ilongero kilichoko wilayani Singida Vijijini, wakamtoa nje na kumpiga hadi kufa mtuhumiwa wa mauaji ya watoto wawili wa familia moja.
Aliyeuawa usiku wa kuamkia juzi ni Mile Nkindwa (20), mkazi wa Ilongelo wilayani hapo, aliyekuwa ametorokea kijiji jirani baada ya kufanya mauaji.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa kituoni kwa tuhuma za mauaji ya watoto wawili wa kike kwa kuwabaka, kuwalawiti na kuwanyonga kisha kuwatumbukiza ndani ya korongo na miili yao kugundulika ikiwa imetapakaa kinyesi na damu.
Habari kutoka kituo hicho zilisema Nkindwa baada ya mauaji hayo alitoroka na kujificha katika kijiji cha Mughamu.
Hata hivyo, mtuhumiwa mwenzake Hamisi Juma Msaghaa (33) amefikishwa mahakamani mjini Singida kujibu mashtaka ya mauaji.
Akielezea tukio hilo, diwani wa Kata ya Ilongelo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Singida, Bw. Ramadhan Samwi, alisema mauaji dhidi ya mtuhumiwa huyo yalifanyika juzi saa 4:00 usiku nje ya kituo hicho.
Alisema pamoja na kuwepo askari wa kutosha kutoka Singida mjini waliokwenda kituoni hapo kumchukua, wananchi walivamia kituo hicho kuanzia saa 3:00 usiku na kuwataka askari wamtoe mtuhumiwa aliyehusika na mauaji ya watoto hao.
Bw. Samwi aliongeza kuwa pamoja na askari kugoma kumtoa mtuhumiwa, wananchi walishinikiza atolewe hatua iliyosababisha wapige risasi hewani ili kuwatawanya lakini wananchi waliwazidi nguvu polisi na kuvunja milango na kumburuza nje mtuhumiwa na kumpiga hadi alipokata roho.
Aliongeza kuwa wanakijiji hao walimshambulia kwa mawe, marungu, fimbo na kila silaha waliyoiona hadi akaaga dunia.
Akifafanua zaidi, diwani alisema marehemu Mile alikamatwa baada ya baba yake akiongozana na mwenyekiti wa Kijiji cha Itamka Bw. Mamu Mloya, kwenda katika kijiji cha Mughamu ambako mtuhumiwa alijificha kwa jamaa zake baada mauaji hayo.
Alieleza kuwa walimnasa na kumfikisha kituo cha polisi cha Ilongelo ambako jioni yake ndipo alipouawa na wananchi hao waliokerwa na mauaji hayo ya kikatili.
Waliokufa katika mkasa huo ni mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mrama iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida pamoja na mdogo wake aliyekuwa akisoma masomo ya awali shuleni hapo.
Watoto hao ni Twaiba Athumani (13) na Zulfa Athumani (7).
Watoto hao wa Bw. Athumani Jumanne, walikumbwa na vifo hivyo vya kikatili Jumatatu iliyopita kati ya saa 12:00 jioni na 2:00 usiku katika shamba la viazi la mwanakijiji mmoja, umbali wa kilomita mbili kutoka nyumbani kwao, wakati walipokwenda kisimani kuchota maji.
Hili ni tukio la tatu katika mwezi huu la wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa kuvamia vituo walimowekwa watuhumiwa wa mauaji kwa lengo la kuwaua.
Mwanzoni mwa mwezi huu, wananchi wa wilaya ya Chato mkoani Kagera walivamia makao makuu ya polisi na kuchoma moto kituo kwa lengo la kumuua mtuhumiwa.
Katika tukio hilo, kulikuwa na uvumi kwamba kuna mwanamke kituoni hapo anashikiliwa na polisi baada ya kukutwa akiwa na ngozi ya binadamu.
Hata hivyo, habari za kipolisi zinaonyesha kuwa uvumi huo haukuwa wa kweli.
Wiki iliyopita, tukio kama hilo lilijiri mkoani Tanga ambapo watu wasiofahamika walivunja ofisi ya kijiji cha Nkogoi wilayani Lushoto na kumuua mtuhumiwa wa mauaji aliyekuwa amefungiwa ofisini humo.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa akisubiri kupelekwa polisi ni kijana wa miaka 22, Yahaya Omari. Yeye anadaiwa kumuua kwa kumpiga rungu kichwani Muhsin Rashid (15).
Marehemu Muhsin alikuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mavumbi.
* SOURCE: Nipashe
Wananchi wavamia kituo cha Polisi Wazo
Yusuf Badi
HabariLeo; Saturday,September 29, 2007 @00:01
Askari kanzu wa Kituo cha Polisi Wazo Dar es Salaam akimkimbiza mwanamke huku akimcharaza viboko baada ya watu zaidi ya 100 kuandamana hadi kwenye kituo hicho wakitaka wenzao watano waliokamatwa juzi katika Kijiji cha Madala Kati waachiwe huru. (Picha na Yusuf Badi).
POLISI wa Kituo cha Wazo Dar es Salaam, jana walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya wakazi zaidi ya 100 wa Kijiji cha Madala wilayani Kinondoni waliovamia kituo hicho wakitaka wenzao watano waliokamatwa juzi waachiwe huru.
Katika tukio hilo, watu wanane walikamatwa papo hapo wakiwamo wanawake wanne na kufanya idadi ya waliokamatwa tangu juzi kufikia 13. Tukio hilo lilitokea saa 4:20 asubuhi, baada ya mmoja wa wananchi hao kudai kuwa waliamua kufanya hivyo kutokana na uonevu uliofanywa na askari hao.
"Wenzetu watano wako ndani, walikamatwa bila makosa yoyote, kwani wao wamenyang'anywa mashamba yao na matajiri. Hawa matajiri wameshinikiza wenzetu wakamatwe kwa nini?" alihoji mmoja wa wakazi hao. Alisema baada ya kusikia Waziri Mkuu Edward Lowassa, jana angezindua ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Wazo, waliamua kuandamana kumfuata kumweleza malalamiko yao.
Hata hivyo kwenye uzinduzi huo, Waziri Mkuu aliwakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Dk. Batilda Buriani. Baada ya kuona hivyo ndipo wananchi hao waliokuwa na hasira walipoamua kwenda kwenye Kituo cha Polisi.
Askari wa kituo hicho walipoona hali inazidi kuwa mbaya upande wao, waliamua kufyatua risasi zaidi ya sita hewani kujaribu kuwatawanya wananchi hao, lakini hawakujali kwani walikuwa wakiendelea kusonga mbele. Ilichukua takribani dakika 10 ilipowasili gari iliyojaa Polisi kusaidia kuwatawanya wananchi hao na kuweza kuwakamata watu wapatao wanane ambao walipigwa na kuumizwa.
Huenda idadi ya waliokamatwa ingeongezeka kutokana na tafrani ya wananchi hao kukimbizana na polisi huku na kule, huku baadhi ya askari kanzu wakiwa na bunduki. Yamekuwapo matukio kadha ya wananchi kulalamikia Jeshi la Polisi, hasa katika vituo vya Kawe, Wazo, Kijiji cha Chasimba, Boko na Bunju, kuhusu baadhi ya askari kutumiwa na matajiri kuwatisha na kuwakamata ovyo wananchi katika jitihada binafsi za kujipatia mashamba.
Inaelezwa wananchi kadha wamekuwa wakipoteza mashamba yao kutokana na vitisho hivyo, jambo ambalo jana liliwatia hasira wananchi hao na kuamua kukivamia kituo hicho bila kuwa na silaha yoyote. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Kandoro, Mkuu wa Wilaya hiyo, Fabian Masawe na viongozi kadha wa serikali walishuhudia vurugu hizo zilizovuruga kwa muda shughuli za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo.
Masawe aliwataka wananchi kupunguza hasira na wafuate taratibu za sheria, ili suala lao lishughulikiwe ipasavyo. Hata hivyo, wananchi hao walilipinga wazo hilo wakidai kuwa hata Mkuu huyo wa Wilaya ni sehemu ya watu wanaotumika kuwadhoofisha katika madai yao ya msingi.
WWananchi wavunja ofisi ya DC, wachoma moto kituo cha polisi
Na Mwandishi Wetu, Ngara
WANANCHI wenye hasira kali wilayani Ngara mkoani Kagera wamefanya wamevunja ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo na kuchoma moto kituo cha Polisi cha wilaya hiyo.
Wananchi hao walifanya vurugu hizo jana jioni baada ya kupata habari za kuhifadhiwa kwa mtuhumiwa wa uchunaji ngozi za binadamu kwenye ofisi hizo.
Baada ya kupatikana kwa mtuhumiwa huyo anayedaiwa kukutwa na ngozi ya binadamu ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, wananchi walitaka kumwadhibu lakini wakazuiliwa na Polisi wa kituo hicho.
Kitendo cha Polisi kuzuia wananchi hao na kwenda kumhifadhi sehemu isiyojulikana kiliwapandisha hasira wananchi hao na kuanza kumsaka ndipo walipovamia ofisi hizo, baada kupata taarifa za uwezekano wa mtuhumiwa huyo kuhifadiwa humo.
Ofisi ya mkuu wa wilaya ilikuwa ya kwanza kuvunjwa na walipomkosa mtuhumiwa huyo waliamua kuhamia Kituo cha Polisi na kukiteketeza kwa moto.
Licha ya kuharibu ofisi hizo na mali zilizokuwepo, vurugu hizo zimedaiwa kuharibu zaidi ya magari mawili yaliyokuwepo kituoni hapo kwa kuyachoma moto.
Aidha, polisi wa kituo hicho akiwemo Mkuu wa Kituo (OCD) walijaribu kutawanya wananchi hao kwa kupiga risasi za moto angani, walioishiwa walikimbia kunusuru maisha yao.
Askari Polisi mmoja wa kituo hicho amejeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini baada ya kupata kipigo kutoka kwa wananchi alipotaka kuwazuia wananchi hao.
Moja ya magari yaliyochomwa moto limebainika kuwa mali ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). gari hilo aina ya Datsun lilikuwa limeegeshwa kituoni hapo.
Majira ilipowasiliana na RCO wa Mkoa wa Kagera Bw. George Mayunga alikiri kusikia habari hizo na kueleza kuwa yeye si msemaji na kwamba yupo kwenye kazi maalumu.
Aliimtaka mwandishi kuzungumza na RPC ambaye hata hiyo hakuweza kupatikana kwa simu yake ya mkononi.
Ndugu wana JF, hii tabia ya wananchi kujichukulia sheria mmikononi imekuwa sugu sasa. Suala la watuhumiwa vibaka kuuawa, watu kuvamia vituo vya polisi nk limekuwa tata sana. Shida iko wapi lakini? Kuna tatizo gani hapa? Utatuzi wa suala hili ni upi? Tufanye nini?